Spika wa Bunge la Iran: Tutamaliza kazi ambayo Israel imeanzisha
(last modified Fri, 13 Jun 2025 12:24:59 GMT )
Jun 13, 2025 12:24 UTC
  • Spika wa Bunge la Iran: Tutamaliza kazi ambayo Israel imeanzisha

Mohammad Baqer Qalibaf Spika wa Bunge la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amelaani uchokozi wa Israel dhidi ya Iran na akatangaza kwamba sasa ni wakati kulipiza kisasi, na kisasi hiki kitatekelezwa.

Spika Qalibaf ametangaza katika taarifa yake kwamba: "Mkono muovu wa genge la jinai na kigaidi la Kizayuni kwa mara nyingine tena umetiwa doa la damu za makamanda na Mujahidina wa Iran, wapendwa kuliko maisha yetu."

Taarifa hiyo imeongeza kuwa: "Kwa kushambulia makazi ya raia, utawala dhalimu wa Kizayuni umeonyesha kuwa ni adui mkubwa wa ubinadamu na adui mbaya zaidi wa taifa la Iran, lakini jibu chungu la mashujaa wa Uislamu na adhabu kali na ya kusikitisha inawangoja wao na waungaji mkono wao.

Spika wa Bunge la Iran amesisitiza kuwa, huu sasa ni wakati wa kulipiza kisasi, na kisasi hiki kitatekelezwa kwa njia mbinu na kwa njia yoyote. Hatutawaacha na tutapiga pigo kali kwenye shingo zao. Walianzisha wao hili, lakini sisi ndio tutakaomaliza.

Mashambulizi ya Israel yalilenga majengo kadhaa ya makazi katika mji mkuu wa Iran, Tehran, pamoja na maeneo kadhaa katika mji wa Tabriz kaskazini-magharibi mwa nchi, na pia katika miji ya Khorramabad, Kermanshah, Boroujerd magharibi mwa Iran, pamoja na Natanz, katikati mwa nchi.

Huduma za safari za ndege zimesitishwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Imam Khomeini mjini Tehran na viwanja vingine vya ndege nchini.

Shambulizi hilo limetokea siku moja baada ya kupitishwa kwa azimio jipya la Bodi ya Magavana ya Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki (IAEA) dhidi ya Iran.