Sura ya Ghaafir, aya ya 16-20 (Darsa ya 859)
Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur’ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.
Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur’ani. Hii ni darsa ya 859 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 40 ya Ghaafir. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 16 na 17 za sura hiyo ambazo zinasema:
يَوْمَ هُم بَارِزُونَ ۖ لَا يَخْفَىٰ عَلَى اللَّهِ مِنْهُمْ شَيْءٌ ۚ لِّمَنِ الْمُلْكُ الْيَوْمَ ۖ لِلَّهِ الْوَاحِدِ الْقَهَّارِ
Siku watakayo dhihiri wao. Hapana kitacho fichikana chochote chao kwa Mwenyezi Mungu. Ufalme ni wa nani leo? Ni wa Mwenyezi Mungu Mmoja Mtenza nguvu.
الْيَوْمَ تُجْزَىٰ كُلُّ نَفْسٍ بِمَا كَسَبَتْ ۚ لَا ظُلْمَ الْيَوْمَ ۚ إِنَّ اللَّهَ سَرِيعُ الْحِسَابِ
Leo kila nafsi italipwa kwa iliyoya chuma. Hapana dhulma leo. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwepesi wa kuhisabu.
Katika aya ya mwisho tuliyosoma katika darsa iliyopita tulieleza kwamba, Allah SW amewapa indhari waja wake kuhusu Siku ya Kiyama kupitia Mitume na vitabu vya mbinguni. Aya hizi tulizosoma zinaielezea Siku ya Kiyama na hali maalumu ya siku hiyo kwa kusema: Siku hiyo sitara na vizuizi vyote vitaondolewa, na kila kitu kitafichuka na kudhihirika. Madaftari ya amali yatafunguliwa, na dhahiri na batini za amali na matendo ya watu zitaonekana. Kwa hivyo hakitafichikana kitu chochote. Ukweli ni kwamba, hata hapa duniani pia hakuna kinachofika mbele ya Mwenyezi Mungu. Lakini pamoja na hayo wanadamu hudhani kwamba, wanaweza kumficha Allah baadhi ya wanayoyafanya. Lakini Siku ya Kiyama itawabainikia kuwa kumbe hakukuwa na kitu chochote walichokifanya kilichofichika mbele ya Mwenyezi Mungu, na mambo yao yote yamesajiliwa na kuhifadhiwa kwa umakini kamili. Wakati watakapofufuliwa, wanadamu watahudhurishwa kwenye uwanja adhimu wa Kiyama wakiwa hadhiri na kujionea kila kitu kwa ujudi wao wote, na hakuna kitakachofichika. Bila shaka hiyo itakuwa mandhari ya kushtusha na kustaajabisha! Siku hiyo utawala na mamlaka mutlaki yatakuwa mikononi mwa Allah SW. Bila shaka hapa duniani pia ni Yeye Mola ndiye Mwenye kuutawala ulimwengu wote na kila kilichomo ndani yake, lakini Siku ya Kiyama utawala na mamlaka hayo yatadhihiri kwa namna nyingine mpya kabisa. Huko hazitakuwepo tena tawala za madhalimu na majabari. Utawala wa Allah SW Siku ya Kiyama juu ya kila kitu utakuwa wa namna ambayo, wanadamu hawatokuwa na mamlaka hata kwa viungo vyao wenyewe. Kwa hiyo atakapotaka Mola, mikono, miguu na viungo vingine vya mwili wa mtu vitatoa ushahidi dhidi ya mtu huyo. Hiyo ni siku ya malipo