Apr 11, 2023 07:10 UTC
  • Akhlaqi Katika Uislamu (55)

Amani ya Allah, rehma na baraka zake ziwe juu yako mpendwa msikilizaji popote pale ulipo wakati huu. Nakukaribisha kusikiliza sehemu ya 55 ya kipindi cha Akhlaqi Katika Uislamu nikiwa na matumaini kuwa, mimi pamoja na wewe tutanufaika na yale tutakayoyasikia katika kipindi hiki ambacho kwa leo kitazungumzia nukta nyingine muhimu za Akhlaqi za Jihadi za dini tukufu ya Uislamu. Endelea kuwa nami basi hadi tamati ya mazungumzo yetu.

Mpendwa msikilizaji, kulingana na vielezo vya kiakhlaqi na vya kufadhilisha suluhu na amani vilivyoko katika utamaduni wa Jihadi wa Uislamu, nukta nyingine muhimu sana inayozipambanua akhlaqi za Jihadi na vita za Uislamu na mifumo mingine ya kijeshi duniani ni dhana ya 'kushinda' na 'kushindwa' vitani. Katika mifumo ya tawala za kibeberu, lengo na maana ya ushindi ni kuzitawala nchi zingine, kutwaa maeneo zaidi ya ardhi, kuwa na sauti ya juu watu wa taifa na mbari fulani, kupora utajiri na maliasili na kukandamiza mavuguvugu ya kupigania uhuru na ukombozi, mambo ambayo katika mfumo wa Jihadi wa Uislamu, sio tu hayana nafasi yoyote, lakini pia yako mbali kabisa na malengo ya Uislamu wa asili yanayomuenzi mwanadamu na kumuonyesha mwongozo sahihi. Kutokana na tofauti hiyo ya mtazamo, maafisa waandamizi wa kijeshi, makamanda na askari wanaoshiriki kwenye medani za mapigano za vita vya kibeberu, miongoni mwa malengo yao makuu huwa ni kunyakua ardhi, kujiongezea maeneo ya kijiografia na kuwa na nafasi na sauti ya juu watu wa taifa, asili na mbari fulani. Na ndio maana, kuwaridhisha watawala madikteta, kupatiwa hadhi na nafasi maalumu, kupandishwa vyeo na kutunukiwa tuzo na nishani ni katika mambo yenye umuhimu mkubwa sana kwao. Lakini katika utamaduni wa Jihadi wa Uislamu, vingi kati ya vielezo hivyo huwa havizingatiwi wala kupewa uzito mkubwa, kwani vikosi na wale wote wanaojitokeza katika medani za vita, hata wawe na nafasi na cheo chochote kile huwa wanaingia kwenye mapigano kwa ajili ya kupata radhi za Mwenyezi Mungu tu. Nao hujihisi wamepata ushindi ikiwa tu waliyofanya yatawawezesha kupata radhi za Mola wao.

Katika aya ya 88 ya Suratu-Tawba, Qur'ani tukufu inaeleza yafuatayo katika kuwazungumzia wapiganaji Waislamu ambao wanajitosa kwenye medani ya Jihadi kwa ikhlasi na kwa ajili ya kupata radhi za Mwenyezi Mungu: "Lakini Mtume na wale walio amini pamoja naye waliwania Jihadi kwa mali zao na nafsi zao. Hao ndio watakao pata kheri nyingi, na hao ndio wenye kufanikiwa".

Kisha katika aya inayofuatia ya 89, Mwenyezi Mungu Aliyetukuka anatuonyesha jinsi amali za Jihadi za watu, zinavyodumu milele kwa sababu ya kufanywa kwa ikhlasi na kwa ajili yake Yeye, aliposema: "Mwenyezi Mungu amewatengenezea Bustani zipitazo mito kati yake, wadumu humo. Huko ndiko kufuzu kukubwa".

Japokuwa mazingira maalumu, ya kipekee na ya milele ya Peponi yana mvuto kwa kila mtu na yanampa utulivu na raha zisizo na kifani, lakini kwa Mujahidina wanaotoa mhanga roho zao katika njia ya Mwenyezi Mungu, kupata radhi zake Yeye Mola ndilo tamanio lao kubwa zaidi kuliko vivutio vyote vya Peponi vinavyotamaniwa na kila mtu. Sehemu ya aya ya 72 ya Suratu-Tawba inalizungumzia hilo kwa kusema: "…na Radhi za Mwenyezi Mungu ndio kubwa kuliko yote. Huko ndiko kufuzu kukubwa". 

Kuwepo mtazamo wa aina hii wa Jihadi katika utamaduni wa Uislamu, ndiko kunakoipa Jihadi muelekeo wa kiimani na kiitikadi; na katika hali hiyo mipaka yote bandia huporomoka na hausalii mpaka mwingine wowote isipokuwa wa itikadi. Na ndio maana mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Imam Khomeini (MA) alikuwa akisema: "Vita vyetu sisi ni vita vya itikadi; na vita vya itikadi huwa havitambui mipaka ya kijiografia". Kwa hiyo dhati ya Jihadi na lengo la Uislamu katika falsafa ya Jihadi ni kuzingatia zaidi ushindi wa fikra kuliko kitu kingine. Na hii ndio siri ya kuzidi kuenea Uislamu kila uchao huko Marekani, Ulaya, Asia, Afrika na katika nchi na pembe zingine za dunia.

