May 22, 2023 12:09 UTC

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur’ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.

Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur’ani. Hii ni darsa ya 851 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 39 ya Az-Zumar. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 54 na 55 ambazo zinasema:

وَأَنِيبُوا إِلَىٰ رَبِّكُمْ وَأَسْلِمُوا لَهُ مِن قَبْلِ أَن يَأْتِيَكُمُ الْعَذَابُ ثُمَّ لَا تُنصَرُونَ

Na rejeeni kwa Mola wenu Mlezi, na silimuni kwake, kabla ya kukujieni adhabu. Kisha hapo hamtanusuriwa.

وَاتَّبِعُوا أَحْسَنَ مَا أُنزِلَ إِلَيْكُم مِّن رَّبِّكُم مِّن قَبْلِ أَن يَأْتِيَكُمُ الْعَذَابُ بَغْتَةً وَأَنتُمْ لَا تَشْعُرُونَ

Na fuateni yaliyo bora kabisa katika yale yaliyo teremshwa kwenu kutoka kwa Mola wenu Mlezi, kabla haijakujieni adhabu kwa ghafla, na hali hamtambui. 

Katika darsa iliyopita tulizungumzia upeo wa maghufira na rehma za Allah, ambazo kwa hakika zinawajumuisha waja wake wote. Baada ya hayo, aya tulizosoma zinayataja mambo mawili kuwa ndio njia ya kupatia rehma kubwa za Mola. Moja ni kutubia madhambi na jengine ni kufuata mafundisho matukufu ya dini. Sambamba na kuashiria tumaini la kupata rehma za Mwenyezi Mungu, aya hizi zinatoa indhari pia kuhusu adhabu ya Mola ili kusisitiza kwamba ikiwa hamtoyaacha matendo maovu mnayofanya na kuendelea kufanya madhambi, basi mtafikwa na adhabu. Ziwe ni adhabu za duniani zitakazokujieni ghafla, au adhabu za akhera zinazowafika wafanya madhambi baada ya kifo; na hakuna yeyote awezaye kuwaokoa. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, ishara ya toba ya kweli ni kusalimu amri na kuyatii kwa dhati maamrisho ya Mwenyezi Mungu. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa tusicheleweshe kutubia, kwani fursa ya uhai ni ndogo na wala hatujui mwisho wake utakuwa lini. Aidha aya hizi zinatuelimisha kwamba, sambamba na kutubia na kurejea kwa Mola kwa moyo na imani, kuna ulazima pia wa kufanya amali njema. Vile vile aya hizi zinatutaka tuelewe kwamba, amali njema za kufanya ni nyingi mno, lakini umri na uwezo wa mtu una mpaka. Kwa hiyo inatakiwa kila wakati tuchague kufanya yaliyo bora zaidi kwa kuzingatia vipaumbele.

Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 56 ambayo inasema:

أَن تَقُولَ نَفْسٌ يَا حَسْرَتَىٰ عَلَىٰ مَا فَرَّطتُ فِي جَنبِ اللَّـهِ وَإِن كُنتُ لَمِنَ السَّاخِرِينَ

Isije ikasema nafsi: Ee majuto yangu kwa yale niliyo poteza upande wa Mwenyezi Mungu, na hakika nilikuwa miongoni mwa wanao fanya maskhara!

