Alkhamisi, tarehe 23 Machi, 2023
Leo ni Alkhamisi tarehe Mosi Ramadhani 1444 Hijria sawa na 23 Machi 2023.
Leo ni siku ya kwanza ya mwezi mtukufu wa Ramadhani kwa mujibu wa kalenda ya Hijria Qamaria; mwezi ambao ndani yake iliteremshwa Qur'ani Tukufu. Ni mwezi wa rehma na baraka tele. Katika kubainisha utukufu wa mwezi huu, Mtume Muhammad SAW amesema, siku za mwezi wa Ramadhani ndizo siku bora zaidi kuliko siku nyingine zote na kuwataka Waislamu wachume na kufaidika kutokana na fadhila na baraka za mwezi huu. Allah SWT anasema: "Hakika tumeiteremsha (Qur'ani) katika usiku wa heshima. Na nini kitakujulisha usiku huo wa heshima ni nini? Laylatul Qadr (usiku huo wa heshima) ni bora kuliko miezi elfu." Tukio la kuhuzinisha moyo la kuuawa shahidi Imam Ali bin Abi Twalib AS na vilevile kuzaliwa mjukuu wa Mtume Muhammad SAW, Imam Hassan AS, ni katika matukio muhimu yaliyotimia katika mwezi huu. Tunamuomba Allah SW atupe baraka za mwezi huu na kutujaalia kuwa miongoni mwa wale wanaofadika na baraka zake.
Katika siku ya kwanza ya mwezi mtukufu wa Ramadhani, kiliteremshwa kitabu cha Suhuf cha Nabii Ibrahim AS. Jina Ibrahim limetajwa mara 69 katika Qur'ani Tukufu kwa heshima na taadhima ambapo maisha yake yameashiriwa kwa njia mbalimbali kama ibra na ruwaza njema kwa waumini. Mwenyezi Mungu amemtaja kuwa ni mtu mwenye kumuabudu Mungu Mmoja. Alikuwa Nabii mkweli kama tunavyosoma katika Suratu Maryam Aya ya 41. Mwenyezi Mungu alimpa yeye na familia yake neema na mamlaka na utawala mkubwa kama tunavyosoma katika Suratun Nisaa Aya ya 54. Kuna vitabu kadhaa vya mbinguni ambavyo waliteremshiwa Mitume kama vile Suhuf cha Ibrahim AS na Nuh AS, Taurati ya Musa AS na Injili ya Isa AS, na kitabu kilicho kamilika kati ya vyote hivyo ni Qur'ani Tukufu.
Siku kama ya leo miaka 1016 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria, alifariki dunia Ibn Sina maarufu kwa jina la Sheikhur Rais, tabibu, mtaalamu wa hisabati, falsafa na mnajimu mkubwa wa Kiirani. Ibn Sina alifariki dunia katika mji wa Hamadan ulioko magharibi mwa Iran akiwa na umri wa miaka 58. Alihifadhi Qur'ani Tukufu akiwa kijana na akapata kusoma elimu za mantiki, uhandisi na utaalamu wa nyota. Baada ya kumtibu Nuh bin Mansur, mmoja wa wafalme wa Kisamani akiwa kijana, Ibn Sina alipata idhini ya kutumia maktaba kubwa ya mfalme huyo. Katika maktaba hiyo, Ibn Sina alipata kusoma vitabu vingi vya elimu tofauti. Abu Ali Sina alitokea kuwa msomi, mwandishi na mtafiti mashuhuri. Miongoni mwa athari muhimu za msomi huyu mkubwa ni pamoja na kitabu cha "Shifaa" kinachohusu elimu ya falsafa, "Qanun" kinachohusu tiba na "Daneshnameh Allai".
Katika siku kama ya leo miaka 712 iliyopita, alizaliwa Ibn Khaldun, mtaalamu wa masuala ya kijamii, mwanasiasa na mwanahistoria Mwislamu. Ibn Khaldun alizaliwa huko Tunisia. Maisha ya Ibn Khaldun yanaweza kugawanywa katika sehemu tatu na sehemu ya kwanza aliitumia katika kusoma elimu tofauti. Alitumia sehemu ya pili ya maisha yake katika siasa na kuhudumia nyadhifa tofauti za utendaji na alifungwa jela kutokana na njama za maadui zake. Baada ya kuachiliwa huru Ibn Khaldun alijitenga na siasa. Hapo ndipo ilipoanza duru ya tatu ya maisha yake ambapo alijishughulisha na utafiti na uandishi. Alimu na msomi huyo alifariki dunia mwaka 808 Hijiria.
Siku kama ya leo miaka 371 iliyopita, yaani sawa tarehe 23 Machi mwaka 1652, yalianza shambulizi la manowari za kijeshi za Uingereza dhidi ya majeshi ya Uholanzi. Amri ya shambulizi hilo ilitolewa na Oliver Cromwell aliyekuwa dikteta wa wakati huo wa Uingereza. Akipata uungaji mkono wa Bunge la Uingereza, Cromwell alimpindua mfalme wa Uingereza na kisha kulivunja bunge la nchi hiyo. Inasemekana kuwa, lengo la kutekeleza shambulio hilo lilikuwa ni kulimaliza nguvu jeshi la Uholanzi ambalo lilikuwa na nguvu kubwa ya majini.
Siku kama ya leo miaka 104 iliyopita, ilianzishwa harakati ya Ufashisti nchini Italia kwa uongozi wa Benito Mussolini. Ufashisti kwa ujumla ni utawala wa kidikteta wenye kufuata aidolojia ya kibaguzi na kiutaifa, kuwakandamiza wapinzani, kukandamiza uhuru na kuzipotosha itikadi na fikra za wananchi. Hayo yalijiri baada ya Mussolini kunyakuwa wadhifa wa uwaziri mkuu nchini Italia mwaka 1922 na kuanza utawala wa kidikteta nchini humo. Muda mfupi baadaye Mussolini alishirikiana na Adolph Hitler, na kuandaa mazingira ya kuanzishwa Vita vya Pili vya Dunia.
Siku kama ya leo miaka 73 iliyopita, liliasisiwa Shirika la Hali ya Hewa Duniani 'WMO'. Shirika hilo linafungamana na Umoja wa Mataifa na taasisi zote za hali ya hewa ulimwenguni hushirikiana na shirika hilo. Miongoni mwa malengo ya kuanzishwa shirika hilo ni kutoa msaada wa elimu ya hali ya hewa kwa wataalamu wa anga, mabaharia, wakulima na shughuli nyingine za kibinadamu. Ni kwa ajili hiyo ndio maana siku ya leo yaani tarehe 23 Machi ikajulikana kuwa Siku ya Hali ya Hewa Duniani.
Na siku kama ya leo miaka 18 iliyopita, sawa na tarehe 3 Farvardin 1384 Hijria Shamsia, alifariki dunia Allamah Sayyid Jalaluddin Ashtiyani, mwanafalsafa na mwanafikra wa Kiislamu baada ya kuugua kwa muda mrefu. Allamah Ashtiyani alizaliwa Ashtiyan katikati mwa Iran na kupata elimu ya msingi katika eneo hilo. Baadaye alielekea katika mji wa Qum na kupata elimu kwa wanachuoni wakubwa kama vile Imam Ruhullah Khomeini, Ayatullahil Udhma Burujerdi na Allamah Tabatabai. Baadaye alielekea katika mji mtakatifu wa Mash'had na kujishughulisha na kulea wanafunzi hadi mwisho wa uhai wake.