Sura ya Az-Zumar, aya ya 11-16 (Darsa ya 841)
Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur’ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.
Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur’ani. Hii ni darsa ya 841 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 39 ya Az-Zumar. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 11 hadi 13 za sura hiyo ambazo zinasema:
قُلْ إِنِّي أُمِرْتُ أَنْ أَعْبُدَ اللَّـهَ مُخْلِصًا لَّهُ الدِّينَ
Sema: Hakika mimi nimeamrishwa nimuabudu Mwenyezi Mungu kwa kumsafia Yeye Dini.
وَأُمِرْتُ لِأَنْ أَكُونَ أَوَّلَ الْمُسْلِمِينَ
Na nimeamrishwa niwe wa mwanzo wa Waislamu.
قُلْ إِنِّي أَخَافُ إِنْ عَصَيْتُ رَبِّي عَذَابَ يَوْمٍ عَظِيمٍ
Sema: Hakika mimi ninaogopa adhabu ya Siku Kubwa nikimuasi Mola wangu Mlezi.
Katika darsa iliyopita tulisoma aya zilizozungumzia umuhimu wa taqwa na ucha Mungu, kutenda wema na ihsani na kuwa na subira na uvumilivu, ambazo ni miongoni mwa alama za waumini wa kweli. Aya hizi tulizosoma zinamhutubu Bwana Mtume Muhammad SAW ya kwamba: Ewe Mtume! watangazie kinagaubaga washirikina, kwamba mimi nimeamriwa na Mwenyezi Mungu niitakase dini yake na kila aina ya shirki na niwe ninamuabudu na kumtii Yeye Allah tu; na vile vile nimeamriwa niwe wa mwanzo na wa mbele katika kumuabudu Mola na kujiepusha na mwenendo na amali yoyote ile ya shirki. Kisha aya zinaendelea kusema: Yeyote atakaye halifu amri ya Allah atafikwa na adhabu; na katika hilo hakuna tofauti baina ya Mtume na Waislamu wengine. Kujisalimisha na kutii maamrisho ya Allah ndio njia itakayomuokoa mtu na ghadhabu za Mola duniani na akhera; na katika hili, jukumu la Mtume ni kubwa zaidi kuliko watu wengine. Mitume wote hawakuwa wakijiona kama wana upendeleo wowote ule kulinganisha na watu wengine, bali wakijihisi, kama walivyo watu wengine, ni waja wa Allah na wakijisalimisha na kutii amri zake Mola. Hii yenyewe ni moja ya hoja zinazothibitisha ukweli wa Utume wao; kinyume na Mitume bandia na wa uongo, ambao badala ya kuwalingania watu kumtii Mwenyezi Mungu, walikuwa wakiwataka wawatii wao; na au wao wenyewe kujiwekea upendeleo maalumu. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, Mitume wametumwa kuwafikishia watu ujumbe wa Mwenyezi Mungu. Hawasemi wala hawafanyi chochote kinachotokana na wao wenyewe. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, kuitakasa ibada ya Allah na aina yoyote ile ya fikra na vitendo vya shirki lilikuwa moja ya majukumu muhimu zaidi ya Mitume. Hali kadhalika aya hizi zinatuelimisha kwamba, katika mahakama ya uadilifu ya Allah Siku ya Kiyama hakutakuwa na tofauti baina ya Mitume na watu wengine, wala wao hawatokuwa na upendeleo maalumu.
Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 14 na 15 ambazo zinasema:
قُلِ اللَّـهَ أَعْبُدُ مُخْلِصًا لَّهُ دِينِي
Sema: Mwenyezi Mungu tu ninamuabudu kwa kumsafia Yeye tu Dini yangu.
فَاعْبُدُوا مَا شِئْتُم مِّن دُونِهِ ۗ قُلْ إِنَّ الْخَاسِرِينَ الَّذِينَ خَسِرُوا أَنفُسَهُمْ وَأَهْلِيهِمْ يَوْمَ الْقِيَامَةِ ۗ أَلَا ذَٰلِكَ هُوَ الْخُسْرَانُ الْمُبِينُ
Basi nyinyi abuduni mpendacho badala ya Yeye. Sema: Hakika walio khasirika ni wale walio jikhasiri nafsi zao na ahali zao Siku ya Kiyama. Tambueni kuwa hiyo ndiyo khasara iliyo dhaahiri.
