Apr 11, 2023 07:02 UTC
  • Akhlaqi Katika Uislamu (53)

Amani ya Allah, rehma na baraka zake ziwe juu yako mpendwa msikilizaji popote pale ulipo wakati huu. Nakukaribisha kusikiliza sehemu ya 53 ya kipindi cha Akhlaqi Katika Uislamu nikiwa na matumaini kuwa, mimi pamoja na wewe tutanufaika na yale tutakayoyasikia katika kipindi hiki ambacho kwa leo kitazungumzia udharura wa kuchunga misingi ya kiakhlaqi na kiutu katika medani za vita kulingana na mafundisho ya dini tukufu ya Uislamu. Endelea kuwa nami basi hadi tamati ya mazungumzo yetu.

Katika kipindi kilichopita tulikumbusha kuwa katika sifa za kipekee za akhlaqi za Jihadi katika Uislamu asili uliofunzwa na Bwana Mtume SAW, mbali na sisitizo la kuimarishwa miundomsingi na uwezo wa kijeshi, ni kuegemea pia mwega wa thamani za kimaanawi; zikiwemo dua, kufanya munajati na kunong'ona na Mwenyezi Mungu Mtukufu. Na kwa sababu hiyo kuchunga "misingi ya kiakhlaqi na kiutu" ni kielezo kingine kinachoupambanua utambulisho na utamaduni wa Jihadi wa Uislamu ukilinganishwa na vita vinavyoanzishwa na mifumo ya kibeberu na kiistikbari.

Katika akthari ya vita ambavyo watawala madikteta wamevianzisha na wanaviendeleza duniani, kwa kuwa lengo la kuanzisha vita hivyo ni kutaka kuwatawala watu, kupora utajiri na maliasili za mataifa, kutaka kuwa na sauti ya juu na kulinda maslahi yao na kuimarisha madaraka yao, kufanya jinai yoyote ile huwa na uhalali kwao wao. Huwa tayari kuteketeza roho za wanawake na watoto wasio na hatia na kuangamiza kila kitu, alimradi tu waweze kufanikisha malengo yao ya kishetani na yaliyo dhidi ya ubinadamu. Vita vikuu vya kwanza na vya pili vya dunia, kushambuliwa miji ya Hiroshima na Nagasaki kwa mabomu ya nyuklia, utumiaji wa silaha za kemikali, za vijidudu na atomiki na kushambulia kinyama mataifa na nchi zinazopigania kujitawala na kuwa na misimamo huru, ni mifano ya wazi ya sura halisi ya vita vinavyoanzishwa na tawala za kibeberu za dunia yetu ya leo, ambazo huko nyuma zilifanya, na hadi sasa zinaendelea kufanya kila aina ya jinai. Lakini katika utamaduni wa Jihadi wa Uislamu "misingi ya kiakhlaqi na kiutu" inachungwa na kupewa nafasi maalumu hata katika vita na mapigano. Kwa kuzingatia kuwa lengo la Mfumo wa Kiislamu si kunyakua ardhi na kuwahodhi watu, ndio maana mipango, sera na hatua zote zinazochukuliwa na mfumo huo katika kilele cha vita na mapigano na adui ni kuhakikisha kuwa wale waliodanganywa na kuhadaiwa wanarejea kwenye mkondo wa njia iliyonyooka na kuupokea Uislamu kwa basira na uelewa kamili.

Moja ya mifano ya wazi na usiosahaulika, ambao unaendelea kung'ara katika historia ya Uislamu na kuipa jamii ya mwanadamu funzo na ilhamu ya kutafakari, ni kadhia ya kukombolewa mji wa Makka. Baada ya Bwana Mtume SAW na masahaba zake kuvumilia tabu, mateso, vitisho, vikwazo na vita vya mtawalia vya makafiri, hatimaye baada ya kupita miaka kadhaa na wakiwa katika kilele cha nguvu na uwezo waliingia katika mji mtukufu wa Makka, wa ardhi yao ya jadi wakiwa na jeshi lililojipanga kwa nidhamu kamili. Walipoingia mjini humo, Waislamu walikuwa na wazo la kulipiza kisasi kwa jeshi lililojawa na khofu la maashrafu na mamwinyi wa Kikureishi, la washirikina ambao kwa muda wa miongo miwili halikuacha kuchukua kila hatua ya kiuadui dhidi yao. Wakiwa katika hamasa, mori na ari ya kufanya hivyo, walipaza sauti zao wakisema: "leo ni siku ya kulipiza kisasi", kiasi cha kuwatetemesha na kuwatia hofu maadui hao wakubwa wa Uislamu. Hata hivyo katika hali ambayo haikutarajiwa hata kidogo, Bwana Mtume SAW, ambaye kwa mujibu wa Qur'ani ni dhihirisho la vilelelezo vyote vya rehma na huruma kwa wanadamu wote duniani, alitoa amri Waislamu watoe nara na kaulimbiu ya "leo ni siku ya rehma, ya kuhurumia na kusamehe"; na baada ya kutangazwa mbiu hiyo ya kutia matumaini, nabii huyo wa rehma alitoa msamaha kwa watu wote.

