May 23, 2023 13:34 UTC
  • Sura ya Ghaafir, aya ya 38-42 (Darsa ya 864)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur’ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.

Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur’ani. Hii ni darsa ya 864 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 40 ya Ghaafir. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 38 hadi 40 za sura hiyo ambazo zinasema:

وَقَالَ الَّذِي آمَنَ يَا قَوْمِ اتَّبِعُونِ أَهْدِكُمْ سَبِيلَ الرَّشَادِ

Na yule aliye amini alisema: Enyi watu wangu! Nifuateni mimi, nitakuongozeni njia ya uongofu.

يَا قَوْمِ إِنَّمَا هَٰذِهِ الْحَيَاةُ الدُّنْيَا مَتَاعٌ وَإِنَّ الْآخِرَةَ هِيَ دَارُ الْقَرَارِ

Enyi watu wangu! Hakika maisha haya ya dunia ni starehe ipitayo tu, na hakika Akhera ndiyo nyumba ya daima.

مَنْ عَمِلَ سَيِّئَةً فَلَا يُجْزَىٰ إِلَّا مِثْلَهَا ۖ وَمَنْ عَمِلَ صَالِحًا مِّن ذَكَرٍ أَوْ أُنثَىٰ وَهُوَ مُؤْمِنٌ فَأُولَٰئِكَ يَدْخُلُونَ الْجَنَّةَ يُرْزَقُونَ فِيهَا بِغَيْرِ حِسَابٍ

Mwenye kutenda uovu hatalipwa ila sawa na huo uwovu wake, na anaye tenda wema, akiwa mwanamume au mwanamke, naye ni Muumini, basi hao wataingia Peponi, waruzukiwe humo bila ya hisabu.

Katika darsa iliyopita tulisema kuwa, Firauni, alidhamiria kumuua Nabii Musa (as) ili kwa dhana yake aweze kuepukana na shari ya mtu anayedai kuwa ni Mtume. Tukaeleza kuwa mmoja wa watu wa utawala wake ambaye alikuwa amemwamini Musa (as), lakini akawa anaficha imani yake, aliamua kwanza kuzungumza na Firauni na wasaidizi wake ili kumrai taghuti huyo abadilishe uamuzi wake wa kumuua Nabii Musa. Maneno yake yaliweza kumuathiri Firauni na kumfanya aakhirishe kwa muda mpango wa kumuua Mtume huyo wa Allah. Pamoja na hayo, ili kumfedhehesha Musa (as) alimuamuru waziri wake aitwaye Hamana ajenge mnara mrefu ili yeye Firauni apande kwenda kuona kama huyo Mungu anayedai Musa, yuko kweli huko mbinguni au la? Ni wazi kwamba Nabii Musa hakuwa amedai hivyo, lakini Firauni aliamua kufanya hivyo ili kuwahadaa watu. Kwa hiyo ilipofika hatua hiyo, yule mja muumini aliyaelekeza maneno yake kwa watu ili kuwaelimisha wasije wakatekwa na kuhadaiwa na maneno ya kichochezi na hatua za kimaonesho za Firauni. Muumini huyo katika jamaa wa Firauni aliwaambia watu: Njia ya kufuata ni hii ninayokuonesheni mimi. Katika maneno yake, aliashiria nukta mbili muhimu: Ya kwanza ni kwamba, kuishi kwa mwanadamu hakuishii katika dunia hii. Maisha ya dunia ni kitu kinachomalizika haraka. Siku hizi chache za uhai zinapita kwa kasi na mauti yatatunyaka sisi sote. Na baada ya kufa tutaelekea katika ulimwengu mwingine, ambayo ndiyo yatakayokuwa makazi yetu ya milele. Na nukta ya pili ni kuwa, yatakayomfaa mtu katika ulimwengu huo ni mema aliyofanya hapa duniani, kwa sababu ulimwengu huo ni wa malipo ya thawabu na adhabu, na dunia hii na ya amali na matendo. Na malipo watakayolipwa watu huko yatafanywa kulingana na amali njema au mbaya walizofanya. Tab'an katika suala hilo hawatafautishwi kwa namna yoyote ile mwanamke na mwanamme bali wote watahukumiwa kwa usawa kamili mbele ya mahakama ya Mwenyezi Mungu. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, mtu muumini huwa daima anafikiria kuwafikishia wenzake mwongozo na wito wa uongofu na wala jukumu hilo halimuondokei wakati wowote ule. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, dunia si ya kudumu; akhera ndiyo ya kudumu na ndiyo makazi ya milele ya mwanadamu. Kwa hiyo kuna ulazima wa mtu kuutumia uhai wake wa hapa duniani kwa namna sahihi na inayostahiki na daima ajitahidi kufanya mambo mema ili yaje yamfae Siku ya Kiyama. Halikadhalika tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba, kufikia ukamilifu wa kiutu na kupata saada ya kufuzu akhera hakuhusiani na jinsia ya mtu; na katika hili hakuna tofauti yoyote baina ya mwanamke na mwanamme. Vile vile aya hizi zinatutaka tujue kuwa, imani bila amali na matendo haimsaidii mtu, kama ambavyo amali zifanywazo bila kuwa na imani huishia hapa duniani na wala hazifiki akhera. Kwa hiyo, imani na amali, kila moja peke yake haviwezi kumfanya mtu afuzu na kuokoka Siku ya Kiyama.

