Mar 02, 2023 02:20 UTC
  • Akhamisi, tarehe Pili Machi, mwaka 2023

Leo ni Alkhamisi tarehe 9 Shaaban 1444 Hijri inasadifiana na tarehe Pili Machi mwaka 2023.

Siku kama ya leo miaka 963 iliyopita aliaga dunia Ibn Barraj mmoja wa mafaqihi na maulamaa mashuhuri wa Misri.

Ibn Barraj alifahamika sana kwa jina la Trablosi kutokana na kuwa kwa muda fulani alikuwa na cheo cha kadhi katika mji wa Trablos yaani Tripoli huko kaskazini mwa Lebanon ya sasa.

Msomi huyo wa Kiislamu alifunzwa na maulamaa kama vile Sayyid Murtadha na Sheikh Tusi. Ibn Barraj ni msomi mtajika wa Kiislamu ambaye fikra na mitazamo yake ilikuwa ikiheshimiwa na mafaqihi wakubwa wa zama hizo.

Katika siku kama ya leo miaka 867 iliyopita inayosadifiana na tarehe 9 Shaaban mwaka 577 aliaga dunia Abul Barakat Abdul Rahman bin Muhammad mashuhuri kwa lakabu ya Ibn Anbari fakihi na mtaalamu wa lugha wa mjini Baghdad.

Alihitimu masomo yake katika skuli mashuhuri ya Nidhamiya mjini Baghdad na kutokana na kufaulu vizuri masomo yake na maarifa mengi aliyokuwa nayo, alianza kufundisha katika skuli hiyo.

Ibn Anbari ameandika vitabu na makala nyingi za kielimu. Kitabu cha al-Asrar al-Arabiyah ni moja ya athari mashuhuri ya alimu huyo.

Siku kama ya leo miaka 127 iliyopita sawa na tarehe Pili Machi mwaka 1896 mwanafikizia wa Kifaransa Henri Becquerel alivumbua nururishi au Radioactivity baada ya kufanya utafiti katika mada za urani na vitu vinginevyo.

Becquerel alikuwa akichunguza urani ndipo alipogundua nururishi. Utafiti wa mwanafikizia huyo wa Kifaransa ulimfanya atunukiwe tuzo ya Nobel mwaka 1903 na miaka mitano baadae aliaga dunia.

Henri Becquerel

Miaka 67 iliyopita katika siku kama hii, nchi ya Morocco ilipata uhuru. Morocco iko kaskazini mwa Afrika katika Ukingo wa Bahari ya Mediterrania na Bahari ya Antlantic na inapakana na Algeria na Sahara Magharibi.

Morocco ilikombolewa na Waislamu mwishoni mwa karne ya Saba Miladia na silsila kadhaa za kifalme zilitawala nchini humo.

Mapambano ya wananchi Waislamu wa Morocco dhidi ya wakoloni wa Uhispania na Ufaransa yalipelekea nchi hiyo kupata uhuru mwaka 1956.

Siku kama ya leo miaka 19 iliyopita, mwafaka na tarehe Pili Machi mwaka 2004, mamia ya watu wasio na hatia waliuawa shahidi na wengine kujeruhiwa katika miripuko kadhaa mikubwa iliyotokea katika shughuli ya kukumbuka kuuawa shahidi Imam Hussein (AS) huko katika miji mitukufu ya Karbala na Kadhimein nchini Iraq.

Katika mwaka huo wananchi Waislamu wa Iraq walifanya maadhimisho hayo kwa hamasa kubwa baada ya utawala wa Saddam Hussein, dikteta wa zamani wa nchi hiyo aliyeng'olewa madarakani, kupiga marufuku kwa miaka kadhaa shughuli zote za aina hiyo.

Miripuko hiyo ya kigaidi ya Karbala na Khadhimein ilitokea ikiwa ni muendelezo wa machafuko yaliyoikumba Iraq tangu nchi hiyo ivamiwe kijeshi na kukaliwa kwa mabavu na Marekani na Uingereza mwaka 2003. 

Karbala

 

Tags