Sura ya Az-Zumar, aya ya 7-8 (Darsa ya 839)
Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur’ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.
Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur’ani. Hii ni darsa ya 839 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 39 ya Az-Zumar. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 7 ya sura hiyo ambayo inasema:
إِن تَكْفُرُوا فَإِنَّ اللَّـهَ غَنِيٌّ عَنكُمْ ۖ وَلَا يَرْضَىٰ لِعِبَادِهِ الْكُفْرَ ۖ وَإِن تَشْكُرُوا يَرْضَهُ لَكُمْ ۗ وَلَا تَزِرُ وَازِرَةٌ وِزْرَ أُخْرَىٰ ۗ ثُمَّ إِلَىٰ رَبِّكُم مَّرْجِعُكُمْ فَيُنَبِّئُكُم بِمَا كُنتُمْ تَعْمَلُونَ ۚ إِنَّهُ عَلِيمٌ بِذَاتِ الصُّدُورِ
Mkikufuru basi Mwenyezi Mungu si mwenye haja nanyi, na wala haridhii kufuru kwa waja wake. Na mkishukuru atakuridhieni. Na wala hatabeba mbebaji mzigo wa mwingine. Kisha marejeo yenu ni kwa Mola wenu Mlezi. Hapo atakwambieni mliyo kuwa mkiyafanya. Hakika Yeye ni Mjuzi wa yaliyomo vifuani.
Katika darsa iliyopita, Qur'ani tukufu ilizungumzia neema za Allah katika uumbaji wa mwanadamu na wanyama wa miguu minne, yaani nyamahoa. Aya hii ya saba ya Suratu-Zumar inazungumzia maudhui ya kushukuru na kuwa washukurivu kwa Mola kwa kueleza kwamba: Baadhi ya watu wanaziona neema za Allah, na huwa washukurivu kwake katika hali zote. Lakini baadhi ya watu wanaghafilika na wala hawajali kuwa wanafaidika na neema za Allah; na wanachofanya ni kuzitumia tu pasi na kuzingatia; na kama watazingatia umuhimu wa neema hizo, basi huwa hawaitakidi kuwa zinatoka kwa Mwenyezi Mungu. Watu hao wanadhani kwamba, neema walizonazo ni matunda na matokeo ya juhudi na bidii zao wenyewe, kwa hivyo hawaoni haja ya kuwa washukurivu. Ukweli ni kwamba Allah SW si mhitaji na wala hana haja ya shukurani za wanadamu. Kwa maana kwamba, hata kama walimwengu wote watakufuru na kumkana Allah SW, au kama wote watakuwa watovu wa shukurani, ni mamoja tu kwake Yeye. Kwa sababu Mwenyezi Mungu aliye Mkwasi si mhitaji hata wa kuwepo kwetu sisi wanadamu sembuse ushukurivu wetu. Hakika ni kwamba, ikiwa Mwenyezi Mungu amewakalifisha waja wake kuwa washukurivu wa neema zake, si kwa sababu Yeye ni mhitaji wa shukurani za wanadamu; hasha wa kalla; ni kwa sababu, kuwa na moyo wa ushukurivu huwajenga watu kiakhlaqi na kimaanawi. Ndiyo maana katika aya ya 14 ya Suratu-Luqman, baada ya Qur'ani tukufu kutoa amri ya kumshukuru Allah imemtaka mwandamu awe mshukurivu pia kwa wazazi wake kutokana na walivyomhangaikia na kwa tabu walizopata kwa ajili yake. Kisha aya ya 7 ya Suratu-Zumar inaashiria kanuni kuu katika mwenendo wa watu na kueleza kwamba: Kila mtu inapasa akubali masuulia na dhima ya matendo yake mwenyewe na awajibike kwa aliyoyafanya. Mtu yeyote yule hana haki ya kuwabebesha watu wengine masuulia ya matendo yake na kujivua na dhima ya aliyoyafanya yeye mwenyewe. Na kwa sababu hiyo, Siku ya Kiyama, Allah SW hatombebesha mtu mzigo wa dhambi za mtu mtu mwengine; na kutokana na elimu yake mutlaki ya ujuzi wa batini na ya ndani ya nafsi za watu na yote waliyoyafanya faraghani na hadharani, atawahesabu na kuwahukumu kwa yale waliyoyafanya. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba, maamrisho ya dini tunayotekeleza kama Sala na Saumu hayamaanishi katu kwamba Mwenyezi Mungu ni mhitaji wa ibada zetu. Lakini kama ambavyo mwalimu huwa anawapa kazi na mazoezi ya masomo wanafunzi wake kwa madhumuni ya kuinua kiwango chao cha elimu, maamrisho ya Allah SW, nayo pia lengo lake ni kuwajenga na kuwainua watu daraja zao kimaanawi. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa, Mwenyezi Mungu anaamiliana na waja wake kwa uadilifu, na kila mtu atalipwa thawabu au adhabu kutokana na amali zake. Na ndiyo maana uhusiano wa kikabila, asili, ukoo n.k hautamfaa mtu Siku ya Kiyama. Vile vile tunajielimisha kutokana na aya hii kwamba, Allah SW anaelewa barabara nia na dhamira zetu sisi wanadamu na anazihesabu amali zetu kulingana na nia zetu.
Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 8 ya sura yetu ya Az-Zumar ambayo inasema:
وَإِذَا مَسَّ الْإِنسَانَ ضُرٌّ دَعَا رَبَّهُ مُنِيبًا إِلَيْهِ ثُمَّ إِذَا خَوَّلَهُ نِعْمَةً مِّنْهُ نَسِيَ مَا كَانَ يَدْعُو إِلَيْهِ مِن قَبْلُ وَجَعَلَ لِلَّـهِ أَندَادًا لِّيُضِلَّ عَن سَبِيلِهِ ۚ قُلْ تَمَتَّعْ بِكُفْرِكَ قَلِيلًا ۖ إِنَّكَ مِنْ أَصْحَابِ النَّارِ
Na taabu inapo mfikia mtu humwomba Mola wake Mlezi naye ameelekea kwake. Kisha akimpa neema kutoka kwake, husahau yale aliyo kuwa akimwitia zamani, na akamfanyia Mwenyezi Mungu washirika ili apoteze watu njia yake. Sema: Starehe na ukafiri wako kwa muda mchache. Kwani hakika wewe utakuwa miongoni mwa watu wa Motoni.
Aya hii inaendeleza maudhui ya aya iliyotangulia iliyozungumzia ushukurivu au utovu wa shukurani wa mwanadamu kwa Allah na kuashiria moja ya mifano ya utovu huo kwa kusema: Baadhi ya watu wanapofikwa na tatizo maishani, kama maradhi au shida za maisha na kiuchumi humwomba sana Mwenyezi Mungu. Humtaka Allah awatatulie matatizo yao na kumwomba awaghufirie na kuwasamehe ikiwa matatizo yaliyowapata yametokana na madhambi au kujisahau kwao. Lakini baada ya kutatuliwa matatizo waliyonayo au wanapojaaliwa neema nyingine mpya na Allah, watu hao hao humsahau Mola na neema alizowapa pamoja na matatizo yaliyopita aliyowatatulia, na kushughulishwa na masuala yao ya kidunia. Baadhi ya wakati, hupumbazwa na kutekwa na dunia mpaka ikafika hadi wakamsahau moja kwa moja Allah na kuwaona wengine wasiokuwa Yeye kwamba ndio sababu ya wao kutengenekewa na kunyookewa katika maisha yao. Kwa hivyo huamua kuwalingania watu wengine pia wawafuate hao wanaowaitakidi wao badala ya Mwenyezi Mungu na kuwa sababu ya kupotoka wenzao hao pia. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba, katika imani za misimu na za vipindi maalumu zinazojitokeza wakati wa shida, mtu humkumbuka Allah katika nyakati fulani fulani tu, lakini humsahau Mola katika muda mwingi wa maisha yake. Imani ya aina hii haina faida wala taathira yoyote. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa, japokuwa matatizo ya maisha humsababishia mtu tabu, shida na misukosuko, lakini yana faida pia kwake. Miongoni mwa faida muhimu za tabu hizo ni kumzindua na kumtoa mtu kwenye usingizi wa mghafala na kujisahau na kumfanya aitambue asili na marejeo yake. Wa aidha aya hii inatuelimisha kwamba, wanadamu wenye imani dhaifu, wakati wanapopata raha na uneemevu, huyasahau matatizo waliyokuwa nayo nyuma na jinsi Allah SW alivyowatatulia matatizo hayo. Vile vile aya hii inatutaka tuelewe kuwa, si kila neema ya duniani ni ishara ya fanaka halisi kwa mtu. Kwani wangapi na wangapi katika makafiri na wamkanushao Mwenyezi Mungu wana neema chungu nzima za duniani, lakini mafanikio yoyote yale ya kidunia ni duni na haba mno kulinganisha na neema za akhera.
Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 839 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atujaalie kuwa waja tunaomkumbuka Yeye wakati wa shida na raha na katika dhiki na neema. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.../