Sura ya Az-Zumar, aya ya 64-70 (Darsa ya 853)
Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur’ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.
Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur’ani. Hii ni darsa ya 853 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 39 ya Az-Zumar. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 64 hadi 66 ambazo zinasema:
قُلْ أَفَغَيْرَ اللَّـهِ تَأْمُرُونِّي أَعْبُدُ أَيُّهَا الْجَاهِلُونَ
Sema: Je! Mnaniamrisha nimuabudu asiye kuwa Mwenyezi Mungu, enyi majaahili?
وَلَقَدْ أُوحِيَ إِلَيْكَ وَإِلَى الَّذِينَ مِن قَبْلِكَ لَئِنْ أَشْرَكْتَ لَيَحْبَطَنَّ عَمَلُكَ وَلَتَكُونَنَّ مِنَ الْخَاسِرِينَ
Na kwa hakika umepewa wahyi wewe na walio kuwa kabla yako: Bila ya shaka ukimshirikisha Mwenyezi Mungu a'mali zako zitapomoka, na lazima utakuwa miongoni mwa wenye kukhasirika.
بَلِ اللَّـهَ فَاعْبُدْ وَكُن مِّنَ الشَّاكِرِينَ
Bali muabudu Mwenyezi Mungu tu, na uwe miongoni mwa wenye kushukuru.
Katika darsa kadhaa zilizopita tumezungumzia maudhui ya tauhidi na shirki. Aya hizi tulizosoma, nazo pia zinaendeleza maudhui hiyo kwa kusema: Mushirikina na waabudu masanamu walijaribu kutumia kila kisingizio ili kumshawishi Bwana Mtume SAW akubali kuyapa heshima na kuyaabudu masanamu yao. Walikuwa wakimwambia: Sisi tuko tayari kusali na kumsujudia Mungu wako kwa sharti kwamba wewe pia uyasujudie masanamu yetu. Katika aya tulizosoma, Mwenyezi Mungu Mtukufu anawahutubu kwa maneno makali watu hao kwamba: Maneno kama haya na matakwa ya aina hii yasiyo na msingi yanatokana na ujahili na kutojua. Kwa sababu itawezekanaje Mtume ambaye ametumwa kuwalingania watu tauhidi, yaani kumwabudu Mola pekee wa haki na kujiweka mbali na shirki na kuabudu masanamu, ayanyenyekee masanamu kwa ajili ya kuwavuta washirikina kwenye dini ya haki! Kisha aya zinaendelea kusema: Ewe Mtume, waambie watu hao, mimi ninamwabudu Mwenyezi Mungu ambaye ni mmoja tu na siko tayari kwa namna yoyote ile kuyanyenyekea na kuyaabudu masanamu yenu. Kwa sababu tauhidi na shirki si katika mambo yanayoweza kufanyiwa muamala; na kila mtu anayeielekea shirki, amali zake njema zinabatilika na kufutika. Na ni wazi kwamba, ikiwa mtu huyo ni Mtume wa Mwenyezi Mungu, bila shaka adhabu yake itakuwa kubwa na kali zaidi, kwa sababu atasababisha kupotoka watu wengine pia. Tujue kwamba, sharti la kukubaliwa amali ni kuamini msingi wa tauhidi, kwani bila ya hilo hakuna amali yoyote ya mtu itakayokubaliwa. Kutokana na athari ya shirki, thawabu na malipo ya amali za mtu hufutika na kutoweka. Kwa sababu shirki ni mithili ya moto, ambao huunguza na kuteketeza amali za mtu. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, kuabudu kitu chochote kile ghairi ya Allah ni alama ya ujinga na ujahili, hata kama mtu ataonekana kidhahiri kuwa na elimu na ujuzi wa mambo chungu nzima. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, tauhidi na kumwabudu Mola pekee wa haki ni mstari mwekundu kwa waumini. Wao hawawi tayari kwa namna yoyote ile kuufanyia muamala na kitu chochote kile. Vile vile tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba, maadui hufanya kila njia waweze kuwapotosha hata Mitume, seuze Waislamu wa kawaida. Halikadhalika aya hizi zinatutaka tuelewe kuwa, kumwabudu Allah ni aina mojawapo ya kuonyesha ushukurivu kwa neema zake Yeye Mola mrehemevu.