Ukweli huu usioweza kukanushika ndio unaoutia wahka na kiwewe Uistikbari na Ubeberu wa dunia na kuufanya udhani kwamba, kwa kuwasha moto wa vita, kuchochea mipasuko na mifarakano, kuandaa mikusanyiko ya kuchoma moto nakala za Qur'ani tukufu na kuchora vikatuni vya kuitovukia adabu na kuivunjia heshima shakhsia tukufu na teule ya Bwana Mtume Muhammad SAW, utaweza kuzuia ushawishi wa fikra safi na sahihi za Uislamu zinazowataalamisha walimwengu na kuziangazia nyoyo zao kwa mwanga wa nuru ya haki. Kwani hata kabla ya hapo pia na kwa muda karne kadhaa, wataalamu wa masuala ya ulimwengu wa Mashariki, yaani Maorientalisti wenye kasumba za Magharibi pamoja na viongozi wa Kanisa, nao pia walijaribu kutumia hila mbalimbali za kutaka kuonyesha kuwa "Uislamu ni dini iliyosimama kwa upanga" ili tu kuzitia doa fikra safi za dini hiyo tukufu, lakini bila kutambua kwamba hatua zao hizo za kutapatapa hazitaweza kuathiri wala kufika popote. Na sababu ni kuwa, Mwenyezi Mungu mwenyewe ameshakata na kukadiria kwa irada yake kwamba hatimaye Uislamu utashinda tu; dini ambayo ujumbe wake umesimama juu ya misingi ya mantiki na fikra zinazomkomboa mwanadamu kwa kumtaalamisha na kumtoa kwenye giza la ujinga na ujahili. Aya ya nane ya Suratu-Saf inabainisha ukweli huo kwa kusema: "Wanataka kuizima nuru ya Mwenyezi Mungu kwa vinywa vyao. Na Mwenyezi Mungu atakamilisha nuru yake ijapo kuwa makafiri watachukia". 

Inafaa ifahamike pia kwamba, Mwenyezi Mungu Muumba wa ulimwengu alishatoa dhamana na hakikisho la Uislamu kuzishinda dini zingine zote, tokea siku ulipodhihiri Uislamu na kutangazwa risala na ujumbe wa ulimwengu mzima aliokuja nao Mtume wake Muhammad SAW pale aliposema katika aya ya tisa ya sura hiyohiyo ya As-Saf: "Yeye ndiye aliye mtuma Mtume wake kwa uwongofu na Dini ya haki ili ipate kuzishinda dini zote, ijapo kuwa washirikina watachukia".

Kama tulivyotangulia kueleza, hakuna sehemu yoyote ya misingi ya Uislamu na ya mfumo wake wa kijeshi ulipozungumziwa ushindi kwa maana ya kuyashinda mataifa au watu wa mbari fulani, bali lengo kuu na la msingi ni ushindi wa fikra ya Uislamu dhidi ya fikra na itikadi zingine, ushindi wa haki dhidi ya batili, ushindi wa elimu na maarifa dhidi ya ujinga na ujahili na hatimaye ushindi wa Uislamu dhidi ya watawala na mifumo ya shirki, ukafiri na ubeberu, kutawala mataifa ya wanyonge na wanaodhulumiwa na kuporomoshwa tawala za kiistikbari katika ulimwengu wa wanadamu. Kwa kujengeka na mtazamo huu, msamiati wa "kushindwa" hauwezi kupatikana popote pale ndani ya kamusi la wanaopigana Jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu. Sababu ni kwamba, wao huwa na moja ya hali mbili tu; ima kuishinda kambi ya wanaoipiga vita dini, au kuuawa shahidi katika njia hiyo yenye malengo ya kiutu na ya kutafuta radhi za Mwenyezi Mungu; hali tukufu ambayo humfikisha Mujahidina kwenye daraja ya juu kabisa ya izza, utukufu, saada na fanaka. Katika sehemu ya kwanza ya aya ya 52 ya Suratu-Tawba, Mwenyezi Mungu Mtukufu anamtaka Mtume wake awaeleze hilo makafiri na washirikina kwa kuwauliza: "Sema: Hivyo mnatutazamia litupate lolote isipo kuwa moja katika mema mawili (ya ushindi au ya kuuawa shahidi)?" Mpendwa msikilizaji, tukiwa na matumaini ya kushuhudia mustakabali ung'arao wa Uislamu, niseme pia kwamba sehemu ya 55 ya kipindi cha Akhlaqi Katika Uislamu imefikia tamati. Hivyo sina budi kukuaga hadi wakati mwingine inshallah, tutakapokutana tena katika sehemu ya 56 na ya mwisho ya kipindi hiki. Namuomba Mola wa haki akubariki; na amani, rehma na baraka zake ziendelee kuwa juu yako…/

 

 

 

Tags