Sura ya Az-Zumar, aya ya 1-4 (Darsa ya 837)
Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur’ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.
Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur’ani. Hii ni darsa ya 837. Baada ya kuhitimisha tarjumi na maelezo ya Sura ya 38 ya S’aad, katika darsa hii tutaanza kutoa tarjumi na maelezo ya sura ya 39 ya Az-Zumar. Suratu-Zumar iliteremshwa Makka na ina jumla ya aya 75. Na kama zilivyo sura nyingine za Makka, aya zake nyingi zinazungumzia masuala ya kiitikadi kama Tauhidi, Ma’adi, yaani kufufuliwa kwa viumbe na Utume. Baada ya utangulizi huo mfupi tunaianza darsa yetu kwa aya ya mwanzo na ya pili za sura hiyo ambazo zinasema:
تَنزِيلُ الْكِتَابِ مِنَ اللَّـهِ الْعَزِيزِ الْحَكِيمِ
Mteremsho wa Kitabu hiki umetokana na Mwenyezi Mungu, Mwenye nguvu, Mwenye hikima.
إِنَّا أَنزَلْنَا إِلَيْكَ الْكِتَابَ بِالْحَقِّ فَاعْبُدِ اللَّـهَ مُخْلِصًا لَّهُ الدِّينَ
Hakika Sisi tumekuteremshia Kitabu hiki kwa Haki. Basi muabudu Mwenyezi Mungu ukimsafia Dini Yeye tu.
Aya hizi zinaashiria hadhi ya Qur’ani katika dini tukufu ya Uislamu na kueleza kwamba: Qur’ani ni maneno ya Allah SW, si maneno ya Bwana Mtume Muhammad SAW, kama ambavyo vitabu vingine vya mbinguni vilivyotangulia pia hayakuwa maneno ya Mitume kama Nabii Musa na Nabii Isa (as), bali yalikuwa maneno ya Mwenyezi Mungu Mtukufu. Lengo la kuteremshwa kitabu hiki, kama ilivyokuwa kwa vitabu vilivyopita, ni kuwaongoza watu wawe na utambuzi sahihi wa Muumba wa ulimwengu na kuondoa kila aina ya upotofu kuhusu asili ya tauhidi na kumwabudu Mungu pekee wa haki. Mwanadamu, kifitra na kimaumbile, anajua kwamba ulimwengu una muumbaji wake, lakini huwa anakosea katika kumtambua muumba huyo. Yeye huwa ima anavifanya vitu au watu kuwa washirika wa Allah katika uumbaji wa ulimwengu, au huvidhani vitu na watu hao ni washirika wa Mola katika upangaji na uendeshaji masuala ya ulimwengu. Kwa hivyo Qur’ani tukufu imekuja kumtambulisha Mungu wa kweli na halisi wa ulimwengu kwa utambuzi ulio sahihi na usio na khurafa na aina yoyote ya upotofu. Ni wazi kwamba, kitabu kilichoteremshwa na Mwenyezi Mungu, yaliyomo ndani yake ni sahihi na ni haki tupu na yametakasika na neno lolote lisilo sahihi na la batili, kwa sababu Yeye Allah ni mwenye nguvu na hekima; na kwake Yeye hakitoki chochote isipokuwa elimu, ujuzi na hekima. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, japokuwa Mwenyezi Mungu hatumwoni kwa macho yetu, lakini kwa kusoma aya za Qur’ani tukufu, tunayasikia maneno yake; na kwa kutaamali na kuyatafakari tunabainikiwa na usahihi na ukweli wa maneno hayo. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, izza, nguvu na utukufu wa kweli unapatikana chini ya kivuli cha elimu na hekima, na mawili hayo (nguvu na hekima) yanahitajiana na yanaandamana pamoja. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba, ibada na kuwa mja wa Allah kunapasa kufanywe kwa ikhlasi na kwa kufuata dini ya haki pasi na kuchanganya na aina yoyote ya shirki, kufru na khurafa.
Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 3 ambayo inasema:
أَلَا لِلَّـهِ الدِّينُ الْخَالِصُ ۚ وَالَّذِينَ اتَّخَذُوا مِن دُونِهِ أَوْلِيَاءَ مَا نَعْبُدُهُمْ إِلَّا لِيُقَرِّبُونَا إِلَى اللَّـهِ زُلْفَىٰ إِنَّ اللَّـهَ يَحْكُمُ بَيْنَهُمْ فِي مَا هُمْ فِيهِ يَخْتَلِفُونَ ۗ إِنَّ اللَّـهَ لَا يَهْدِي مَنْ هُوَ كَاذِبٌ كَفَّارٌ
Hakika Dini Safi ni ya Mwenyezi Mungu tu. Na wale wanao wafanya wenginewe kuwa ni walinzi badala yake (husema): Sisi hatuwaabudu ila wapate kutujongeza tu kumkaribia Mwenyezi Mungu - Hakika Mwenyezi Mungu atahukumu baina yao katika wanayo khitalifiana. Hakika Mwenyezi Mungu hamwongoi aliye mwongo, kafiri.