ya amali kwa thawabu au iqabu; na kila mtu atayaona matunda ya amali zake. Ukweli ni kwamba fikra na amali tunazofanya duniani huwa zinaziathiri nafsi na roho zetu, athari ambayo husalia hadi Siku ya Kiyama, ambayo huwa ndio msingi wa malipo tutakayopata siku hiyo. Hapa duniani wanadamu wanadhulumiana laisal kiasi, na kila mwenye nguvu na uwezo humdhulumu mwenzake ili kujistarehesha na kujinufaisha zaidi. Lakini Siku ya Kiyama mtu hatokuwa na uwezo wa kumdhulumu mwenzake, kwa sababu mamlaka na utawala mutlaki utakuwa ni wa Allah SW peke yake, na Yeye Mola si mwenye kuwadhulumu waja wake. Bali atamlipa kila mtu thawabu au adhabu kulingana na amali zake, na tab'an hilo litafanyika haraka na kwa wepesi mkubwa. Kinyume na zilivyo mahakama za duniani, ambazo baadhi ya wakati huchukua miezi kadhaa au mwaka mzima hadi kutoa hukumu ya kesi, Siku ya Kiyama kazi ya kuhesabiwa watu amali zao itafanyika haraka; na kila mtu ataijua hatima yake bila kuchelewesha. Madhumuni ya hilo ni kuhakikisha waovu hawapewi fursa au muhula hata mdogo wa kupumua. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, tusidhani kama kuna kitu tunachoweza kumficha Mwenyezi Mungu, kwa sababu Siku ya Kiyama siri zote zitafichuka na haitawezekana kuficha au kukana kitu chochote kile. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, hakuna yeyote ambaye amali na matendo yake hayatohesabiwa Siku ya Kiyama. Na msingi wa malipo ya thawabu au adhabu atakayotoa Allah utatokana na tuliyoyafanya duniani, si matarajio hewa aliyonayo mtu, nasaba yake au uhusiano wake na yeyote yule. Aidha aya hizi zinatutaka tujue kwamba, ijapokuwa Mwenyezi Mungu ni mwenye mamlaka yasiyo na mshindani katika ulimwengu wote wa uumbaji, na ni wa pekee asiye na mfano katika kuitawala dunia, lakini hatomdhulumu wala kumuonea mtu yeyote.
Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 18 hadi ya 20 ambazo zinasema:
وَأَنذِرْهُمْ يَوْمَ الْآزِفَةِ إِذِ الْقُلُوبُ لَدَى الْحَنَاجِرِ كَاظِمِينَ ۚ مَا لِلظَّالِمِينَ مِنْ حَمِيمٍ وَلَا شَفِيعٍ يُطَاعُ
Na waonye siku inayo karibia, wakati nyoyo zitakapo fika kooni, nao wamejaa huzuni. Madhaalimu hawatakuwa na rafiki, wala mwombezi wa kuitikiwa.
يَعْلَمُ خَائِنَةَ الْأَعْيُنِ وَمَا تُخْفِي الصُّدُورُ
(Mwenyezi Mungu) anajua khiyana ya macho na yanayo ficha vifua.
وَاللَّهُ يَقْضِي بِالْحَقِّ ۖ وَالَّذِينَ يَدْعُونَ مِن دُونِهِ لَا يَقْضُونَ بِشَيْءٍ ۗ إِنَّ اللَّهَ هُوَ السَّمِيعُ الْبَصِيرُ
Na Mwenyezi Mungu huhukumu kwa haki; lakini hao wanao waomba badala yake hawahukumu chochote. Hakika Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye kusikia Mwenye kuona.
