May 22, 2023 08:31 UTC

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur’ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.

Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur’ani. Hii ni darsa ya 844 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 39 ya Az-Zumar. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 24 ya sura hiyo ambayo inasema:

أَفَمَن يَتَّقِي بِوَجْهِهِ سُوءَ الْعَذَابِ يَوْمَ الْقِيَامَةِ ۚ وَقِيلَ لِلظَّالِمِينَ ذُوقُوا مَا كُنتُمْ تَكْسِبُونَ

Je! Atakaye kuwa anapambana kwa uso wake na adhabu mbaya kabisa Siku ya Kiyama (ni sawa na watenda wema?) Na wataambiwa wenye kudhulumu: Onjeni hayo mliyo kuwa mkiyachuma!

Aya ya mwisho tuliyosoma katika darsa iliyopita ilizungumzia makundi mawili ya watu walioongoka na waliopotoka. Aya hii inaendeleza maudhui hiyo pia kwa kuyalinganisha makundi hayo mawili na kubainisha hatima yao itakavyokuwa Siku ya Kiyama. Aya inauliza: Je, mtu itakayembidi aikabili kwa uso wake adhabu kali yenye kuumiza ya Allah, atakuwa sawa na mtu ambaye siku hiyo atakuwa kwenye upeo wa raha na amani?! Siku hiyo hali ya madhalimu watakaoadhibiwa motoni itakuwa ya kuumiza na kusononesha mpaka itawabidi waikabili adhabu kwa nyuso zao, kwa sababu mikono na miguu yao itakuwa imefungwa kwa pingu na minyororo. Japokuwa huko motoni viungo vyote vya mtu muovu vitakuwa vinaungua, lakini kutajwa uso peke yake kumefanywa kutokana na umuhimu na nafasi yake maalumu katika viungo vya mwili, ikiwa ni pamoja na kwamba kuwatambua watu huwa kunafanyika kwa kutumia sura zao. Isitoshe, kuungua uso ni hasasi zaidi na ni vigumu zaidi kuliko viungo vingine vya mwili. Aya hii haisemi: Onjeni adhabu ya amali, bali inasema: Onjeni amali zenu. Ni sawa na anavyokemewa mpishi aliyepika chakula kibaya kisichoweza kulika anapoambiwa: Onja wewe mwenyewe ujue ulichokipika! Kuziona amali kama zilivyo Siku ya Kiyama, ndicho kitu kinachotajwa katika istilahi za kidini kama kudhihiri kwa sura ya amali. Maana yake ni mtu kuja kuona Siku ya Kiyama sura halisi ya amali zake na kuonja ladha ya uovu huo; na si kwamba Allah atampa adhabu iliyo mbali na tofauti na amali zenyewe alizofanya. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba, adhabu ya moto ni matokeo ya amali za mtu hapa duniani, ambazo zinajidhihirisha kwa sura ya moto wenye kuteketeza huko akhera. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa Siku ya Kiyama, mtu atazishuhudia amali alizofanya hapa duniani.

Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 25 na 26 ambazo zinasema:

كَذَّبَ الَّذِينَ مِن قَبْلِهِمْ فَأَتَاهُمُ الْعَذَابُ مِنْ حَيْثُ لَا يَشْعُرُونَ

Walio kuwa kabla yao walikadhibisha, na ikawajia adhabu kutoka pahala wasipo patambua.

فَأَذَاقَهُمُ اللَّـهُ الْخِزْيَ فِي الْحَيَاةِ الدُّنْيَا ۖ وَلَعَذَابُ الْآخِرَةِ أَكْبَرُ ۚ لَوْ كَانُوا يَعْلَمُونَ

Basi Mwenyezi Mungu akawaonjesha hizaya katika uhai wa duniani. Na bila ya shaka adhabu ya Akhera ni kubwa zaidi; laiti wangeli jua!