Tunaihitimisha darsa yetu hii kwa aya ya 41 na 42 ambazo zinasema:

وَيَا قَوْمِ مَا لِي أَدْعُوكُمْ إِلَى النَّجَاةِ وَتَدْعُونَنِي إِلَى النَّارِ

Na enyi watu wangu! Kwa nini mimi nakuiteni kwenye uwokofu, nanyi mnaniita kwenye Moto? 

تَدْعُونَنِي لِأَكْفُرَ بِاللَّهِ وَأُشْرِكَ بِهِ مَا لَيْسَ لِي بِهِ عِلْمٌ وَأَنَا أَدْعُوكُمْ إِلَى الْعَزِيزِ الْغَفَّارِ

Mnaniita nimkufuru Mwenyezi Mungu na nimshirikishe na kitu ambacho sina elimu nacho, nami nakuiteni kwa Mwenye nguvu Mwingi wa maghufira? 

Kutokana na maelezo ya aya hizi inaonesha kuwa, baada ya hatua aliyofikia, muumini katika jamaa wa Firauni hakuweza tena kuficha imani yake, kwa hivyo akalazimika kueleza bayana na kwa uwazi zaidi msimamo wake kuhusu tauhidi na shirki. Kwa hiyo akawaelekea wakubwa wa kaumu yake waliomshauri aache ulinganiaji aliofanya, na kuwaambia: Nyinyi mumeathiriwa na shirki na mnamuitakidi Firauni, ambaye hahusiki kwa namna yoyote katika uumbaji au uendeshaji wa ulimwengu huu, kuwa ni mungu; na kwamba uendeshaji wa mambo yenu uko mikononi mwake. Mnavyoamini, yeye ndiye mwenye uwezo wa kukuamulieni kila jambo, na nyinyi mna wajibu wa kumtii. Nyinyi mnavifanya vitu kuwa washirika wa Mwenyezi Mungu bila ya kuwa na mantiki wala hoja yoyote; na mkazikubali fikra hizo za khurafa na uzushi kwa makisio na dhana tu. Mnanitaka nimkufuru Mungu pekee wa haki na kumpangia washirika bila kuwa na elimu na ujuzi wowote wa jambo hilo. Nyinyi mnanitaka mimi nizikubali imani zenu batili na potofu, wakati ninajua kwamba fikra na amali hizi za shirki hazina matokeo mengine isipokuwa kunifanya mimi pia nifikwe na hatima sawa na yenu ya adhabu ya moto. Njia mnayonitaka nifuate ni ya giza, hatari na ya upotofu, lakini mimi ninakuelekezeni kwenye njia yenye mwanga; yaani njia ya Mwenyezi Mungu, Muweza na Mwenye Nguvu, lakini pia ni Msamehevu na Mwenye kughufiria madhambi. Mimi ninakutakeni muachane na wote mnaowashirikisha na Mwenyezi Mungu, wawe ni vitu au binadamu. Nakutakeni mumtii na kumuabudu Mwenyezi Mungu tu, ambaye qudra na utawala wake umeenea ulimwengu wote na rehma na uraufu wake umevienea viumbe vyote, hususan wale wanaotubia kwa kuacha kufuata njia ya upotofu. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, mtu muumini asiwe na hofu kwa kuwa peke yake katika kuwalingania watu haki; na aitangaze tu haki kwa hoja na mantiki; na wala asiingiwe na shaka wala kuathiriwa na umati mkubwa wa kundi la upotofu. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, kufuzu na kuokoka kwa mtu kunategemea imani ya tauhidi na kufanya amali njema. Kumuitakidi mtu au kitu chochote kuwa ni mshirika wa Allah katika uendeshaji wa masuala ya ulimwengu kutamsababishia anuai za hilaki, mateso na adhabu duniani na akhera. Aidha aya hizi zinatuelimisha kwamba, shirki haina msingi wowote wa akili na mantiki; ni imani ya uzushi ambayo baadhi ya wakati hutokana na ujinga, na wakati mwingine husababishwa na hawaa na matamanio ya mtu ya kupata matakwa yake ya binafsi. Wa aidha aya hizi zinatutaka tujue kuwa, mbali na Allah SWT kuwa katika upeo wa juu kabisa wa qudra, uwezo na nguvu, lakini wakati huohuo rehma na usamehevu wake unawaenea waja wake wote. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 864 ya Qur’ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atughufirie madhambi yetu, atukubalie dua zetu na aufanye mwema mwisho wetu. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/