May 22, 2023 13:18 UTC
  • Sura ya Ghaafir, aya ya 34-37 (Darsa ya 863)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur’ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.

Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur’ani. Hii ni darsa ya 863 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 40 ya Ghaafir. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 34 ya sura hiyo ambayo inasema:

وَلَقَدْ جَاءَكُمْ يُوسُفُ مِن قَبْلُ بِالْبَيِّنَاتِ فَمَا زِلْتُمْ فِي شَكٍّ مِّمَّا جَاءَكُم بِهِ ۖ حَتَّىٰ إِذَا هَلَكَ قُلْتُمْ لَن يَبْعَثَ اللَّهُ مِن بَعْدِهِ رَسُولًا ۚ كَذَٰلِكَ يُضِلُّ اللَّهُ مَنْ هُوَ مُسْرِفٌ مُّرْتَابٌ

Na alikwisha kujieni Yusuf zamani kwa dalili zilizo wazi, lakini nyinyi mliendelea katika shaka kwa yale aliyo kuleteeni; mpaka alipo kufa mkasema: Mwenyezi Mungu hataleta kabisa Mtume baada yake. Kama hivyo Mwenyezi Mungu humwacha kupotea anaye pindukia mipaka katika maasi anaye jitia shaka.

Katika darsa iliyopita tulisema kuwa, muumini katika watu wa Firauni, ambaye alikuwa miongoni mwa jamaa zake wa karibu na mtu wa utawala wake alitumia njia na mbinu tofauti ili kuzima njama ya taghuti huyo ya kumuua Nabii Musa (as). Katika aya tuliyosoma, muumini huyo anaashiria historia ya Nabii Yusuf (as) na kusema: Yusuf alikuwa mmoja wa Mitume wa Mwenyezi Mungu na haujapita muda mrefu sana tangu alipoondoka. Lakini licha ya kuja na hoja mbali mbali za kuthibitisha Utume wake, watu wengi walitafuta visingizio visivyo na maana wala mantiki ili kutilia shaka wito wake na kutoyakubali maneno ya haki aliyowaambia, yenye hoja za wazi, zenye kufahamika na kukubalika. Na baada ya yeye kuaga dunia, walitamani Mwenyezi Mungu asiwaletee Mtume mwengine, ili waweze kuendelea kufanya anasa, maovu na vitendo vyao vingine vichafu bila kukemewa wala kulalamikiwa na mtu yeyote. Ni wazi kwamba watu wa aina hii hawana haja ya kuisikia na kuikubali haki. Wanachotaka wao ni kufuata hawaa na matamanio ya nafsi zao, kwa hiyo wanajikosesha wenyewe uongofu wa Allah. Kuamiliana namna hii na Mitume na mafundisho waliyokuja nayo, ambayo ni aina mojawapo ya shaka ya kufurutu mpaka, humfanya mtu apotoke. Ni wazi kwamba kutilia jambo shaka kunakubaliwa na elimu na akili timamu; lakini haifai kubaki na shaka au kutawaliwa na dhana mbaya isiyo na msingi, kwani hali hiyo huzusha wasiwasi katika fikra na matendo ya mtu na kumfanya asiweze kuendelea na kupiga hatua. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba, mwenendo, imani na mielekeo ya kaumu zilizopita inaacha taathira kwa vizazi vyao vinavyofuatia. Kwa hiyo, kwa kutambua historia ya kaumu hizo inawezekana kutabiri mwenendo wa vizazi vya baada yao pia. (Ni kwa kuzingatia hilo, ndio muumini katika watu wa Firauni akawaambia kina Firauni ya kwamba, ikiwa nyinyi leo hamumwamini Musa, huko nyuma mlikataa kumuamini Yusuf pia). Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa, kama shaka itamfanya mtu atafakari na kulitafiti jambo, hapo huwa na thamani; lakini kama ataendelea kubaki nayo tu mpaka ikamtia kwenye dhana mbaya na kumdumaza kifikra, huwa ni kitu chenye madhara. Vile vile aya hii inatuelimisha kuwa, kupotoka duniani na akhera ndio adhabu itayowafika watu ambao, kwa sababu ya hawaa na matamanio ya nafsi zao waliamua kupinga bila hoja wito wenye mantiki wadhiha na ya wazi uliolinganiwa na Mitume.

Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 35 ambayo inasema:

الَّذِينَ يُجَادِلُونَ فِي آيَاتِ اللَّهِ بِغَيْرِ سُلْطَانٍ أَتَاهُمْ ۖ كَبُرَ مَقْتًا عِندَ اللَّهِ وَعِندَ الَّذِينَ آمَنُوا ۚ كَذَٰلِكَ يَطْبَعُ اللَّهُ عَلَىٰ كُلِّ قَلْبِ مُتَكَبِّرٍ جَبَّارٍ

 Wale ambao wanajadiliana katika Ishara za Mwenyezi Mungu bila ya dalili yoyote iliyo wafikia, ni chukizo kubwa mbele ya Mwenyezi Mungu na mbele ya walio amini. Hivi ndivyo Mwenyezi Mungu apigavyo muhuri juu ya kila moyo wa jeuri anaye jivuna.