Moja ya hali muhimu zaidi za akhera ambayo imeashiriwa katika baadhi ya aya za Qur'ani ni ya kujuta wanadamu kwa walivyoutumia umri wao duniani, na ndio maana moja ya majina ya Kiyama ni "Yaumul-Hasrah" yaani Siku ya Majuto. Wakati mtu atakapohudhurishwa kwenye uwanja wa baada ya kufufuliwa na kushuhudia kwa macho yake matokeo ya kupuuza kwake kufanya mema, dharau ya kutojali maamrisho ya Mola na maovu aliyotenda, hapo atapaza sauti ya kilio cha majuto huku majonzi makubwa yaliyochanganyika na uchungu usio na mfano vikiwa vimejaa moyoni mwake. Siku ya Kiyama, wafanya madhambi wataonyesha majuto kwa sababu ya kuzifanyia shere na stihzai aya na Mitume wa Mwenyezi Mungu. Kwa sababu, chanzo hasa cha kupotoka na kupotea kwao kilikuwa ni huko kuzifanyia kwao stihzai aya za wito wa haki na wajumbe wa Allah. Kiujumla watu wote watajuta Siku ya Kiyama na kutamani laiti wangeliweza kurudi tena duniani na kujitayarishia zawadi na masurufu ya kuwafaa akhera; lakini majuto yatakuwa na faida gani wakati hakutakuwa na njia tena ya kurudi duniani! Bila shaka baadhi ya maulamaa wa dini watakuwa na majuto makubwa zaidi kuliko watu wengine; na hii ni kwa sababu hawakuifanyia kazi elimu waliyojaaliwa. Siku ya Kiyama watu watafahamu kwamba amali zitakazokuwa na thamani huko akhera ni zile zilizofanywa kwa ikhlasi kwa ajili ya Allah. Hapo watabaini kwamba, mengi waliyojitahidi kufanya duniani, japokuwa kidhahiri yalikuwa mambo mema na ya kheri, lakini kwa sababu waliyafanya kwa ria na kujionesha, hayakuweza kufika kwenye mahakama ya malipo Siku ya Kiyama, bali yaliishia papa hapa duniani. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba, kadiri tutakavyopuuza kufanya amali njema hapa duniani, tutakwenda kujuta na kujisikitikia huko akhera. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa, Siku ya Kiyama ni siku ya kukiri na kuungama dhidi ya nafsi zetu na kujuta kwa tuliyoyafanya hapa duniani. Aidha tunajielimisha kutokana na aya hii kwamba, wale waliokuwa wakizifanyia stihzai aya za Qur'ani na hukumu za Allah hapa duniani, Siku ya Kiyama watajuta kwa waliyoyafanya, lakini majuto ni mjukuu; yatakuja kwa kuchelewa na hayatowafalia kitu wakati huo.

Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 57 na 58 ambazo zinasema:

أَوْ تَقُولَ لَوْ أَنَّ اللَّـهَ هَدَانِي لَكُنتُ مِنَ الْمُتَّقِينَ

Au ikasema: Ingeli kuwa Mwenyezi Mungu ameniongoa, bila ya shaka ningeli kuwa miongoni mwa wenye kumchamngu. 

أَوْ تَقُولَ حِينَ تَرَى الْعَذَابَ لَوْ أَنَّ لِي كَرَّةً فَأَكُونَ مِنَ الْمُحْسِنِينَ

Au ikasema inapo ona adhabu: Lau ningeli pata kurudi, ningeli kuwa miongoni mwa wafanya mema.

Aya hizi zinaendeleza yale yaliyoashiriwa katika aya zilizotangulia kuhusu huzuni na majuto watakayokuwa nayo watu Siku ya Kiyama kwa kuzungumzia yale yatakayosemwa wakati huo na mtu aliyekwisha hukumiwa kuingia motoni na kueleza kwamba: Atakapowaona watu wa peponi wanaelekea huko kutokana na mema mengi waliyoyafanya, mtu huyo atatamani awe kwenye safu yao na kuandamana nao ili kwenda kuneemeka kwa neema zisizo na kikomo za peponi. Hapo atasema: Laiti kama Mwenyezi Mungu angekuwa ameniongoa, na mimi pia, kama walivyo watu wa peponi, ningejiepusha na madhambi duniani na kuwa miongoni mwa wachaMungu. Mtu mhalifu atayasema hayo ili kujaribu kujitoa hatiani. Wakati itakapomkabili adhabu na kuushuhudia Moto wa Jahanamu kwa macho yake, atatamani aruhusiwe arudi tena duniani akayasafishe mabaya aliyoyatanguliza kwa kufanya amali njema na za kheri ili kuwa miongoni mwa waja wema. Bila shaka na ni wazi kwamba maneno yake hayo si sahihi na wala ombi lake hilo pia halina msingi. Kwa sababu Mwenyezi Mungu alituma Mitume ili watu wote wafikiwe na uongofu; kwa hiyo yeyote ambaye hakuongoka, ni yeye mwenyewe hakutaka hivyo; na hakuna shaka kuwa, ombi lake la kutaka kurudi duniani siku hiyo halitatekelezeka. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, thamani na umuhimu wa taqwa utadhihirika Siku ya Kiyama. Kwa hakika kitakachomfaa mtu Siku ya Kiyama ni taqwa na uchaji Mungu wake, si mali na utajiri wala madaraka na umashuhuri. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, ikiwa mtu hataufuata uongofu wa Allah, ajue kwamba njia yoyote nyingine atakayoichagua kufuata haitaweza kumuokoa na kumfanya afuzu huko akhera. Vile vile tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba, wafanya madhambi wataihusudu hali waliyonayo wacha Mungu na kutamani nao pia wangekuwa kama wao. Halikadhalika aya hii inatuelimisha kuwa, uchajiMungu na wema ni mambo mawili yatakayomuokoa mtu Siku ya Kiyama. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 851 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah azijaze imani na taqwa nyoyo zetu na atuwafikishe kuwa na ikhlasi katika amali zetu. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.../