May 22, 2023 12:33 UTC
  • Sura ya Ghaafir, aya ya 7-9 (Darsa ya 856)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur’ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.

Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur’ani. Hii ni darsa ya 856 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 40 ya Ghaafir. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 7 ya sura hiyo ambayo inasema:

الَّذِينَ يَحْمِلُونَ الْعَرْشَ وَمَنْ حَوْلَهُ يُسَبِّحُونَ بِحَمْدِ رَبِّهِمْ وَيُؤْمِنُونَ بِهِ وَيَسْتَغْفِرُونَ لِلَّذِينَ آمَنُوا رَبَّنَا وَسِعْتَ كُلَّ شَيْءٍ رَّحْمَةً وَعِلْمًا فَاغْفِرْ لِلَّذِينَ تَابُوا وَاتَّبَعُوا سَبِيلَكَ وَقِهِمْ عَذَابَ الْجَحِيمِ

Wale wanao beba A'rshi, na wanao izunguka, wanamsabihi na kumhimidi Mola wao Mlezi, na wanamuamini, na wanawaombea msamaha walio amini kwa kusema: Mola wetu Mlezi! Umekienea kila kitu kwa rehema na ujuzi. Basi wasamehe walio tubu na wakaifuata Njia yako, na waepushe na adhabu ya Jahannamu.

Kwa mujibu wa aya za Qur'ani, malaika ni viumbe watendaji katika mfumo wa ulimwengu; na katika mambo mengi, ni wasita na waunganishi baina ya Mwenyezi Mungu na wanadamu. Aya hii tuliyosoma inaashiria upande mwingine wa mawasiliano baina ya malaika na wanadamu kwa kueleza kwamba: Malaika waliojikurubisha kwa Allah SW, ambao wako kwenye kitovu cha tadbiri na uendeshaji wa mfumo wa ulimwengu, yaani Arshi ya Allah SW, mbali na wao wenyewe kuwa wenye kumhimidi na kumsabihi Allah Jalla Fi U’laahu, wanawaombea pia waumini kwake Yeye Mola na kuwatakia msamaha na maghufira. Katika dua na maombezi yao, malaika hao wanasema: Ewe Mola, Wewe ni Mjuzi wa makosa yao, na wakati huohuo rehma zako hazina mpaka na zinakienea kila kitu; basi yasamehe makosa ya wanaotubia na usiwaache wafikwe na adhabu ya Moto. Kwa hakika aya hii inawapa bishara waumini, kwamba wabebaji wa Arshi ya Mola aliyetukuka, ambao ni miongoni mwa nguvu za ghaibu zenye taathira kubwa zaidi katika ulimwengu, wanakusaidieni nyinyi pia na kukuungeni mkono. Daima wao wanakuombeeni dua na wanamuomba Mwenyezi Mungu akughufirieni na akurehemuni kwa rehma zake zisizo na ukomo, akusahemeni makosa yenu na akuepusheni na adhabu ya Moto. Wanamuomba Allah akujaalieni mfaulu hapa duniani na mkafuzu na kuokoka huko akhera; na hicho ni kitu kikubwa zaidi cha kuwaliwaza na kuwapa moyo waumini. Wakati mtu anapohisi kuwa dunia haikomei kwenye mfumo wa kimaada na ulimwengu wa hisi, bali kuna nguvu ya ghaibu pia hapa duniani inayomhami na kumpa auni, jambo hilo hutoa msukumo mkubwa kwake katika dunia hii iliyojaa tabu na machungu na mambo ya hatari. Na hisia hiyo humpa mtu matumaini, ukakamavu na uwezo wa kusimama imara katika njia ya Allah. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba, ni bishara njema na jambo la kutia matumaini, kuwepo malaika waliojikurubisha kwa Allah, ambao wanawahami na kuwaombea maghufira waumini. Hii yenyewe huwapa faraja wafuasi wa dini ya Mwenyezi Mungu na kuwapa uthabiti katika njia ya haki wanayofuata. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa, kuwaombea dua wenzako ni amali yenye thamani na inayopendeza. Na kama wanavyofanya malaika, tujifunze kwao kwa kuwaombea dua wenzetu na kuwatakia mema na ya kheri kwa Mwenyezi Mungu. Vilevile aya hii inatuelimisha kwamba, imani sahihi na amali njema ndiyo kamba ya kumuunganisha mja na Mola wake. Ikiwa fundo la kamba hii litakuwa limekaza barabara, mwanadamu ataokoka na hilaki na maangamizi duniani na akhera.

Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 8 na ya 9 ambazo zinasema:

رَبَّنَا وَأَدْخِلْهُمْ جَنَّاتِ عَدْنٍ الَّتِي وَعَدتَّهُمْ وَمَن صَلَحَ مِنْ آبَائِهِمْ وَأَزْوَاجِهِمْ وَذُرِّيَّاتِهِمْ ۚ إِنَّكَ أَنتَ الْعَزِيزُ الْحَكِيمُ

Mola wetu Mlezi! Na waingize katika Bustani za Milele ulizo waahidi. Na (uwape haya) pia wale walio fanya mema miongoni mwa wazee wao na wake zao na dhuriya zao. Hakika Wewe ni Mwenye nguvu, Mwenye hikima.

وَقِهِمُ السَّيِّئَاتِ ۚ وَمَن تَقِ السَّيِّئَاتِ يَوْمَئِذٍ فَقَدْ رَحِمْتَهُ ۚ وَذَٰلِكَ هُوَ الْفَوْزُ الْعَظِيمُ

Na waepushe na maovu; kwani umwepushaye na maovu siku hiyo, hakika umemrehemu; na huko ndiko kufuzu kukubwa.

Aya hizi zinaendeleza maudhui iliyozungumziwa katika aya iliyotangulia kuhusu maghufira na msamaha ambao malaika wanawaombea waumini na kueleza kwamba: Sio tu malaika wanawaombea waumini kwa Allah awafutie madhambi yao na kuwaepusha na adhabu, lakini pia wanawaombea waishi kwenye Pepo ya milele wakiwa pamoja na watu wa familia zao. Bila shaka wanaokusudiwa na malaika hao ni wale jamaa wa familia zao wenye ustahiki wa kuingia peponi. Kwa sababu Siku ya Kiyama uhusiano wa kifamilia, uwe wa nasaba kwa uzawa au wa sababu kwa ndoa hautaweza kumfanya mtu awe pamoja na baba au mama yake au kando ya mwanawe, mkewe au mumewe; kwa sababu sharti la kuingia peponi ni imani sahihi na amali njema. Pamoja na hayo, lipo tumaini kwamba endapo watu wa peponi watamwomba Mwenyezi Mungu awaweke pamoja nao wazazi wao, au wake, waume na watoto wao, na ikawa kila mmoja katika watu hao walioombewa, anao ule ustahiki japo wa kiwango cha chini wa kuingia peponi, Yeye Mola kwa rehma na ukarimu wake anaweza kusamehe mapungufu yao watu hao na kuwaweka pamoja na jamaa zao wa peponi. Na hilo linaendana na izza na hekima ya Allah SW. Na ndiyo maana katika aya aya 21 ya Suratu-T'ur, Mwenyezi Mungu Mtukufu ameahidi kwa kusema: Na walio amini na dhuriya zao wakawafuata kwa imani tutawakutanisha nao dhuriya zao. Ahadi hii inabainisha thamani ya familia na kudumishwa uhusiano wa kiudugu na kifamilia mbele ya Allah. Kisha aya zinaendelea kuzungumzia dua ya malaika kwa waumini, ya kuwekwa mbali na maovu na mabaya duniani na akhera na kulielezea hilo kama ishara ya rehma za Allah kwa waumini hao. Kwa hakika lengo hasa ni kuwafanya waumini wa kweli waingie peponi kwa utulivu wa nafsi, heshima na ukarimu. Ni wazi kwamba ikiwa mtu atakuwa miongoni mwa wenye kuombewa dua na malaika na akaokoka na moto na kuingizwa peponi, atakuwa amefikia daraja ya juu kabisa ya saada na uokovu, kitu ambacho ubora wake hauwezi kutasawarika kwa mwanadamu. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, kuwaombea wengine dua ndio mwenendo wa malaika na mawalii wa Mwenyezi Mungu. Badala ya kuwalaani na kuwaapiza watu walioteleza na waliopotoka, tuwaombee kwa Mola awaghufirie na kuwarehemu. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, bila mtu kusafika na madhambi hatokuwa na ustahiki wa kuingia peponi. Aidha aya hizi zinatuelimisha kwamba, saada na uokovu mkubwa unapatikana kwa mtu kuepukana na madhara ya kimaada na kimaanawi. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 856 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atupe mema duniani na akatupe mema akhera na atulinde na adhabu ya moto, sisi na jamaa zetu. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/