IRGC: Tutatoa jibu zito kufuatia mashambulizi ya Israel dhidi ya Iran
Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, IRGC, limelaani vikali shambulizi la kijeshi lililofanywa na Israel dhidi ya ardhi ya Iran, ambalo limepelekea kuuawa kwa Kamanda Mkuu wake, Meja Jenerali Hossein Salami.
Kupitia salamu za rambirambi zilizotolewa Ijumaa, IRGC imeto pole zake kwa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, familia za waathiriwa pamoja na wananchi na serikali ya Iran kufuatia kuuawa kwa shahidi Salami.
IRGC imemsifu marehemu kamanda wake mkuu kama mmoja wa makamanda mahiri wa chombo hicho katika nyanja za kielimu, kitamaduni, kiusalama na kijeshi, ambaye alisimama kidete na kwa hekima kutetea malengo ya Mapinduzi ya Kiislamu ya mwaka 1979 na taifa la Iran.
Taarifa ya IRGC imesema: "Tuna uhakika kuwa wananchi wa Iran, taifa tukufu lenye misimamo ya kimapinduzi, watabaki salama na kwa amani licha ya jinai hii ya kinyama."
IRGC imebainisha kuwa tayari kulikuwa na mikakati na hatua zilizowekwa kukabiliana na matukio ya aina hii, ikiongeza kuwa maelezo kamili kuhusu hujuma hiyo ya kijinai na hatua kali zitakazochukuliwa zitabainishwa mbele ya taifa la Iran.
Kamanda huyo wa IRGC ameuawa shahidi katika shambulizi la alfajiri ya leo Ijumaa, Juni 13, lililofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel.
Mashambulizi ya Israel yalilenga majengo kadhaa ya makazi katika mji mkuu wa Iran, Tehran, pamoja na maeneo kadhaa katika mji wa Tabriz kaskazini-magharibi mwa nchi, na pia katika miji ya Khorramabad, Kermanshah, Boroujerd magharibi mwa Iran, pamoja na Natanz, katikati mwa nchi.
Huduma za safari za ndege zimesitishwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Imam Khomeini mjini Tehran na viwanja vingine vya ndege nchini.
Shambulizi hilo limetokea siku moja baada ya kupitishwa kwa azimio jipya la Bodi ya Magavana ya Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki (IAEA) dhidi ya Iran.
Aidha, limefanyika siku mbili kabla ya kuanza kwa duru nyingine ya mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja kati ya Iran na Marekani yanayotarajiwa kufanyika mjini Muscat, Oman, tarehe 15 Juni.
Tehran na Washington zimekuwa zikifanya duru tano za mazungumzo tangu Aprili 12, zikihusisha upatanishi wa Oman, kwa lengo la kufikia makubaliano kuhusu mpango wa nyuklia wa kiraia wa Iran na kuondolewa vikwazo dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu.