Apr 11, 2023 07:14 UTC
  • Akhlaqi Katika Uislamu (56)

Amani ya Allah, rehma na baraka zake ziwe juu yako mpendwa msikilizaji popote pale ulipo wakati huu. Nakukaribisha kusikiliza sehemu ya 56 na ya mwisho ya kipindi cha Akhlaqi Katika Uislamu nikiwa na matumaini kuwa, mimi pamoja na wewe tutanufaika na yale tutakayoyasikia katika kipindi chetu cha leo ambacho kitakamilisha mifululizo yetu kwa kuzungumzia maudhui muhimu sana ya Jihadi ya Nafsi. Endelea kuwa nami basi hadi tamati ya mazungumzo yetu.

Kwa auni na taufiki ya Mwenyezi Mungu mpendwa msikilizaji tumeweza katika sehemu 55 za kipindi hiki kukuletea mifululizo ya uchambuzi na maelezo kuhusu utamaduni wa akhlaqi za Kiislamu katika pande zote, kuanzia mtu binafsi, za kijamii, kifamilia, kiutamaduni, kiuchumi, kisiasa na kijihadi, tukiwa na matumaini kuwa yote tuliyozungumzia yamekuwa na manufaa kwako. Katika mfululizo huu wa 56 na wa mwisho, na kama nilivyotangulia kueleza, tutatupia jicho maudhui muhimu sana na yenye uzito wa kipekee ya "Jihadi ya Nafsi". Ili kuelewa umuhimu wa aina yake wa Jihadi ya Nafsi itoshe tu kusema kwamba, ikiwa mtu atashindwa na kufeli katika jihadi hii, basi hapana shaka, hatoweza kufanikiwa kwa namna yoyote ile katika nyuga zingine za akhlaqi tulizozungumzia. Kwa maneno mengine, Jihadi ya Nafsi ni kiandalio cha mazingira na mwega mkubwa zaidi wa utoaji msukumo, ambao huweza kumsaidia mtu kuvikwea vidaraja na kufikia kwenye kilele cha saada, utukukaji na ukamilikaji wa kiutu katika nyuga za kiakhlaqi; na kuviondoa vizingiti na vizuizi vyote vinavyomkwamisha kufikia lengo hilo. Hii ni kwa sababu, chanzo na chimbuko la hulka zote chafu kama ubinafsi, ghururi, kiburi, ufuska, kutojidhibiti kufanya lolote lile, uchu wa madaraka, utumwa wa hawaa na matamanio ya nafsi na kwa ufupi yote yanayopingana na maadili mema, ni mtu kufuata matashi na matamanio ya nafsi yake. Ni kama alivyonena Maulavi, malenga mbobezi na mwanafikra mtajika wa Kiirani katika ubeti wa moja ya mashairi yake ya kwamba "mama wa masanamu yote, ni sanamu-nafsi la wewe mwenyewe". Katika sehemu inayofuatia ya shairi hilo, Maulavi anasema, kuyavunja masanamu ya mawe na ya vitu visivyo na uhai si kazi ngumu, lakini kupambana na sanamu-nafsi lililojijengea pango ndani kabisa ya nafsi ya mtu ni kazi ngumu sana na yenye uzito mkubwa mno, kiasi kwamba kulivunja sanamu hilo, kama ilivyoeleza Qur'ani ni jambo lisiloyumkinika bila ya kupata auni na msaada wa Mwenyezi Mungu, kama isemavyo aya ya 53 ya Suratu-Yusuf ya kwamba: …"Kwa hakika nafsi ndiyo iamrishayo mno uovu, isipo kuwa ile ambayo Mola wangu Mlezi ameirehemu".

Ili tuweze kubaini na kukielewa zaidi kitisho cha nafsi ya mwanadamu iamrishayo maovu tuisikilize kwa pamoja Hadithi ifuatayo kutoka kwa Imam Jaafar Sadiq AS. Mtukufu huyo amesema: Wakati Mtume SAW alipoliandaa na kulituma jeshi kwenda kwenye medani ya vita kupambana na adui, siku jeshi hilo la Waislamu liliporudi na ushindi kutoka vitani, haukupita muda Mtume wa Allah aliwaambia wapiganaji hao: "Heko kwa watu walioivuka Jihadi Ndogo na kujiandaa kwa Jihadi Kubwa". Wapiganaji wa jeshi la Uislamu wakauliza kwa mshangao: "Ewe Mjumbe wa Allah, ni nini madhumuni ya Jihadi hiyo iliyo kubwa zaidi?" Bwana Mtume akasema: "Ni Jihadi ya kupambana na nafsi". (Wasaailu-Shia' 11, uk. 122)

