Sura ya Ghaafir, aya ya 10-12 (Darsa ya 857)
Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur’ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.
Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur’ani. Hii ni darsa ya 857 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 40 ya Ghaafir. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 10 ya sura hiyo ambayo inasema:
إِنَّ الَّذِينَ كَفَرُوا يُنَادَوْنَ لَمَقْتُ اللَّـهِ أَكْبَرُ مِن مَّقْتِكُمْ أَنفُسَكُمْ إِذْ تُدْعَوْنَ إِلَى الْإِيمَانِ فَتَكْفُرُونَ
Kwa hakika wale walio kufuru watanadiwa: Bila ya shaka kukuchukieni Mwenyezi Mungu ni kukubwa kuliko kujichukia nyinyi nafsi zenu, mlipo kuwa mnaitwa kwenye Imani nanyi mkakataa.
Katika darsa iliyopita tulizungumzia rehma zisizo na ukomo za Allah SW kwa waumini na waja wema. Aya hii, mkabala wake, inabainisha ghadhabu kubwa za Mola kwa watu wanaosimama kuipinga haki kutokana na inadi na ukaidi; na ijapokuwa haki wanaifahamu lakini hawaiamini. Wakati makafiri watakapoyaona matokeo ya amali zao Siku ya Kiyama watajuta na kuhuzunika na watakuwa wakijinyonga na kujisokota kwa ukubwa wa adha na uchungu watakaokuwa nao. Watazilaumu nafsi zao kwa nini walichagua njia ya batili na pia watawaapiza na kuwalaani viongozi na marafiki zao waliowavuta na kuwaingiza kwenye njia hiyo. Siku ya Kiyama watu walioikufuru haki watakuwa na uadui mkubwa sana baina yao, lakini malaika wasimamizi wa motoni watawaambia: Ghadhabu za Mwenyezi Mungu kwenu nyinyi makafiri mliokaidi haki, ni kubwa zaidi kuliko hayo mateso ya kinafsi na hivyo mnavyoapizana na kulaaniana nyinyi kwa nyinyi. Kwa sababu Mitume wa Allah walikunadieni na kukuiteni kwenye njia sahihi ya haki, lakini mkaamua kwa uelewa na kwa makusudi kuwapinga na kuwakadhibisha walinganiaji hao wa tauhidi. Mliikimbia nuru ya uongofu mkaikimbilia njia ya kufuru na upotofu; na mlichofanya hasa ilikuwa ni kuwatusi na kuwadunisha watu ambao Allah aliwatuma, ili waje kukuelekezeni kwenye uongofu. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba, kuipiga vita haki, kukufuru na kukabiliana na Mitume wa Allah huandamwa na ghadhabu kubwa za Mola. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa, adhabu ya Mwenyezi Mungu huwastahikia watu baada ya kutimiziwa dhima na kuwafikia wito wa uongofu.
Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 11 ambayo inasema:
قَالُوا رَبَّنَا أَمَتَّنَا اثْنَتَيْنِ وَأَحْيَيْتَنَا اثْنَتَيْنِ فَاعْتَرَفْنَا بِذُنُوبِنَا فَهَلْ إِلَىٰ خُرُوجٍ مِّن سَبِيلٍ
Watasema: Mola wetu Mlezi! Umetufisha mara mbili, na umetuhuisha mara mbili! Basi tunakiri madhambi yetu. Basi je, ipo njia ya kutoka?
