May 22, 2023 08:25 UTC

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur’ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.

Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur’ani. Hii ni darsa ya 843 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 39 ya Az-Zumar. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 22 ya sura hiyo ambayo inasema:

أَفَمَن شَرَحَ اللَّـهُ صَدْرَهُ لِلْإِسْلَامِ فَهُوَ عَلَىٰ نُورٍ مِّن رَّبِّهِ ۚ فَوَيْلٌ لِّلْقَاسِيَةِ قُلُوبُهُم مِّن ذِكْرِ اللَّـهِ ۚ أُولَـٰئِكَ فِي ضَلَالٍ مُّبِينٍ

Je, yule ambaye Mwenyezi Mungu amemfungulia kifua chake kwa Uislamu, na akawa yuko kwenye nuru itokayo kwa Mola wake Mlezi (ni sawa na mwenye moyo mgumu?) Basi ole wao wenye nyoyo ngumu zisio mkumbuka Mwenyezi Mungu! Hao wamo katika upotofu wa dhaahiri.

Qur'ani na wahyi wa mbinguni ni mithili ya matone ya mvua yanayodondoka juu ya ardhi ya nyoyo za watu. Kama ambavyo ni ardhi zenye rutuba tu na utayari wa kulainishwa na maji ya mvua ndizo zinazonufaika na matone ya uhai ya mvua, vivyo hivyo ni nyoyo zenye utayari tu wa kinafsi na zilizorehemewa na Mola ndizo zinazonufaika na aya za Kitabu kitukufu cha Allah cha Qur'ani. Watu wote hawana hali na misimamo sawa katika kuikubali haki. Qur'ani imewataja baadhi yao kuwa ni watu wenye vifua vipana na ukunjufu wa nafsi na baadhi yao ni wenye nyoyo ngumu zilizojikunja. Aya inazungumzia athari ya imani juu ya Allah katika maisha ya mtu na kueleza kwamba: Kuuwekea mpaka ulimwengu kwa upande mmoja tu wa kimaada huufinya uono na mtazamo wa mtu juu ya maisha na pande zake tofauti. Mtu anayemkanusha Mwenyezi Mungu huiona saada na fanaka yake iko kwenye raha za kimaada na manufaa ya kidunia tu; na kwa sababu hiyo roho yake huwa imefinyika na kudhikika. Lakini mtu anayemwamini Mwenyezi Mungu na ambaye huwa na imani juu ya ulimwengu wa ghaibu huiona dunia kuwa ni utangulizi wa maisha ya akhera; na roho yake huwa na uwezo na ukunjufu wa kiwango cha juu. Kumwamini Allah kunapanua uwezo wa mtu na kufungua upeo wa uono wake. Upeo wa uono wa mtu kama huyo haukomei kwenye umri wa miaka 70 au 80 unaomalizika kwa kifo, bali yeye huuona mbele yake ulimwengu wa milele na usio na mwisho wa baada ya kifo. Roho ya mtu kama huyo huwa pana na iliyokunjuka na huzinduka na kutanabahi inapopata ishara ndogo tu ya mawaidha na ukumbusho. Anapotingwa na giza totoro la matatizo na misukosuko ya dunia, mwanga wa nuru inayomwangazia kutoka kwenye Kitabu cha Mwenyezi Mungu, humuonyesha njia sahihi ya kutokea na kuufuata mkondo wa maisha kwa salama na amani. Mkabala na kundi hili, kuna watu ambao hata mawaidha makubwa kabisa au hoja nzito kabisa, haziwi na taathira yoyote kwao. Roho na fikra za watu hao zimefinyika; ni dhahiri kuwa hamna nafasi yoyote iliyosalia ndani ya nafsi zao ya kuipokea haki na ukweli. Hao ni watu wenye nyoyo yabisi zisizo na nuru kutokana na kukosekana uongofu wa Allah ndani ya mioyo yao. Lakini ni wazi pia kwamba, watu wamkanushao au wanaomsahau Mwenyezi Mungu huwa daima wamo katika hali ya tafrani, hofu na wasiwasi, kwa sababu mauti kwao wao, yana maana ya mwisho wa kila kitu chao. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba, athari ya imani juu ya Allah humfanya mtu awe na kifua kipana na kuongeza upeo wa uoni wake. Imani inazidisha uwezo wa mtu; na mtu muumini, daima hutii na kusalimu amri mbele ya haki. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa, mtu muumini huweza kuyakata masafa ya njia ngumu ya maisha yenye misitu na nyika kwa mwanga wa nuru ya Allah, na kuivuka hatari ya kuteleza na kuporomokea kwenye lindi la maangamizi na maharibiko ya maisha. Halikadhalika aya hii inatufunza kwamba, shirki, ukafiri na kuikadhibisha haki huufanya moyo uwe mgumu na yabisi. Na uyabisi wa moyo huzuia nuru ya Allah kupenya ndani yake, na matokeo yake ni mtu kuselelea kwenye giza la dhalala na upotofu.

Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 23 ambayo inasema:

اللَّـهُ نَزَّلَ أَحْسَنَ الْحَدِيثِ كِتَابًا مُّتَشَابِهًا مَّثَانِيَ تَقْشَعِرُّ مِنْهُ جُلُودُ الَّذِينَ يَخْشَوْنَ رَبَّهُمْ ثُمَّ تَلِينُ جُلُودُهُمْ وَقُلُوبُهُمْ إِلَىٰ ذِكْرِ اللَّـهِ ۚ ذَٰلِكَ هُدَى اللَّـهِ يَهْدِي بِهِ مَن يَشَاءُ ۚ وَمَن يُضْلِلِ اللَّـهُ فَمَا لَهُ مِنْ هَادٍ

Mwenyezi Mungu ameteremsha hadithi nzuri kabisa, Kitabu chenye kufanana na kukaririwa; husisimka kwacho ngozi za wenye kumkhofu Mola wao Mlezi. Kisha ngozi zao na nyoyo zao hulainika kwa kumkumbuka Mwenyezi Mungu. Huo ndio uwongofu wa Mwenyezi Mungu, na kwa huo humwongoa amtakaye. Na ambaye ameachwa na Mwenyezi Mungu kupotea, basi hapana wa kumwongoa.

Aya hii inaendeleza maudhui ya aya iliyotangulia kwa kuashiria kwanza sifa kadhaa maalumu za Qur'ani tukufu na kisha inafanya ulinganishaji kati ya waumini na makafiri kama ilivyofanywa na aya zilizotangulia. Aya za Qur'ani hazikinzani na wala hakuna aya yoyote yenye mgongano na aya nyingine. Kwa hiyo kuna mshabaha na mlingano baina yao. Kama ambavyo Muumba na muumbwaji hawawezi kulinganishwa, maneno ya Muumba pia hayawezi kulinganishwa na maneno ya kiumbe wake; na Qur'ani ni maneno ya Muumba na ndio maneno bora kabisa. Maneno ya Allah SW ndani ya Qur'ani yanafuata mtindo maalumu na wa aina ya pekee unaoyapambanua na kuyatafautisha na maneno mengineyo hata ya Bwana Mtume SAW. Japokuwa Qur'ani iliteremshwa kupitia Nabii huyo wa rehma, na Waislamu waliisikia kupitia kinywa chake kitukufu, lakini kuna tofauti kubwa mno baina ya aya za Qur'ani na Hadithi za Bwana Mtume zilizokusanywa kwenye vitabu vya Hadithi. Japokuwa aya zote za Qur'ani zinafanana kwa namna fulani na zinasimamia ghaya na lengo moja, lakini mara nyingi mbinu inayotumiwa na kitabu hicho cha mbinguni huwa ni ya kulinganisha na kuzungumzia hali mbili kinzani za maudhui moja. Yaani kwa kutumia kanuni isemayo: Kila kitu hufahamika kwa kilicho kinyume chake, Qur'ani tukufu hutumia mbinu ya kuyalinganisha mafundisho ya haki yenye mantiki na hoja madhubuti na hoja dhaifu na zisizo na msingi za batili. Qur'ani aidha inatanabahisha juu ya matokeo ya kuchagua njia ya haki au batili ili kwa kutambua na kulinganisha njia zote hizo mbili, watu wachague kwa hiari yao njia bora ya kufuata. Kwa mfano, baadhi ya aya zinazungumzia imani na waumini, na baadhi zinazungumzia ukafiri na waliokufuru. Baadhi ya aya zinahusu malipo ya thawabu atakayopata mtu na baadhi zinabainisha adhabu na ikabu itakayompata kwa kuasi na kutofuata haki. Sehemu moja ya aya za kitabu hicho zinabainisha ya halali na wajibu, na sehemu nyingine inahusu ya haramu na yaliyokatazwa kufanya. Aidha baadhi ya aya zinazungumzia uongofu na njia za kuufikia, na baadhi yao zinauelezea upotofu na mambo yanayomsababishia mtu kuufuata. Kwa kutumia mbinu hiyo ya ulinganishaji, Qur'ani tukufu inawatia watu hamu na raghaba ya kupima uhasi na uchanya, na ubaya na uzuri wa kila kitu, kisha kuchagua njia bora ya kufuata. Nukta nyingine ni kwamba, watu waumini huwa na hali mbili za hofu na matumaini kwa wakati mmoja. Wanapoutazama udhaifu wao, makosa wayafanyayo na upungufu wao, hujawa na woga na hofu ya kuchelea adhabu ya Allah, lakini wakati huo huo wanapofikiria uraufu na ukarimu wa Mola wao, nyoyo zao hupata utulivu kwa sababu huwa wanatumai kupata maghufira na rehma zake. Hakuna shaka kuwa, aya za Qur'ani zimeteremshwa kwa ajili ya watu wote. Lakini ni wale tu walio tayari kuikubali haki ndio wanaonufaika na uongofu wake; lakini wale wanaoikana haki wanaukosa uongofu wa kitabu hicho na kuishia kwenye dhalala na upotofu. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba, Qur'ani ndiyo maneno bora na mema zaidi kuliko maneno mengine yoyote yale. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa, aya za Qur'ani hazikinzani, bali zote zina ghaya na lengo moja. Wa aidha aya hii inatuelimisha kwamba, wakati waumini wanaposoma aya za adhabu hujawa na hofu na wanaposoma aya za rehma hupata matumaini. Vile vile aya hii inatufunza kuwa, Mwenyezi Mungu amewawekea watu wote sababu za kuufikia uongofu na wala Qur'ani haikuteremshwa kwa ajili ya kuwaongoza watu maalumu. Ni kitabu cha uongofu kwa watu wote, lakini ni wale wanaoitafuta haki tu ndio wanaonufaika na nuru ya uongofu wake. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 843 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atujaalie kuwa wenye kuisoma na kuifahamu Qur'ani na kuifanya kuwa katiba na muongozo wa kuufuata kivitendo katika maisha yetu ya kila siku. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.../