Sura ya Az-Zumar, aya ya 46-50 (Darsa ya 849)
Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur’ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.
Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur’ani. Hii ni darsa ya 849 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 39 ya Az-Zumar. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 46 ya sura hiyo ambayo inasema:
قُلِ اللَّـهُمَّ فَاطِرَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ عَالِمَ الْغَيْبِ وَالشَّهَادَةِ أَنتَ تَحْكُمُ بَيْنَ عِبَادِكَ فِي مَا كَانُوا فِيهِ يَخْتَلِفُونَ
Sema: Ewe Mwenyezi Mungu! Muumba wa mbingu na ardhi! Mjuzi wa yasiyo onekana na yanayo onekana! Wewe utahukumu baina ya waja wako katika waliyo kuwa wakikhitalifiana.
Aya ya 45 tuliyosoma katika darsa iliyopita ilizungumzia chuki za washirikina kwa imani ya tauhidi na utegemezi na unyenyekevu wao kwa miungu yao bandia na waunganishi wao hao hewa wa kidunia wa kuwapatia shufaa na uombezi kwa Mwenyezi Mungu. Aya tuliyosoma inaendeleza maudhui hiyo na kumhutubu Bwana Mtume Muhammad SAW ya kwamba: Jitenge nao na umuelekee Mola wako pekee wa haki, ambaye ndiye Muumba wa mbingu na ardhi na Mjuzi wa yote ya siri; kwani Siku ya Kiyama, Yeye atakuja kuhukumu baina ya waja wake kuhusu yale waliyokuwa wakihitalifiana. Siku ya Kiyama, Allah ndiye atakayekuwa hakimu na mtawala mutlaki, aliye Mjuzi wa siri zote. Hitilafu na tofauti zitamalizika kwa hukumu atakayotoa. Katika mahakama ya Siku ya Kiyama, wale wakaidi waliopotoka, hawatakuwa na njia ya kuukana ukweli; na watakiri na kuungama kwamba njia waliyofuata ilikuwa ya makosa; lakini kuungama kwao huko hakutakuwa na faida yoyote kwao wakati huo. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba, kinyume na watu waliozielekeza nyoyo zao na mapenzi yao kwa asiyekuwa Allah, sisi tumuelekee na kumtegemea Yeye Mola, ambaye ndiye Muumba wa ulimwengu. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa, yule aliyeumba mbingu na ardhi, ndiye mjuzi wa mambo yote ya viumbe wake, yakiwemo ya dhahiri na yaliyofichikana. Aidha tunajielimisha kutokana na aya hii kwamba, hukumu ya Allah kwa watu itatokana na elimu na ujuzi wake mutlaki wa kutambua ya dhahiri na yaliyofichikana.
Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 47 na 48 ambazo zinasema:
وَلَوْ أَنَّ لِلَّذِينَ ظَلَمُوا مَا فِي الْأَرْضِ جَمِيعًا وَمِثْلَهُ مَعَهُ لَافْتَدَوْا بِهِ مِن سُوءِ الْعَذَابِ يَوْمَ الْقِيَامَةِ ۚ وَبَدَا لَهُم مِّنَ اللَّـهِ مَا لَمْ يَكُونُوا يَحْتَسِبُونَ
Na lau kuwa walio dhulumu wangeli kuwa na vyote viliomo duniani na pamoja navyo vingine kama hivyo, bila ya shaka wangeli vitoa kujikomboa katika adhabu mbaya Siku ya Kiyama. Na yatawadhihirikia kwa Mwenyezi Mungu wasiyo kuwa wakiyatazamia.
وَبَدَا لَهُمْ سَيِّئَاتُ مَا كَسَبُوا وَحَاقَ بِهِم مَّا كَانُوا بِهِ يَسْتَهْزِئُونَ
Na utawadhihirikia ubaya wa waliyo yachuma, na yatawazunguka waliyo kuwa wakiyafanyia mzaha.