Moja ya hakika ambazo makafiri huwa wanazikana kila siku, ni ya kuwepo kwa ulimwengu wa baada ya kifo na kuhudhurishwa waja katika Siku ya Kiyama. Wao wanaamini kwamba, kila kitu cha mwanadamu kinamalizika kwa kifo na hakuna chochote kinachosalia kutokana na kiumbe huyo. Lakini itakapokuja kushuhudiwa hali na hakika ya Siku ya Kiyama, utandu wa mghafala utaondoka na macho ya yakini ya watu wote yatafumbuka. Makafiri watakiri kuwa waliikanusha na kuikataa bila ya hoja, haki na ukweli wa wazi kabisa waliofikishiwa na Mitume. Kwa hiyo katika kuungama makosa yao hayo watasema: Mola wetu Mlezi ametufisha na kutuhuisha, tena si mara moja, bali mara mbili. Mara ya kwanza ni pale ulipomalizika uhai wetu, ambapo tulikufa kimwili, kisha Allah akatupa uhai wa barzakhi. Na mara ya pili, ni baada ya kumalizika umri wa dunia nzima, ambapo tulikufa katika maisha ya barzakhi, kisha Allah akatufufua tena mara ya pili Siku ya Kiyama. Kwa maelezo hayo, madhumuni ya aya hii yako wazi kabisa kwamba, maana ya kufishwa mara mbili, ni mauti ya mwisho wa maisha ya mtu na mauti ya baada ya barzakhi. Na makusudio ya kuhuishwa mara mbili, ni kuwa hai tena katika ulimwengu wa barzakhi na kufufuliwa tena Siku ya Kiyama. Alaa kulli haal, makafiri wataukiri ukweli huu kwa kutaka Mwenyezi Mungu awasamehe makosa waliyofanya huko nyuma na kuwarudisha tena duniani ili wakajirekebishe, kwa kuacha amali na matendo yao mabaya na maovu waliyofanya au angalau wapate njia ya kuokoka na moto. Watafanya hivyo, wakati kuungama na kujuta kwao huko Siku ya Kiyama hakutakuwa na faida yoyote, wala hakutakuwa sababu ya kuwawezesha warudi duniani au watolewe motoni. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba, Siku ya Kiyama, wenye madhambi watatamani warudi tena duniani. Kwa hiyo maadamu tungali tuko duniani tuitumieni fursa hii kutubia, kwa kujirekebisha makosa yetu na kuyaacha maovu tunayofanya ili tusije tukawa miongoni mwa watakaokuja kutamani siku hiyo tamanio hili, ambalo haitawezekana kuthibiti na kutekelezeka. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa, wale wanaokanusha maisha ya baada ya kifo wajue kuwa tutayapitia mara mbili maisha hayo. Ya kwanza ni pale tutapokuwa hai tena baada ya kifo katika ulimwengu wa barzakhi. Na ya pili ni wakati tutakapofufuliwa baada ya kusimama Kiyama.
Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 12 ambayo inasema:
Hayo ni kwa sababu alipoombwa Mwenyezi Mungu peke yake mlikataa. Na aliposhirikishwa mliamini. Basi hukumu ni ya Mwenyezi Mungu Mtukufu Mkuu.
ذَٰلِكُم بِأَنَّهُ إِذَا دُعِيَ اللَّـهُ وَحْدَهُ كَفَرْتُمْ ۖ وَإِن يُشْرَكْ بِهِ تُؤْمِنُوا ۚ فَالْحُكْمُ لِلَّـهِ الْعَلِيِّ الْكَبِيرِ
Aya hii inakitaja chanzo cha ukafiri kuwa ni aina mojawapo ya shirki, kwa maana kwamba, baadhi ya watu huwa hawako tayari kuyachambua na kuyanasibisha na Allah masuala yanayohusu mwanadamu na dunia, bali husema: Mungu ndiye Muumba wetu, lakini baada ya kutuumba ametuachia kila jambo tujiamulie sisi wenyewe. Kwa hiyo linapokuja suala la tadbiri na uendeshaji wa mambo yao na ya ulimwengu, watu hao huyaendea machaguo mengine ghairi ya Allah SW. Ni kama zinavyoeleza aya nyingine za Qur’ani, kwamba watu hao hawakanushi uumbaji wa Mwenyezi Mungu, lakini hawaukubali ulezi na uendeshaji wake katika mfumo wa uumbaji. Baadhi ya wakati, hutaka wao wenyewe wakae mahali pa Mwenyezi Mungu kwa kuwatungia wanadamu wenzao sheria na kuwapangia na kuwaamulia nini wafanye na nini wasifanye. Na wakati mwengine, kutokana na ujinga na ujahili wao, hutingwa na mambo ya uzushi na khurafa, wakaviitakidi vitu mbali mbali kuwa na nguvu na uwezo maalumu, kana kwamba vitu hivyo ndivyo vyenye taathira kuu katika hatima na majaaliwa yao. Watu hao ni pamoja na wale wanaoabudu nyota na masanamu. Pamoja na hayo ni wazi kwamba fikra na matendo ya watu kama hao hapa duniani hayakuwa yakifanywa katika hali ya kupitikiwa na kwa sadfa tu. Kwa hiyo kutokana na kujengeka na fikra za aina hiyo, hata kama watarejeshwa tena duniani wataendelea kufanya mambo na vitendo hivyo hivyo bila kubadilika chochote katika mwenendo wao. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba, ikhlasi katika tauhidi na kumpwekesha Allah na kujiepusha na kila aina ya shirki ndio njia itakayomwezesha mtu kuokoka Siku ya Kiyama. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa, kama tulivyoashiria, katika shirki, mwanadamu anaitakidi kuwa Allah SW ndiye Muumba, lakini huamini kuwa katika uendeshaji wa masuala ya ulimwengu kuna vitu vingine vyenye kuathiri; na kwa hiyo huvielekea na kuviomba vitu hivyo. Alaa kulli hal, ukafiri mutlaki wa kukanusha kuwepo kwa Mwenyezi Mungu, na pia kumfanya Yeye Mola ana mshirika, yote mawili yatamuingiza mtu motoni. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 857 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atuepushe na kila ya shirki, kubwa na ndogo, tunayoijua na tusiyoijua. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/