Apr 22, 2023 01:34 UTC
  • Jumamosi, 22 Aprili, 2023

Leo ni Jumamosi tarehe Mosi Mfunguo Mosi Shawwal 1444 Hijria sawa na tarehe 22 Aprili 2023 Miladia.

Leo ni tarehe Mosi Shawwal inayosadifiana na Idi tukufu ya al-Fitr. Idul Fitri ni miongoni mwa sikukuu kubwa katika dini tukufu ya Kiislamu. Baada ya kukamilisha ibada ya funga, kuomba na kujipinda kwa ibada katika mwezi mtukufu wa Ramadhani, Waislamu hufanya sherehe katika siku hii kubwa wakimshukuru Mola Manani kwa kuwawezesha kukamilisha ibada huyo. Iddi al Fitr ni kuuaga mwezi mtukufu wa Ramadhani ambao ni mwezi wa ibada na kujisafisha. Katika siku kama hii ya leo ni haramu kufunga saumu yoyote na Waislamu baada ya juhudi za mwezi mzima za kupambana na nafsi na kuchuma matunda ya ucha-Mungu hukusanyika pamoja na kusali Sala ya Iddul Fitr. Kuhusiana na utukufu wa siku hii Mtukufu Mtume (saw) anasema: "Mtu yeyote atakayemuasi Mwenyezi Mungu katika siku ya Idi, basi ni kama mtu aliyemuasi Mwenyezi Mungu siku ya miadi, yaani Siku ya Kiama." Kwa mnasaba wa siku hii adhimu, Redio Tehran inatoa mkono wa pongezi, heri na fanaka kwa Waislamu wote duniani. ***

 

Siku kama ya leo miaka 1191 iliyopita yaani tarehe Mosi Shawwal mwaka 253, Hijria alifariki dunia mpokezi mashuhuri wa Hadithi wa Ahlusunna, Imam Muhammad Ismail Bukhari. Abu Abdullah Muhammad Ismail aliyekuwa mashuhuri kwa jina la Imam Bukhari ni miongoni mwa wanazuoni wakubwa wa Hadithi wanaoaminiwa na Ahlusunna. Alisafiri sana kwa ajili ya kutafuta Hadithi za Mtume (saw). Kitabu mashuhuri zaidi cha mwanazuoni huyo ni kile cha ‘Jamius Swahih’ maarufu kama Sahihi Bukhari. Vitabu vingine mashuhuri vya mwanazuoni huyo ni ‘Al-Adabul Mufrad’, ‘Al-Jaamiul-Kabiir’ na ‘Tarikhul-Kabir an Taraajam Rijaal-Sanad.’ ***

Siku kama ya leo miaka 875 iliyopita, sawa na tarehe Mosi Shawwal mwaka 569 Hijiria alifariki dunia Said Bin Mubarak maarufu kwa jina la Ibn Dahhan, mfasiri, mwanafasihi na malenga wa Kiislamu. Ibn Dahhan alizaliwa mjini Baghdad na baada ya kumaliza masomo yake ya awali, alianza kusoma lugha sambamba na kupokea hadithi kutoka kwa wanazuoni wakubwa wa zama zake. Mtaalamu huyo mkubwa wa lugha alitilia maanani taaluma ya fasihi hususan katika kusoma mashairi na hivyo kuwa mfano wa kuigwa na wanafunzi wake katika usomaji mashairi. Aidha alilipa umuhimu mkubwa suala la kuhuisha baadhi ya vitabu vilivyosahaulika kiasi kwamba mwishoni alipoteza uwezo wake wa kuona katika kazi hiyo. ***

 

Miaka 838 iliyopita katika siku kama hii ya leo ya tarehe Mosi Shawwal alifariki dunia Abu Abdallah Muhammad bin Omar Razi mashuhuri kwa jina la Fakhrurazi msomi na mwanazuoni mashuhuri wa Kiislamu. Alizaliwa katika mji wa Rey jirani na Tehran na alifanikiwa kwa haraka kujifunza elimu mbalimbali za Kiislamu kama Fiqihi, Tafsiri, Falsafa na Mantiki kutokana na kipaji kikubwa alichokuwa nacho. Mwanazuoni huyo ameandika vitabu vingi. Miongoni mwa vitabu vya Fakhrurazi ni Sherh Nahaj al-Balagha, Nihayat al-Uquul wa Siraj al-Quluub. ***

 

