Nov 27, 2022 04:57 UTC
  • Mchango wa Maulamaa wa Kishia Katika Uislamu (58)

Ni matumaini yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji popote pale mlipo na karibuni katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Mchango wa Maulamaa wa Kishia Katika Uislamu, ili tuweze kwa pamoja kufungua ukurasa mwingine katika kurasa za historia ya Maulamaa na wanazuoni wa Kishia pamoja na mchango wao katika Uislamu.

 

Kipindi chetu kilichopita kilimalizia kumzungumzia Ayatullah Muhammad Hassan bin Baqir mashuhuri kwa lakabu ya Swahib al-Jawahir. Tulieleza kuwa, umashuhuri mkubwa wa Sheikh Muhammad Hassan Najafi unatokana na kitabu alichokiandika cha Jawahir al-Kalam. Kipindi chetu cha leo ambacho ni sehemu ya 58 kitaanza kuwazungumia Maulamaa walioishi katika karme ya 14 Hijria. Leo kipindi chetu kitatupia jicho kwa mukhtasari historia na maisha ya Ayatullah Sheikh Abul-Hassan Muhammad Baqir Qaini Birjandi mashuhuri kwa lakabu ya Muhadith Birjandi. Natumai mtajiunga nami hadi mwisho wa kipindi chetu juma hili.

Karne ya 14 Hijria inaweza kutajwa kuwa karne ya kuchanua na kustawi elimu na maarifa katika vyuo vikuu mbalimbali vya kidini (Hawza). Katika karne hii walileleka, kukulia na kuondokea Maulamaa na Shakhsia wakubwa katika miji midogo na mikubwa ya Iran na katika maeneo mengine ya ardhi za Kiislamu ambao majina na utajo wao umebakia katika historia. Miongoni mwao ni Ayatullah Sheikh Abul-Hassan Muhammad Baqir Qaini Birjandi, fakihi, mwanaisimu, mshairi na mwanateolojia mkubwa wa Kiiran.

Muhammad Baqir alizaliwa Mfunguo Sita Rabiul-Awwal 1276 Hijria katika kijiji Gazar, moja ya viunga vya mji wa Birjand, makao makuu ya mkoa wa Khorasan Kusini katika Iran ya leo. Familia yake yote ilikuwa ya watu wa elimu, fadhila, mashairi na fasihi ya lugha. Aidha mababu zake wa upande wa baba na upande wa mama pia, walikuwa wasomi na wanazuoni waliokuwa wachamungu, wenye zuhdi na waliokuwa wameipa mgongo dunia ambao daima walisimama kidete mbele ya dhulma ya madhalimu na kuwa kimbilio la wanyonge na waliodhulumiwa.

 

Baba yake ni Mulla Muhammad Hassan Qaini aliyekuwa mmoja wa Maulamaa maarufu na watajika katika mji wa Birjand katika zama hizo na mwalimu ambaye wanafunzi wake wengi baada yake waliondokea kuwa walimu mahiri. Babu yake alikuwa mmoja wa wanafunzi wa Allama Muhammad Baqir Majlisi mwandishi wa kitabu cha Bihar al-Anwar na alikuwa na maktaba kubwa ambayo ilichomwa moto katika vurugu na machafuko ya mwishoni mwa utawala wa ukoo wa Safavi nchini Iran na akthari ya vitabu vyenye thamani vikaporwa.

Allama Mulla Muhammad alisoma kwa baba yake mpaka alipofikisha umri wa miaka 12 na kujifunza kwake fasihi ya lugha na masomo ya awali na ya msingi. Baada ya hapo akiwa na shabaha ya kujiendeleza zaidi alielekea katika shule ya Ja’afariyah Qain. Ilikuwa imepita miaka miwili tu tangu awasili katika shule hiyo, wakati mmoja wa viongozi wa serikali alipotembelea skuli hiyo ambapo aliwataka walimu wa shule hiyo kuja na mkakati na mpango ambao utasaidia kupatia ufumbuzi matatizo ya kodi. Hakuna mwalimu na mtu yeyote aliyefanikiwa kutatua hilo. Muhammad Baqir licha ya kuwa umri mdogo mno wakati huo alijibu swali hilo. Jambo hilo lilipelekea ahamishiwe katika Shule ya Mirza Ja’afar katika mji wa Mash’had.

Muhammad Baqir Qaini alisoma fikihi, usul, falsafa na teolojia kwa muda wa miaka sita kwa Maulamaa wakubwa wa zama hizo huko Mash’had. Akiwa na umri wa miaka 20 alielekea katika Chuo Kikuu cha Kidini (Hawza) cha Najaf, Iraq. Alibakia katika mji huo kwa muda wa miaka 4 na mwaka 1300 Hijria alikwenda katika mji wa Samarra na kuhudhuria kwa muda wa miaka 6 masomo ya Ayatullah Mirza Shirazi Marjaa mkubwa wa Kishia katika zama hizo. Kwa amri ya mwalimu wake huyo, alianza kuandika kitabu cha Wathiqat al-Fuqahaa na mwalimu wake huyo alimshaajisha na kumpa moyo sana hasa baada ya kusoma na kuona alichokiandika. Hali hiyo ilimpa nguvu na msukumo wa kukamilisha kitabu hicho.