Aya hii inaendeleza maudhui ya aya iliyotangulia kuhusu utaratibu wa hukumu ya Allah Siku ya Kiyama na kueleza kwamba: Wale wote ambao walikuwa madhalimu hapa duniani watapatwa na adhabu kali kabisa; na bali si hasha wakadhihirikiwa siku hiyo na adhabu ambazo hapo kabla hata hawakuwa wakizitasawari. Neno dhulma katika mafundisho ya Qur'ani linajumuisha dhulma ya kifikira na kiitikadi kama shirki na ukafiri; na vile vile linajumuisha dhulma ambayo mtu anawafanyia watu wengine iwe ni katika familia au jamii. Lakini ni wazi kwamba hatari na madhara ya dhulma ya kifikra na kiutamaduni ni makubwa zaidi kuliko dhulma ya kijamii. Kwa sababu dhulma ya kijamii huwa mara nyingi inaweza kufidiwa, lakini dhulma ya kiutamaduni, wakati mwengine huwa sababu ya kupotoka vizazi na vizazi na jamii kadha wa kadha na kusababisha janga na maafa. Kwa hiyo kurekebisha na kufidia maafa yake inakuwa vigumu zaidi pia. Bila shaka adhabu kali itakayowapata watenda maovu itatokana na uadilifu wa Allah; na Yeye Mola si mwenye kutenda dhulma hata chembe kwa hata madhalimu pia. Kwa hiyo aya zinaendelea kueleza kwamba: Adhabu hiyo ni dhihirisho la amali zao chafu walizofanya duniani, ambazo siku hiyo zitajiakisi na kuonekana kwa sura ya moto unaounguza na kuteketeza. Wakati walipokuwa duniani, watu hao walikuwa wakifikiria kulimbikiza mali na utajiri na wakidhani kwamba watafuzu na kuwa na saada kwa sababu ya mali na utajiri mkubwa walionao. Kwa hiyo waliyafanyia shere na stihzai yale waliyosikia, pamoja na maonyo waliyopewa kuhusu Siku ya Kiyama. Walipoonywa na waja wema kuhusu yatakayojiri Siku ya Kiyama waliyachukulia hayo kuwa ni mambo ya udhanifu yatamkwayo na watu wajinga na wasiostaarabika. Lakini watakapohudhurishwa siku hiyo kwenye uwanja wa kufufuliwa viumbe, watashuhudia kwa macho yao jinsi yale waliyoyafanyia shere na stihzai yatakavyowaingiza kwenye adhabu ya hilaki; na yale waliyochuma na kuyalimbikiza duniani yatakavyoshindwa kuwafaa kwa namna yoyote ile. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, nguvu na madaraka, na mali na utajiri wa dunia havitaweza kumsaidia mtu kwa lolote huko akhera, hata kama utajiri wa dunia nzima utakuwa milki ya mtu huyo. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, adhabu ya moto ni dhihirisho la amali mbaya na chafu alizofanya mtu hapa duniani. Vile vile aya hizi zinatutaka tujue kwamba, Siku ya Kiyama ni siku ya kufichuka na kudhihirika, ambapo siri zote zitashuhudiwa waziwazi. Mwanadamu atabainikiwa siku hiyo na hakika ya Pepo na Moto. Aidha aya hizi zinatutaka tutahadhari na kuzifanyia stihzai hukumu, imani na thamani za dini; kwani kufanya hivyo kutatuletea majonzi na majuto Siku ya Kiyama.
Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 49 na 50 ambazo zinasema:
فَإِذَا مَسَّ الْإِنسَانَ ضُرٌّ دَعَانَا ثُمَّ إِذَا خَوَّلْنَاهُ نِعْمَةً مِّنَّا قَالَ إِنَّمَا أُوتِيتُهُ عَلَىٰ عِلْمٍ ۚ بَلْ هِيَ فِتْنَةٌ وَلَـٰكِنَّ أَكْثَرَهُمْ لَا يَعْلَمُونَ
Na dhara inapo mgusa mtu hutuomba. Kisha tunapo mpa neema zitokazo kwetu, husema: Nimepewa haya kwa sababu ya ilimu yangu. Sio! Huo ni mtihani! Lakini wengi wao hawajui!
قَدْ قَالَهَا الَّذِينَ مِن قَبْلِهِمْ فَمَا أَغْنَىٰ عَنْهُم مَّا كَانُوا يَكْسِبُونَ
Walikwishayasema haya walio kuwa kabla yao, lakini hayakuwafaa waliyo kuwa wakiyachuma.
Aya hizi zinaashiria moja ya sifa za watu wasio washukurivu na kusema: Kawaida ya watu wengi ni kumkumbuka na kumwomba Allah wanapofikwa na shida, misukosuko na matatizo. Lakini hilo huwa ni jambo la muda na la kupita tu, kwani anapoondokewa na shida na matatizo aliyonayo, mtu humsahau Mola wake na kusema: Elimu na ujuzi wangu mwenyewe ndivyo vilivyoniwezesha kutatua matatizo niliyokuwa nayo na kupata neema na yote niliyonayo. Qur'ani inawajibu watu wa aina hiyo wanaojiona na kujivuna kwa kuwaambia: Hayo mliyopewa ni mtihani tu wa kukupimeni kama mtakuwa washukurivu wa neema za Mwenyezi Mungu au mtazikufuru neema hizo mlizopewa. Kisha aya zinaeleza kwamba, tabia ya kuamiliana hivyo na neema za Allah imekuwepo katika zama zote za historia, kwa watu waliojaaliwa kuwa na mali na utajiri au hadhi na madaraka kumsahau Mwenyezi Mungu na kudhani kwamba, yale waliyochuma, yatawatosheleza hapa duniani na huko akhera pia. Ilhali yote waliyochuma, hayawezi kuzuia kuthibiti irada ya Mwenyezi Mungu kuhusiana na wao hapa duniani, wala huko akhera hayatoweza kuwaepusha na adhabu kutokana na amali zao mbaya walizofanya. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba mwanadamu hubaini upungufu na udhaifu wake wakati wa dhiki, matatizo na misukosuko ya maisha. Misukosuko hiyo humzindua mtu na kuhuisha fitra na maumbile yake ya kumjua Mwenyezi Mungu; na matokeo yake huwa ni kumuelekea na kumwomba Mola wake. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, raha na neema apatazo mwanadamu humghafilisha kumdhukuru na kumkumbuka Mola wake na kumtia ghururi na majivuno. Wa aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba, shida na raha, yote mawili ni njia ya kumtahini na kumpima mtu ili kuidhihirisha hakika yake na hivyo kuwapambanua waja washukurivu mkabala na walio watovu wa shukurani. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 849 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah, atujaalie kuwa wenye kumshukuru Yeye katika hali zote za maisha yetu. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/