Sura ya Az-Zumar, aya ya 9-10 (Darsa ya 840)
Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur’ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.
Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur’ani. Hii ni darsa ya 840 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 39 ya Az-Zumar. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 9 ya sura hiyo ambayo inasema:
أَمَّنْ هُوَ قَانِتٌ آنَاءَ اللَّيْلِ سَاجِدًا وَقَائِمًا يَحْذَرُ الْآخِرَةَ وَيَرْجُو رَحْمَةَ رَبِّهِ ۗ قُلْ هَلْ يَسْتَوِي الَّذِينَ يَعْلَمُونَ وَالَّذِينَ لَا يَعْلَمُونَ ۗ إِنَّمَا يَتَذَكَّرُ أُولُو الْأَلْبَابِ
Je! Afanyaye ibada nyakati za usiku kwa kusujudu na kusimama akitahadhari na Akhera, na akitaraji rehema za Mola wake Mlezi...Sema: Ati watakuwa sawa wale wanao jua na wale wasio jua? Hakika wanao kumbuka ni watu wenye akili tu.
Katika darsa iliyopita tulisoma aya zilizowazungumzia watu ambao huwa wanamtaja na kumkumbuka Allah pale tu wanapokuwa na shida na dhiki; lakini wasipokuwa kwenye hali hizo humsahau au hata humkufuru Mola wao. Aya ya tisa tuliyosoma inafanya ulinganishaji kwa kusema: Je watu wa aina hiyo, wanaweza kuwa sawa na watu wanaomkumbuka Allah katika kila hali, iwe ni katika shida na dhiki au raha na faraja? Hao ni watu ambao huamka usiku wa manane, wakasali na kufanya ibada kwa ajili ya kupata rehma za Mola wao na ili waepushwe na adhabu ya Moto. Moja ya sifa za mawalii wa Allah ni kuinuka usiku kwa ajili ya kusali, kuomba dua na kusoma Qur'ani. Baadhi ya Waislamu wa kawaida husali Sala za faradhi kwa karaha na ili kutimiza wajibu tu; na pia hufunga Saumu kwa kujidhikisha na kujilazimisha tu. Lakini kinyume na watu hao, waumini wa kweli, wenye imani thabiti na yakini juu ya Allah na Siku ya Kiyama, husali Sala zao za faradhi na kutekeleza ibada zingine za wajibu kwa hamu na shauku; lakini pia huamka usiku wa manane kwa ajili ya kusali Sala za Sunna, kufanya ibada nyinginezo na kunong'ona na Mola wao Muumba. Ni wazi kwamba watu wa aina hii huwa na matumaini ya kupata rehma za Allah na wakati huohuo huwa na hofu ya kufikwa na adhabu yake. Yaani daima huwa wanaishi katika hali ya hofu na matumaini, jambo ambalo huwafanya wasikate tamaa wala wasiingiwe na ghururi ya kupata rehma zisizo na ukomo, za Allah SW. Kisha aya inamhutubu Bwana Mtume SAW kwamba: Watangazie watu kuwa, wanaojua na wasiojua, katu hawawi sawa. Na ni watu wenye akili makini na timamu tu ndio wanaotambua tofauti iliyopo kati ya makundi mawili hayo ya watu. Watu hao ni wenye kuaidhika; na huchagua kufuata njia ya saada. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba, kwa mujibu wa mafundisho ya Qur'ani, usiku si wakati uliotengwa kwa ajili ya kupumzika na kulala tu, bali ni fursa mwafaka pia ya mja kupata faragha ya kunong'ona na kutaradhia hali kwa Allah SW. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa, wenye elimu na wajuzi wa kweli, huwa ni watu wanaokithirisha ibada, dua na kumdhukuru Mola wao. Wa aidha tunajielimisha kutokanana na aya hii kwamba, inapasa kuwepo na wastani na uwiyano kati ya hofu juu ya adhabu ya Allah na matumaini ya kupata rehma zake Mola. Na hivyo ndivyo walivyo waja halisi wa Mwenyezi Mungu; yaani wanahofia hatima yao itakavyokuwa akhera na pia wana matumaini ya kupata fadhila na rehma za Mola.
Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 10 ambayo inasema:
قُلْ يَا عِبَادِ الَّذِينَ آمَنُوا اتَّقُوا رَبَّكُمْ ۚ لِلَّذِينَ أَحْسَنُوا فِي هَـٰذِهِ الدُّنْيَا حَسَنَةٌ ۗ وَأَرْضُ اللَّـهِ وَاسِعَةٌ ۗ إِنَّمَا يُوَفَّى الصَّابِرُونَ أَجْرَهُم بِغَيْرِ حِسَابٍ
Sema: Enyi waja wangu mlio amini! Mcheni Mola wenu Mlezi. Wale wafanyao wema katika dunia hii watapata wema. Na ardhi ya Mwenyezi Mungu ni pana. Hakika wenye subira watapewa ujira wao bila ya hisabu.
Aya zilizotangulia zimewalinganisha watu wenye ghururi na watovu wa shukurani, mkabala na wale wenye kutubia na wenye kumtii Allah; na vile vile baina ya wajuzi wenye elimu mkabala na wajinga wasiojua kitu. Aya hii ya 10 inaashiria baadhi ya sifa za waja halisi wa Allah, ya kwanza kabisa ikiwa ni taqwa na uchaji Mungu. Kwa mujibu wa aya hii, ucha Mungu ndio alama ya muumini wa kweli. Hali ambayo humfanya mtu aone haya na aibu kufanya maovu na madhambi mbele ya Mola wake na hivyo kujizuia na kujiepusha kufanya vitendo hivyo. Hata hivyo taqwa na uchaji Mungu peke yake hautoshi; inahitajika pia ihsani na matendo mema. Taqwa ni mithili ya breki inayomkinga na kumuepusha mtu na hatari na mitelezo ya kupindukia kwenye lindi la maangamizi; na amali njema ni mithili ya injini imara inayomwezesha mja kupiga hatua na kusonga mbele. Kuwa mwema kwa kauli na matendo ni moja ya masharti ya imani ya kweli juu ya Allah. Kwa hivyo mtu anayedai kuwa ni muumini, lakini akawa si mwema katika kauli na matendo yake, kudai kwake huko hakuna ukweli. Kudai kwa mtu huyo hakukubaliki mbele ya Allah, na wala hatopata thawabu na malipo yoyote mema huko Akhera kwa amali na matendo yake hayo. Baada ya maelezo hayo, aya inaashiria jinsi waumini wa kweli walivyo tayari kuhajiri kwa ajili ya Allah na kuusia kwamba: Kila mtapokabiliwa na matatizo katika mji au mahali popote pale kwa ajili ya kulinda dini na imani zenu, basi hameni mhamie mahali pengine; wala msiruhusu mapenzi na mazoea mliyonayo kwa mji au nchi yenu yaathiri na kuidhuru dini yenu. Ni kama walivyofanya masahaba wa Mtume wenu; kwani walipokabiliwa na misukosuko na mateso, walihajiri Makka wakahamia Madina ili kuepukana na madhila ya washirikina na kuinusuru dini ya Allah. Bila shaka mtu kuhajiri mahali alikozaliwa au alikozoea kuishi na kuhamia mahali pengine huandamana na tabu na matatizo mbali mbali. Kwa sababu hiyo, aya hii inaendelea kueleza kwamba: Watu wanaoonyesha subira na wakavumilia shida na tabu mbali mbali kwa ajili ya Allah, Yeye Mola atawapa thawabu na malipo kamili kwa rehma na ukarimu wake na si kulingana na uzito wa amali zao. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba, imani, ucha Mungu na wema, ni mambo yanayolazimiana; mtu hawezi kufuzu na kuipata saada pasi na matatu yote hayo kujumuika pamoja. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa, kama itamlazimu mtu kuhajiri na kuhama kwao alikozaliwa au mahali anakoishi kwa ajili ya kulinda imani yake, basi itapasa afanye hivyo kwa ajili ya Allah na kuzivumilia shida, tabu na matatizo yatakayotokana na hatua hiyo ili kuweza kupata rehma za Mola. Aidha aya hii inatuelimisha kwamba, malipo ya thawabu yanaendana na jitihada zetu. Chambilecho wahenga, hakuna Pepo ya bure. Kufanya na kuendeleza juhudi humjenga na kumuinua mtu na kumfikisha kwenye daraja za juu mbele ya Allah. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 840 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah azifanye thabiti imani zetu, atusamehe makosa yetu na aufanye mwema mwisho wetu. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/