Jenerali Ali Fadavi: Iran itaifanya Israel kujutia mashambulizi yake
Naibu Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC), Brigedia Jenerali Ali Fadavi, amesema kuwa Iran iko tayari kulipiza kisasi kikubwa dhidi ya Israel kufuatia mashambulizi ya hivi karibuni dhidi ya ardhi ya Iran, akisisitiza kuwa hatua hiyo itaiumiza na kuiaibisha Israel na washirika wake.
Amesema: “IRGC, kupitia matawi na nyanja zake zote, ikiwa sambamba na muungano wa Muqawama, iko katika hali ya utayari wa juu kutekeleza operesheni ya maamuzi ambayo itasababisha majuto makubwa kwa utawala wa Kizayuni unaoua watoto na waungaji mkono wake wa Marekani, pindi tu agizo rasmi litakapotolewa."
Akiendelea kufafanua, amesema: “IRGC haijapoteza hata saa 24 bila kutekeleza jukumu lake la kuongeza uwezo na utayari wake. Siku kama ya leo ni ushahidi kwamba tuko tayari kutekeleza operesheni inayofaa, kwa wakati unaofaa, mara tu amri itakapotolewa.”
Fadavi amesisitiza kuwa: “Majukumu tuliyopewa tunayatekeleza kikamilifu ndani ya IRGC kote nchini. Kila kitu kinafanyika kwa mpangilio na umakini. Uwezo wote tulionao, kijeshi, kiusalama na kimkakati, —uko tayari kwa ajili ya hatua itakayowafanya maadui zetu wajutie vitendo vyao.”