Sura ya Az-Zumar, aya ya 5-6 (Darsa ya 838)
Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur’ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.
Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur’ani. Hii ni darsa ya 838 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 39 ya Az-Zumar. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 5 ya sura hiyo ambayo inasema:
خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ بِالْحَقِّ ۖ يُكَوِّرُ اللَّيْلَ عَلَى النَّهَارِ وَيُكَوِّرُ النَّهَارَ عَلَى اللَّيْلِ ۖ وَسَخَّرَ الشَّمْسَ وَالْقَمَرَ ۖ كُلٌّ يَجْرِي لِأَجَلٍ مُّسَمًّى ۗ أَلَا هُوَ الْعَزِيزُ الْغَفَّارُ
Ameumba mbingu na ardhi kwa Haki. Huufunika usiku juu ya mchana, na huufunika mchana juu ya usiku. Na amelitiisha jua na mwezi, kila kimoja kinakwenda mpaka muda kilicho wekewa. Jueni mtanabahi! Yeye ndiye Mwenye nguvu, Mwenye kughufiria!
Katika darsa iliyopita tulisoma aya zilizozungumzia umoja pekee wa Mwenyezi Mungu katika uumbaji na uendeshaji masuala ya ulimwengu na kubainisha kwamba imani, amali na masuala yote ya kidini inapasa yawe na ikhlasi na yatakasike na kila aina ya shirki na khurafa ili yaweze kukubaliwa na Allah SW. Baada ya hayo, aya tuliyosoma inamuelezea Mwenyezi Mungu, Mola pekee wa haki kwa kusema: Uumbaji wa nyota na sayari zote likiwemo jua na mwezi umefanywa na Yeye, na Yeye pia ndiye aliyeweka kanuni zinazotawala katika vitu hivyo. Njia ambazo kila moja kati ya nyota, jua na mwezi zinapitia zimeainishwa na Allah SW na zina athari na matokeo maalumu. Kwa mfano, matokeo ya mzunguko wa sayari ya dunia kujizunguka yenyewe na kulizunguka jua, ni kupatikana usiku na mchana na misimu tofauti ya mwaka. Hakuna shaka yoyote kuwa, uumbwaji wa vitu vyote hivyo umetokana na hekima na kwa lengo kubwa, na si kwamba majimui hiyo ya maumbo yenye adhama na yenye kustaajabisha imetokea kwa sadfa tu na bila ya lengo wala madhumuni yoyote. Kwa sababu hiyo aya hii inasisitiza kwamba, mfumo wa uumbaji ni wa haki. Kisha aya inaendelea kueleza kwamba, harakati na mwendo wa sayari unafanyika kwa mahesabu na makadirio ya muda maalumu na kwamba harakati ya kila moja kati ya maumbo hayo katika njia zao maalumu itaendelea, mpaka hatimaye itafika siku yatasita kufanya hivyo. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba, kwa mujibu wa aya hii tuliyosoma, mfumo wa uumbaji umetokana na haki na una lengo maalumu; na kwa mujibu wa aya ya pili ya sura hii ya Az-Zumar, mfumo wa sharia na wa uteremshwaji wa vitabu vya mbinguni pia umetokana na haki na kwa lengo maalumu. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa, mzunguko wenye nidhamu maalumu wa sayari za angani, wa kila moja kufuata njia yake unafanyika kwa mahesabu maalumu na kwa amri ya Allah SW. Harakati hiyo itaendelea mpaka wakati aliouainisha na kuukadiria Yeye Mola.
Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 6 ya sura yetu ya Az-Zumar ambayo inasema:
خَلَقَكُم مِّن نَّفْسٍ وَاحِدَةٍ ثُمَّ جَعَلَ مِنْهَا زَوْجَهَا وَأَنزَلَ لَكُم مِّنَ الْأَنْعَامِ ثَمَانِيَةَ أَزْوَاجٍ ۚ يَخْلُقُكُمْ فِي بُطُونِ أُمَّهَاتِكُمْ خَلْقًا مِّن بَعْدِ خَلْقٍ فِي ظُلُمَاتٍ ثَلَاثٍ ۚ ذَٰلِكُمُ اللَّـهُ رَبُّكُمْ لَهُ الْمُلْكُ ۖ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ ۖ فَأَنَّىٰ تُصْرَفُونَ
Amekuumbeni kutokana na nafsi moja, kisha akamfanya mkewe kutokana na nafsi hiyo hiyo. Na akakuleteeni wanyama wa mifugo jozi nane. Anakuumbeni katika matumbo ya mama zenu, umbo baada ya umbo, katika viza vitatu. Huyo ndiye Mwenyezi Mungu Mola wenu Mlezi. Ufalme ni wake. Hapana Mola isipo kuwa Yeye. Basi nyinyi mnageuzwa wapi?
