Sura ya Az-Zumar, aya ya 33-37 (Darsa ya 846)
Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur’ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.
Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur’ani. Hii ni darsa ya 846 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 39 ya Az-Zumar. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 33 na 34 za sura hiyo ambazo zinasema:
وَالَّذِي جَاءَ بِالصِّدْقِ وَصَدَّقَ بِهِ ۙ أُولَـٰئِكَ هُمُ الْمُتَّقُونَ
Na aliye ileta Kweli na akaisadikisha - hao ndio wachamngu.
لَهُم مَّا يَشَاءُونَ عِندَ رَبِّهِمْ ۚ ذَٰلِكَ جَزَاءُ الْمُحْسِنِينَ
Watapata watakacho taka kwa Mola wao Mlezi. Hayo ndiyo malipo ya watendao mema.
Watu Siku ya Kiyama watagawika makundi mawili: Watu wa tauhidi waliompwekesha Allah na mushirikina, waliomshirikisha Mola wao. Katika darsa iliyopita tulisoma aya iliyoashiria hatima ya washirikina, ambao inadi, ukaidi na kuipiga vita kwao haki vitawafanya waingizwe motoni. Aya hizi zinawazungumzia watu wa tauhidi kwa kusema: Wao waliisikia haki na ukweli wakaumini na kufikia daraja ya taqwa na uchaMungu. Hao ni watu ambao, wanayaamini ndani ya nyoyo zao maneno ya Allah, na katika kauli na matendo yao ni wafanyaji tablighi ya dini na watekelezaji wa kweli wa mafundisho yake. Watu wa aina hii hujitakasa na kila aina ya unafiki, ria na ufanyaji mambo kwa kujionyesha. Kinyume na mushirikina, ambao mwishowe wataishia kwenye adhabu ya moto wa Jahanamu, hatima ya waumini wa kweli ni kwenda kuishi kwenye Pepo ya milele. Huko watakuwa wameandaliwa na Mola chochote zitakachotamani nafsi zao, iwe ni vitu vya kufurahisha na kuburudisha vya kimaada au hadhi, raha na daraja za kimaanawi. Bila shaka waumini halisi ni wafanyaji amali njema na wenye kuwatendea wenzao wema na ihsani; na watapewa malipo mema hayo kutokana na imani zinazoambatana na matendo. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, ukweli katika kauli na matendo ni sharti la kwanza la imani juu ya Allah; kwani kusema uongo hakuendani na dhati ya imani. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, tablighi huwa na matunda na athari pale mfikishaji wa wito huo wa dini anapokuwa mtekelezaji wa anayoyalingania, vyenginevyo yumkini hata ikawa na matokeo hasi na mabaya. Aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba, neema na fadhila za Allah za huko peponi hazitakuwa na kikomo wala mpaka wowote bali zitafuata irada na matakwa ya watu wenyewe wa peponi. Halikadhalika tunajifunza kutokana na aya hizi kuwa, uchaMungu na kutenda wema ni misamiati miwili iliyotumiwa ndani ya Qur'ani, yenye kukamilishana.
Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 35 ambayo inasema:
لِيُكَفِّرَ اللَّـهُ عَنْهُمْ أَسْوَأَ الَّذِي عَمِلُوا وَيَجْزِيَهُمْ أَجْرَهُم بِأَحْسَنِ الَّذِي كَانُوا يَعْمَلُونَ
Ili Mwenyezi Mungu awafutie uovu zaidi walio ufanya na awalipe ujira wao kwa wema zaidi ya walio kuwa wakiutenda.
