Hujuma ya kikatili ya Israel dhidi ya Iran yalaaniwa vikali Kimataifa
Jumuiya ya kimataifa imejitokeza kwa sauti moja kulaani vikali mashambulizi ya kijeshi yaliyofanywa na Israel dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, ikitaja kitendo hicho kuwa ni ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa na tisho kubwa kwa amani ya Mashariki ya Kati.
Saudi Arabia
Ufalme wa Saudi Arabia umezitaja hujuma hizo kama “mashambulizi ya kinyama dhidi ya taifa ndugu na la Kiislamu la Iran”, na kuitaka jamii ya kimataifa kuchukua hatua za haraka kukomesha jinai hiyo.
Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Saudi Arabia imesema: "Tunalaani kwa nguvu zote mashambulizi haya ambayo yanavunja mamlaka ya Iran na kuhatarisha usalama wake, kinyume kabisa na sheria na taratibu za kimataifa."
Riyadh imesisitiza kuwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linapaswa kubeba jukumu la kuzuia mzozo huo kupanuka.
Oman
Oman, ambayo imekuwa mpatanishi mkuu kati ya Iran na Marekani, pia imelaani mashambulizi hayo na kuulaumu moja kwa moja “utawala wa Kizayuni” kwa kuchochea mzozo huo.
Taarifa rasmi kutoka Muscat imeyataja mashambulizi hayo kuwa yanayoharibu fursa za kidiplomasia na kutishia kwa kiasi kikubwa uthabiti wa eneo.
Oman imeyataja mashambulizi hayo kama “kitendo haramu, cha kichochezi na kisicho na hekima”, ambacho kimelenga moja kwa moja miundombinu ya kiserikali ya Iran.
Pakistan
Wizara ya Mambo ya Nje ya Pakistan imebainisha “wasiwasi mkubwa” juu ya kile ilichokiita “uvunjaji wa wazi wa mamlaka na mipaka ya Iran.”
Taarifa hiyo imesema: "Pakistan inalaani vikali mashambulizi ya kijeshi ya Israel ndani ya ardhi ya Iran. Kitendo hiki kinakiuka wazi sheria za kimataifa na Katiba ya Umoja wa Mataifa." Taarifa hiyo ambayo imetolewa na Waziri Mkuu Msaidizi na Waziri wa Mambo ya Nje Ishaq Dar kupitia mtandao wa X imesema: “Tunalaani kwa nguvu zote mashambulizi haramu ya Israel dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Kitendo hiki kimetikisa msingi wa sheria ya kimataifa na dhamira ya ubinadamu.”
Hamas
Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina, Hamas, imesema Ijumaa kuwa mashambulizi hayo ni “taharuki hatari” inayoweza kuyumbisha eneo zima.
“Iran inalipia gharama ya msimamo wake wa wazi wa kuunga mkono Palestina na mapambano yake,” imesema taarifa ya Hamas.
Indonesia
Indonesia, kupitia Wizara yake ya Mambo ya Nje pamoja na ubalozi wake mjini Tehran, imesema inalaani vikali shambulizi la Israel na kulitaja kuwa “linalohatarisha amani ya kieneo na kukiuka sheria za kimataifa.”
Cuba
Rais Miguel Díaz-Canel wa Cuba, amelaani mashambulizi hayo akiyaita “uchochezi wa hali ya juu” ambao unaweza kuathiri kwa njia isiyotabirika usalama wa kikanda na wa kimataifa.
Venezuela
Caracas imetoa taarifa ikisema kuwa mashambulizi hayo yanaongeza ukurasa mwingine katika “rekodi nyeusi ya jinai za utawala wa Netanyahu”, na kuyataja kama kitendo cha uchokozi kisichokubaliana na dhamira ya amani ya jamii ya kimataifa.
Japan
Takeshi Iwaya, Waziri wa Mambo ya Nje wa Japan, amesema Tokyo “inalaani vikali mashambulizi ya angani ya Israel dhidi ya Iran.”
“Tunatoa wito kwa pande zote kujizuia na kupunguza mivutano. Amani ya Mashariki ya Kati ni muhimu mno kwa Japan.”
Umoja wa Mataifa
Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, amesema:
“Katibu Mkuu analaani hatua yoyote ya kijeshi ya kuchochea mzozo Mashariki ya Kati, hasa mashambulizi ya Israel dhidi ya maeneo ya nyuklia ya Iran wakati mazungumzo muhimu ya kidiplomasia yanaendelea.”
India
Wizara ya Mambo ya Nje ya India imesema inafuatilia kwa karibu hali inavyoendelea:
“India ina wasiwasi mkubwa kuhusu mzozo unaoendelea kati ya Iran na Israel, na inahimiza matumizi ya njia za kidiplomasia kupunguza mvutano na kushughulikia vyanzo vya mgogoro.”