Dec 18, 2022 04:12 UTC
  • Jumapili, 18 Disemba, 2022

Leo ni Jumapili tarehe 23 Mfunguo Nane Jamadul-Awwal 1444 Hijria sawa na tarehe 18 Disemba 2022 Miladia.

Miaka 137 iliyopita katika siku kama ya leo kulingana na kalenda ya Hijria, aliaga dunia Sayyid Muhammad Ibrahim mashuhuri kwa lakabu ya Sayyidul Ulamaa, alimu na fakihi wa Kiislamu wa nchini India. Alikuwa mmoja miongoni mwa maulama watajika na mahiri mwanzoni mwa karne ya 14 Hijria. Baada ya kufariki dunia baba yake, Muhammad Ibrahim alichukua jukumu la kueneza mafundisho ya dini katika baadhi ya miji ya India. Mwanazuoni huyo alifanya hima kubwa ya kueneza misingi na itikadi za Kiislamu katika ardhi ya India. Vilevile ameandika vitabu na makala nyingi. ***

Sayyid Muhammad Ibrahim mashuhuri kwa lakabu ya Sayyidul Ulamaa

 

Miaka 108 iliyopita katika siku kama ya leo, Uingereza iliikoloni rasmi Misri. Inafaa kukumbusha kwamba, wakati wa Vita vya Kwanza vya Dunia, utawala wa Othmania ulikuwa muitifaki wa madola yaliyokuwa yakiipinga Uingereza yaani Ujerumani na Austria. Uingereza nayo ikiwa na lengo la kukabiliana na kitendo hicho, iliikalia kwa mabavu Misri, ambayo hadi katika kipindi hicho ilikuwa chini ya udhibiti na utawala wa Othmania. Harakati za ukombozi za wananchi wa Misri dhidi ya mkoloni Mwingereza zilizaa matunda mwaka 1922, ambapo nchi hiyo ilijitangazia uhuru wake. ***

Bendera ya Misri

 

Katika siku kama ya leo miaka 84 iliyopita msomi wa Ujerumani, Otto Hahn, alifanikiwa kupasua kiini cha atomu, hatua ambayo ilikuwa mwanzo wa zama za atomu. Mtaalamu huyo wa kemia alizaliwa mwaka 1879 huko Frankfurt na kupata shahada ya uzamivu katika taaluma ya kemia. Tangu wakati huo alijishughulisha na utafiti katika taaluma ya fizikia. Baada ya utafiti mkubwa na katika siku kama hii ya leo Otto Hahn alifanikiwa kupasua kiini cha atomu. Hatua hiyo iliibua nishati kubwa ambayo baadaye ilianza kutumika katika vinu na mabomu ya nyuklia. Mwaka 1944 Otto Hahn alitunikiwa tuzo ya Nobel katika taaluma ya kemia. ***

Otto Hahn

 

Tarehe 18 Disemba miaka 43 iliyopita, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipasisha makubaliano ya kufuta aina zote za ubaguzi dhidi ya wanawake. Makubaliano hayo yana lengo la kuondoa dhulma zinazofanywa dhidi ya wanawake duniani. Hata hivyo makubaliano hayo, kama yalivyo mengine mengi ya kimataifa, yanatawaliwa na mitazamo ya kimaada ya Magharibi inayosisitiza usawa wa jinsia mbili za mwanamke na mwanaume katika kila kitu. Hii ni katika hali ambayo mwanamke na mwanaume wanatofautiana kimwili na kiroho. Kwa sababu hiyo dini za Mwenyezi Mungu hususan Uislamu unasisitiza kuwa njia ya kuwakomboa wanawake ni kuwatayarishia mazingira ya uadilifu kwa kutilia maanani uwezo wao wa kimwili na kiroho. ***

Kamisheni ya kufuta aina zote za ubaguzi dhidi ya wanawake