Sura ya Ghaafir, aya ya 13-15 (Darsa ya 858)
Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur’ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.
Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur’ani. Hii ni darsa ya 858 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 40 ya Ghaafir. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 13 na 14 za sura hiyo ambazo zinasema:
Yeye ndiye anaye kuonyesheni Ishara zake, na anakuteremshieni kutoka mbinguni riziki. Na hapana anaye kumbuka ila anaye rejea.
Basi mwombeni Mwenyezi Mungu mkimsafia Dini Yeye tu, na wajapochukia makafiri.
Katika darsa iliyopita tulisoma aya zilizoelezea hatima ya washirikina na makafiri Siku ya Kiyama. Aya tulizosoma zinazungumzia tauhidi na ishara zake na kusema: Ishara za Mungu pekee wa haki, zilizoko katika alivyoviumba, ambavyo vimekuzungukeni na kila siku mnaviona na mnashughulika navyo, ni nyingi sana. Kwa maneno mengine, alama na ishara zake zinaonekana wazi katika kila kitu cha ulimwengu wa viumbe. Mbingu na ardhi, milima, mabonde na bahari, anuai za viumbe wa majini, ndege wa angani na wanyama wanaoishi ardhini, vyote hivyo ni alama na ishara zilizo dhahiri shahiri mbele ya macho yenu. Kisha aya zinaeleza kwamba, Yeye Allah anakuteremshieni riziki kutoka mbinguni. Katika ishara zake muhimu zaidi, ambayo ni sababu ya kupatikana uhai wa mimea, miti na binadamu wote, ni matone ya mvua na miale ing'arayo ya mwanga wa jua, ambavyo vyote viwili vinashuka kutoka mbinguni na bila ya viwili hivyo itashindikana kuishi ardhini. Lakini pamoja na kuwepo ishara zote hizo katika ulimwengu, macho na nyoyo zilizozibwa na utando wa mghafala haziwezi kuona chochote. Kwa hakika wanaoweza kukumbuka kwa kuziona aya na ishara hizo, ni wale wanaotaka kurejea kwa Allah, wakafuata njia yake na wakazitakasa nyoyo na nafsi zao na mambo machafu. Ni kama isemwavyo, kwamba mtu aliyelala kweli, huamka pale anapoamshwa; lakini mtu anayejifanya tu kuwa amelala, ambaye hana nia ya kuinuka, yeye hata umuite kwa sauti gani, hatoamka na kuinuka. Kisha aya zinaendelea kueleza kwamba: Kwa kuwa sasa mumeshabaini kuwa Mwenyezi Mungu SW hana mshirika yeyote katika uumbaji wa ulimwengu na vyote vilivyomo ndani yake, basi msimtafutie mshirika katika kumuabudu. Itakaseni dini yake kwa kuifuata kwa ikhlasi na wala msiwafanye wengine kuwa washirika wake katika upangaji sheria. Hapana shaka kuwa mnapoyafanya haya, huwa mnawaudhi na kuwaumiza sana makafiri wenye inadi na taasubi, lakini msihofu chochote, bali itakaseni na itakelezeni dini yenu kwa ajili ya Allah hata kama kufanya hivyo hakutowapendeza makafiri. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, ulimwengu uliotuzunguka, umejaa ishara za tauhidi. Inatosha kuuangalia kwa jicho la moyo ulimwengu na mazingira yaliyotuzunguka ili kuweza kujitambua kuwa sisi ni viumbe, na tunaye aliyetuumba. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, uumbwaji wa kila kiumbe chenye uhai ni katika ishara za Mwenyezi Mungu; na kudhaminiwa na Yeye Mola riziki anayohitajia kila kiumbe ili aweze kuendelea kuishi, ni ishara yake nyingine! Aidha aya hizi zinatuelimisha kwamba, kuitakasa dini na kila aina ya khurafa, bidaa na uzushi na kuachana na mila na desturi batili pamoja na kufutilia mbali kanuni zinazopingana na dini ni katika ishara za imani ya kweli na ya ikhlasi. Vile vile aya hizi zinatutaka tusiwe na mawazo ya kutaka kuwaridhisha watu katika masuala ya kiitikadi. Tuikubali haki na ukweli na kuufuata, hata kama kufanya hivyo kutawachukiza makafiri na wapinzani wa haki.
Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 15 ambayo inasema:
Ndiye Mwenye daraja za juu, Mwenye A'rshi. Hupeleka Roho kwa amri yake juu ya amtakaye katika waja wake, ili kuonya Siku ya Mkutano.
Aya hii inabainisha baadhi ya sifa na vitendo vya Mwenyezi Mungu Mtukufu; na katika kuendeleza yaliyoashiriwa katika aya zilizotangulia kuhusu kuitakasa na kuitekeleza dini kwa ikhlasi, inasema: Kila pale waumini wanapokuwa na ikhlasi zaidi katika dini yao, daraja zao hupanda juu zaidi, kama ambavyo baina ya Mitume pia, wale waliofaulu zaidi mitihani waliyopewa na Allah na wakaweza kuipandisha ikhlasi yao hadi kwenye mpaka wa juu zaidi, wamepata hadhi na utukufu wa daraja ya juu zaidi. Naam, Allah huipandisha juu daraja ya kila mtu kulingana na kiwango cha ikhlasi yake. Kisha aya inaeleza kwamba: Yeye Allah ndiye mwenye Arshi; na qudra na mamlaka yake yametawala na kuuenea ulimwengu wote; utawala wake hauna mshindani na wala hakuna nguvu na utawala wowote ule uwezao kukabiliana na Yeye. Wakati aya zilizotangulia zilitaja ishara za Allah SW katika uumbaji, aya hii zinaendelea kutaja ishara za Mola katika mfumo wa upangaji sheria na kusema: Mwenyezi Mungu hakuwaacha wanadamu kama walivyo na wafanye vyovyote watakavyo, bali mbali na riziki za kimaada anazowaruzuku viumbe wote, kwa upande wa binadamu, wao amewawekea pia riziki ya kimaanawi. Wasita na waunganishi wa riziki hiyo ni malaika na Mitume, ambao kupitia wao, maonyo na indhari za Allah zinawafikia wanadamu na kuwatahadharisha kwamba kuna Siku ya Kiyama. Kwa hakika Siku ya Kiyama ni siku ya mkutano; mkutano wa mwanadamu na Mola wa ulimwengu, tab’an si wa kuonana kwa uoni wa macho, kwa sababu Yeye Allah Jalla Fi Ulaah si mwenye umbo. Hiyo ni siku ya kukutana pia viongozi wa haki na viongozi wa batili pamoja na wafuasi wao; siku ya kukutana waja wema na wabaya; siku ya kukutana mtu na amali na matendo aliyofanya na siku ambayo dhalimu atakabiliana na kuonana ana kwa ana na aliyemdhulumu, ilhali hakuwa akifikiria hata chembe kuwepo kwa siku hiyo. Naam, lengo la vitabu vyote vya mbinguni na mafundisho ya Mitume ni kuwahadharisha waja wa Mwenyezi Mungu kuhusu siku hiyo ya mkutano mkubwa. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba, njia ya dini ni ya kujijenga kimaanawi na kufikia kwenye ukamilifu wa kiutu; na kila anayejitahidi katika hilo, Allah humuinua na kuipandisha juu hadhi na daraja yake. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa, malaika wa wahyi humteremshia mtu yeyote amtakaye Allah, yale ambayo Yeye Mola ameamuru ateremshiwe mtu huyo. Halikadhalika aya hii inatufunza kwamba, Mitume ni wateule wa Mwenyezi Mungu, na Yeye Mola anawachagua waja hao kwa hekima na kulingana na ujuzi wake mutlaki. Vile vile aya hii inatuelimisha kuwa, Mitume wanampa maonyo mwanadamu kuhusu hatari zinazomkabili katika njia ya maisha anayoipita; na wanafanya hivyo kutokana na huruma na kwa kumtakia heri kiumbe huyo. Kwa hivyo kila mwenye kuzingatia maonyo hayo hufuzu na kuifikia saada na kila mwenye kuyapuuza huhasirika na kuangamia. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 858 ya Qur’ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah, atughufirie madhambi yetu, azikubali toba zetu na aufanye mwema mwisho wetu. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/