Apr 11, 2023 07:07 UTC
  • Akhlaqi Katika Uislamu (54)

Amani ya Allah, rehma na baraka zake ziwe juu yako mpendwa msikilizaji popote pale ulipo wakati huu. Nakukaribisha kusikiliza sehemu ya 54 ya kipindi cha Akhlaqi Katika Uislamu nikiwa na matumaini kuwa, mimi pamoja na wewe tutanufaika na yale tutakayoyasikia katika kipindi hiki ambacho kwa leo kitazungumzia nafasi ya suluhu katika mafundisho ya dini tukufu ya Uislamu. Endelea kuwa nami basi hadi tamati ya mazungumzo yetu.

Bila shaka mpendwa msikilizaji ungali unakumbuka kuwa katika kipindi kilichopita tulieleza kwamba kuchunga misingi ya kiakhlaqi na kiutu katika medani za vita ni moja ya sifa muhimu za mfumo wa kijeshi wa Uislamu wa asili alioulingania Bwana Mtume Muhammad SAW.

Ni vyema ukatambua pia kuwa katika utamaduni wa Uislamu sahihi unaojali kuishi kwa amani na masikilizano, suluhu ni suala linalopewa hadhi na nafasi ya juu. Na huu ni wito wa kudumu uliotolewa na Mwenyezi Mungu kwa waumini kama isemavyo aya ya 208 ya Suratul Baqarah: “Enyi mlio amini! Ingieni nyote kwenye suluhu na mapatano"…, na kisha aya inaendelea kusema: … “wala msifuate nyayo za She'tani; hakika yeye kwenu ni adui aliye wazi”.

Katika mtazamo wa ujumla, ujumbe unaofikishwa na aya hii ni kwamba, suluhu na mapatano ndilo lengo tukufu linalopiganiwa na Mwenyezi Mungu na dini yake; na vita na mapigano yasiyo na mantiki na ya maangamizi ni lengo la kishetani tu ambalo tawala zenye sifa za kishetani zinaitwisha jamii ya wanadamu na kuisababishia hasara na madhara yasiyoweza kufidika.

Kwa hivyo katika utamaduni wa Uislamu wa asili unaomwongoza mwanadamu kwa kumpa basira na kumfikisha kwenye saada na fanaka, suluhu ndilo suala la msingi, kwa maana kwamba Uislamu hutoa amri ya kupigana vita pale tu maadui wenye chuki na vinyongo na dini hiyo ya Mwenyezi Mungu wanaposhupalia na kupiga upatu wa kuanzisha vita. Inapofikia hatua hii, na kama tulivyoeleza katika kipindi kilichopita, ndipo Mwenyezi Mungu mwingi wa rehma na huruma, aliyeanzisha msingi huo wa suluhu, anapowahutubu waumini kama isemavyo aya ya 190 ya Suratul Baqarah ya kwamba: “Na piganeni katika Njia ya Mwenyezi Mungu na wale wanao kupigeni, wala msianze uadui. Kwani Mwenyezi Mungu hawapendi waanzao uadui”. Lakini hata inapofikia hatua hii, Uislamu unakuwa tayari pia kukubali pendekezo la suluhu endapo adui atakuwa tayari kufanya hivyo; yaani kama atakomesha vita alivyoanzisha na kuwa tayari kufikia suluhu ya kweli, kama aya ya 90 ya Suratu-Nisaa inavyotuambia: “…  Basi wakijitenga nanyi, wasipigane nanyi, na wakakuleteeni amani, basi Mwenyezi Mungu hakukupeni njia kupigana nao”.

Pamoja na hayo, inawezekana Waislamu walioingia vitani wakapatwa na wasiwasi wa kwamba kuna dhamana na uhakika gani kuwa adui ataheshimu suluhu aliyoitangaza? Ili kuwaondolea wasiwasi huo na kuwapa utulivu wa moyo na nafsi, Mwenyezi Mungu alimwagiza Bwana Mtume SAW afanye kama aya ya 61 ya Suratul Anfal inavyosema: “Na wakielekea amani nawe pia elekea, na mtegemee Mwenyezi Mungu. Hakika Yeye ndiye Mwenye kusikia Mwenye kujua”.