Ifuatayo sasa ni aya ya 67 ambayo inasema:
وَمَا قَدَرُوا اللَّـهَ حَقَّ قَدْرِهِ وَالْأَرْضُ جَمِيعًا قَبْضَتُهُ يَوْمَ الْقِيَامَةِ وَالسَّمَاوَاتُ مَطْوِيَّاتٌ بِيَمِينِهِ ۚ سُبْحَانَهُ وَتَعَالَىٰ عَمَّا يُشْرِكُونَ
Na wala hawakumhishimu Mwenyezi Mungu kama anavyo stahiki kadiri yake. Na Siku ya Kiyama ardhi yote itakuwa mkononi Mwake, na mbingu zitakunjwa katika mkono Wake wa kuume. Subhanahu wa Taa'la Ametakasika na Ametukuka na wanayo mshirikisha nayo.
Aya hii inaendeleza maudhui iliyozungumziwa katika aya zilizotangulia na kueleza kwamba: Washirikina hao wanaotoa mapendekezo hayo ya kifidhuli kwa Mtume wa Allah na kumtaka ayape heshima masanamu yao, kwa hakika hawajaijua hadhi ya Mwenyezi Mungu, mpaka wameamua kuishusha hadhi ya jina lake lililotakasika kwa kuliweka daraja moja na masanamu yao. Ukweli ni kwamba chanzo cha shirki ni kukosa kuwa na maarifa na ufahamu sahihi kuhusu Mwenyezi Mungu; Mola ambaye ni Muumba wa viumbe wote, ambaye tadbiri na uendeshaji wa masuala ya ulimwengu uko mikononi mwake; na viumbe vyote vinamhitajia Yeye ili kuweza kuendelea kubaki. Siku ya Kiyama, ardhi na mbingu zote zitakuwa mikononi mwa Allah SW. Kutumiwa tashbihi hiyo kumefanywa ili kubainisha qudra na adhama ya Mwenyezi Mungu na uwezo wake mutlaki wa kuudhibiti ulimwengu; ili watu wote watambue kuwa, Siku ya Kiyama nguvu na mamlaka ya kila kitu hayatokuwa mikononi mwa mtu au kitu chochote kile ghairi ya Allah SW na ufunguo wa uokovu na utatuzi wa matatizo yote utakuwa kwenye mamlaka yake. Naam, Mwenyezi Mungu Mtukufu ametakasika kuwa na mshirika wa aina na namna yoyote ile. Na bila shaka washirikina watakuja kubaini hakika hii, wakati ambapo hakutakuwa na njia tena ya kurudi duniani. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba, shirki ni ishara ya kutoelewa hadhi ya Allah na kutozingatia adhama ya elimu, nguvu na uwezo wake mutlaki. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa, mbingu yenye adhama kubwa itadogeka na kufinyika kwa nguvu na uwezo mutlaki wa Muumba wake ambaye ni Allah SW, utadhani ni karatasi iliyofikichika baada ya kukunjwa kunjwa mkononi.
Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 68 hadi 70 ambazo zinasema:
وَنُفِخَ فِي الصُّورِ فَصَعِقَ مَن فِي السَّمَاوَاتِ وَمَن فِي الْأَرْضِ إِلَّا مَن شَاءَ اللَّـهُ ۖ ثُمَّ نُفِخَ فِيهِ أُخْرَىٰ فَإِذَا هُمْ قِيَامٌ يَنظُرُونَ
Na litapulizwa barugumu, wazimie waliomo mbinguni na waliomo ardhini, isipo kuwa aliye mtaka Mwenyezi Mungu. Kisha litapulizwa mara nyengine. Hapo watainuka wawe wanangojea.
وَأَشْرَقَتِ الْأَرْضُ بِنُورِ رَبِّهَا وَوُضِعَ الْكِتَابُ وَجِيءَ بِالنَّبِيِّينَ وَالشُّهَدَاءِ وَقُضِيَ بَيْنَهُم بِالْحَقِّ وَهُمْ لَا يُظْلَمُونَ
Na ardhi itang'ara kwa Nuru ya Mola wake Mlezi, na Kitabu kitawekwa, na wataletwa Manabii na mashahidi, na patahukumiwa baina yao kwa haki, wala hawatadhulumiwa.
