May 22, 2023 13:02 UTC
  • Sura ya Ghaafir, aya ya 29-33 (Darsa ya 862)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur’ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.

Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur’ani. Hii ni darsa ya 862 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 40 ya Ghaafir. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 29 ya sura hiyo ambayo inasema:

يَا قَوْمِ لَكُمُ الْمُلْكُ الْيَوْمَ ظَاهِرِينَ فِي الْأَرْضِ فَمَن يَنصُرُنَا مِن بَأْسِ اللَّهِ إِن جَاءَنَا ۚ قَالَ فِرْعَوْنُ مَا أُرِيكُمْ إِلَّا مَا أَرَىٰ وَمَا أَهْدِيكُمْ إِلَّا سَبِيلَ الرَّشَادِ

Enyi watu wangu! Leo mna ufalme, mmeshinda katika nchi; basi ni nani atakaye tusaidia kutuokoa na adhabu ya Mwenyezi Mungu kama ikitufikia? Firauni akasema: Sikupeni rai ila ile niliyo iona, wala sikuongozeni ila kwenye njia ya uwongofu.

Katika darsa iliyopita tulisema kuwa, mtu mmoja muumini katika utawala wa Firauni alijaribu kutumia lugha yenye hoja nzito na za mantiki ili kuzuia nia ovu ya taghuti huyo ya kutaka kumuua Nabi Musa (as). Baadhi ya maneno ya muumini huyo tuliyaashiria katika darsa hiyo ya 861. Aya tuliyosoma inaendelea kumnukuu alipomhutubu Firauni na wasadizi wake kwamba: Nyinyi leo mnatawala katika ardhi hii kubwa ya Misri na mnadhibiti mambo yote kwa kila hali, na yeye Musa hana uwezo wa kufanya chochote dhidi yenu. Lakini kama mtamuua, huenda ahadi anayotoa ikawa ya kweli mkafikwa na adhabu ya Mwenyezi Mungu na kuupoteza utawala. Basi fikirieni vizuri kuhusu athari na matokeo ya mnalotaka kufanya. Inavyoonekana, maneno ya muumini huyo yaliwaathiri na kuwalainisha watu wa karibu na Firauni, lakini Firauni mwenyewe alishikilia mtazamo na msimamo wake kwamba lazima Musa (as) auawe kwa kusema, hakuna njia isipokuwa hii; na hatua sahihi ya kuchukua ni hii tu niliyoamua mimi. Hii, tab'an ndio sifa ya majabari na mataghuti wote katika zama zote za historia, ya kujiona wao ndio wenye akili na ujuzi wa kila jambo, na kuhisi rai na mitazamo yao wao tu ndio sahihi. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba, tusiwe na ghururi kwa sababu ya madaraka na kwa kujiona tumestakimu, kwani Allah SW akitaka, vyote hivyo vitatutoka na kutoweka. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa, ni wajibu wa waumini kuwapa indhari na maonyo watu waovu na wahalifu na kuwakataza maovu wanayofanya, hata kama wanayemkabili kumuonya na kumkataza atakuwa mtawala jabari na dhalimu kama Firauni. Vile vile aya hii inatutaka tujue kwamba, hata kama mtu hatokuwa na nafasi na cheo kama cha Firauni, lakini kama hayajali maonyo anayopewa na anajiona mjuzi na mwenye akili kuliko watu wote, ajijue kwamba ana tabia ya kifirauni inayotokana na hulka ya kujikweza na kutaka kuwa juu ya watu wote.

Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 30 na 31 ambazo zinasema:

وَقَالَ الَّذِي آمَنَ يَا قَوْمِ إِنِّي أَخَافُ عَلَيْكُم مِّثْلَ يَوْمِ الْأَحْزَابِ

Na akasema yule aliye amini: Enyi watu wangu! Hakika mimi nakukhofieni mfano wa siku za makundi, 

مِثْلَ دَأْبِ قَوْمِ نُوحٍ وَعَادٍ وَثَمُودَ وَالَّذِينَ مِن بَعْدِهِمْ ۚ وَمَا اللَّهُ يُرِيدُ ظُلْمًا لِّلْعِبَادِ

Mfano wa hali ya watu wa Nuhu na A'di na Thamudi na wale wa baada yao. Na Mwenyezi Mungu hataki kuwadhulumu waja.

