Sura ya Az-Zumar, aya ya 71-75 (Darsa ya 854)
Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur’ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.
Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur’ani. Hii ni darsa ya 854 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 39 ya Az-Zumar. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 71 na 72 ambazo zinasema:
وَسِيقَ الَّذِينَ كَفَرُوا إِلَىٰ جَهَنَّمَ زُمَرًا ۖ حَتَّىٰ إِذَا جَاءُوهَا فُتِحَتْ أَبْوَابُهَا وَقَالَ لَهُمْ خَزَنَتُهَا أَلَمْ يَأْتِكُمْ رُسُلٌ مِّنكُمْ يَتْلُونَ عَلَيْكُمْ آيَاتِ رَبِّكُمْ وَيُنذِرُونَكُمْ لِقَاءَ يَوْمِكُمْ هَـٰذَا ۚ قَالُوا بَلَىٰ وَلَـٰكِنْ حَقَّتْ كَلِمَةُ الْعَذَابِ عَلَى الْكَافِرِينَ
Na wale walio kufuru watasukumwa kwenye Jahannamu kwa makundi. Mpaka watakapo ifikia itafunguliwa milango yake, na walinzi wake watawaambia: Kwani hawakukujilieni Mitume miongoni mwenu wakikusomeeni Aya za Mola wenu Mlezi na kukuonyeni kukutana na siku yenu hii? Watasema: Ndio! Lakini limekwisha thibiti neno la adhabu juu ya makafiri.
قِيلَ ادْخُلُوا أَبْوَابَ جَهَنَّمَ خَالِدِينَ فِيهَا ۖ فَبِئْسَ مَثْوَى الْمُتَكَبِّرِينَ
Itasemwa: Ingieni milango ya Jahannamu mdumu humo. Basi ni ubaya ulioje wa makaazi ya wanao takabari!
Katika darsa iliyopita tulisema kuwa Siku ya Kiyama mahakama ya Mwenyezi Mungu itaendeshwa kwa kuhudhurishwa mashuhuda tofauti pamoja na madaftari ya amali za watu, ambapo hatima ya kila mtu itaainishwa kwa haki na uadilifu na kuamuliwa kama atakuwa mja wa motoni au peponi. Baada ya hayo, aya tulizosoma zinasema: Itakapotolewa hukumu ya watu wa motoni, watu hao watakokotwa makundi makundi kupelekwa motoni, kwa sababu hawatokuwa tayari kwenda huko wao wenyewe. Kwa mujibu wa maelezo ya Qur'ani, malaika wahusika watawakokota watu hao hadi kwenye milango ya Jahanamu na hapo ndipo milango hiyo itafunguliwa. Walinzi wa huko watawalaumu na kuwakemea watu wa motoni kwa uchaguzi usio sahihi waliofanya duniani kwa kuwauliza, kwani nyinyi hawakukujieni Mitume waliotokana na nyinyi wenyewe, wakakusomeeni aya za Mola wenu na kukutahadharisheni kila mara kuhusu mkutano wa siku hii ya leo?! Kwa nini mliyakadhibisha maneno ya Mitume na kuyapuuza maonyo waliyokupeni? Mlidhani kukadhibisha au kujighafilisha kwenu na Kiyama kunafungulieni njia ya kufanya lolote mpendalo? Imekuwaje sasa mmefikwa na hatima hii? Ni wazi kuwa katika hali hiyo, watu wa motoni hawatakuwa na la kufanya isipokuwa kuungama kuwa walichagua njia ambayo haikuwa sahihi; na wakati huo Allah atakuwa ameshakata hukumu ya adhabu yao, hukumu ambayo haitabadilishwa. Mazungumzo hayo na malaika wa motoni yatamalizikia hapo, na wao wataambiwa piteni kwenye milango ya Jahanamu mkabakie na kuselelea humo milele; ni mahala pabaya palioje hapo kwa waliotakabari. Nukta ya kuzingatia hapa ni kwamba, chimbuko hasa la kukufuru na kupotoka watu wa motoni ni kiburi, ghururi na ukaidi wao wa kuikataa haki. Wao walikuwa daima wakitakabari mbele ya haki na hawakuiacha njia ya upotofu waliyokuwa wakifuata hadi mwisho wa uhai wao. Hakuna shaka kuwa matokeo ya kushupalia kukufuru na kuzikanusha aya za Mwenyezi Mungu ni kuselelea motoni milele. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, wale wanaotakabari hapa duniani na kukadhibisha maneno ya haki ya Mitume watadhalilika Siku ya Kiyama. Mfano wake ni jinsi malaika watakavyoamiliana nao kwa kuwakokota wakati wanawapeleka Motoni. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, hakuna yeyote atakayeingizwa motoni kabla ya kutimiziwa dhima ya kufikishiwa haki. Siku ya Kiyama, mtu muovu ataungama makosa yake na kukiri kuwa wito wa haki ulimfikia lakini hakuwa tayari kuukubali. Vile vile tunajifunza kutokana na aya hizi kwamba, sababu ya watu kufikwa na adhabu ni kukufuru kwao; na chanzo cha ukafiri ni kutakabari mbele ya haki.
Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 73 na 74 ambazo zinasema:
وَسِيقَ الَّذِينَ اتَّقَوْا رَبَّهُمْ إِلَى الْجَنَّةِ زُمَرًا ۖ حَتَّىٰ إِذَا جَاءُوهَا وَفُتِحَتْ أَبْوَابُهَا وَقَالَ لَهُمْ خَزَنَتُهَا سَلَامٌ عَلَيْكُمْ طِبْتُمْ فَادْخُلُوهَا خَالِدِينَ
Na walio mcha Mola wao Mlezi watapelekwa Peponi kwa makundi, mpaka watakapo fikilia, nayo milango yake imekwisha funguliwa. Walinzi wake watawaambia: Salaam Alaikum, Amani iwe juu yenu! Mlikuwa wema. Basi ingieni humu mkae milele.
وَقَالُوا الْحَمْدُ لِلَّـهِ الَّذِي صَدَقَنَا وَعْدَهُ وَأَوْرَثَنَا الْأَرْضَ نَتَبَوَّأُ مِنَ الْجَنَّةِ حَيْثُ نَشَاءُ ۖ فَنِعْمَ أَجْرُ الْعَامِلِينَ
Nao watasema: Alhamdulillah, Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu aliye tutimizia ahadi yake, na akaturithisha ardhi, tunakaa katika Bustani popote tupendapo. Basi ni malipo mazuri yaliyoje ya watendao!
Kinyume na makafiri watakaoingizwa motoni kwa kudunishwa na kudhalilishwa, waumini na watenda mema watapelekwa peponi makundi makundi kwa heshima na taadhima, huku wakikuta milango ya huko ikiwa tayari imeshafunguliwa kwa ajili yao. Wakifika hapo, walinzi wa peponi ambao ni malaika wa rehma, watawaamkia kwa maamkizi ya amani huku wakiwakaribisha kuingia kwenye pepo hiyo ya makazi yao ya milele. Hapo watu wa peponi watamhimidi na kumshukuru Allah kwa kuwatimizia ahadi yake ya kuwaingiza kwenye Pepo iliyotukuka. Tufahamu pia kwamba, kama ambavyo makafiri waliotakabari wataishia motoni milele, waumini waliotenda mema, nao pia wataishi peponi milele. Japokuwa watu wema (kama walivyo watu wengine) wameishi umri mfupi wa maisha ya duniani, hiyo inaonesha kuwa, hata kama wangeishi kipindi kingine cha maelfu ya miaka, wangetii na kutekeleza amri za Mola wao. Hiyo ni sifa iliyokuwa imejengeka katika ujudi wao, iliyobadilika na kuwa hulka thabiti na tabia ya kudumu katika nafsi zao. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, ili kuifikia Pepo, imani tupu haitoshi, bali inalazimu iambatane na taqwa na uchaMungu. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, wakati watu wema watakapoanza kuingia peponi watamhimidi na kumshukuru Allah, kwa sababu kupata neema yoyote ile kunahitaji ushukurivu; sikwambii itapokuwa ni neema adhimu ya Pepo, ambayo Allah SW atawatunukia waja wake hao kwa rehma zake. Aidha aya hizi zinatutaka tufahamu kwamba, hatuwezi kuipata Pepo bila ya amali njema. Imani na uchaMungu humfikisha mtu peponi, unapoandamana na juhudi za ufanyaji amali njema katika njia ya Allah; na si kwa kujipweteka tu bila matendo na kujitenga kwa kujiweka mbali na jamii.
Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 75 ambayo inasema:
وَتَرَى الْمَلَائِكَةَ حَافِّينَ مِنْ حَوْلِ الْعَرْشِ يُسَبِّحُونَ بِحَمْدِ رَبِّهِمْ ۖ وَقُضِيَ بَيْنَهُم بِالْحَقِّ وَقِيلَ الْحَمْدُ لِلَّـهِ رَبِّ الْعَالَمِينَ
Na utawaona Malaika wakizunguka pembeni mwa Arshi ya Mwenyezi Mungu, wakimsabihi na kumhimidi Mola wao Mlezi. Na patahukumiwa baina yao kwa haki na patasemwa: Sifa zote njema ni za Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wa viumbe vyote!
Aya hii, ambayo ni aya ya mwisho ya Suratu-Zumar inamhutubu Bwana Mtume Muhammad SAW ya kwamba: Siku hiyo utawaona malaika wameizunguka Arshi ya Mwenyezi Mungu Mtukufu wakingojea kutekeleza amri za Mola wao kuhusiana na waja wake. Siku hiyo watu watahukumiwa kwa haki na uadilifu, na malaika na watu wa peponi watamhimidi na kumshukuru Mola wao Mtukufu. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba, malaika walinzi wa Motoni na malaika walinzi wa Peponi, wote ni watekelezaji wa amri za Allah SW; na hawatekelezi lolote lile ghairi ya amri za Mola. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa, kumhimidi na kumsabihi Allah ni mambo mawili yanayoandamana. Hamdu na shukrani zinamtahikia yule auendeshaye ulimwengu kwa hekima, busara na tadbiri, ambaye utendaji wake hauna chembe ya ila, kasoro wala nuksani. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 854 ya Qur’ani imefikia tamati na ndiyo inayotuhitimishia pia tarjumi na maelezo ya sura ya 39 ya Qur’ani tukufu ya Az-Zumar. Inshallah tuwe tumeaidhika na kufaidika na yote tuliyojifunza katika sura hii. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/