Sura ya Az-Zumar, aya ya 29-32 (Darsa ya 845)
Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur’ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.
Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur’ani. Hii ni darsa ya 845 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 39 ya Az-Zumar. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 29 ya sura hiyo ambayo inasema:
ضَرَبَ اللَّـهُ مَثَلًا رَّجُلًا فِيهِ شُرَكَاءُ مُتَشَاكِسُونَ وَرَجُلًا سَلَمًا لِّرَجُلٍ هَلْ يَسْتَوِيَانِ مَثَلًا ۚ الْحَمْدُ لِلَّـهِ ۚ بَلْ أَكْثَرُهُمْ لَا يَعْلَمُونَ
Mwenyezi Mungu amepiga mfano wa mtu mwenye mabwana washirika wanao hitalifiana, na wa mtu mwengine aliye khusika na bwana mmoja tu. Je! Wako sawa katika hali zao? Alhamdulillahi, Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu! Lakini wengi wao hawajui.
Katika aya ya 27 sura hii ya Az-Zumar tuliyosoma katika darsa iliyopita, Allah SW amesema, amepiga mifano ya kila namna ndani ya Qur'ani ili watu wapate kukumbuka. Aya tuliyosoma ya 29 imetumia lugha ya mifano ya umithilishaji ili kubainisha taswira ya washirikina na hali ya fazaa na ubabaikaji waliyonayo. Aya inasema: Chukulia mfano wa mtumwa mwenye mabwana kadhaa ambao kila mmoja wao anatoa amri yake kwa mtumwa huyo. Mmoja anamwambia: Fanya hili na mwingine anamkataza jambo hilo hilo kwa kumwambia usifanye. Mtumwa huyo hubabaika na kuhamanika akijiuliza, atekeleze amri na katazo la yupi kati ya mabwana zake hao? Kwani akipuuza kutekeleza amri ya yeyote kati yao ataadabishwa na kuadhibiwa na bwana aliyemuasi, na kunyimwa chakula, nguo na mahitaji yake mengine ya maisha. Lakini mkabala na mtumwa huyo, aya inaashiria pia mtumwa mwingine ambaye ana bwana mmoja tu na hana wajibu na jukumu jengine isipokuwa kumtii bwana wake huyo. Ni wazi kwamba mtumwa huyo hatokuwa na hamaniko wala hatobabaika hata chembe katika ufanyaji mambo; na daima atakuwa anaridhiwa na bwana wake na kutimiziwa mahitaji yake yanayopasa kutimizwa. Wakati Nabii Yusuf (as) alipokuwako jela, naye pia alitumia umithilishaji unaofanana na wa aya tuliyosoma kwa ajili ya kuwalingania tauhidi wafungwa wenzake alipowaambia, kama aya ya 39 ya Suratu-Yusuf inavyosema: Enyi wafungwa wenzangu wawili! Je, mabwana wengi wanao farikiana wao kwa wao ni bora au Mwenyezi Mungu Mmoja Mwenye nguvu? Naam! Hivi ndivyo ilivyo hali ya washirikina na wampwekeshao Allah SW. Shirki humfanya mtu ababaike na kuhamanika na kumnyima umakinifu na utulivu wa ndani ya nafsi. Lakini mtu ampwekeshaye Allah, huwa anamtii na kumfuata Mungu mmoja tu; na matumaini yake yote anayaelekeza kwenye rehma za Mola huyo pekee. Bila shaka na inasikitisha kwamba, watu wengi huwa wanajisahau kwa kutozingatia hata chembe tofauti ya shirki na tauhidi katika maisha yao. Badala ya kujitenga na kujiweka mbali na mambo ya shirki na kuelekea kwenye tauhidi halisi, kila siku huelekeza matumaini na matarajio yao kwa mtu fulani au kitu fulani. Huwa kwa hakika ni mateka na watumwa wa huyu na yule au hiki na kile wanachokikumbatia kwa ujudi wao wote. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba, katika mambo yake yote, mtu wa tauhidi huwa anafikiria kufanya yale tu yatakayompatia radhi za Allah SW, lakini mtu mushriki anafikiria jinsi ya kuwaridhisha watu kadhaa, wakati kuwaridhisha wote hao ni jambo lisiloyumkinika, kwa sababu matashi na matakwa ya watu huwa yanatafautiana sana. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa, athari za shirki na tauhidi hazihusiani na Siku ya Kiyama tu. Kama tutalinganisha, hata hapa duniani pia tutaona kuwa, watu wa tauhidi wana maisha ya utulivu na ya matumaini makubwa, lakini mushirikina wanaishi kwa hofu, wasiwasi na tafrani.
Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 30 na 31 ambazo zinasema:
إِنَّكَ مَيِّتٌ وَإِنَّهُم مَّيِّتُونَ
Kwa hakika wewe utakufa, na wao watakufa.
ثُمَّ إِنَّكُمْ يَوْمَ الْقِيَامَةِ عِندَ رَبِّكُمْ تَخْتَصِمُونَ
Kisha hakika mtagombana Siku ya Kiyama mbele ya Mola wenu Mlezi.
Mwisho wa maisha ya makundi yote mawili ya wanaompwekesha na wanaomshirikisha Allah ni kifo; na hakuna mwanadamu yeyote atakayeishi milele hapa duniani. Hata Mitume, ambao ni waja wateule wa Mwenyezi Mungu hawatafautishwi na wanadamu wengine katika kanuni hii aliyoiweka Mola. Ikiwa maadui wa Bwana Mtume wanakaa kwa matarajio ya kushuhudia mauti yake, aya inasema, wajue kwamba na wao pia watakufa. Ni kama inavyolibainisha hilo kwa njia ya suali sehemu ya mwisho ya aya ya 34 ya Suratul-Anbiyaa inaposema: Basi je! Ukifa wewe (Mtume), wao wataishi milele? Lakini kifo si mwisho wa maisha ya mwanadamu, bali na mlango wa kuingilia ulimwengu wa milele wa akhera. Siku ya Kiyama na baada ya kufufuliwa viumbe, waumini na washirikina watakabiliana na kujadiliana kuhusu ukweli na uongo na kuwa haki na batili imani na itikadi zao. Ni kana kwamba washirikina watakuwa hawajawa tayari kukubali kwamba, fikra na itikadi zao zilikuwa batili, kwa hiyo watataka kuzitetea na kuzikingia kifua. Hata hivyo hautapita muda ila Allah SW atahukumu baina yao na kuainisha hatima ya kila mmoja wao. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, mauti ni kaida na utaratibu aliowahukumia Allah wanadamu wote, na hakuna mtu yeyote anayesameheka na hukumu hiyo. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, katika mahakama ya Siku ya Kiyama, makundi mbali mbali ya watu yatashutumiana, huku kila mmoja akijaribu kujitoa hatiani yeye mwenyewe na kumtia hatiani mwenzake, lakini hakimu wa mahakama ya siku hiyo ni Allah SW aliye na ujuzi, uwezo na uadilifu mutlaki na atahukumu baina ya watu kwa haki na uadilifu.
Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 32 ambayo inasema:
فَمَنْ أَظْلَمُ مِمَّن كَذَبَ عَلَى اللَّـهِ وَكَذَّبَ بِالصِّدْقِ إِذْ جَاءَهُ ۚ أَلَيْسَ فِي جَهَنَّمَ مَثْوًى لِّلْكَافِرِينَ
Basi ni nani dhaalimu mkubwa zaidi kuliko yule aliye msingizia uwongo Mwenyezi Mungu na kuikadhibisha kweli imfikiapo? Je! Siyo katika Jahannamu makazi ya hao makafiri?
Aya hii inaendeleza maudhui ya aya iliyotangulia kuhusu kuhudhurishwa watu wote katika mahakama ya Siku ya Kiyama kwa kuashiria kundi moja la watu waliokadhibisha wito wa haki waliofikishiwa na Mwenyezi Mungu na wakakataa kuufuata. Watu wasio na imani kabisa ambao wanakanusha kuwepo kwa Mwenyezi Mungu au washirikina, ambao kutokana na itikadi zao zilizochanganyika na shirki wanamnasibishia Allah mambo yasiyostahiki, wote hao wameyakadhibisha maneno ya haki ya Mola wao na kuyaitakidi kuwa ni uongo. Ni wazi kwamba matendo maovu na potofu ya watu hao wanayofanya duniani yatasababisha waingizwe motoni huko akhera. Lakini kinyume na wakadhibishaji hao, kuna waja waumini, ambao wao wameyasadikisha maneno ya haki ya Mola wao. In shaa Allah tutakuja kulizungumzia kundi la watu hao katika darsa yetu ijayo. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba, dhulma kwa fikra na utamaduni wa jamii ni kubwa zaidi kuliko hata dhulma ya kiuchumi na kijamii. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa, inadi, ubishi, ukaidi na taasubi zisizo na maana ni miongoni mwa mambo yanayomfanya mtu akabiliane na haki na kuamua kuyakanusha na kuyakataa maneno anayoambiwa bila hata kutafakari kwanza kama ni sahihi au la. Wapenzi wasikilizaji, darasa ya 845 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atuonyeshe haki na atupe taufiki ya kuifuata na atuonyeshe batili na atuwezeshe kuiepuka. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/