Siku kama ya leo miaka 299 iliyopita, alizaliwa Königsberg, Ujerumani na katika familia ya kati Immanuel Kant, mwanafalsafa mkubwa wa nchi hiyo. Baada ya kuhitimu masomo yake katika fani ya hisabati, theolojia na falsafa Kant alijishughulisha na kazi ya ufundishaji vijijini. Baadaye na akiwa na umri wa miaka 46 msomi huyo alifanikiwa kuwa muhadhiri wa falsafa katika chuo kikuu cha mji alikozaliwa wa Königsberg. Katika miaka yote ya utafiti wake na kufundisha falsafa, alipata kuandika vitabu tofauti ambavyo baadhi vipo katika maktaba kubwa duniani. Kadhalika mwanafalsafa huyo mkubwa alifanikiwa kuasisi mfumo wa kifikra maalumu katika uga huo. Kwa imani ya Immanuel Kant, ndani ya mwanadamu kuna hisia maalumu ya kitabia ambayo huweza kutoa hukumu kwamba kitendo hiki ni chema na kile ni kiovu. Hii ikiwa na maana kwamba, mwanadamu binafasi anaweza kutenda mema na maovu, lakini ile hisia yake ya kitabia ndio huweza kumueleza kwamba kitendo fulani ni chema au kibaya na kwamba lau kama si kuwepo kwa hisia hiyo, basi mwanadamu asingeweza mwenyewe kujilaumu baada ya kutenda jambo fulani. Immanuel Kant alifariki dunia tarehe 12 Februari 1904 mjini Königsberg akiwa na umri wa miaka 80 huku akiwa ameishi maisha yake yote akiwa kapera. ***

Immanuel Kant

 

Siku kama hii ya leo miaka 128 iliyopita wananchi wa Cuba kwa mara nyingine tena walianzisha mapambano ya kupigania uhuru wao kutoka kwa wakoloni wa Uhispania. Hayo yalikuwa mapambano yao ya tatu katika nusu ya pili ya karne ya 19 Miladia kwa ajili ya kutaka kujitawala. Uhispania ilituma wanajeshi laki tatu nchini humo kwa ajili ya kupambana na wanamapinduzi hao. Kufuatia vurugu hizo Marekani ilitumia fursa hiyo na kwa kisingizio cha kulipuliwa meli yake ya kivita karibu na pwani ya Cuba mwaka 1898 Miladia, kuingia katika vita hivyo dhidi ya Uhispania. Manuari za kivita za Uhispania ziliangamizwa katika maji ya Cuba na hatimaye nchi hiyo ya Amerika ya Latini ikakaliwa kwa mabavu na Marekani. ***

 

Miaka 119 iliyopita katika siku kama hii ya leo alizaliwa mwanafizikia na mtengenezaji wa bomu la atomiki wa Marekani Robert Oppenheimer. Kabla ya Vita vya Pili vya Dunia mtaalamu huyo alifanya utafiti kuhusiana na jinsi ya kupasua atomu na kupata nishati ya nyuklia. Wakati wa vita hivyo alipewa wadhifa wa kusimamia kitengo cha utafiti katika Wizara ya Vita ya Marekani na chini ya usimamizi wake yakatengenezwa mabomu matatu ya kwanza ya nyuklia. Hata hivyo, wakati Marekani ilipoishambulia Japan kwa mabomu ya nyuklia mwaka 1945, makumi ya maelfu ya watu wasio na hatia waliuawa katika kipindi kifupi, hali iliyomfanya Oppenheimer kujutia kitendo chake hicho na akatoa wito wa kutumiwa nishati ya atomiki katika masuala ya amani. ***

Robert Oppenheimer.

 

Miaka 75 iliyopita mwafaka na siku kama hii ya leo, yaani tarehe 22 Aprili 1948, Wazayuni waliushambulia mji wa bandari wa Haifa huko kaskazini magharibi mwa Palestina wakati wa kukaribia kuanzishwa utawala haramu wa Israel. Wazayuni waliwauwa shahidi Wapalestina 500 katika mashambulizi hayo makubwa na kuwajeruhi wengine 200 ambao walikuwa wanawake na watoto waliokimbilia huko Haifa wakisubiri kupelekwa katika maeneo mengine. ***

 

Siku kama ya leo miaka 44 iliyopita Imam Khomeini (M.A) mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alitoa amri ya kuundwa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (SEPAH). Kwa mujibu wa amri hiyo, jukumu kuu la jeshi hilo ni kulinda Mapinduzi ya Kiislamu dhidi ya maadui wa ndani na nje. Baada ya kuundwa, jeshi la SEPAH lilikabiliana na makundi yaliyopinga Mapinduzi ya Kiislamu, yaliyoanzisha mapambano ya silaha katika pembe mbalimbali za Iran na kuweza kuzima njama za maadui. Aidha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi liliweza kudhihirisha uwezo mkubwa wakati wa vita vya kulazimishwa kati ya Iraq na Iran vilivyoanzishwa na utawala wa dikteta Saddam Hussein kwa lengo la kuyaangamiza Mapinduzi ya Kiislamu na kuigawa Iran.

 

Tags