Sura ya Az-Zumar, aya ya 38-41 (Darsa ya 847)
Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur’ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.
Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur’ani. Hii ni darsa ya 847 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 39 ya Az-Zumar. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 38 ya sura hiyo ambayo inasema:
وَلَئِن سَأَلْتَهُم مَّنْ خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ لَيَقُولُنَّ اللَّـهُ ۚ قُلْ أَفَرَأَيْتُم مَّا تَدْعُونَ مِن دُونِ اللَّـهِ إِنْ أَرَادَنِيَ اللَّـهُ بِضُرٍّ هَلْ هُنَّ كَاشِفَاتُ ضُرِّهِ أَوْ أَرَادَنِي بِرَحْمَةٍ هَلْ هُنَّ مُمْسِكَاتُ رَحْمَتِهِ ۚ قُلْ حَسْبِيَ اللَّـهُ ۖ عَلَيْهِ يَتَوَكَّلُ الْمُتَوَكِّلُونَ
Na ukiwauliza: Ni nani aliye ziumba mbingu na ardhi. Bila ya shaka watasema: Mwenyezi Mungu. Sema: Je! Mnawaonaje wale mnao waomba badala ya Mwenyezi Mungu, ikiwa Mwenyezi Mungu akitaka kunidhuru, wao wanaweza kuniondolea dhara yake? Au akitaka kunirehemu, je, wao wanaweza kuzuia rehema yake? Sema: Mwenyezi Mungu ananitosheleza. Kwake Yeye wategemee wanao tegemea.
Aya hii inaendeleza yale yaliyozungumziwa katika aya tulizosoma katika darsa iliyopita kuhusu watu walioongoka na waliopotoka na kuashiria maudhui moja muhimu kwa kusema: Washirikina, walikuwa wanaukubali uumbaji wa Mwenyezi Mungu na wakiamini kwamba, Allah SW ndiye aliyeuumba ulimwengu wakiwemo wanadamu; lakini wakiitakidi pia kuwa vitu au watu wengine wana nafasi na taathira katika majaaliwa yao, kama kwamba baada ya Mwenyezi Mungu kuumba ulimwengu, aliwaachia watu au vitu hivyo kuendesha masuala ya wanadamu; na Yeye mwenywe akajiweka kando katika kusimamia uendeshaji wa masuala ya ulimwengu. Washirikina wa zama zile na hata wa sasa, wanaviabudu na kuviomba vitu mbali mbali ambavyo havina uwezo wowote wa kumuepushia mtu madhara wala kumnufaisha kwa chochote kile. Yawe ni masanamu ya mawe na miti ya zama za Bwana Mtume SAW au masanamu ya mahekalu ya wahindu wa zama hizi, yote hayo hayana hata chembe ya uwezo wa kusaidia kutatua matatizo ya mwanadamu. Kuyanyenyekea masanamu na kuyaabudu, humpotosha mtu kwa kumtoa kwenye njia ya haki na kumuelekeza kwenye hilaki na maangamizi. Aya inamalizia kwa kusema: Lakini waumini, badala ya kuvielekea vitu ambavyo vyenyewe ni viumbe vya Mwenyezi Mungu, na ambavyo, kama vilivyo viumbe vyengine, navyo pia vinaendeshwa na Allah, wanatawakali na kumtegemea Yeye Mola pekee. Baada ya kujitahidi kutekeleza wajibu wao kwa usahihi, wanamtegemea Allah kwa ajili ya matokeo ya juhudi zao hizo na wanamwomba awajaalie lile lenye kheri na wao. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba, waabudu masanamu walikuwa wanaukubali uumbaji wa Mwenyezi Mungu, lakini walikuwa wakiamini pia kwamba masanamu yana nafasi katika kuwashufaia na kuwakidhia haja zao; na kwa hivyo wakiyaabudu kwa kuyaona ni wasita na kiunganishi baina yao na Mwenyezi Mungu. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa, faida na hasara na manufaa na madhara yanategemea makadirio ya Allah na si yale tunayodhania sisi na kuyaona kidhahiri. Kwa hivyo badala ya kutegemea vitu ambavyo ni viumbe kama sisi, tutawakali na kumtegemea Allah tu peke yake.
Zifuatazo sasa ni aya za 39 na 40 ambazo zinasema:
قُلْ يَا قَوْمِ اعْمَلُوا عَلَىٰ مَكَانَتِكُمْ إِنِّي عَامِلٌ ۖ فَسَوْفَ تَعْلَمُونَ
Sema: Enyi watu wangu! Fanyeni mwezavyo, mimi pia nafanya. Basi punde mtajua,
مَن يَأْتِيهِ عَذَابٌ يُخْزِيهِ وَيَحِلُّ عَلَيْهِ عَذَابٌ مُّقِيمٌ
Ni nani itakaye mfikia adhabu ya kumhizi, na itakaye mshukia adhabu ya daima.