Aya hii inaendeleza maudhui ya aya zilizotangulia kuhusu ikhlasi katika dini na kutilia mkazo nukta hiyo kwa kusema: Dini na imani safi ya ikhlasi inaweza kupatikana kwa Allah pekee; na yale yote yanayotokana na akili na fikra ya mwanadamu yanachanganyika na shirki, khurafa na upotofu. Ni Allah SW tu ndiye mwenye kuweza kujitambulisha Yeye mwenyewe kwa usahihi kwa mwanadamu na kumfunza kiumbe huyo njia na namna ya kumwabudu na kudhihirisha uja wake kwake. Aidha analolikubali Allah ni dini safi na ya ikhlasi; na aina yoyote ile ya shirki na ria katika fikra na amali huyafanya matendo mema ya mja yasitakabaliwe na Yeye Mola. Ni kama alivyosema Bwana Mtume SAW alipomueleza mtu aliyesema: Sisi tunatoa mali zetu kuwapa wahitaji ili watu watutaje kwa wema; ambapo mtukufu huyo alimwambia mtu huyo: Mwenyezi Mungu anaikubali amali inayofanywa kwa ikhlasi tu, yaani kwa ajili yake Yeye tu. Kisha aya inaashiria moja ya ishara za kuwa mbali na ikhlasi katika dini na kueleza kwamba: Kutokana na washirikina kudhani kwamba mtu hawezi kumwomba na kuwasiliana naye Mwenyezi Mungu moja kwa moja, walikuwa wanaviabudu baadhi ya viumbe kwa anuani ya kuwa ni wasita na viunganishi vitakatifu baina yao na Mwenyezi Mungu, na wakawa wanavishirikisha katika kumwabudu kwao Allah. Ilhali Yeye Mola hajaidhinisha katu jambo kama hilo, bali wao walikuwa wakimsingizia na kumnasibishia tu Allah mambo hayo kutokana na fikra potofu na za shirki kwa kuabudu asiyekuwa Yeye. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba, itikadi zilizobuniwa na wanadamu, hata kama zitakuwa na kiwango chochote cha masuala ya kimanawi na ya maarifa ya kinafsi ya kumtambua Allah, lazima zitachanganyika na anuai za khurafa na upotofu katika fikra na matendo; na dini safi na halisi ni ile tu iliyoteremshwa na Mwenyezi Mungu, Mola aliyetukuka na aliyetakasika. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa, watu waliopotoka kifikra, wanatafuta hoja za kuhalalisha upotofu wao ili waweze kuwavuta na kuwateka watu wengine kwenye itikadi yao; ni kama washirikina walivyokuwa wakidai kuyafanya masanamu kuwa wasita na kiunganishi baina yao na Mwenyezi Mungu. Vile vile tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba, hisi za kumjua Allah na kutaka kujikurubisha kwake, ni jambo linalopendwa na viumbe wote, lakini wengi wao hukosea katika njia na utaratibu wanaotumia kwa ajili ya kujikurubisha kwa Mola.
Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 4 ya sura yetu ya Az-Zumar ambayo inasema:
لَّوْ أَرَادَ اللَّـهُ أَن يَتَّخِذَ وَلَدًا لَّاصْطَفَىٰ مِمَّا يَخْلُقُ مَا يَشَاءُ ۚ سُبْحَانَهُ ۖ هُوَ اللَّـهُ الْوَاحِدُ الْقَهَّارُ
Lau kuwa Mwenyezi Mungu angeli taka kujifanyia mwana, basi bila ya shaka angeli teua amtakaye katika alio waumba. Subhanahu, Ametakasika na hayo! Yeye ni Mwenyezi Mungu Mmoja, Mtenza nguvu.
Aya hii inaendeleza maudhui iliyozungumziwa katika aya iliyotangulia, iliyoashiria mfano mmoja wa shirki katika kumwabudu Mwenyezi Mungu na kueleza kwamba: Baadhi ya washirikina walikuwa wakiwadhania pia malaika kuwa ni mabinti wa Mwenyezi Mungu na wakawa wanawaabudu; kama ambavyo Wakristo pia wanamuitakidi Nabii Isa mwana wa Maryam kuwa ni mwana wa Mungu, na hivyo wanamwabudu. Ilhali Allah SW hana mwana, na ametakasika na sifa hiyo ya kuwa na mwana. Na lau kama angelitaka kujifanyia mwana katika mmoja wa viumbe wake, angelilitangaza hilo ili viumbe wote wamjue mwana huyo na kumwabudu. Lakini mbali na hayo, Allah ni ujudi wa kipekee na hakuna maujudi au kitu chochote chenye mfanano, mshabaha au kilicho mithili yake Yeye, hata kitu au mtu huyo aweze kuhesabika kuwa ni mwana wa Mungu. Yeye amekitawala na kukidhibiti kila kitu na hakuna nguvu yoyote ya kukabiliana na Yeye, hata ahitaji kuwa na mwana na aliye mfano wa Yeye. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba, Allah SW hana mwana wa kupanga wala wa kutokana na Yeye mwenyewe, kwa sababu kutaka kuwa na mwana ni alama ya kuwa mhitaji, ilhali Allah SW si mhitaji kwa namna yoyote ile na wala hana haja ya kumfanya mwana yeyote katika viumbe vyake. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa, Mwenyezi Mungu ni wa pekee asiye na mfanowe, wala hakuna kitu wala kiumbe chochote kilicho mfano wa Yeye. Kwa hivyo kila fikra na itikadi inayomshabihisha na kumfanya Allah kuwa na aliye mfano naye inakinzana na kwenda kinyume na sifa ya upekee wa Mola na haikubaliki kuanzia katika msingi wake. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 837 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atupe maarifa na utambuzi wa kumjua kwa namna inavyostahiki na atuepushe na kila aina ya shirki. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/