Sura ya Az-Zumar, aya ya 59-63 (Darsa ya 852)
Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur’ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.
Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur’ani. Hii ni darsa ya 852 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 39 ya Az-Zumar. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 59 na 60 ambazo zinasema:
بَلَىٰ قَدْ جَاءَتْكَ آيَاتِي فَكَذَّبْتَ بِهَا وَاسْتَكْبَرْتَ وَكُنتَ مِنَ الْكَافِرِينَ
Wapi! Bila ya shaka zilikujia Ishara zangu, nawe ukazikadhibisha, na ukajivuna, na ukawa miongoni mwa makafiri!
وَيَوْمَ الْقِيَامَةِ تَرَى الَّذِينَ كَذَبُوا عَلَى اللَّـهِ وُجُوهُهُم مُّسْوَدَّةٌ ۚ أَلَيْسَ فِي جَهَنَّمَ مَثْوًى لِّلْمُتَكَبِّرِينَ
Na Siku ya Kiyama utawaona walio msingizia uwongo Mwenyezi Mungu nyuso zao zimesawijika. Je! Si katika Jahannamu makaazi ya wanao takabari?
Katika darsa iliyopita tuliwazungumzia watu ambao wakati watakapoishuhudia adhabu ya Moto, ndipo watazinduka kwenye usingizi wa mghafala na kujuta na kuusikitikia umri wao walioupoteza duniani. Watatamani laiti wangeweza kurudi tena duniani ili wakajirekebishe na kufidia makosa waliyofanya huko nyuma. Baada ya hayo, aya tulizosoma zinasema: Si kwamba Mwenyezi Mungu hakutimiza dhima yake kwenu na kutokuleteeni njia na sababu za kuutambua na kuufikia uongofu; bali ukweli ni kwamba mlipokuwa duniani walikujieni Mitume na vitabu vya mbinguni kwa ajili ya kukuelekezeni kwenye uongofu. Kama mngelitumia akili zenu, mngeweza bila tabu kuubaini ukweli wa maneno yao na kunufaika na muongozo wao. Lakini moyo wa kutakabari mliokuwa nao ulikufanyeni muikanushe dini ya haki na kutoukubali wito wa Mitume; na matokeo yake ni leo kufikwa na adhabu ya Moto. Adhabu ambayo inazisawijisha nyuso na kuwafanya watu wa Motoni waapizane na kuchukiana wenyewe kwa wenyewe. Hakuna shaka kuwa kusawijika na kupiga weusi nyuso za makafiri na wakanushaji haki Siku ya Kiyama, kutaakisi fedheha na aibu itayowapata. Hiyo ni siku ya kubainika hakika ya fikra na amali za watu na kudhihiri siri zilizofichika za matendo yao. Watu ambao hapa duniani wana nyoyo nyeusi na zenye kiza cha upotofu, huku amali zao kama zilivyo fikra zao zikiwa ni nyeusi na zimetitia, huko akhera hali yao hiyo ya batini itadhihirika katika dhahiri yao, na kuzifanya nyuso na sura zao zititie na kupiga weusi pia. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, Mwenyezi Mungu hawaadhibu watu pasi na kutimiza dhima yake kwao kwa njia ya akili na wahyi. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, hulka ya kutakabari ndio chanzo halisi cha kukufuru na kuikana haki. Aidha aya hizi zinatuelimisha kwamba, Siku ya Kiyama dhahiri na batini za watu zitakuwa moja na hali ya sura zao itakuwa sawa na ya nyoyo zao. Wale ambao wana nyoyo chafu, uchafu huo wa nyoyo utadhihirika kwenye sura zao pia na kuzifanya zipige weusi.
Ifuatayo sasa ni aya ya 61 ambayo inasema:
وَيُنَجِّي اللَّـهُ الَّذِينَ اتَّقَوْا بِمَفَازَتِهِمْ لَا يَمَسُّهُمُ السُّوءُ وَلَا هُمْ يَحْزَنُونَ
Na Mwenyezi Mungu atawaokoa wenye kujikinga kwa ajili ya kufuzu kwao. Hapana uovu utao wagusa, wala hawatahuzunika.