Muhammad Baqqir Qaini alikamilisha masomo yake akiwa na umri wa miaka 30 huko Iraq na kufanya safari Makka kwa ajili ya kwenda kutekeleza ibada tukufu ya Hija. Baada ya hapo alirejea katika mji aliozaliwa wa Birjand na kuoa. Akiwa mjini humo shakhsia wakubwa wa Birjand walimtaka achukue jukumu la uongozi wa Kiislamu ili aweze kupatia ufumbuzi hitilafu za wananchi zilizokuwako kuhusiana na namna ya kutoa zaka, khumsi na mengineyo. Alichukua jukumu hilo baada ya kuomba idhini kutoka kwa walimu wake.

Katika siku za awali za kuwasili kwake katika mji wa Birjand, Amir Alam ndiye aliyekuwa mtawala wa eneo hilo, hivyo akamualika katika kikao. Katika kikao hicho, alikuweko pia Mulla Ibrahim Hanafi, mmoja wa wasomi na wanazuoni wa Ahlu Sunna. Alimu huyo wa Kisuni alikuwa mashuhuri kwa kubobea katika taaluma na elimu za teolojia na mdahalo na kila mara alikuwa akifanya mdahalo na Maulamaa wa Kishia mara hii pia alifanya mjadala na Allama Birjandi katika suala la Uimamu. Mdahalo huo ulimalizika kwa Allama Birjandi kumshinda Mulla Ibrahim na hilo likapelekea kuwa sababu ya kuwa mashuhuri baina ya watu. Kuanzia wakati huo, wakazi wote wa eneo la Qain na Birjand na hata wananchi wa Afghanistan Masuni Mahanafi na Mashia wakawa wakimrejea alimu na mwanazuoni huyo wakiwa na maswali mbambali ya madhehebu zao naye akiwajibu na kuwapa miongozo kwa mujibu wa itikadi na madhehebu yao na kutoa fatuwa mbalimbali kwa mujibu wa madhehebu tofauti. Hilo lilipelekea apatiwe lakabu ya “Muft al-Fariqein” yaani Mufti wa makundi mawili. Ilikuwa imepita miaka mitatu tu tangu mwanazuoni huyo awasili Birjand wakati Amir Alam, mtawala wa wakati huo wa eneo hili alipoaga dunia na mwanawe akashika hatamu za uongozi.

Shule ya Mirza Ja’afar katika mji wa Mash’had.

 

Mbali na mwanazuoni huyu kujihusisha na kufundisha alikuwa mahiri pia katika kualifu na kuandika vitabu katika maudhui muhimu kama Fikihi, Usul, historia, tafsiri, hadithi, teolojia na fasihi. Ameacha takribani athari 62 ambazo akthari yake zimeandikwa kwa hati na mkono wake ambazo zinapatikana katika Maktaba ya marehemu Ayatullahil-Udhma Mar’ashi Najafi katika mji wa Qom aliyekuwa mmoja wa wanafunzi wake.

Moja ya vitabu vyake mashuhuri ni Kibrit Ahmar ambapo pamoja na mambo mengine ndani yake amebainisha kwa mapana na marefu adabu za kupanda katika mimbari na kutoa muhadhara, nafasi ya mimbari na faida zake na fadhila za mawaidha. Anaeleza katika sehemu moja ya kitabu chake hicho kwamba, siyo kila mtu anastahiki kupanda mimbari na kutoa mawaidha. Anataja sifa 20 kama masharti ya mwenye kupanda mimbari na kutoa waadhi ambayo anapaswa kuyakamilisha.

Katika sehemu nyingine ya kitabu chake hicho, Allama Muhammad Baqir Birjandi anabainisha mitazamo yake na kupinga vikali harakati za kupotosha tukio la Ashura na harakati ya Imam Hussein (as). Aidha katika kitabu hicho, anakosoa baadhi ya upotoshaji wa Ashura. Kitabu hiki kimechapishwa mara chungu nzima nchini India na Iran kama ambavyo kimetarjumiwa kwa lugha ya Kiurdu.

Msomi huyo alikuwa mahiri pia katika uga wa isimu na fasimu ya lugha ambapo alikuwa akitunga mashairi kwa lugha mbili za Kiarabu na Kifarsi. Mwanawe yaani Ayatullah Sheikh Muhammad Hussein Aayati Dhiyai amekusanya takribani beti 2,000 za mashairi yaliyotungwa na baba yake.

Maktaba ya marehemu Ayatullahil-Udhma Mar’ashi Najafi katika mji wa Qom

 

Ayatullah Birjandi alikuwa akiamini kwamba, watu wote wanapaswa na ni wajibu kwao kujifunza mbinu za kijeshi na upiganaji na kujiandaa kikamilifu kwa ajili ya siku ambayo kutatokea jihadi. Yeye mwenyewe alikuwa akichukua bunduki yake kila siku na kwenda na kundi fulani la watu kwa ajili ya kufanya mazoezi ya kulenga shabaha. Alimu huyu aliishi katika zama za watawala wasio na ustahiki wa Qajar nchini Iran ambapo ingia toka ya maajinabi nchini Iran ilikuwa imekithiri sambamba na matakwa yao yasiyo na mwisho kwa utawala wa wakati huo hapa nchini.

Hatimaye Allama Muhammad Baqir Birjandi aliaga dunia usiku wa kuamkia Ijumaa tarehe 14 Mfunguo Tatu Dhul-Hija 1352 Hijria akiwa na umri wa miaka 76 na kuacha nyuma hazina na dafina kubwa ya elimu.

Wapenzi wasikilizaji muda wa kipindi chetu kwa leo umefikia tamati, tukutane tena wiki ijayo.

Wassalaam Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh