Sura ya Ghaafir, aya ya 21-25 (Darsa ya 860)
Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur’ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.
Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur’ani. Hii ni darsa ya 860 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 40 ya Ghaafir. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 21 na 22 za sura hiyo ambazo zinasema:
أَوَلَمْ يَسِيرُوا فِي الْأَرْضِ فَيَنظُرُوا كَيْفَ كَانَ عَاقِبَةُ الَّذِينَ كَانُوا مِن قَبْلِهِمْ ۚ كَانُوا هُمْ أَشَدَّ مِنْهُمْ قُوَّةً وَآثَارًا فِي الْأَرْضِ فَأَخَذَهُمُ اللَّهُ بِذُنُوبِهِمْ وَمَا كَانَ لَهُم مِّنَ اللَّهِ مِن وَاقٍ
Kwani hawatembei katika ardhi wakaona vipi ulikuwa mwisho wa walio kuwa kabla yao? Walikuwa na nguvu zaidi kuliko wao na athari katika nchi. Na Mwenyezi Mungu aliwatia mkononi kwa sababu ya madhambi yao. Na wala hapakuwa na wa kuwalinda na Mwenyezi Mungu.
ذَٰلِكَ بِأَنَّهُمْ كَانَت تَّأْتِيهِمْ رُسُلُهُم بِالْبَيِّنَاتِ فَكَفَرُوا فَأَخَذَهُمُ اللَّهُ ۚ إِنَّهُ قَوِيٌّ شَدِيدُ الْعِقَابِ
Hayo ni kwa sababu walikuwa wanawajia Mitume wao kwa hoja zilizo wazi, lakini wakawakataa, ndipo Mwenyezi Mungu akawakamata. Bila ya shaka Yeye ni Mwenye nguvu, Mkali wa kuadhibu.
Katika darsa iliyopita tulizungumzia hatima na mwisho mbaya wa watu waovu Siku ya Kiyama. Aya tulizosoma zinawataka watu watalii na kusoma historia ya waliotangulia na kuhoji: Kwa nini wao hawakutafakari kuhusu hali za watu waliokuwa wakiishi katika maeneo tofauti ya dunia na kuona ni hatima gani iliwafika watu hao kutokana maovu na madhambi waliyofanya, ili na wao wakapata funzo na ibra na kuepuka kufuata njia waliyofuata watu hao. Aya hizi zinawahutubu wanadamu kwamba, kama watatembea sehemu tofauti za dunia watajionea magofu na mabaki ya makasri na majengo mbali mbali ya tokea huko nyuma yaliyoachwa na watu hao. Kuna siku watu majabari na watawala madhalimu waliiishi kwenye majengo na makasri hayo na kuwatawala watu, lakini hii leo hakuna athari yao yoyote iliyobaki; na hata katika majengo na makasri yao, ni magofu tu ndiyo yaliyosalia. Kuona athari hizo za historia zilizoachwa na kaumu zilizopita kunaweza kuwa funzo la mazingatio kwetu sisi, ili tujue kwamba madhalimu wataondoka tu, hata kama pale wanapofikia kilele cha nguvu na madaraka yao watakuwa na suhula na nyenzo za kila aina. Sehemu inayofuatia ya aya inasema: Sisi tulitimiza dhima yetu ya kuwafikishia uongofu kwa kuwapelekea Mitume. Lakini badala ya kuikubali haki, walifuata njia ya ukafiri na ukanushaji, wakaikataa na kuipinga haki. Kwa hiyo ikawafika adhabu ya Mola hapa duniani, bila kudhani kama yupo mwenye nguvu kubwa zaidi kuliko wao, anayeweza kusambaratisha haiba na uwezo wao. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, kufanya safari za matembezi na utalii kwa lengo maalumu na kwa ajili ya kupata mafunzo yenye ibra ni jambo lililousiwa na Qur’ani. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, kutalii na kuchunguza historia za waliopita ni jambo la lazima na la busara ili kuweza kujua njia sahihi ya maisha inayopasa kufuata katika dunia ya sasa. Vile vile aya hizi zinatutaka, tusiingiwe na ghururi na kujivuna kwa sababu ya nguvu na nyenzo nyingi na kubwa za kiuchumi, kielimu, kiteknolojia na au hata za kijeshi, kwa sababu vyote hivyo si lolote si chochote mbele ya nguvu na irada ya Allah SW. Halikadhalika aya hizi zinatutaka tujue kwamba, adhabu ya Mwenyezi Mungu haiko akhera pekee. Wakati mwingine, Allah SW huwaonjesha madhalimu makali ya adhabu yake papa hapa duniani. Wa aidha aya hizi zinatuelimisha kuwa, Mwenyezi Mungu hawaadhibu watu mpaka awe ametimiza dhima juu yao ya kuwafikishia uongofu.
Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 23 na 24 ambazo zinasema:
وَلَقَدْ أَرْسَلْنَا مُوسَىٰ بِآيَاتِنَا وَسُلْطَانٍ مُّبِينٍ
Na kwa hakika tulimtuma Musa pamoja na Ishara zetu na hoja zilizo wazi,
إِلَىٰ فِرْعَوْنَ وَهَامَانَ وَقَارُونَ فَقَالُوا سَاحِرٌ كَذَّابٌ
Kwa Firauni na Hamana na Qaruni, wakasema: (Huyu) ni mchawi, mwongo mkubwa.