Kinyume na hatima ya kundi la kwanza, la watu ambao wataishia motoni huku nyuso zao zikiwa zimesawijika na kutitia, aya tuliyosoma inasema, njia ya kuokoka na adhabu ya Siku ya Kiyama ni takua na uchaMungu; na kubainisha kwamba, Mwenyezi Mungu Mtukufu atawaokoa waliomcha Yeye na kwa hiyo watafuzu na kuifikia saada ya akhera. Saada ni hizo raha za kudumu na neema za milele. Ijapokuwa kula vyakula vitamu na kunywa vinywaji vinavyoburudisha kunampa mtu raha, lakini hiyo si ishara ya furaha na saada. Kwa sababu raha za aina hiyo si za kudumu, bali hutoweka baada ya muda mfupi tu. Lakini raha kama ya kujifunza elimu na ujuzi inaweza kuwa chachu ya saada kwa mtu, kwa sababu raha za kugundua hakika ya mambo na kupata ujuzi wake ni za kudumu na kuendelea. Raha na furaha za duniani, hata kama zitadumu kwa muda fulani, lakini si lolote si chochote kulinganisha na raha na starehe za akhera, kutokana na umri mfupi wa maisha ya duniani. Kwa hiyo saada ya kweli inapatikana kwenye mambo yatakayompa mtu huko akhera furaha ya kuendelea na ya milele kwa kumuondolea kila aina ya majonzi na huzuni na kumuepusha na kila dhara na hatari. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba, takua na uchaMungu katika maisha ya dunia ndio wenzo wa uokovu na kuifikia saada huko akhera. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa, takua ni ngao inayomkinga na kumlinda mtu na maovu na mabaya. Siku ya Kiyama, wachaMungu wataepushwa na kila baya na wala hawatapatwa na majonzi na huzuni.
Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 62 na 63 ambazo zinasema:
اللَّـهُ خَالِقُ كُلِّ شَيْءٍ ۖ وَهُوَ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ وَكِيلٌ
Mwenyezi Mungu ndiye Muumba wa kila kitu, na Yeye ndiye Mlinzi juu ya kila kitu.
لَّهُ مَقَالِيدُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ ۗ وَالَّذِينَ كَفَرُوا بِآيَاتِ اللَّـهِ أُولَـٰئِكَ هُمُ الْخَاسِرُونَ
Yeye anazo funguo za mbingu na ardhi. Na wale walio zikataa Ishara za Mwenyezi Mungu, hao ndio wenye hasara.
Maudhui kuu ya aya za sura hii ya Az-Zumar imejikita zaidi katika kuzungumzia tauhidi na shirki. Kwa hiyo aya tulizosoma zinazungumzia tena suala la tauhidi kwa kuashiria kwamba, tadbiri na uendeshaji wa masuala ya ulimwengu pamoja na ulinzi na utunzaji wake uko mikononi mwa aliyeuumba. Msidhani kwamba Allah SW ameuumba ulimwengu kisha akauacha kama ulivyo au akamkabidhi yeyote yule hatamu za uendeshaji wa mambo yake. Hasha wa kalla! Aya hizi kwa hakika ni kama zinatoa tanbihi na kuupigia vijembe mtazamo wa washirikina na waabudu masanamu. Inafaa tueleze hapa kwamba washirikina wengi wanakubali kuwa Mwenyezi Mungu ndiye Muumba wa wanadamu na ulimwengu, lakini wanadhani kuwa vitu wanavyoviabudu wao vina taathira katika maisha yao; yaani wanahisi tadbiri na uendeshaji wa masuala ya ulimwengu viko mikononi mwa wanavyoviabudu na ndivyo vinavyowalinda na kuwafanya watengenekewe katika mambo yao. Kwa mtazamo wa Qur’ani, watu wanaowaelekea wengine badala ya Allah na kuwaitakidi kuwa wana taathira katika masuala ya ulimwengu, hao ndio waliokula hasara kubwa. Kwa sababu wamemuacha Mmiliki halisi wa ulimwengu wote na ambaye funguo za mbingu na ardhi ziko mikononi mwake Yeye, na badala yake wakaviendea vitu dhaifu na duni, visivyo na uwezo wa kunufaisha wala kudhurisha kwa lolote lile; na kwa sababu hiyo haviwezi kumuepusha mtu na hatari. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, ulimwengu wote unamhitajia Allah katika uumbwaji wake na kuendelea kubaki kwake. Kwa maneno mengine, Yeye Allah ndiye Muumba wa ulimwengu na pia ndiye Mola na Mlinzi wake. Kwa hivyo kutenganisha kwa namna yoyote uumbaji wa Allah na Uola wake wa kuwa Mlezi wa alivyoviumba ni aina mojawapo ya shirki. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, tauhidi ni mtazamo unaopasa kutawala katika hali zote za maisha ya mwanadamu na wala haijifungi na sehemu fulani tu ya maisha ya kiumbe huyo. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 852 ya Qur’ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atuonyeshe haki na atupe taufiki ya kuifuata, na atuonyeshe batili na atuwezeshe kuiepuka. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/