Aya hii inatoa ufafanuzi zaidi wa kuwatambulisha watu waliopindukia mpaka katika shaka, wakawa hawako tayari kukubali neno lolote la haki na kueleza kwamba, hao ni watu wanaopenda mijadala na kubishana tu, na si kuifahamu haki na kuiamini. Kwa hiyo chochote utachowaambia hawatokitafakari; na bila ya kuwa na hoja ya msingi ya kutoa, watayakataa tu maneno ya haki. Kwa kutumia lugha ya mazungumzo na majadiliano, huwa wanajaribu kujionyesha kuwa ni watu wa mantiki, lakini walivyo hasa, ni watu wakaidi na wenye kiburi. Kwa hiyo hoja yoyote utayowapa wataitafutia kisingizio chochote ili kuikataa. Hapana shaka kuwa, kutetea batili na kupinga bila hoja aya za Mwenyezi Mungu, kuna athari na matokeo yenye madhara, yakiwemo ya kupotoka mtu mbishi na mkaidi. Sababu ni kuwa, kuifanyia haki inadi na ukaidi huudumaza uwezo wa kufikiri wa mtu akashindwa kutambua usahihi wa mambo. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba, majadiliano ni moja ya njia zinazotumika katika midahalo ya kielimu, tab’an kwa mtu anayetafuta ukweli, si anayezungumza bila hoja wala mantiki, akapinga maneno ya wenzake kutokana na kiburi na ukaidi. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa, haifai waumini kuwa watu wanaojadili mambo bila mantiki, bali inapasa wazungumze kwa mantiki kiasi cha kuwafanya watu wengine wahisi kuwa, kama watazungumza bila hoja na mantiki, wayasemayo hayatokuwa na thamani kwao.

Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 36 na 37 ambazo zinasema:

وَقَالَ فِرْعَوْنُ يَا هَامَانُ ابْنِ لِي صَرْحًا لَّعَلِّي أَبْلُغُ الْأَسْبَابَ

Na Firauni akasema: Ewe Hamana! Nijengee mnara ili nipate kuzifikia njia,

أَسْبَابَ السَّمَاوَاتِ فَأَطَّلِعَ إِلَىٰ إِلَٰهِ مُوسَىٰ وَإِنِّي لَأَظُنُّهُ كَاذِبًا ۚ وَكَذَٰلِكَ زُيِّنَ لِفِرْعَوْنَ سُوءُ عَمَلِهِ وَصُدَّ عَنِ السَّبِيلِ ۚ وَمَا كَيْدُ فِرْعَوْنَ إِلَّا فِي تَبَابٍ

Njia za mbinguni ili nikamwone Mungu wa Musa. Na kwa hakika mimi bila ya shaka namjua kuwa ni mwongo tu. Na hivi ndivyo Firauni alivyo pambiwa ubaya wa vitendo vyake, na akazuiliwa Njia. Na vitimbi vya Firauni havikuwa ila katika kuangamia tu. 

Katika hali na mazingira yale hasasi, yule mtu muumini na shujaa alifanya kazi kubwa, kwa kujitahidi kutumia njia tofauti ili kuzibadilisha nia chafu za Firauni na watu wake. Hatimaye maneno yake mazito na ya busara yalimgusa Firauni, yakateteresha azma aliyokuwa nayo ya kumuua Nabii Musa (as) na akaghairi kufanya hivyo. Pamoja na hayo, ghururi aliyokuwa nayo Firauni haikumtoka; na katika kuendeleza hatua zake za kishetani na kiafriti akaibuka na wazo jengine jipya la kuamuru ujengwe mnara mrefu wa kupanda kuelekea mbinguni ili kwa dhana yake akafuatilie habari kuhusu Mungu wa Musa. Hapana shaka, hiyo ilikuwa hila tu ya kutaka kuwahadaa watu, kwa sababu Musa (as) hakuwa amedai kwamba Mungu wangu mimi yuko mbinguni, au ni mwenye kuweza kugusika na kuonekana, hata itoshe kwa mtu kukwea kipando kirefu ili aweze kumuona na kusikia maneno yake. Firauni alitaka kufanya vitimbi na uafriti huo ili kuzighilibu na kuziteka akili za watu wa kawaida, ziache kufikiria suala la Utume wa Nabii Musa kutakowafanya wamsaidie na kuungana naye Mtume huyo wa Allah. Utumiaji mbinu za kuhadaa watu ilikuwa moja ya hatua chafu alizokuwa akichukua Firauni. Hapana shaka chanzo cha kupotoka kwake ni kiburi, ghururi na ubinfasi aliokuwa nao, ambavyo vilimpambia matendo yake maovu akayaona mazuri. Kwa sababu hiyo, akashindwa kuifuata njia ya haki, njama zake zikafeli na mwishowe akaangamia. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, watu wasio na hoja na mantiki hujaribu kufanya vitimbi na makeke ili kuziathiri fikra na mitazamo ya watu kwa manufaa yao. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, kujionyesha kuwa na nguvu na kuhadaa watu ni moja ya mbinu zinazotumiwa na tawala za kidhalimu na kitaghuti kwa ajili ya kuwatwisha watu mitazamo yao na kuzidi kuwadhibiti na kuwatawala. Aidha aya hizi zinatuelimisha kwamba, ghururi na kiburi humpambia mtu maovu yake akayaona ni mambo mazuri na hivyo kutofikiria kujisahihisha na kujirekebisha. Hali kadhalika aya hizi zinatutaka tujue kuwa, mataghuti daima huwawekea waumini vikwazo na vizuizi. Hata hivyo ikiwa waumini watasimama imara na kwa uthabiti katika njia ya haki, mwisho wake watashinda na madhalimu watahasirika na kupata hasara kubwa. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 863 ya Qur’ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah azijaze subira nyoyo zetu, azifanye thabiti imani zetu na atulinde na shari za maadui zetu. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/