Tajiriba ya vita vikuu vya dunia inaonyesha kuwa, watu waliokuwa na kiu na uchu wa madaraka, walitumia mbinu ya kuua kwa halaiki watu wasio na hatia ili waweze kupata ushindi katika vita; na walikuwa wakiandaa mazingira ya kueneza hofu na vitisho ili kwa kufanya hivyo, waweze kuyapigisha magoti mataifa kwa kuvunja nguvu ya upinzani na muqawama wa mataifa hayo yaliyokuwa yakikabiliana na madola ya kishetani na yasiyojali utu. Lakini katika mfumo wa kijeshi wa Uislamu, vitendo vya utoaji vitisho na mauaji ya kikatili na ya kinyama hayana nafasi yoyote.

Wakati Bwana Mtume SAW alipokuwa akiandaa jeshi la Waislamu na kupanga safu za wapiganaji wake kwa ajili ya kukabiliana na maadui wasio na mantiki na washupaliaji vita, kabla ya kuwapeleka kwenye medani ili kubariziana na maadui, alikuwa akiwausia masahaba zake kwa kuwaambia: "msitumie hila na hadaa, msifanye usaliti, msizifanyie vitendo vya ukatili maiti za maadui, msikate mti wowote isipokuwa mtapokuwa hamna budi na wala msiwaue wazee, watoto na wanawake". (Wasaailu-Shia, Juzuu ya 11)

Mwongozo huu wa Bwana Mtume SAW unaonyesha kwa uwazi kabisa kwamba, iwe ni katika shwari au hamkani ya vita, misingi ya kiakhlaqi na kiutu, inapasa ichungwe na kuheshimiwa kwa hali yoyote ile, kiasi kwamba hata maliasili zikiwemo za miti na mimea hazipasi kuharibiwa bila ya sababu ya lazima; na kwa upande wa watu, jeshi la Kiislamu linatakiwa lipambane na wale tu waliojizatiti kwa zana za kivita, wakajipanga na kujiweka tayari kulishambulia jeshi la Waislamu. Kuhusiana na nukta hii, sehemu ya mwisho ya aya ya 194 ya Suratul-Baqarah inatuambia: "Anaye kushambulieni nanyi mshambulieni, kwa kadiri alivyo kushambulieni. Na mcheni Mwenyezi Mungu. Na jueni kwamba Mwenyezi Mungu yu pamoja na wachamngu".

Sehemu ya mwisho ya aya hii imebeba ujumbe wa mazingatio, nao ni kwamba imani juu ya Mwenyezi Mungu ndio msukumo muhimu zaidi wa kuwawezesha Waislamu kuchunga misingi ya kiakhlaqi na kiutu katika medani za vita. Kwa maneno mengine ni kuwa, katika kilele cha vita, mori na moto wa ulipizaji kisasi, uteketezaji na kufanya uharibifu hutokota ndani ya nyoyo za watu; ambapo kushikamana na taqwa na kuchunga mipaka ya Mwenyezi Mungu huwa ndicho kitu pekee kinachoweza kumdhibiti na kumfanya mpiganaji achukue hatua sahihi.

Kwa mujibu wa maandiko sahihi ya historia, katika vita vya Ahzab, ambavyo Bwana Mtume SAW alivielezea kuwa ni siku ukafiri wote ulipojipanga kukabiliana na Uislamu wote, Ali (AS) aliingia uwanjani kubariziana na Amr Ibn Abd Wud, mpiganaji jabari wa Kikureishi ambaye hakukuwa na mwenye ujasiri wa kupambana naye. Baada ya Ali (AS) kumzidi mbinu shujaa huyo wa makureishi kwa kumbwaga chini na kumkalia kifuani, Ibn Abd Wud, ambaye hakudhani katu kama atakuja kushindwa na kijana mdogo wa miaka ishirini na ushei tu, alimtemea mate usoni Ali (AS) kwa hasira. Hata hivyo Ali (AS) alidhibiti hasira zake na kurudi nyuma ili kuonyesha kwamba hakuwa amekwenda kubariziana naye kwa ajili ya kulipiza kisasi, bali alijitosa kwenye medani ya Jihadi kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, kuihami dini yake ya haki ya Uislamu na kuutokomeza ukafiri; na kwamba katika kufanya hivyo misingi ya kiakhlaqi na mipaka ya Mwenyezi Mungu haipasi kuvukwa kwa namna yoyote ile. Lakini baada ya kutulia ghadhabu zake, Ali (AS) alimrudia tena na kummaliza Amr Ibn Abd Wud, aliyekuwa dhihirisho kamili la ukafiri wa zama hizo na kuuletea ushindi mkubwa Uislamu na Waislamu. Na kwa maelezo hayo mpendwa msikilizaji, niseme pia kuwa sehemu ya 53 ya kipindi cha Akhlaqi Katika Uislamu imefikia tamati. Hivyo sina budi kukuaga hadi wakati mwingine inshallah, tutakapokutana tena katika sehemu ya 54 ya kipindi hiki. Namuomba Mola wa haki akubariki; na amani, rehma na baraka zake ziendelee kuwa juu yako…/