May 22, 2023 12:57 UTC
  • Sura ya Ghaafir, aya ya 26-28 (Darsa ya 861)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur’ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.

Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur’ani. Hii ni darsa ya 861 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 40 ya Ghaafir. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 26 ya sura hiyo ambayo inasema:

وَقَالَ فِرْعَوْنُ ذَرُونِي أَقْتُلْ مُوسَىٰ وَلْيَدْعُ رَبَّهُ ۖ إِنِّي أَخَافُ أَن يُبَدِّلَ دِينَكُمْ أَوْ أَن يُظْهِرَ فِي الْأَرْضِ الْفَسَادَ

Na Firauni akasema: Niachieni nimuuwe Musa, naye amwite Mola wake Mlezi! Hakika mimi nachelea asije kubadilishieni dini yenu, au akadhihirisha uharibifu katika nchi.

Katika darsa iliyopita tulizungumzia juhudi alizofanya Nabii Musa (as) za kumlingania Firauni na watu wake wito wa tauhidi wa kumwabudu Mola pekee wa haki na kumtaka aache kuwatesa na kuwaadhibu Bani Israil. Aya tuliyosoma inasema: Baada ya kulinganiwa wito huo ulioambatana na miujiza, burhani na hoja madhubuti, Firauni, ambaye alikuwa na hulka ya kiburi na kujikweza aliwageukia wasaidizi wake na watu wake na kuwaambia: Kama tutamwacha Musa hivi hivi, atawachochea watu wafanye uasi dhidi ya utawala wetu, ataibadilisha dini ya watu na kuitumbukiza jamii kwenye lindi la ufisadi na uharibifu. Firauni alitaja sababu mbili hapa za uamuzi aliochukua wa kutaka kumuua Musa (as), akisema: Ninahofia asije akaibadilisha dini yenu, au asije akaeneza uharibifu katika nchi. Hivyo kama nitamnyamazia, Musa ataziathiri mno na kwa kasi nyoyo za watu na kuifanya dini ya Mungu mmoja iipiku dini ya kuabudu masanamu. Kwa hiyo jambo lenye maslahi, ni mimi kumuua yeye haraka iwezekanavyo. Bila shaka katika mtazamo na mantiki ya Firauni dini haikuwa kitu kingine isipokuwa kumwabudu yeye au masanamu yao. Dini kwa mtazamo wa taghuti huyo ilikuwa kitu cha kumwezesha kuwahadaa na kuwapumbaza watu tu na wenzo wa kuupa utakatifu utawala wake wa kijabari, wa umwagaji damu na wa kiimla. Na ufisadi kwa mtazamo wake Firauni, ni harakati ya watu waliosimama dhidi ya utawala wake wa kidhalimu na ya kutaka watu wanyonge wajikomboe na kufuta athari za shirki na ibada ya masanamu katika jamii. Bila shaka mbinu hiyo ya kipropaganda kwa ajili ya kukabiliana na haki haitumiwi na Firauni peke yake, bali katika zama zote za historia majabari na waharibifu wote wamekuwa wakitumia visingizio bandia na vya aina hii ili kuhalalisha jinai na vita vyao dhidi ya waja wateule wa Allah. Kama ambavyo leo hii pia, tunashuhudia mifano hai ya watu wa aina hiyo katika pembe hii na ile ya dunia. Alaa kulli hal, kwa kutoa sababu hizo, Firauni alisema, njia pekee ya kufanya ni kumuua Musa kwa kumwambia: Kama unayodai ni kweli, kwamba wewe umetumwa na Mungu, basi mwite huyo Mungu wako aje akuokoe. Pamoja na hayo, akthari ya washauri wa Firauni hawakuafiki rai yake hiyo. Kwa sababu walikuwa wakijua kwamba, kutokana na hadhi aliyokuwa nayo Nabii Musa (as) kwa Bani Israil, kumuua yeye kutaibua upinzani mkali na kuchochea uasi. Isitoshe, dini yake itapata waumini na wafuasi wengi na utawala utapoteza kikamilifu udhibiti wa hali ya mambo. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba, mantiki ya tawala za kidikteta na kifirauni ni kuwanyamazisha na kuwaua viongozi wa haki. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa, kwa kuwa watawala madikteta na mataghuti wanajua kwamba kuendelea hali iliyopo ndiko kunakowafanya wabaki madarakani, huitangaza harakati yoyote ya kuleta marekebisho katika jamii kuwa ni uchochezi wa kuleta ufisadi na kuvuruga amani na uthabiti. Wao huwaita warekebishaji wa kidini na kijamii kuwa ni watu waharibifu, wenye nia ya kuchafua nidhamu ya jamii. Vile vile aya hizi zinatuelimisha kwamba, kama utulivu na amani utakuwepo katika mifumo ya kidikteta, sababu yake ni uminyaji na ukandamizaji unaofanywa na askari wa utawala na si utulivu na amani halisi inayopasa kuandamana na uhuru wa fikra na maoni.

Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 27 ambayo inasema:

وَقَالَ مُوسَىٰ إِنِّي عُذْتُ بِرَبِّي وَرَبِّكُم مِّن كُلِّ مُتَكَبِّرٍ لَّا يُؤْمِنُ بِيَوْمِ الْحِسَابِ

Na Musa akasema: Mimi najikinga kwa Mola wangu Mlezi na Mola wenu Mlezi anilinde na kila mwenye kiburi asiye iamini Siku ya Hisabu.

Katika kuvikabili vitisho vya kuuliwa alivyotoa Firauni dhidi yake, Nabii Musa (as) alijibu bila hofu na kwa utulivu kamili kwamba, wa kunikinga na kunilinda mimi ni vitisho vyenu ni Mwenyezi Mungu, ambaye ndiye Mola wangu mimi na wenu nyinyi pia; asipotaka Yeye, nyinyi hamna nguvu na uwezo wa kufanya lolote lile. Ni Mungu huyo, ambaye wakati nilipozaliwa na nyinyi mkiwa na dhamira ya kuniua, alimuamuru mama yangu anitie kwenye kisusu na kukitosa kwenye Mto Nile; kisha wewe ukaniopoa majini kwa mikono yako mwenyewe na kunilea chini ya uangalizi wako. Leo pia Mungu huyo huyo ndiye mlinzi wangu; na natumai kwamba atanilinda na shari ya madikteta na waistikbari kama wewe. Lakini kama Yeye atahukumu mimi nife shahidi katika njia hii, niko tayari kwa hilo na wala sina hofu yoyote moyoni. Mimi nimejisabilia kwake, na ninajua lile atakalo Yeye ndilo litalokuwa, si lile mlitakalo nyinyi. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba, tusihofu vitisho vya adui. Tujilinde kwa Allah kwa sababu tujue kwamba mambo yetu yote yako mikononi mwake Yeye na hakuna nguvu yoyote iliyo kubwa na ya juu zaidi ya nguvu zake. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kwamba, kiburi na kutakabari ni hulka ya kifirauni, hata kama mwenye hulka hiyo hatokuwa Firauni. Halikadhalika tunajielimisha kutokana na aya hii kuwa, kutakabari mbele ya haki humfanya mtu asimwamini Allah na Siku ya Malipo.

Tunaihitimisha darsa yetu ya leo kwa aya ya 28 ambayo inasema:

‏ وَقَالَ رَجُلٌ مُّؤْمِنٌ مِّنْ آلِ فِرْعَوْنَ يَكْتُمُ إِيمَانَهُ أَتَقْتُلُونَ رَجُلًا أَن يَقُولَ رَبِّيَ اللَّهُ وَقَدْ جَاءَكُم بِالْبَيِّنَاتِ مِن رَّبِّكُمْ ۖ وَإِن يَكُ كَاذِبًا فَعَلَيْهِ كَذِبُهُ ۖ وَإِن يَكُ صَادِقًا يُصِبْكُم بَعْضُ الَّذِي يَعِدُكُمْ ۖ إِنَّ اللَّهَ لَا يَهْدِي مَنْ هُوَ مُسْرِفٌ كَذَّابٌ

Na akasema mtu mmoja Muumini, katika watu wa Firauni aliye ficha Imani yake: Mtamuuwa mtu kwa sababu anasema Mola wangu Mlezi ni Mwenyezi Mungu? Na hali naye amekujieni na hoja zilizo wazi? Na akiwa ni mwongo basi uwongo wake ni juu yake mwenyewe, na akiwa ni mkweli yatakufikeni baadhi ya hayo anayo kuahidini. Hakika Mwenyezi Mungu hamwongoi apindukiaye mipaka, mwongo mkubwa. 

Miongoni mwa watu wa kasri la Firauni, alikuwepo jamaa yake mmoja ambaye alikuwa amemwamini Nabii Musa (as), lakini alikuwa akificha imani yake ili katika lahadha hatari na hasasi aweze kumsaidia Musa (as). Wakati alipobaini kwamba Firauni ameshadhamiria kumuua Nabii Musa, na maisha ya Mtume huyo wa Allah yako hatarini, alisimama kishujaa, na kwa lugha yenye mguso mkubwa na mantiki nzito akaweza kumuokoa Musa na njama hiyo. Alitumia mantiki hiyo kumkabili Firauni na kumwambia: Madai ya Musa ni kwamba, Mungu ambaye ni Muumba ndiye Mola wa ulimwengu pia; na tadbiri na upangaji wa mambo yote uko mikononi mwake Yeye; Yeye amemtuma Musa kwa ajili ya kuwaelekeza watu kwenye uongofu na amempa miujiza pia kwa ajili ya kuthibitisha ukweli wa Utume wake. Kwa hiyo msifanye pupa kuchukua hatua dhidi yake; kaeni mtafakari vizuri matokeo ya mnayotaka kufanya, kwani mnaweza mkaja mkajuta. Kisha akawaambia: Madai ya Musa yana moja ya hali mbili tu; ama anasema kweli au anasema uongo. Kama anasema uongo, hatima ya uongo wake itamrejea mwenyewe na atafedheheka mbele ya watu. Lakini kama ayasemayo ni kweli, basi baadhi ya yale aliyoahidi kuhusu adhabu ya Mwenyezi Mungu yatathibiti na nyinyi mtaangamizwa. Kwa hiyo si jambo la busara kwa sisi kuchukua hatua ya kumuua. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba, Nabii Musa (as) alijikinga kwa Allah dhidi ya vitisho vya Firauni na pia Mola Mwenyezi alimuamuru mmoja wa watu wa Firauni ampe msaada Mtume wake huyo. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa, baadhi ya wakati huwa kuna ulazima wa kuficha imani na kufanya kazi kwenye vyombo vya utawala wa kidhalimu kwa ajili ya kuepuka vitisho na mashinikizo ya madhalimu au kutekeleza majukumu muhimu; na kufanya hivyo hakuna mgongano wowote na imani ya mtu kwa Allah SW. Aidha aya hii inatutaka tuweke kando taasubi na ukereketwa tunapozungumza na wapinzani kwa kutowaambia, tunayosema sisi ndio kweli na nyinyi hamko sawa. Bali tutumie mbinu ile ile iliyotumiwa na muumini katika watu wa Firauni. (Yeye alisema, Musa ama anasema kweli au anasema uongo. Kama anasema kweli, yale aliyoahidi yatatokea na matokeo ya ukweli wake yataonekana. Na kama anasema uongo, madhara yake yatamrudia mwenyewe). Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 861 ya Qur’ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah azijaze subira nyoyo zetu, azifanye thabiti imani zetu na atulinde na shari za maadui zetu. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/