Hakuna shaka kuwa kutawakali na kumtegemea Mwenyezi Mungu ndio mwega na msukumo mkubwa na wa uhakika zaidi wa kimaanawi. Lakini hiyo haimaanishi katu kwamba, tujibweteke tu pasi na kukabiliana na njama na kuhalifu ahadi na makubaliano kunakofanywa na maadui. Maana hasa ya kutawakali kwa Mwenyezi Mungu ni kudumu, katika muda wote wa misukosuko ya vita, kuwa na utulivu wetu wa kiroho na kifikra na kutotegemea mbinu na uwezo wetu tu tulionao, bali tuwe na yakini kwamba nusra na ushindi unatokana na Mwenyezi Mungu tu, ambaye ni dhihirisho la juu kabisa la nguvu zote katika ulimwengu. Wakati Imam Ali (AS) alipompeleka Misri Malik Ashtar kuwa Liwali wa huko, alimweleza yafuatayo kuhusiana na suluhu, katika mwongozo wake uliokuwa na ilhamu ya maneno matukufu ya Qur'ani: "Usiikatae katu suluhu inayopendekezwa na adui ambayo ndani yake zinapatikana radhi za Mwenyezi Mungu, kwani suluhu italipa jeshi utulivu na kuweza kujizatiti upya; kwa wewe mwenyewe itakuondolea wasiwasi na kwa watu, itawaletea amani. Lakini pia uwe makini, uwe na hadhari, kwani si hasha lengo la adui la kukubali suluhu likawa ni kuja kukushtukiza. Kwa hivyo uwe na uono wa mbali na uache kujenga tu dhana njema bila ya nadhari na bila ya kuwa na sababu"... (sehemu ya Barua ya 53)

Kulingana na miongozo hii wadhiha na ya wazi kabisa iliyomo katika utamaduni wa Jihadi wa Uislamu, "suluhu na mapatano" ni msingi na kanuni kuu, kwa maana kwamba, madamu ingali ipo njia ya kuleta suluhu na kupatikana utulivu, Uislamu unalikubali suala hilo na kuamini kwa dhati kwamba, njia ya kuziteka fikra na nyoyo ni ile inayosimama juu ya misingi ya hoja za akili na mantiki; na hiyo ndiyo njia endelevu na ya kudumu. Ni kinyume na ushupaliaji na uwashaji moto wa vita usio na mantiki yoyote ufanywao na watawala wenye uchu; moto wa vita ambao hauna matokeo mengine ghairi ya kuchochea vinyongo na chuki, kushamirisha mauaji ya halaiki, kuteketeza majengo, kuvuruga amani na usalama na kusababisha hasara zisizohesabika za mali na roho za watu.

Nukta ya mwisho inayohusiana na msingi mkuu wa suluhu katika Uislamu ni kutiliwa mkazo pia suluhu ya haki na uadilifu. Ni suluhu ambayo haki za kiuadilifu za vita zinazingatiwa ndani yake. Ni suluhu ambayo hakuna haki inayoporwa na kukanyagwa ndani yake, ni suluhu inayozingatia katika hali zote manufaa ya pande zilizo katika vita na kuziletea nchi na mataifa amani na utulivu. Qur'ani tukufu imelipa uzito na umuhimu mkubwa suala la kuleta suluhu kama isemavyo aya ya tisa ya Suratul-Hujuraat kuhusiana na hata Waislamu wenyewe ya kwamba: "Na ikiwa makundi mawili katika Waumini yanapigana, basi yapatanisheni… na kisha sehemu ya mwisho ya aya hiyo inamalizia kwa kusema: … "Hakika Mwenyezi Mungu anawapenda wanao hukumu kwa haki". Huku tukitamani tuje kushuhudia siku ya kuondoka wingu zito la vita lililougubika ulimwengu; na suluhu, amani na utulivu kutanda kwenye anga ya jamii ya wanadamu, niseme pia mpendwa msikilizaji ya kwamba sehemu ya 54 ya kipindi cha Akhlaqi Katika Uislamu imefikia tamati. Hivyo sina budi kukuaga hadi wakati mwingine inshallah, tutakapokutana tena katika sehemu ya 55 ya kipindi hiki. Namuomba Mola wa haki akubariki; na amani, rehma na baraka zake ziendelee kuwa juu yako…/

 

 

 

 

 

Tags