May 22, 2023 12:28 UTC
  • Sura ya Ghaafir, aya ya 1-6 (Darsa ya 855)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur’ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.

Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur’ani. Baada ya kukamilisha tarjumi na maelezo ya sura ya 39 ya Az-Zumar, katika darsa hii ya 855 tutaanza kutoa tarjumi na maelezo ya sura ya 40 ya Ghaafir. Suratu-Ghaafir imeteremshwa Makka na ina aya 85. Kama zilivyo sura nyingine za Makka, sehemu kubwa ya aya za sura hii inazungumzia masuala ya kiimani na kiitikadi kama Tauhidi, Utume na Maadi. Katika aya ya tatu ya Suratu-Ghaafir, Allah SW ametajwa kwa jina la "Ghafir", yaani mwenye kughufiria na kusamehe madhambi; na kwa sababu hiyo, sura hii imepewa jina la Ghafir. Lakini kwa kuzingatia pia kwamba karibu aya 20 za Suratu-Ghaafir zimezungumzia kisa cha muumini miongoni mwa watu wa Firauni, sura hii inaitwa pia Suratu-Muumin. Baada ya utangulizi huo mfupi, sasa tunaianza darsa yetu ya leo kwa aya ya mwanzo hadi ya tatu ambazo zinasema:

حم

Hamiim.

تَنزِيلُ الْكِتَابِ مِنَ اللَّـهِ الْعَزِيزِ الْعَلِيمِ

Uteremsho wa Kitabu umetoka kwa Mwenyezi Mungu, Mwenye nguvu, Mwenye kujua,

غَافِرِ الذَّنبِ وَقَابِلِ التَّوْبِ شَدِيدِ الْعِقَابِ ذِي الطَّوْلِ ۖ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ ۖ إِلَيْهِ الْمَصِيرُ

Mwenye kughufiria dhambi na anayekubali toba, Mkali wa kuadhibu, Mwenye ukarimu; hakuna aabudiwaye ila Yeye; marejeo ni Kwake.

Sura hii, kama zilivyo sura zingine 28 za Qur'ani, imeanza kwa herufi za mkato, ambapo kama tulivyowahi kueleza huko nyuma, kwa kuzingatia aya inayofuata baada yake, hicho ni kibainishi cha adhama ya Qur'ani tukufu. Yaani, kitabu hiki chenye adhama yote hii na ambacho kimeteremshwa na Mwenyezi Mungu Mwenye izza na hekima, kimetokana na herufi na alfabeti hizi hizi za kawaida za Kiarabu, ambazo nyinyi wanadamu wote pia mnaweza kuzitumia, lakini nyinyi hamuna uwezo wa kuleta kitabu mfano wake. Aya inayofuatia inamuelezea Allah kwa sifa tano, ambazo zinatoa bishara na pia onyo na indhari. Kwa upande mmoja zinawapa matumaini wafanya madhambi kwamba kama mtatubia, Mwenyezi Mungu atakughufirieni na kukusameheni madhambi yenu. Na kwa upande mwingine, zinawaonya na kuwatahadharisha kuwa, kama wataendelea kufanya dhambi na kukiuka mipaka ya maamrisho ya Allah, basi adhabu kali inawangojea. Kisha sehemu inayofuatia ya aya inatilia mkazo nukta kwamba, Mungu ambaye neema zake zimekienea kila kitu ndiye anayestahiki kuabudiwa; na ghairi ya Yeye, hakuna mtu au kitu chochote kile chenye ustahiki wa kuabudiwa. Isitoshe, baada ya kifo, viumbe wote watarejea kwake Yeye na watapaswa kuwajibika kwa waliyoyafanya duniani. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, Qur'ani ni maneno ya Mwenyezi Mungu aliyetukuka, ambayo yameteremshwa kwa muhtawa mwepesi kulingana na uwezo wa ufahamu wa mwanadamu. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, Qur'ani ni dhihirisho la elimu isiyo na mpaka ya Allah SW. Kwa hiyo hakuna mantiki yoyote yenye uwezo wa kukabiliana nayo. Aidha aya hizi zinatuelimisha kwamba, kushikamana na Qur'ani ndiko kunakoweza kuwapa nguvu na izza Waislamu duniani, kwa sababu imeteremshwa na Mwenyezi Mungu ambaye ni mwenye nguvu na izza na mjuzi na mwenye hekima. Vile vile aya hizi zinatutaka tuelewe kuwa, uteremsho wa kitabu cha Qur'ani umefanywa kwa ajili ya kumtambulisha mwanadamu asili na marejeo yake ili aweze kufuata njia ya ukamilifu na kumkurubisha kwa Mola wake.

Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 4 hadi ya 6 ambazo zinasema:

مَا يُجَادِلُ فِي آيَاتِ اللَّـهِ إِلَّا الَّذِينَ كَفَرُوا فَلَا يَغْرُرْكَ تَقَلُّبُهُمْ فِي الْبِلَادِ

Habishani katika Aya za Mwenyezi Mungu ila wale waliokufuru; basi usikughuri utembezi wao mijini.

كَذَّبَتْ قَبْلَهُمْ قَوْمُ نُوحٍ وَالْأَحْزَابُ مِن بَعْدِهِمْ ۖ وَهَمَّتْ كُلُّ أُمَّةٍ بِرَسُولِهِمْ لِيَأْخُذُوهُ ۖ وَجَادَلُوا بِالْبَاطِلِ لِيُدْحِضُوا بِهِ الْحَقَّ فَأَخَذْتُهُمْ ۖ فَكَيْفَ كَانَ عِقَابِ

Walikadhibisha kabla yao kaumu ya Nuh na makundi (mengine) baada yao; na kila umma uliazimia juu ya Mtume wao ili wamkamate; na walibishana kwa upotovu ili kuipindua haki, kwa hiyo Niliwakamata; basi ilikuwaje adhabu Yangu!

وَكَذَٰلِكَ حَقَّتْ كَلِمَتُ رَبِّكَ عَلَى الَّذِينَ كَفَرُوا أَنَّهُمْ أَصْحَابُ النَّارِ

Na hivyo ndivyo lilivyowathibitikia neno la Mola wako wale waliokufuru ya kwamba, wao ni watu wa Motoni.

Aya hizi zinamfariji Bwana Mtume Muhammad SAW pamoja na Waislamu wa mwanzoni mwa Uislamu na wa vizazi vya baada yao, kwamba ikiwa baadhi ya watu wanasimama kukabiliana na dini yenu na wamedhamiria kuipiga vita haki na kuifuta, hayo yasikukatisheni tamaa na kukuvunjeni moyo au kukudhoofisheni. Kwa sababu hivyo ndivyo imekuwa katika zama zote za historia, kwa makafiri na wenye inadi ya dini kula njama na kuwapiga vita, si wafuasi tu wa dini ya Mwenyezi Mungu, bali hata Mitume wake pia, ili kuwazuia wasifuate njia ya haki. Leo hii pia tunashuhudia madola madhalimu na ya kiistikbari yanavyotunisha misuli yao kupitia uitishaji makongamano, safari na majadiliano ya kisiasa, manuva na mazoezi ya kijeshi pamoja na kuasisi miungano baina yao, ili kuyatisha na kuyatia hofu mataifa ya dunia. Lakini wanachopaswa kufanya waumini, ni kujihadhari wasihadaike na ubabe na makeke hayo ya maadui, wala wasitishike au kughilibiwa na nguvu zao za kidhahiri. Tab'an historia imeshuhudia watu wengi wa aina hiyo na ikaonyesha kuwa watu hao ni dhaifu walioje kuweza kuzikabili adhabu za Mwenyezi Mungu. Hapana shaka kuwa haki, ndiyo hatimaye inayokuwa mshindi; na kutokana na maovu wanayofanya watu hao, wajue kwamba wanajiandalia adhabu kali ya Mola duniani na akhera. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, ukafiri ndio chimbuko la kila aina ya ubishi na inadi ya kupinga na kuipiga vita haki. Tujihadhari tusije kwa namna yoyote ile kusimama dhidi ya haki na kuamua kuibisha na kuipinga kwa sababu ya tamaa na matakwa ya kidunia. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, tusitaraji kwamba watu wote wataiamini haki; na wala kukufuru na kukadhibisha kwao kusitudhoofishe na kutufanya tupoteze matumaini katika njia ya haki tunayofuata. Halikadhalika aya hizi zinatutaka tujue kwamba, viongozi wa ukafiri huwa wanafanya makeke na vitimbi vingi ili kuidhoofisha haki na kuwatia hofu Waislamu. Hata hivyo hayo yasiwatie kiwewe waumini. Wajihadhari wasije wakahadaiwa na njama zao na wasimame imara na kuwa thabiti katika msimamo wao. Aidha aya hizi zinatuelimisha kuwa, wakanushaji na wapingaji haki wamewakadhibisha Mitume wa Mwenyezi Mungu na kula njama dhidi yao; na hutumia hila na mbinu mbali mbali za kueneza propaganda dhidi ya haki ili kuidhoofisha na kuifuta. Na pia aya hizi zinatuelimisha kwamba, moja ya taratibu za Allah ni kuwaadhibu makafiri wakaidi na wanaoipiga vita haki. Lakini bila shaka hilo linafanyika kwa msingi wa haki na uadilifu. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 855 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atuoneshe haki na atupe taufiki ya kuifuata na atuoneshe batili na atuwezeshe kuiepuka. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/