Milipuko mikubwa yasikika Tehran na maeneo mengine ya Iran
Milipuko mikubwa ilisikika mapema asubuhi ya Ijumaa katika maeneo kadhaa ya mji mkuu wa Iran, Tehran, na pia katika mikoa mingine nchini.
Ripoti za vyombo vya habari zimenukuu jeshi la Israel likisema kuwa limetekeleza mashambulizi ya anga katika maeneo mbalimbali ya Iran.
Kwa mujibu wa Press TV ya Iran miongoni mwa waliouawa ni wanawake na watoto.
Aidha kwa mujibu wa ripoti ya shirika la habari la Fars, karibu saa tisa alfajiri kwa saa za Tehran, milipuko mikubwa ilisikika kutoka maeneo mbalimbali ya Tehran.
Benjamin Netanyahu, waziri mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel, katika taarifa rasmi, alitangaza kuwa Israel imeanzisha operesheni ya kijeshi yenye malengo maalum dhidi ya Iran.
Katika mashambulizi hayo, Meja Jenerali Salami, Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC), na Meja Jenerali Rashid, kamanda wa Kituo cha Khatam al-Anbiya cha IRGC, wamethibitishwa kuuawa shahidi.
Aidha, Muhammad Mahdi Tehranchi, mwanasayansi wa nyuklia na rais wa Chuo Kikuu Huria cha Kiislamu cha Iran (Islamic Azad University), pia ameripotiwa kuuawa shahidi.
Katika jiji la Tehran, majengo kadhaa, yakiwemo yale ya Narmak, mtaa wa Shahid Mahallati, mtaa wa Shahid Chamran, na maeneo ya Chitgar, yamelengwa na mashambulizi hayo.
Wakati huo huo, taarifa zimepokewa kuhusu mashambulizi mengine katika maeneo mbalimbali ya nchi kama vile Hamadan na Natanz. Hadi sasa, hakuna taarifa rasmi au thabiti kuhusu kiwango cha uharibifu au idadi ya waathirika.
Waziri wa vita wa Israel, Israel Katz amesema kuwa kufuatia “shambulio hilo la Israel dhidi ya Iran”, hali ya tahadhari ya kiusalama imetangazwa katika maeneo yote 'Israel'.
Katz alionya kuwa kuna matarajio kuwa Iran itajibu mashambulizi hayo kwa kutumia makombora na ndege zisizo na rubani (drones) dhidi ya Israel katika siku zijazo.