Aya hizi zinatutaka tukatae kufuata imani na mienendo potofu ya jamii tunayoishi ndani yake. Ni kama alivyoamrishwa Bwana Mtume SAW na Allah SW aitangazie waziwazi kaumu yake, jamaa na marafiki zake kwamba mimi, sikubali kuabudu masanamu, bali ninamuabudu na kumnyenyekea Allah tu, Mola pekee wa haki. Kama nyinyi mnahisi kuwa njia yenu ndio sahihi, basi endeleeni kuifuata; na mimi pia nitaendelea kufuata njia inayotokana na imani yangu juu ya Allah, ili tuone nini itakuwa hatima na mwisho wa amali zangu na amali zenu. Madhumuni ya aya hii yanafanana na ya aya ya mwisho ya Suratul-Kafirun, ambapo kwa kuisoma aya ile, Bwana Mtume SAW alieleza kinagaubaga kwamba katu hatofanya mapatano ya aina yoyote na washirikina wala kuridhia kwa namna yoyote ile kufuata dini yao potofu, aliposema: Mimi nina dini yangu, na nyinyi mna dini yenu. Kisha aya inaendelea kutoa onyo na indhari kwa washirikina kwa kuwataka wajihadhari na matendo yao, kwa sababu watapatwa na ghadhabu na adhabu ya Mwenyezi Mungu hapa duniani na pia huko akhera. Na bila shaka kama watafikwa na adhabu hiyo, hayo yatakuwa matokeo ya amali zao wenyewe, kwani Allah hamuadhibu mtu kwa kumdhulumu au kumuonea. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, mtu muumini huwa imara na mwenye irada na azma thabiti na wala hakubali kutumbukia kwenye lindi la mazingira machafu ya anuai za ufisadi na upotofu. Mtu kama huyo hafuati mkumbo wa fikra na imani zisizo sahihi zilizotawala katika jamii. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, viongozi wa dini walikuwa wakibainisha kinagaubaga na bila mzaha misimamo yao. Katika suala la imani na itikadi za dini, walikuwa hawakubali kupatana na maadui wa haki wala kulegeza msimamo wao hata chembe.
Tunaihitimisha darsa yetu ya leo kwa aya ya 41 ambayo inasema:
إِنَّا أَنزَلْنَا عَلَيْكَ الْكِتَابَ لِلنَّاسِ بِالْحَقِّ ۖ فَمَنِ اهْتَدَىٰ فَلِنَفْسِهِ ۖ وَمَن ضَلَّ فَإِنَّمَا يَضِلُّ عَلَيْهَا ۖ وَمَا أَنتَ عَلَيْهِم بِوَكِيلٍ
Hakika Sisi tumekuteremshia Kitabu kwa ajili ya watu wote kwa Haki. Basi mwenye kuongoka ni kwa nafsi yake, na mwenye kupotoka bila ya shaka amepotoka kwa khasara yake. Na wewe si mlinzi juu yao.
Aya hii inaashiria jukumu la Bwana Mtume Muhammad SAW katika kupokea Wahyi na kuufikisha kwa watu na kueleza kwamba: Mwenyezi Mungu amemfunulia kwa njia ya Wahyi Mtume wake na kwa msingi wa haki na ukweli yale yanayohitajika kwa ajili ya kuwaelekeza watu kwenye uongofu. Na yeye Bwana Mtume pia ameyafikisha hayo kwa watu katika sura ya kitabu kilichoandikwa na cha kubakia milele, pasi na kupunguza chochote. Baada ya kuwafikia wahyi huo, baadhi ya watu wanayakubali maneno yake na hivyo kufaidika na uongofu wa Mola wao katika maisha yao, na baadhi ya watu wanayakataa kutokana na taasubi, ukaidi na inadi au kwa sababu ya kufuata mambo kiurithi na kwa hiyo wanaselelea kwenye upotofu. Ni wazi kwamba ndoto na matamanio ya Bwana Mtume, ambaye ni mwalimu na muongozaji mwenye huruma wa wanadamu, ni kuona watu wote wanaiamini haki, lakini kama baadhi yao hawataki kuamini, haiwezekani kuwalazimisha waamini kwa nguvu na kujifanya mlezi na msimamizi wao. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba, msingi wa Qur'ani ni kubainisha haki na hakika za ulimwengu wa maumbile. Yote yaliyomo ndani ya kitabu hicho ni haki, wala hamna hata chembe ya batili. Qur'ani imeteremshwa ili mwanadamu azingatie miongozo yake na kuweza kuielewa njia sahihi ya uongofu na kuifuata. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa, watu wana hiari na wako huru katika kuchagua njia ya kufuata, lakini wakubali pia kubeba dhima na masuulia ya njia wanayochagua pamoja na matokeo ya uchaguaji wao. Vile vile aya hii inatuelimisha kwamba, jukumu la Mitume ni kufikisha ujumbe wa Wahyi wa Mola wao, si kuwalazimisha watu waukubali na kuufuata. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 847 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atuoneshe haki na atupe taufiki ya kuifuata na atuoneshe batili na atuwezeshe kuiepuka. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/