Aya hii inazungumzia hali ya makafiri duniani na kueleza kwamba: Katika zama zote za historia, watu waliowakadhibisha Mitume na mafundisho ya mbinguni waliyokuja nayo, walishushiwa adhabu na Mwenyezi Mungu hata hapa duniani pia. Iwe ni wale walioionja adhabu hiyo kwa kuiona kama ilivyo, au wale iliowapata kwa athari zake zisizo za kimaada. Inafaa tufafanue hapa kwamba, baadhi ya adhabu ni za kuhilikisha mwili, kama adhabu zilizoteremshwa kwa kaumu za Manabii Nuh na Lut (as) na kwa watu kama Firauni na Qaruni; lakini baadhi ya adhabu ni za mateso ya kiroho na kinafsi kwa watu. Kwa mfano, pamoja na suhula zote zilizoko katika jamii zilizoendelea za zama hizi, msongo wa mawazo ni moja ya maradhi yaliyozagaa kwa watu wa jamii hizo. Sababu ni kuwa, mtu anayejitenga na Mwenyezi Mungu na umaanawi, hakuna kitu chochote kile kinachoweza kumtosheleza na kumkinaisha katika dunia hii; na kwa hiyo baada ya muda fulani hupatwa na msongo wa mawazo. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, sehemu moja ya taathira za matendo ya watu waovu hudhihiri hapa duniani, na sehemu nyingine itadhihiri huko akhera. Vile vile baadhi ya adhabu zina sura ya kimwili na baadhi yao zina taathira ya kiroho na kinafsi. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, hata kama baadhi ya adhabu hudhihiri papa hapa duniani, lakini adhabu ya akhera ni kubwa zaidi, ina ukali mkubwa zaidi na ya kudumu kwa muda mrefu zaidi. Wa aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba, Allah SW ana hiari ya kuwapa adhabu atakavyo waovu na madhalimu; na anaweza kuwaadhibu kwa njia wasiyoifikiria na kwa namna wasiyoitarajia.

Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 27 na 28 ambazo zinasema:

وَلَقَدْ ضَرَبْنَا لِلنَّاسِ فِي هَـٰذَا الْقُرْآنِ مِن كُلِّ مَثَلٍ لَّعَلَّهُمْ يَتَذَكَّرُونَ

Na hakika tumewapigia watu mifano ya kila namna katika hii Qur'ani ili wapate kukumbuka.

قُرْآنًا عَرَبِيًّا غَيْرَ ذِي عِوَجٍ لَّعَلَّهُمْ يَتَّقُونَ

Qur'ani ya Kiarabu isiyo na upogo, ili wamche Mungu.

Aya hizi zinagusia tena maudhui ya sifa maalumu za Qur'ani tukufu na kukamilika kwa kitabu hicho cha mbinguni katika mambo yote kwa kusema: Qur'ani hii, ambayo lengo lake ni kuwaelekeza watu kwenye uongofu, imetaja ndani yake kila linalofanikisha kuwafikisha watu kwenye saada na fanaka. Kwa hakika Qur'ani ni nuru ya uongofu inayong'ara muda wote na kuwaonyesha watu njia sahihi ya kufuata. Kuutambua mfumo wa uumbaji na kuzingatia siri na maajabu yake, sharia wadhiha na madhubuti za kuwezesha kufuata kwa usahihi njia ya maisha, maisha yaliyotukuka ya waja wema na mwisho mbaya wa waovu na madhalimu, ulimwengu wa baada ya kifo na mahakama kuu ya Siku ya Kiyama, hayo na mengineyo ambayo mwanadamu anayahitajia kwa ajili ya kufuzu na kupata saada ya duniani na akhera yametajwa kwa mifano hai ndani ya kitabu hicho ili watu wapate kuzinduka na kutoka kwenye usingizi wa mghafala. Kisha aya zinaielezea Qur'ani kwa kusema, lugha ya kitabu hicho ni wadhiha na ya ufasaha, aya zake zina urari na ulinganifu, na tafsiri yake ni safi na iko wazi kabisa. Hamna upogo au upotofu ndani yake, wala mgongano na mkinzano katika muhtawa na maelezo yake. Katika hitimisho la maelezo haya inapasa tuseme kwamba, pamoja na yote yaliyobainishwa kuhusu sifa maalumu za kitabu hicho, lengo la kuteremshwa Qur'ani ni kuwafanya watu wamche Mwenyezi Mungu na kuacha madhambi na matendo maovu. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, Qur'ani ni kitabu kilichokamilika na kinachojumuisha kila kitu. Kimekusanya ndani yake pasi na kubakisha chochote kile katika yanayohitajiwa na wanadamu. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, baadhi ya wakati, lugha ya kumithilisha na kushabihisha huwa na taathira zaidi kwa watu kuliko ya utumiaji hoja. Kwa sababu hiyo, kwa ajili ya kuwaaidhi watu, Qur'ani tukufu imetumia sana lugha ya kumithilisha na ya upigaji mifano. Halikadhalika tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba, lugha iliyotumiwa na Qur'ani ni wadhiha, ya fasaha na nyepesi kufahamika. Ni kitabu kilichotakasika na upotofu, upogo au mgongano wa aina yoyote ile. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 844 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atusamehe makosa yetu, atakabali dua zetu na aufanye mwema mwisho wetu. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/