Aya hii inaendeleza maudhui iliyozungumziwa na aya iliyotangulia kuhusu uumbaji wa sayari za angani na kuashiria uumbwaji wa viumbe wa ardhini akiwemo mwanadamu na wanyama kwa kusema: Nyinyi nyote mumeumbwa kutokana na asili ya mwanadamu mmoja, ambaye mke wake pia alitokana na jinsi yake mwenyewe. Chimbuko na asili ya watu wote inarejea kwa Adam na Hawa, ambao ndio wanadamu wa mwanzo waliokuweko katika sayari ya dunia; na kutokana na wawili hao ndipo kikathiri na kuenea kizazi cha wanadamu katika dunia hii. Kisha aya inaashiria wanyama wa mifugo ambao tangu maelfu na maelfu ya miaka iliyopita hadi sasa wamekuwa wakimdhaminia mwanadamu nyama, bidhaa za maziwa, mavazi na kipando, na kueleza kwamba: Ni Yeye Mwenyezi Mungu Mtukufu ndiye aliyekutiishieni aina nane hizo za jozi za dume na jike za wanyama wa mifugo kwa ajili ya huduma na mahitaji yenu ya kimaisha. Ng'ombe, kondoo, mbuzi na ngamia, ni aina hizo za wanyama, ambao madume na majike yao, kila mmoja anamhudumia na kumdhaminia mwanadamu mahitaji yake mbali mbali. Kisha aya hii ya 6 ya Suratu-Zumar inaashiria awamu za uumbwaji wa mwanadamu ndani ya tumbo la mama yake na kueleza kwamba: Katika mahali palipofichika na pasipoonekana na jicho la baba na mama, kimehifadhika ndani ya matabaka matatu imara ya fuko la uzazi la mama, kitoto kichanga. Mwenyezi Mungu anaikuza mbegu ya uzazi awamu kwa awamu na kuibadilisha kutoka hali ya sura moja hadi nyingine, mpaka baada ya miezi tisa anapoileta duniani katika umbo lililokamilika la mtoto mchanga. Kwa kumalizia, aya hii inawahutubu wakanushaji wa kuwepo kwa Mwenyezi Mungu na wale wanaomshirikisha Yeye Mola ya kwamba: Huyu ndiye Mwenyezi Mungu, ambaye ni Muumba wenu na pia ndiye Mola wenu; na wala hakuna yeyote ghairi ya Yeye mwenye nguvu na uwezo kama huo wa uumbaji. Basi kwa nini mnapotoka na kuwaendea wengine wasiokuwa Yeye? Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba, wanadamu wote wa kila kaumu, rangi, lugha na asili wanatokana na baba na mama mmoja, chimbuko na asili moja; kwa hivyo wote wako sawa. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa, japokuwa mwanamke na mwanamme wana tofauti kadhaa kimwili, lakini wote wawili wanatokana na asili moja na wako sawa kiutu na katika kufikia ukamilifu wa kiutu. Vile vile aya hii inatuelimisha kwamba, uumbwaji wa mwanadamu unafanyika katika awamu kadhaa; na kipindi chake cha hali ya kiinitete, ni moja ya miujiza ya Allah iliyojificha. Adhama ya muujiza huo inabainika na kudhihirika zaidi kwa kuzaliwa mtoto mchanga. Wa aidha aya hii inatutaka tujue kuwa, Mwenyezi Mungu Mtukufu ndiye Muumba wetu, mpangaji na mwendeshaji wa mambo yetu, na vile vile mmiliki wa nafsi zetu. Neema zote tulizonazo, tujue kwamba zinatokana na Yeye; tumwamini Yeye na tumtegemee Yeye tu. Kwa sababu wengine wote, kama tulivyo sisi, ni viumbe na wamilikiwa wa Yeye Allah. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 838 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atujaalie kuwa na maarifa sahihi ya kumjua Yeye, na azijaze nyoyo zetu imani sahihi na mapenzi ya kweli juu yake, kwa kutekeleza aliyotuamrisha na kujiepusha na aliyotukataza. Wassalamu Aalykum Warahamtullahi Wabarakatuh…/