Jan 21, 2023 09:05 UTC
  • Akhlaqi Katika Uislamu (51)

Amani ya Allah, rehma na baraka zake ziwe juu yako mpendwa msikilizaji popote pale ulipo wakati huu. Nakukaribisha kusikiliza sehemu ya 51 ya kipindi cha Akhlaqi Katika Uislamu nikiwa na matumaini kuwa, mimi pamoja na wewe tutanufaika na yale tutakayoyasikia katika kipindi hiki ambacho kwa leo kitaendelea kuzungumzia umuhimu na nafasi ya Akhlaqi za Jihadi katika Uislamu. Endelea kuwa nami basi hadi tamati ya mazungumzo yetu.

Katika mfululizo uliopita wa kipindi hiki tulieleza kwamba Uislamu si dini iliyosimama na kuenea kwa upanga kama inavyodaiwa na wapinzani wake na tukalijibu dai hilo kwa kubainisha kuwa, ikiwa adui hatainua silaha na kuanzisha vita, Uislamu utaamiliana naye kwa njia za amani, hoja, burhani na mantiki za hekima; na ghaya na lengo la dini hiyo tukufu litabaki kuwa ni kuiongoza na kuionyesha jamii ya mwanadamu njia iliyonyooka, ya saada na ukamilifu wa kiutu. Lakini pale maadui wanapoanzisha hujuma za mtutu wa bunduki, mafunzo na mafundisho ya Kiislamu yanawaamuru na kuwataka Waislamu wasimame kupambana na kukabiliana na hujuma hizo. Na kwa msingi huo, kulingana na mtazamo wa Uislamu unaoendana na uhalisia wa mambo, Jihadi ya kukabiliana na njama za maadui ni jambo la lazima na lisiloepukika; na lina hadhi na nafasi maalumu katika dini hiyo.

Katika aya zake nyingi, Qur'ani tukufu inatoa mwito wa kukabiliana na wanaopiga vita dini na viranja wa uwashaji moto wa vita wa kambi ya ukafiri na kumtaka Bwana Mtume SAW na waumini wapigane Jihadi kama aya ya 73 ya Suratu-Tawba inavyosema: "Ewe Nabii! Pambana na makafiri na wanaafiki, na wakazanie. Na makaazi yao ni Jahannamu, na huo ndio mwisho mbaya". 

Katika kuonyesha hadhi tukufu na umuhimu wa kipekee wa Jihadi na kupigana vita katika njia yake, Mwenyezi Mungu Mtukufu anatueleza kwamba wale wanaopigana katika njia yake, wana hadhi ya kupendwa na kuridhiwa na Yeye Mola kama aya ya nne ya Suratu-S'saf inavyosema: "Kwa hakika Mwenyezi Mungu anawapenda wanao pigana katika Njia yake kwa safu kama jengo lilio kamatana".

Na naam, ni wazi kwamba moja ya matamanio na matarajio makubwa zaidi ya kila mja anayemwamini Mwenyezi Mungu ni kufikia daraja ya kuwa mja anayependwa na Yeye Mola; lakini hakuna shaka yoyote kuwa tamanio hilo linaweza kupatikana katika medani ya amali na matendo. Qur'ani tukufu inalieleza hilo kama ifuatavyo katika aya ya 20 ya Suratu-Tawba: "Wale walio amini, na wakahama, na wakapigana Jihadi katika Njia ya Mwenyezi Mungu kwa mali zao na nafsi zao, hao wana cheo kikubwa zaidi mbele ya Mwenyezi Mungu. Na hao ndio wenye kufuzu". Kwa mujibu wa aya hii, Mwenyezi Mungu Mtukufu anawatambulisha kuwa wamefuzu wale watu ambao wanautumia uwezo na kila walichonacho, katika medani za mapambano na Jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu kwa ajili ya kuulinda Uislamu; na badala ya dunia hii ya kupita na yenye mwisho, wanafikiria mustakabali wa milele katika ulimwengu mwingine wa akhera, ambao katika aya inayofuatia ya 21 maneno matukufu ya wahyi wa Qur'ani yanauelezea hivi: "Mola wao Mlezi anawabashiria rehema zitokazo kwake, na radhi, na Bustani ambazo humo watapata neema za kudumu". Kumalizika na kuwa na mwisho starehe zenye kuhadaa za dunia, na kuendelea na kubaki milele neema za ulimwengu wa kudumu wa akhera kumetiliwa mkazo mara kwa mara katika aya nyingi za Qur'ani tukufu, ambapo sehemu ya mwisho ya aya ya 21 tuliyosoma pia imelisisitiza hilo iliposema:"…humo watapata neema za kudumu", ikibainisha ukweli huo, unaotiliwa mkazo zaidi katika aya inayofuatia ya 22 isemayo: "Watadumu humo milele. Hakika kwa Mwenyezi Mungu yapo malipo makubwa".

Katika uhitimishaji wa maudhui za aya hizi imetumiwa misemo "daraja na hadhi kubwa mbele ya Mwenyezi Mungu", "huko ndiko kufuzu", "bishara ya rehma nyingi za Mola", "kufikia cheo na daraja ya kupata radhi za Mwenyezi Mungu", "kuingia kwenye Pepo ya milele" na "kulipwa malipo makubwa mbele ya Mwenyezi Mungu", yote hayo yakimaanisha hadhi maalumu na ya juu mno ya Jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu, katika utamaduni na mafundisho ya Uislamu.

Kwa ilhamu inayopatikana katika aya hizi, Bwana Mtume SAW aliibainisha kwa sura na namna nyingine thamani na uzito wa mchango wa mujahidina na wanaopigana katika njia ya Mwenyezi Mungu aliposema: "Amali za waja wote wa Allah zikilinganishwa na thamani ya wanaopigana Jihadi katika njia ya Allah ni mithili ya ndege mbayuwayu aliyechota maji ya bahari pana kwa ncha ya mdomo wake". (Kanzul-Ummal, Hadithi ya 10,680)

Katika kipindi kifupi cha kuasisi utawala mjini Madina, Bwana Mtume SAW alishiriki sana na akatoa mchango mkubwa katika vita vya Jihadi vya Badr, Uhud na Ahzab; na ili kuwabainishia Waislamu utukufu na hadhi ya juu mno iliyonayo Jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu na kupambana na maadui na wavamizi wa ardhi za Waislamu, alikuwa akiwaambia masahaba zake: "Lindo la usiku mmoja katika njia ya Allah (kwenye medani za vita) lina fadhila na thamani zaidi kuliko usiku na mchana elfu moja, ambao usiku wake unapitishwa kwa ibada na mchana wake kwa funga". (Kanzul-Ummal)

Nukta muhimu sana iliyotiliwa mkazo mkubwa katika mtazamo wa Uislamu kuhusiana na Jihadi ni kwamba, watu pekee wanaofanikiwa kushiriki kwenye medani za mapambano ya haki dhidi ya batili ni wale ambao wamejijenga na kujisafisha katika kila hali; na kwa upande wa kiroho na kimaanawi wamefikia daraja ya kutunukiwa hadhi maalumu mbele ya Mola Mwenyezi. Na kwa maelezo hayo mpendwa msikilizaji, niseme pia kuwa sehemu ya 51 ya kipindi cha Akhlaqi Katika Uislamu imefikia tamati. Hivyo sina budi kukuaga hadi wakati mwingine inshallah, tutakapokutana tena katika sehemu ya 52 ya kipindi hiki. Namuomba Mola wa haki akubariki; na amani, rehma na baraka zake ziendelee kuwa juu yako…/