Apr 11, 2023 06:57 UTC
  • Akhlaqi Katika Uislamu (52)

Amani ya Allah, rehma na baraka zake ziwe juu yako mpendwa msikilizaji popote pale ulipo wakati huu. Nakukaribisha kusikiliza sehemu ya 52 ya kipindi cha Akhlaqi Katika Uislamu nikiwa na matumaini kuwa, mimi pamoja na wewe tutanufaika na yale tutakayoyasikia katika kipindi hiki ambacho kwa leo kitaendelea kuzungumzia Akhlaqi za Jihadi katika Uislamu. Endelea kuwa nami basi hadi tamati ya mazungumzo yetu.

Kama nilivyotangulia kueleza mpendwa msikilizaji, mfululizo wetu wa leo, utaendeleza maudhui ya Akhlaqi za Jihadi katika utamaduni wa Uislamu wa asili uliolinganiwa na kufunzwa na Bwana Mtume Muhammad SAW.

Moja ya sifa maalumu na za kipekee inayoufanya utamaduni wa Jihadi wa Uislamu uwe na nafasi ya juu kulinganisha na harakati za kivita na kijeshi za mfumo wa ubepari unaotawala duniani, ni nia na ikhlasi anayokuwa nayo muumini anayekwenda kwenye medani za Jihadi ya kufanya hivyo kwa ajili ya kutafuta radhi za Mwenyezi Mungu tu. Kwa msingi huo, vita vinavyopiganwa katika Uislamu vinajibari na kujiweka mbali kabisa na nia na malengo yanayochochewa na taasubi, chuki na ukereketwa wa kiutaifa, kijiografia, rangi au asili za watu. Sababu ni kuwa, lengo hasa la Uislamu ni kuwaelekeza watu kwenye uongofu na kuwakomboa na unyongeshaji wa watawala madikteta na mataghuti na tawala za kidhalimu, ambazo dhulma na uonevu wao haviwezi tena kustahamilika.

Kutokana na kuwa na mtazamo huu, kabla wanajihadi wote wa kambi ya haki kuingia kwenye medani ya mapambano ya haki dhidi ya batili, huwa wanawekeana ahadi na Mola wao kwamba hawatapigana vita hivyo kwa nia au lengo jengine lolote lile ghairi ya kutetea njia ya Mwenyezi Mungu ya Uislamu. Na hilo linabainishwa kwa uwazi kabisa na aya ya 111 ya Suratul-Tawba inayosema: " Hakika Mwenyezi Mungu amenunua kwa Waumini nafsi zao na mali zao kwa kuwa wao watapata Pepo. Wanapigana katika Njia ya Mwenyezi Mungu - wanauwa na wanauwawa. Hii ni ahadi aliyo jilazimisha kwa Haki katika Taurati na Injili na Qur'ani. Na nani atimizae ahadi kuliko Mwenyezi Mungu? Basi furahini kwa biashara yenu mliyo fanya naye. Na huko ndiko kufuzu kukubwa".

Ni jambo lisilo na shaka yoyote kuwa kuingia kwenye medani za vita kuna madhara ya roho za watu na mali zao pia; na tajiriba imeonyesha kuwa, kuna watu wengi sana ambao, kutokana na kwenda vitani kwa nia ya kuneemeka kwa vitu na kunufaika kimaada, au kwa malengo megineyo, wameishia kujuta au kusibiwa na msongo wa mawazo huku wakitamani, wasingelikwenda vitani laiti kama wangejua. Lakini kwa wale wanaojitosa kwenye medani za vita na Jihadi kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, wao hawaingiwi na chembe ya shaka wala hawapatwi na majuto katika hali yoyote ile, kwa sababu wana yakini kuwa wamewekeana ahadi ya kweli na Mola wao; na kwa hivyo hujiweka tayari kuyakabili hata kwa roho zao masaibu na madhara yoyote yanayowafika bila kujutia chochote. Maneno matukufu ya wahyi yanalieleza hilo kama ifuatavyo katika aya ya 146 ya Suratu-Aal Imran: "Na Manabii wangapi walipigana na pamoja nao Waumini wengi wenye ikhlasi! Hawakufanya woga kwa yaliyo wasibu katika Njia ya Mwenyezi Mungu, wala hawakudhoofika wala hawakuwa wanyonge. Na Mwenyezi Mungu huwapenda wanao subiri". 

Miongoni mwa nyenzo zenye taathira kubwa katika medani za vita ni kuwa na nguvu na uwezo mkubwa kisilaha. Na ndio maana siku zote yamekuwapo na yanaendelea kuwepo mashindano ya uundaji na umiliki wa silaha baina ya madola makubwa; na ni kwa sababu hiyo pia, ndipo Mwenyezi Mungu Mtukufu akatoa amri ndani ya Qur'ani ya kuimarishwa mihimili ya nguvu za kijeshi ya Ulimwengu wa Kiislamu kwa ajili ya kukabiliana na madola ya kishetani. Lakini kwa kuwa wanajihadi wa kambi ya haki wanaingia vitani kwa nia na kwa ajili ya kutafuta radhi za Mwenyezi Mungu, kwa hivyo sambamba na kujiimarisha na kuongeza nguvu na uwezo wao wa kijeshi siku baada ya siku, wanautegemea pia mwega na msukumo wa msaada wa kimaanawi katika kupambana na maadui zao, kwa sababu wana yakini kwamba, silaha tupu bila egemeo la kimaanawi ni sawasawa na chuma cha karatasi tu. Na ndio maana dua, munajati na kushtakia shida kwa Mwenyezi Mungu ni miongoni mwa vitu vyenye taathira chanya na vyenye kutoa mchango mkubwa katika medani za vita na makabilianao na adui.

Hussein Ibn Ali (AS), -ambaye alilelewa na kukulia kwenye chuo cha Utume na kuzisikia dua alizokuwa akiomba babu yake Bwana Mtume SAW katika medani za vita na akasikia pia munajati na dua za baba yake, Ali (AS) katika mapambano ya Jihadi-, katika usiku wa kuamkia Siku ya Ashura, akiwa amekabiliwa na adui aliyekuwa katika kilele cha majigambo, makeke na nguvu za kijeshi, alilitaka jeshi la adui huyo limpe fursa katika usiku huo ya kusimama kwa ajili ya Sala, kunong'ona na Mola wake na kusoma Qur'ani. Na hata katika adhuhuri ya Ashura, wakati askari makatili na wasio na huruma wa jeshi la kidhalimu la kina Yazid lilipoanzisha mashambulio dhidi yake na wafuasi wake, mtukufu huyo aliitekeleza faradhi ya Sala, ambayo ni dhihirisho kamili la mawasiliano baina ya mja na Muumba wa ulimwengu, ili kuwafunza walimwengu kwamba, katika raha na shida, utulivu na misukosuko ya maisha, hususan katika kilele cha moto wa vita, inapasa mtu aombe hifadhi kwenye bora ya kimbilio, yaani Mwenyezi Mungu Azza wa Jalla, ambaye ni dhihirisho la nguvu za kweli katika ulimwengu, ili kuweza kuwa imara na thabiti na kuimarisha irada na uwezo wake.

Qur'ani tukufu imetuonyesha mifano kadhaa ya msukumo na msaada wa kimaanawi waliopewa Waislamu katika sura tofauti, ukiwemo ule ulioelezewa katika aya ya 123 hadi 125 za Suratu-Aal Imran kuhusiana na Vita vya Badr, ambao ni wa kuteremka Malaika waliokwenda kulisaidia jeshi la Uislamu katika kukabiliana na jeshi la Makureishi na kulishinda jeshi hilo licha ya kuwa kubwa zaidi mara kadhaa kulinganisha na la Waislamu kwa idadi ya wapiganaji na zana za kivita. Katika aya ya tisa hadi 11 za Suratul-Ahzab, Qur'ani inazungumzia kimbunga na upelekwaji wa wapiganaji wasioonekana, ambapo wakati Waislamu walipoingiwa na hofu kubwa kutokana na nguvu za jeshi la maadui na hata wakatetereka na kuingiwa na shaka, Mwenyezi Mungu aliwateremshia msaada huo wa ghaibu na kuwawezesha kushinda vita hivyo.

Mfano mwengine wa misaada ya ghaibu ya Mwenyezi Mungu ni woga na hofu liliyojazwa jeshi la ukafiri, ambao Qur'ani imeuzungumzia kuhusu kundi la Mayahudi wa Madina kama sehemu ya aya ya pili ya Suratul-Hashr inavyosema: "na akatia woga katika nyoyo zao. Wakawa wanazibomoa nyumba zao kwa mikono yao na mikono ya Waumini. Basi zingatieni enyi wenye macho!"

Katika zama zetu hizi pia tunaweza kuashiria ushindi mkubwa iliopata Iran katika vita vya miaka minane vya Kujihami Kutakatifu vya kukabiliana na uvamizi wa kinyama wa utawala wa Baathi wa Iraq, ambapo kwa kutegemea imani, dua na kukesha usiku kwa ibada wapiganaji wake, Jamhuri ya Kiislamu iliweza kuibuka mshindi katika vita hivyo. Aidha ushindi wa Hizbullah ya Lebanon katika Vita vya Siku 33 na ushindi wa wananchi mashujaa wa Palestina katika Vita vya siku 22, wote hao dhidi ya Wazayuni; na ushindi ambao inshaallah utapatikana muda si mrefu ujao, wa wananchi wa Yemen dhidi ya muungano wa kijeshi unaoongozwa na utawala mtenda jinai wa Aal Saud; yote hiyo ni mifano ya wazi ya kuthibitisha kuwa mbali na zana za kivita, tegemeo kubwa zaidi la wanajihadi ni msaada wa ghaibu wa Mwenyezi Mungu na msukumo adhimu wa dua na umaanawi. Na kwa maelezo hayo basi mpendwa msikilizaji niseme pia kwamba, sehemu ya 52 ya kipindi cha Akhlaqi Katika Uislamu imefikia tamati. Hivyo sina budi kukuaga hadi wakati mwingine inshallah, tutakapokutana tena katika sehemu ya 53 ya kipindi hiki. Namuomba Mola wa haki akubariki; na amani, rehma na baraka zake ziendelee kuwa juu yako…/