Aya hizi zinaendelea kubainisha hali ya Siku ya Kiyama kwa kueleza kwamba: Msidhani Siku ya Kiyama iko mbali, kwa hiyo mfanye chochote kile kinachozipendeza nafsi zenu; jueni kwamba Kiyama kiko karibu na mtakuja kuwajibika kwa yote muyafanyayo. Kiyama ni siku ambayo, kutokana hofu na mshtuko atakaokuwa nao mtu, utadhani roho itakuwa inakaribia kumtoka na moyo unataka kung'oka na kumtokea kooni. Hii ni tashbihi inayobainisha upeo wa juu kabisa wa hali ngumu, ya dhiki na ya tabu isiyomithilika ya Siku ya Kiyama. Naam, hofu ya kufedheheka mbele za watu na wasiwasi wa hisabu makini ya Allah kwa amali zake mtu na adhabu inayomngojea mtu huyo, yote hayo yatawashtua na kuwafadhaisha watu kwa namna isiyoweza kuelezeka kwa maneno yoyote yale. Nyoyoni watajawa na huzuni na majonzi makubwa, lakini ndimi zao zitafumbwa na hawatokuwa na uwezo wa kutamka chochote ili angalau wapumue kidogo na kupata utulivu. Sababu ni kwamba watahudhurishwa mbele ya Mola muadilifu na hawatoweza kupaza sauti zao wala kupiga makelele. Katika hali na mazingira hayo magumu, kila mtu atatamani marafiki zake au wenye satua na ushawishi wasimame kumsaidia, lakini Qur'ani inasema: Hakutakuwa na rafiki wala muombezi, atakayeweza kumsaidia mtu katika hali hiyo au angalau kumpoza na kumliwaza mtu huyo. Kwa sababu watu wote watashughulishwa na hisabu za amali zao na hakuna atakayeweza kumsaidia mwenzake. Kisha aya zinaashiria elimu na ujuzi usio na mpaka wa Mwenyezi Mungu Mtukufu na kueleza kwamba: Pale watu wengine walipokuwa hawana habari, wakati jicho lako linatazama yaliyoharamishwa, huku ukidhani kuwa hakuna anayekuona, Allah SW alikuwepo hapo kushuhudia khiyana iliyofanywa na jicho lako. Na alikuwa na habari pia ya batini yako, ya nia chafu na dhamira mbaya ya ndani ya moyo wako. Bila shaka khiyana ya macho inaweza kuwa ya namna tofauti. Mtu kumuangalia mwanamke asiye maharimu yake, au kuwatizama watu kwa jicho la dharau na la kuwadunisha, yote hayo ni katika mifano ya khiyana ya macho. Hapana shaka, kama mtu ataamini kwamba kuna Siku ya Kiyama ya kuja kuhesabiwa amali zake kwa umakini, kiasi kwamba hata fikra, nia na tazamo la jicho lake, vyote hivyo vinahifadhiwa na vitahesabiwa, bila shaka moyo wake utajengeka na taqua na ufanyaji mambo mema. Naam, Mwenyezi Mungu, ambaye ni mjuzi wa hata harakati za siri za jicho na yaliyofichika ndani ya vifua na mioyo yetu, Siku ya Kiyama ndiye atakayehukumu baina ya watu. Ni hakimu wa pekee; na ghairi yake Yeye hakuna mwingine yeyote awezaye kuhukumu kwa haki. Kwa kuwa asiyekuwa Allah hana elimu na ujuzi wa ya dhahiri na batini, hawezi kuhukumu kwa usahihi; na bila shaka anaweza kudhulumu na kumnyima mtu haki yake. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, mlango wa kuingilia Kiyama ambao ni kifo uko karibu mno. Tujue kwamba kifo hakiko mbali, kwa hiyo tujiandae nacho. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, mshtuko na fazaa ya mahakama ya Siku ya Kiyama kwa upande mmoja; na huzuni na majuto juu ya amali alizotanguliza kwa upande mwingine, vitamdhikisha na kumtaabisha mno mtu muovu, lakini hatokuwa na uwezo hata wa kusema kitu au kupiga mayowe. Vile vile aya hizi zinatuelimisha kwamba, Siku ya Kiyama ni siku ya upweke kwa waovu. Marafiki na wenye satua hawatoweza kuwasaidia waovu kwa lolote, na kimsingi hakuna atakayemfikiria mwenzake. Halikadhalika aya hizi zinatufunza kuwa, imani kwamba, Mwenyezi Mungu anaijua hata nia na dhamira na yaliyofichikana moyoni, humzuia mtu kufanya dhulma na uovu na ni wenzo bora wa kudhibiti tabia na matendo yake. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 859 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah azitakase nyoyo zetu na unafiki, na amali zetu na ria, na ndimi zetu na kusema uongo, na macho yetu na khiyana. Hakika Yeye ni mjuzi wa khiyana za macho na yaliyofichwa na nyoyo zetu. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/