Ijapokuwa Firauni alikuwa ameng’ang’ania msimamo na dhamira aliyokuwa nayo ya kumuua Nabii Musa (as) yule muumini katika watu wake hakusitisha juhudi zake za kumlingania taghuti huyo. Aliashiria hatima ya waliotangulia kwa matumaini kwamba, asaa Firauni na watu wake watazinduka na kuangalia upya uamuzi wao. Alisema: Nyinyi mnajua hatima iliyozifika kaumu za Nuh, Aad na Thamud na za baada yao. Mnajua kwamba licha ya kuwa na tamaduni kongwe, ni hatima gani ilizipata kaumu hizo na vipi ziliangamizwa kwa sababu ya kuasi na kushikilia kufuata shirki na ukafiri! Kaumu ya Nuh iliangamizwa kwa tufani na dhoruba kali, kaumu ya Aadi kwa upepo mkali na wa kutisha na kaumu ya Thamud kwa ukelele wa kuhilikisha. Mimi nahofia utamaduni na ustaarabu wa Misri usije ukafikwa na hatima kama ya kaumu hizo, nao pia ukatoweka. Yaliyowafika watu hao yalikuwa matokeo ya matendo yao maovu, kuwakadhibisha au hata kuwaua Mitume; na si kwamba Mwenyezi Mungu anawadhulumu na kuwaonea waja wake. Kwa sababu, Yeye amewaumba, akawaneemesha kwa neema chungu nzima; na huamiliana nao kila mara kwa upole na urahimu; kwa hiyo ni uasi na uchupaji wao mipaka waja ndio unaowafanya wafikwe na adhabu. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, kutaamali na kuzingatia hatima za waliotangulia kunamsaidia mtu kutambua njia sahihi ya kufuata katika mustakabali; na hii ni nukta ambayo Qur’ani inaitilia mkazo sana. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, kama imani na mwenendo usio sahihi vitafikia hadi ya kuwa ada na mazoea ya mtu, ajue kwamba yuko kwenye ukingo wa shimo la maangamizi; na hatima na mwisho wake uko hatarini. Ni kama zilivyokuwa kaumu zilizopita, ambazo itikadi na amali potofu zilikuwa ndio ada na mazowea yao na daima zikawa zinaikadhibisha na kuipinga haki. Wa aidha aya hizi zinatutaka tujue kwamba, baadhi ya wakati, balaa na masaibu ya dunia hutokana na ghadhabu za Allah kwa sababu ya mwenendo na matendo yetu.

Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 32 na 33 ambazo zinasema:

‏ وَيَا قَوْمِ إِنِّي أَخَافُ عَلَيْكُمْ يَوْمَ التَّنَادِ

Na enyi watu wangu! Hakika mimi nakukhofieni Siku ya mayowe.

يَوْمَ تُوَلُّونَ مُدْبِرِينَ مَا لَكُم مِّنَ اللَّهِ مِنْ عَاصِمٍ ۗ وَمَن يُضْلِلِ اللَّهُ فَمَا لَهُ مِنْ هَادٍ

Siku mtakapo geuka kurudi nyuma. Hamtakuwa na wa kukulindeni kwa Mwenyezi Mungu. Na mwenye kuhukumiwa na Mwenyezi Mungu kupotea, basi huyo hana wa kumwongoa.

Muumini katika watu wa Firauni aliendelea kumpa indhari Firauni na wasaidizi wake kwa kuwaambia: Kama adhabu ya Mwenyezi Mungu itashushwa kama ilivyozifika kaumu zilizopita, tujue kwamba hakutakuwa na pa kukimbilia na kupata hifadhi ya kuokoa maisha yetu na kusalimika na adhabu ya Mwenyezi Mungu. Siku hiyo tutaitana na kuombana msaada, lakini sauti hazitafika popote kwa sababu kila mtu atafikiria kuiokoa nafsi yake na wala hatoweza kumsaidia mwenzake. Atakayeweza kuokoka siku hiyo ni yule aliyefuata njia ya uongofu ya Allah na akayafanya mafunzo na mafundisho ya Mitume kuwa ndio dira ya maisha yake. Ni wazi kwamba yeyote atakayekhitari kufuata njia ghairi ya hiyo, ataishia kwenye dhalala na upotofu na kuikosesha nafsi yake uongofu ulioletwa na Allah. Katika aya hizi, kupotoka kwa waja kumenasibishwa na Mwenyezi Mungu, lakini ukweli ni kwamba upotofu huo ni matokeo ya amali ovu za mtu na machaguo yasiyo sahihi aliyofanya, ambayo ndiyo sababu ya Allah kumwacha mtu huyo kama alivyo aselelee kwenye hali aliyo ya upotofu. Kwa maneno mengine, Mwenyezi Mungu hamuondoi mtu kwenye njia ya uongofu, lakini makafiri na wafanya maovu hujitafutia wenyewe sababu za kuukosa uongofu na kutumbukia kwenye lindi la maangamizi ya upotofu kutokana na kukufuru na kughiriki kwao kwenye dimbwi la madhambi. Ni mithili ya mtoto aliyeshikwa mkono na baba yake ili aweze kutembea. Huyo bila shaka ataanguka tu na kuumia endapo atataka atembee mwenyewe bila kusaidiwa. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, katika majukumu ya waumini na watu wenye huruma ni kuwatahadharisha waovu na matokeo mabaya ya matendo yao. Ni kama walivyo wazazi wanaomwonya mtoto wao asiukaribie moto na kumtahadharisha na hatari ya kufanya hivyo. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa kuongoka na kupotoka kuko mikononi mwa Allah ijapokuwa utangulizi wake unatokana na mtu mwenyewe. Halikadhalika aya hizi zinatutaka tujue kwamba, hakuna njia ya tatu baada ya uongofu na upotofu. Ikiwa mtu hatochagua kufuata uongofu wa Allah ataishia kwenye dhalala; na hakuna chaguo la tatu baada ya mawili hayo. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 862 ya Qur’ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atuonyeshe haki na atupe taufiki ya kuifuata na atuonyeshe batili na atuwezeshe kuiepuka. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/