Kutokana na Hadithi hii inabainika wazi kuwa, japokuwa Jihadi ya mapigano ya silaha ya kupambana na adui ni nzito na ngumu mno, haihimiliki kirahisi na inasababisha madhara na hasara chungu nzima, lakini Jihadi ya Nafsi ni ngumu na nzito zaidi kuliko hiyo maradufu. Na ndiyo maana Bwana Mtume SAW amevitaja vita vya kijeshi kuwa ni Jihadul-As'ghar, yaani Jihadi Ndogo Zaidi na vita vya kupambana nafsi akaviita Jihadul-Akbar, yaani Jihadi Kubwa Kabisa. Na katika Hadithi nyingine, Nabii huyo wa rehma amesema: "Mtu shujaa na mwenye nguvu zaidi ni yule anayeishinda na kuidhibiti nafsi yake". (Hiyohiyo, uk. 123)

Kama inavyokuwa katika medani za mapigano ya kijeshi, ambako inahitajika azma imara na irada madhubuti na isiyoyumba ili kuweza kumshinda adui, kuyashinda matamanio ya nafsi inayoamrisha maovu, nako pia inapasa kuandamane na uamuzi na msimamo thabiti ili kuweza kusimama imara kuukabili wasiwasi na ushawishi wake wa mtawalia na kutoyumba wala kusalimu amri mbele yake. Kwa bahati mbaya, azma na irada hii inakosekana kwa watu wengi. Na ndio maana huwa rahisi kwa wao kuathiriwa na matamanio ya nafsi na wasiwasi wa shetani, wakaikengeuka njia iliyonyooka ya Allah na kuporomoka na hivyo kupoteza hadhi na daraja iliyotukuka ya utu waliyotunukiwa na Yeye Mola. Kuhusiana na hili, Mwenyezi Mungu anasema katika aya ya 115 ya Suratu-T'aha: "Na hapo zamani tuliagana na Adam, lakini alisahau, wala hatukuona kwake azma kubwa".

Tofauti nyingine iliyopo kati ya Jihadi Ndogo na Jihadi Kubwa ni kwamba kupambana na adui wa nje anayekabiliana ana kwa ana na mwanadamu kunaonekana waziwazi; na mapigano ya aina hiyo huwa yanaendelea kwa muda, uwe mfupi au mrefu na mwishowe hufikia kikomo. Lakini Jihadi ya Nafsi ni ya kupambana na adui wa ndani, katika hali zote za shida na raha za maisha na ambaye anaendelea kuwa tishio kwa mtu hadi lahadha ya mwisho ya maisha yake. Katika dua tunazomwomba Mwenyezi Mungu ni kusema: "Ewe Mola, ninajilinda kwako na nafsi isiyotosheka". Dua hii inabainisha kuwa, bila auni na msaada wake Yeye Mola, mwanadamu hawezi kujivua pingu nzito za nafsi, ambayo kila mara huwa inamuamrisha mabaya na maovu. Ni kama asemavyo tena Jalaluddin Maulavi katika moja ya mashairi yake: "Wewe uko pamoja na adui mkubwa wa nafsi uliyegandana naye, utapambana vipi ilhali huzijui mbinu za kubariziana naye?"

Katika medani ya mapambano hayo, wawezao kubariziana, ni wale waliozijenga na kuzitakasa nafsi zao, kwa kuyadhibiti matamanio ya nafsi na kuzivua nyoyo zao uchu wa kukumbatia mapambo ya dunia na vivutio vyake vinavyoghilibu na kuhadaa vya mali na utajiri, mamlaka na madaraka; na wakasamehe kila walichonacho kuanzia mali mpaka roho zao wakajitosa kwenye medani za Jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu.

Katika aya ya 40 na 41 za Suratu-Naziat, Qur'ani tukufu inabainisha nafasi na hadhi ya watu hao kwa kusema: "Na ama yule anaye ogopa kusimamishwa mbele ya Mola wake Mlezi, na akajizuilia nafsi yake na matamanio, Basi huyo, Pepo itakuwa ndiyo makaazi yake!"

Mpendwa msikilizaji tumuombe Mola Mwenyezi kwa pamoja atuwezeshe kushinda katika Jihadi Ndogo na Kubwa na kufikia daraja ya juu ya utukufu wa kimaanawi. Na kwa dua hiyo, niseme pia kuwa kipindi cha Akhlaqi katika Uislamu kimefikia tamati. Ni matarajio yangu kwamba umenufaika na yote tuliyozungumzia katika mifululizo 56 ya kipindi hiki. Kwa mara nyingine nimuombe tena Mola wa haki akubariki; na amani, rehma na baraka zake ziendelee kuwa juu yako…/