وَوُفِّيَتْ كُلُّ نَفْسٍ مَّا عَمِلَتْ وَهُوَ أَعْلَمُ بِمَا يَفْعَلُونَ
Na kila nafsi italipwa kwa yale iliyo yafanya, na Yeye anayajua sana wanayo yatenda.
Baada ya aya iliyotangulia kuashiria nguvu na uwezo wa Allah SW Siku ya Kiayama, aya hizi zinaelezea jinsi utakavyokuwa mwisho wa dunia na kuanza kwa Kiyama kwa kubainisha kwamba, utakapotolewa ukelele mmoja tu wa mbinguni viumbe vyote vitakufa, kisha baada ya muda utapigwa ukelele mwengine, tahamaki viumbe vyote vimeshakuwa hai tena, vimesimama wima vikisubiri kuhesabiwa amali zao. Kwa maneno mengine ni kwamba, kwa irada na amri moja tu ya Allah, hakuna kiumbe chochote si mbinguni wala si ardhini kitakachobakia hai, bali vyote vitakufa. Kama ambavyo, kwa irada nyingine ya Mola, wafu wote watafufuka na kuhudhurishwa kwenye mahakama ya Kiyama. Lakini ni wazi pia kwamba, kwa yeyote atakaye Allah, ataweza kuepushwa na mauti, jambo ambalo litayumkinika pia kwa baadhi ya malaika kama Jibril, Israfil na Mikail. Siku hiyo, ambapo wanadamu wote watakuwa hai tena kwa mara ya pili, ardhi itang’ara kwa nuru ya Mola wake; na nuru ya ukweli itatawala na kuangaza, kiasi kwamba hakuna chochote kitakachoweza kukanushika. Mapazia ya vizuizi vilivyoficha siri vitaondoka na hakika ya amali za kheri na za shari za watu itadhihirika. Kiasi kwamba, hakuna pazia wala kizuizi chochote kitakachoziba muono wa macho ya watu; na kila kitu kitakuwa wazi na wadhiha kutokana na nuru ya Mwenyezi Mungu. Siku hiyo yataletwa madaftari ya amali na kuchunguzwa, yakiwa yamekusanya ndani yake kubwa na dogo la amali alizofanya mtu. Mitume na mashuhuda watahudhurishwa; na watu watahukumiwa kwa haki pasi na kudhulumiwa yeyote. Ni wazi kuwa katika mahakama ambayo hakimu wake ni Allah SW, ardhi ikiwa inang’aa kwa nuru ya uadilifu wake, huku wakiwepo Mitume na mashuhuda wa uadilifu, haitatolewa hukumu isipokuwa ya haki. Katika mahakama ya aina hiyo, hakuna uwezekano wa kufanyika hata chembe ya dhulma na uonevu; na ni wazi kuwa kila mtu ataona matokeo ya amali zake pasi na kupunjwa wala kupunguziwa chochote. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, uhai na mauti ya viumbe wote wakiwemo wanadamu, vinategemea irada ya Allah SW na vinaweza kumjia na kumuondokea mtu wakati wowote ule. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, kumalizika kwa ulimwengu na kujiri kwa Kiyama na kufufuliwa viumbe kutatokea ghafla moja, si tukio la kujiri hatua kwa hatua na la kuchukua muda. Aidha aya hizi zinatuelimisha kwamba, mahakama ya Siku ya Kiyama itaendeshwa kwa kuhudhurishwa madaftari ya amali za watu na mashuhuda wao; na amali na matendo ya watu yatahukumiwa kwa haki na uadilifu. Vile vile tunajielimisha kutokana na aya hizi kuwa, katika dunia hii kuna baadhi ambao ni mashuhuda wa mienendo na matendo yetu. Amali zetu zinasajiliwa na kuhifadhiwa na malaika; na Mitume na mashuhuda maalumu wana uelewa wa tunayoyafanya. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 853 ya Qur’ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atupe mema duniani, na akatupe mema akhera na atulinde na adhabu ya Moto. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/