Moja ya maombi ya waja wema na wamchao Mungu kwa Mola Mwenye Enzi aliyetukuka ni kuwaghufiria na kuwasamehe mabaya waliyotenda na kuwalipa thawabu kutokana na amali zilizo njema zaidi walizofanya. Naye Allah SW anawatakabalia ombi lao hilo kwa kuwasamehe madhambi waliyofanya na kuwapa malipo bora kwa mema waliyotenda. Inafaa tubainishe hapa kwamba, kuwa na taqwa au uchaMungu maana yake si kuwa na umaasumu, ambao humkinga na kumuepusha mtu mchaji Mungu na kuteleza kwa namna yoyote ile akafanya dhambi, bali ni sifa na hali inayomfanya mtu asiyaendee madhambi na maasi na hata kujizuia na kujiepusha na mambo yanayomfanya aikaribie dhambi. Lakini pamoja na hayo, upo uwezekano wa mtu kama huyo kuteleza akafanya dhambi bila kupenda. Hakika ya taqwa ni mithili ya ngao anayobeba mpiganaji vita ili kujikinga na dhoruba ya mishale anayovurumishiwa na maadui; lakini kama tujuavyo si hasha baadhi ya mishale ikapenya kwenye ngao hiyo na kumchoma mwilini. Muhimu ni kwamba mpiganaji anapokuwa na ngao yake mkononi, huwa na hadhari muda wote na hujiweka tayari kukabili shambulio la adui. Lakini kama tujuavyo si hasha baadhi ya watu wakaamua kuiweka kando ngao ya taqwa na kuamua kufuata matamanio ya nafsi na wasiwasi wa shetani. Lakini rehma na fadhila kubwa za Allah zinawashukia waja wamchao Yeye Mola; na kutokana na juhudi wanazofanya za kujiepusha na madhambi, pale wanapoteleza wakatenda dhambi bila ya kupenda Allah huwasamehe; na katika thawabu wanazopata huwalipa malipo bora zaidi ya amali walizofanya; kwa sababu nia za kutenda mema za waja hao, siku zote huwa kubwa zaidi ya mema yenyewe wanayofanikiwa kuyafanya. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba, lenye umuhimu wa kwanza ni nia, kusudio na lengo la mtu. Yaani kama atajitahidi kujiepusha na dhambi, Mwenyezi Mungu atafumbia macho maovu yake na kumpa malipo bora kabisa kwa mema aliyoyafanya. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa, kujitakasa na madhambi na athari zake mbaya ni utangulizi wa kupata fadhila na rehma za Allah.
Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 36 na 37 ambazo zinasema:
أَلَيْسَ اللَّـهُ بِكَافٍ عَبْدَهُ ۖ وَيُخَوِّفُونَكَ بِالَّذِينَ مِن دُونِهِ ۚ وَمَن يُضْلِلِ اللَّـهُ فَمَا لَهُ مِنْ هَادٍ
Je! Mwenyezi Mungu si wa kumtoshea mja wake? Na ati wanakutishia kwa hao wenginewe wasio kuwa Yeye! Na aliye hukumiwa na Mwenyezi Mungu kupotea hana wa kumwongoa.
وَمَن يَهْدِ اللَّـهُ فَمَا لَهُ مِن مُّضِلٍّ ۗ أَلَيْسَ اللَّـهُ بِعَزِيزٍ ذِي انتِقَامٍ
Na ambaye Mwenyezi Mungu anamwongoa hana wa kumpoteza. Je! Mwenyezi Mungu si Mwenye nguvu anaye weza kulipiza?
Aya hizi zinaendeleza maudhui ya aya iliyotangulia kuhusu kuwalinganisha waumini na makafiri na kumhutubu Bwana Mtume SAW ya kwamba: Wao badala ya kuyakubali maneno ya haki wameamua kukabiliana na wewe na kukutisha, ilhali wewe Mwenyezi Mungu anakutosha, na bila ya idhini yake Yeye, hakuna mtu yeyote awezaye kukudhuru, kama ambavyo huko nyuma pia alimuokoa Nabii Ibrahim (as) asiungue ndani ya moto, akamnusuru Nabii Musa (as) na hatari ya Firauni dhalimu na jabari na akamlinda Nabii Isa (as) na waliodhamiria kumuua kwa kumsulubu msalabani. Kisha aya zinaendelea kuashiria uongofu na upotofu na kueleza kwamba: Yeyote atakayeukubali na kuufuata wito wa uongofu wa Allah atasalimika na hatari ya kupotoka; na kila atakayeukataa wito wa uongofu wa Mola, hatoifikia saada hata kama atajidhani kuwa ameongoka. Kwa kumalizia, aya tulizosoma zinatilia mkazo nukta moja kwa kuhoji: Kwani washirikina na makafiri hawajui kwamba hawataweza abadani kukabiliana na Allah na kuishinda irada yake? Na kwani hawaelewi pia kwamba Mwenyezi Mungu ana kisasi na watu wanaoamua kukabilina na Mitume wake na mafundisho waliyokuja nayo? Na kisasi anachowalipizia watu hao ni huko kupotea kwao na kuishia kwenye dhalala. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, kama mtu atakuwa mja halisi akamtii Mwenyezi Mungu, basi yeye Mola anamtosha na atakuwa mlinzi wake. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, mtu muumini humtegemea Allah katika kukabiliana na vitisho vya adui; na badala ya kutishika kwa nguvu na suhula za adui, huendelea kusimama imara katika njia ya haki kwa kutawakali kwa Mwenyezi Mungu na kuelekeza matumaini yake yote kwake Yeye. Halikadhalika aya hizi zinatuelimisha kwamba, kupotoka kwa mtu hakutokei bila sababu au utangulizi; mtu hukosa nuru ya uongofu, akapotoka na kuishia kwenye dhalala kutokana na athari ya amali na matendo yake ya upotofu. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 846 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah, azifanye thabiti imani zetu, atusamehe makosa yetu na aufanye mwema mwisho wetu. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/