Mar 31, 2023 02:08 UTC
  • Ijumaa, tarehe 31 Machi, 2023

Leo ni Ijumaa tarehe 9 Ramadhani 1444 Hijria sawa na Machi 31 mwaka 2023.

Miaka 427 iliyopita katika siku kama ya leo yaani tarehe 31 Machi mwaka 1596, alizaliwa Rene Descartes mwanafalsafa, mwanahisabati na mwanafizikia wa Kifaransa. Descartes alifikia daraja ya uhadhiri wa chuo kikuu baada ya kuhitimu masomo ya falsafa na hisabati. Msomi huyo wa Kifaransa alifanya safari kwa kipindi fulani katika nchi mbalimbali na baadaye aliishi Uholanzi na kuanza kufanya utafiti. Rene Descartes aliitambua hisabati kuwa ni elimu kamili miongoni mwa elimu nyinginezo na kutaka kutumiwa elimu hiyo katika taaluma nyinginezo. Miongoni mwa vitabu vya mwanafalsafa huyo ni Principles Of Philosophy, The Passions of the Soul na Discourse on the Method.

Rene Descartes

Siku kama ya leo miaka 119 iliyopita, alifariki dunia Ayatullah Sheikh Muhammad Bahari Hamadani. Ayatullah Bahari Hamadani alikuwa mmoja wa maulama wakubwa na mtaalamu mashuhuri wa elimu ya Irfan wa karne ya 13 na 14 Hijiria wa nchini Iran. Baada ya kuhitimu masomo yake ya awali, Ayatullah Sheikh Muhammad Bahari Hamadani alielekea Najaf, Iraq na baada ya kukamilisha masomo yake alijishughulisha na kazi ya ufundishaji. Miongoni mwa athari zake ni pamoja na kitabu kinachoitwa 'Tadhkiratul-Muttaqiina.'

Ayatullah Sheikh Muhammad Bahari Hamadani

Siku kama ya leo miaka 75 iliyopita, garimoshi lililokuwa likitoka Cairo, Misri likielekea katika bandari ya Haifa huko Palestina lililipuriwa kwa bomu, ikiwa ni katika mwendelezo wa mauaji ya umati yaliyokuwa yakifanywa na Wazayuni maghasibu dhidi ya Wapalestina. Wapalestina 40 waliuawa na wengine 60 kujeruhiwa katika jinai hiyo iliyofanywa na kundi moja la Kizayuni. Siku nne kabla ya mlipuko huo, garimoshi jingine lililipuliwa huko Palestina na Wazayuni waliokuwa na silaha na kuuwa Wapalestina 24. Wapalestina wengine 61 walijeruhiwa.

Haifa

Na siku kama ya leo miaka 44 iliyopita, nchi wanachama wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu zilisimamisha uanachama wa Misri katika jumuiya hiyo na nchi nyingi wanachama zikakata uhusiano wao na Cairo. Nchi za Kiarabu zilichukua msimamo huo mkali baada ya rais wa zamani wa Misri, Anwar Sadat, kusaini hati ya mapatano ya Camp David na utawala wa Kizayuni wa Israel mwezi Januari mwaka 1978.

Anwar Sadat