Katika aya zilizotangulia, Bwana Mtume SAW alitakiwa awaambie watu kwamba, mimi nimetumwa niitangaze dini ya Allah kwa ikhlasi na kumwabudu Yeye Mola kwa ikhlasi kamili. Katika aya hizi tulizosoma mtukufu huyo anasema: Katika amali zangu, mimi nimefanya hivyo pia; kwanza ni kwa sababu ni Allah pekee ndiye ninayemwabudu, si yeyote asiyekuwa Yeye. Pili, katika huko kuabudu kwangu, simshirikishi mtu au kitu chochote kile na Yeye. Kisha akawahutubu washirikina kwamba: Mimi nimekulinganieni dini safi na iliyotakasika; sasa kama hamuikubali, abuduni chochote mtakacho, lakini mjue kwamba mnajitia kwenye maharibiko na hasara kubwa. Kwa sababu kwa kumwabudu asiyekuwa Allah, mutakuwa mumejiingiza kwenye hasara kubwa na ya dhahiri, nyinyi wenyewe na familia zenu Siku ya Kiyama. Msidhani kama hasara ya mali ndio hasara kubwa zaidi. Hasara ya kweli ni ile atakayopata mtu huko akhera. Siku ambayo watu waovu wataelewa kwamba, uwezo, vipawa na rasilimali zote walizojaaliwa wamezipoteza bure; kwani badala ya kuzitumia kwa ajili ya kufikia ukamilifu wa kiutu na kupata saada na fanaka ya milele, hawakuchuma na kuambulia chochote zaidi ya hasara. Isitoshe, wakati huo hakutakuwa na njia yoyote ya mtu kufidia makosa aliyofanya huko nyuma. Hiyo ni hasara ya dhahiri kabisa. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, Mitume walikuwa wa mbele katika kutekeleza maamrisho ya Allah. Kabla ya wafuasi wao, wao walikuwa wa mwanzo katika kutekeleza amri za Mola, tena kwa ujudi wao wote. Katu hawakuwa walinganiaji tu wa haki kwa watu, kisha wao wenyewe wakawa si watekelezaji wa kile wanachokilingania. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, moja ya majukumu muhimu zaidi ya Mitume ni kuitakasa na kuisafisha dini ya Allah ni kila aina ya shirki, khurafa, uzushi na upotofu. Kwa sababu yote hayo ni mambo yenye madhara makubwa kwa dini. Vile vile tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba, Mitume wameamrishwa kufikisha ujumbe wa dini ya Mwenyezi Mungu kwa watu wote, lakini wanajua kama kundi miongoni mwa watu hawatayakubali maneno yao ya haki. Lakini pamoja na hayo hawajuti wala hawakati tamaa, bali wanaendelea kufanya kazi waliyopewa na Mola wao. Wa aidha aya hizi zinatutaka tufahamu kwamba, mwanadamu ana dhima si kwa nafsi yake mwenyewe tu, bali pia kwa familia yake. Kuwalea watoto kwa mujibu wa mafunzo na thamani za kidini ni moja ya majukumu ya wazazi katika familia.
Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 16 ambayo inasema:
لَهُم مِّن فَوْقِهِمْ ظُلَلٌ مِّنَ النَّارِ وَمِن تَحْتِهِمْ ظُلَلٌ ۚ ذَٰلِكَ يُخَوِّفُ اللَّـهُ بِهِ عِبَادَهُ ۚ يَا عِبَادِ فَاتَّقُونِ
Yataweka juu yao mat’abaka ya Moto, na chini yao mat’abaka. Kwa hayo Mwenyezi Mungu anawakhofisha waja wake. Enyi waja wangu! Nicheni Mimi!
Aya hii inabainisha hali ya watu watakaopata hasara ya kweli Siku ya Kiyama na kueleza kwamba: Mienge ya moto itawazunguka watu hao kila upande na hawatakuwa na popote pa kukimbilia. Hili kwa hakika ni onyo na indhari kwa watu wote, kwamba ikiwa hapa duniani hawatashika njia ya taqwa na kumcha Mwenyezi Mungu, wanaweza kufikwa na hatima hiyo chungu Siku ya Kiyama. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba, shirki na ukafiri na kumsahau Allah humletea mtu maafa na maangamizi. Mtu anayehitari kufuata njia ya shirki na ukafiri hapa duniani, huko akhera atapatwa na adhabu na ghadhabu za Allah zitakazokuwa katika sura ya moto mkali wenye kuhilikisha, utakaomzunguka na kumvaa kila upande. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa, njia pekee ya kuepukana na adhabu ya Moto ni kumcha Allah na kujiepusha na madhambi. Dhambi ni mitihili ya mada inayozalisha moto; kwa hivyo ni kwa kuipeuka mada hiyo tu ndipo tutaweza kuuzuia kuwaka Moto wa Jahanamu. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 841 ya Qur’ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atupe mema duniani, na atupe mema akhera na atulinde na adhabu ya Moto. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/