Aya hizi zinaashiria moja ya mifano ya historia kuhusu adhabu ya Allah ya hapa duniani na kueleza kwamba: Mwenyezi Mungu alimtuma Nabii Musa (as) na akamshushia miujiza kwa ajili ya kumfikishia uongofu aliye mfano wa mtawala dhalimu yaani Firauni, mfano wa wasaidizi wa mtawala kama huyo, yaani Hamana na mtajiri wa kaumu yake kama Qaruni. Kwa msaada wa Mwenyezi Mungu, Nabii Musa alikuwa akifanya miujiza ambayo ilikuwa ishara ya mfungamano wake na ulimwengu wa mbinguni. Mbali na miujiza, Mtume huyo alikuwa pia na hoja na uthibitisho usioweza kukanushika wa ukweli wa utume wake. Lakini msimamo wa Firauni dhalimu na taghuti pamoja na watu wake kwa Musa (as) ulikuwa ni kuifanyia shere miujiza yake kwa kuiita uchawi na mazingaombwe na kuukadhibisha wito aliokuja nao kutoka kwa Allah kwa kudai kwamba ni uongo mtupu. Tab’an historia inaonyesha kuwa, vinara wa udhalimu na ukafiri wamejaribu kila mara kutumia mbinu ya uenezaji uongo na tuhuma chafu ili kufifisha ukweli wa maneno ya waja wateule wa Mwenyezi Mungu na kuzuia yasiwe na taathira kwa watu. Na kwa sababu hiyo Nabii Musa (as) alipewa jukumu la kwenda kuhitimisha dhulma zinazofanywa na watawala madhalimu na wamwagaji damu na kujenga jamii yenye misingi ya haki na uadilifu. Ni wazi kwamba kukubaliwa na watu wito wa Nabii Musa kulimfanya Firauni na watu wake washindwe kuyatumia vibaya na kwa maslahi yao mamlaka na madaraka yao ili waendelee kuwanyonya na kuwadhulumu watu vyovyote watakavyo. Kwa hiyo ili kulinda maslahi yao haramu wakaamua kukabiliana vikali na Musa na wafuasi wake. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, Mitume hawakutumwa kulingania tu watu wamwabudu Mungu mmoja, lakini walitakiwa wawakabili madhalimu pia ili kuondoa dhulma na uonevu katika jamii. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, wakati mwingine, utajiri na madaraka huwa chanzo cha uasi na kuhalifu kutii amri za Allah na kukanyaga haki za watu. Aidha aya hizi zinatuelimisha kwamba, mantiki na miujiza ya Mitume iko wadhiha na inafahamika kwa uwazi kabisa, lakini uchu wa tamaa za vitu vya kimaada na hulka ya kutakabari viliwafanya baadhi ya watu waikatae haki.
Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 25 ambayo inasema:
فَلَمَّا جَاءَهُم بِالْحَقِّ مِنْ عِندِنَا قَالُوا اقْتُلُوا أَبْنَاءَ الَّذِينَ آمَنُوا مَعَهُ وَاسْتَحْيُوا نِسَاءَهُمْ ۚ وَمَا كَيْدُ الْكَافِرِينَ إِلَّا فِي ضَلَالٍ
Basi alipo waletea Haki inayo toka kwetu, walisema: Waueni watoto wanaume wa wale walio muamini na wawacheni hai wanawake wao. Na haviwi vitimbi vya makafiri ila katika upotovu.
Baada ya Firauni na waziri wake Hamana kubaini kwamba hawana mantiki wala hoja ya maana ya kutoa dhidi ya hoja na miujiza ya Nabii Musa (as) waliamua kupanga njama kadhaa za kukabiliana na Mtume huyo. Aya hii inaashiria moja ya mipango yao hiyo ya kishetani. Katika awamu ya kwanza, waliamua kuwaua watu wanaume na vijana waliomwamini Musa (as) na kuwageuza watumwa na wajakazi wanawake wao. Lengo lao lilikuwa ni kuwakandamiza na kuwaadhibu vikali wafuasi wa Mtume huyo ili asitokee mtu yeyote wa kumuamini; na endapo atatokea yeyote atakayethubutu kufanya hivyo, basi wamuulie mbali. Bila shaka huu ndio mwenendo wa tawala zote za kidhalimu na kiistikbari katika zama zote za historia, wa kutumia mbinu tofauti za kuiharibu kwa kuipotosha au kuikandamiza rasilimaliwatu na muhimu ya vijana wa jamii mbalimbali. Lakini katika kadhia ya Nabii Musa (as) mashinikizo na njama za kila aina zilizofanywa na Mafirauni hazikuweza kuuzuia wito wa Mtume huyo; na kinyume na walivyotaka wao, kaumu ya Bani Israil ilizidi kuwa madhubuti na ikaamua kufuata njia ya istikama na kusimama imara kukabiliana na madhalimu. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba, kuua na kuweka vizuizini watu ni mbinu ambayo madhalimu na waistikbari wamekuwa wakiitumia katika zama zote za historia. Kwa hiyo mashinikizo hayo yasiwadhoofishe waumini na kuwazuia kufuata njia ya haki. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa, maadui hupanga njama za kukiharibu na kukiangamiza kizazi cha vijana kwa kutumia vita na umwagaji damu au mbinu nyinginezo ikiwemo ya kueneza uchafu na ufuska. Vilevile aya hii inatutaka tujue kwamba, maadui huwa daima wanakula njama dhidi ya harakati ya kweli ya wanaofuata haki. Lakini kama waumini watainusuru dini ya haki, njama hizo za maadui zitafeli na hatimaye haki itaishinda batili. Hii ndiyo ahadi ya Allah SW.
Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 860 ya Qur’ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah azijaze subra nyoyo zetu, azifanye thabiti imani zetu na atupe ushindi dhidi ya maadui zetu. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/