May 23, 2023 13:39 UTC
  • Sura ya Ghaafir, aya ya 43-47 (Darsa ya 865)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur’ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.

Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur’ani. Hii ni darsa ya 865 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 40 ya Ghaafir. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 43 na 44 za sura hiyo ambazo zinasema:

لَا جَرَمَ أَنَّمَا تَدْعُونَنِي إِلَيْهِ لَيْسَ لَهُ دَعْوَةٌ فِي الدُّنْيَا وَلَا فِي الْآخِرَةِ وَأَنَّ مَرَدَّنَا إِلَى اللَّهِ وَأَنَّ الْمُسْرِفِينَ هُمْ أَصْحَابُ النَّارِ

Bila ya shaka mnaye niitia (kumuabudu) hastahiki wito duniani wala Akhera. Na hakika marejeo yetu ni kwa Mwenyezi Mungu. Na wanao pindukia mipaka ndio watu wa Motoni!

فَسَتَذْكُرُونَ مَا أَقُولُ لَكُمْ ۚ وَأُفَوِّضُ أَمْرِي إِلَى اللَّهِ ۚ إِنَّ اللَّهَ بَصِيرٌ بِالْعِبَادِ

Basi mtayakumbuka ninayo kuambieni. Nami namkabidhi Mwenyezi Mungu mambo yangu. Hakika Mwenyezi Mungu anawaona waja (wake).

Katika darsa iliyopita tulisema kuwa, wakati muumini katika jamaa wa Firauni alipofikia hatua ya kuwakabili watu na kuzungumza nao moja kwa moja aliacha kufanya taqia, yaani kuficha imani yake, akawaeleza bayana kuhusu tauhidi na shirki pamoja na athari na matokeo yake. Aya tulizosoma zinaendelea kusimulia aliyowaeleza watu hao aliposema: Nyinyi mnanitaka niache kumwabudu Mungu pekee wa haki na kuabudu masanamu yenu, ilhali masanamu haya yasiyo na hisi yoyote, hayamsaidii mtu duniani wala akhera; hayawezi kusema wala kumuongoza mtu njia yoyote na wala hayana uwezo wa kutatua tatizo au kumuondolea mtu shida yoyote aliyo nayo. Mwisho wetu na marejeo yetu sote ni kwa Mwenyezi Mungu; na tutasailiwa na kuwajibika kwa tuliyoyafanya. Ni wazi kwamba, yeyote anayeabudu masanamu badala ya Mwenyezi Mungu, makazi yake Siku ya Kiyama yatakuwa motoni, kwa sababu ameiacha njia ya haki na amepindukia mipaka aliyowekewa. Enyi watu! Nakuelezeni kinagaubaga kwamba, mimi nimemwamini Allah na nimemsabilia na kumkabidhi Yeye mambo yangu yote; sihofu wala siogopi vitisho vyenu, wala sitishiki kwa wingi wenu na nguvu zenu. Sababu ni kuwa, nimeisabilia nafsi yangu kwa Yule ambaye qudra na nguvu zake hazina kikomo; na anazielewa vyema hali za waja wake pamoja na fikra na matendo yao. Lakini kinachosikitisha ni kwamba, mtakuja kubaini ukweli wa maneno yangu mtakaposimamishwa mbele ya mahakama ya Mwenyezi Mungu, pale ghadhabu na adhabu ya Mola itapokuwa imeshakukabilini. Wakati huo mtakuwa mumechelewa, kwa sababu hakutakuwa na njia ya kurudi tena duniani. Kwa lugha yake wadhiha na ya ufasaha, muumini katika watu wa Firauni alisimama imara kukabiliana na kaumu yake, akatangaza wazi imani yake na kuipambanua njia yake ya tauhidi na ile ya shirki waliyoifuata watu wa kaumu yake. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, tutumie hoja na mantiki kubainisha imani yetu juu ya Allah na kumkana kila asiyekuwa Yeye; na tutumie njia hiyo kuwalingania wengine pia kumwamini na kumuabudu Mwenyezi Mungu SWT. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, israfu haiko katika mali tu; kuufuja mtu umri wake, uwezo na kipaji chake katika njia za batili na upotofu ni miongoni mwa vielelezo vikubwa vya israfu; na kutamfanya afikwe na adhabu kali. Kwa hiyo tuwe makini na tuwe na hadhari katika kuchagua njia ya kufuata maishani. Halikadhalika tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba, baada ya kutekeleza wajibu wetu, tujilinde kwa Mwenyezi Mungu SWT na vitisho na njama za maadui na kumtegemea Yeye Mola tu, kwa sababu qudra na uwezo wa Allah uko juu ya uwezo na nguvu zote. Wa aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kuwa, tusabilie na kukabidhi mambo yetu yote kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa sababu Yeye ni Mjuzi na Mwenye uelewa kamili wa hali zetu.

Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 45 na 46 ambazo zinasema:

فَوَقَاهُ اللَّهُ سَيِّئَاتِ مَا مَكَرُوا ۖ وَحَاقَ بِآلِ فِرْعَوْنَ سُوءُ الْعَذَابِ

Basi Mwenyezi Mungu akamlinda na ubaya wa hila walizo zifanya. Na adhabu mbaya itawazunguka watu wa Firauni.

النَّارُ يُعْرَضُونَ عَلَيْهَا غُدُوًّا وَعَشِيًّا ۖ وَيَوْمَ تَقُومُ السَّاعَةُ أَدْخِلُوا آلَ فِرْعَوْنَ أَشَدَّ الْعَذَابِ

Wanaonyeshwa Moto asubuhi na jioni. Na itapo fika Saa ya Kiyama (patasemwa): Waingizeni watu wa Firauni katika adhabu kali kabisa! 

Muumini katika jamaa wa Firauni alijilinda kwa Allah SWT na vitisho vikali vya kina Firauni na njama zao. Mwenyezi Mungu Mtukufu alizima njama zao, akamlinda na nia zao ovu na akamfanya imara na mwenye moyo thabiti katika njia ya imani na tauhidi. Lakini kinyume na muumini huyo, Allah SWT aliwaadhibu adhabu kali Firauni na watu wake kwa sababu ya inadi na ukaidi waliyoifanyia haki na uadui wao kwa walinganiaji wa njia ya uongofu. Kama tujuavyo, kwa mujibu wa aya nyingine za Qur’ani, Nabii Musa (as) na Bani Israil waliuvuka salama Mto Nile, na Firauni na wafuasi wake waliomfuata katika upotofu waliangamizwa kwa kugharikishwa kwenye mto huo. Hata kama Firauni na watu wake walighariki majini lakini kiuhakika waliuingia moto wa barzakhi; na mpaka Siku Kiyama wataendelea kuonja adhabu kutwa kucha, asubuhi na jioni; na tab’an aina hiyo ya adhabu ni ya barzakhi, lakini aina nyingine iliyoashiriwa ni adhabu kali zaidi ya Siku ya Kiyama. Kwa mujibu wa aya za Qur’ani, baada ya ulimwengu huu, na katika kipindi cha baada ya kufa hadi kufufuliwa Siku ya Kiyama, mwanadamu anaishi katika ulimwengu mwingine uitwao barzakhi. Katika kipindi hicho huonjeshwa sehemu malipo yake ya raha za peponi au adhabu ya motoni. Hakika ulimwengu wa barzakhi ni moja ya bustani za peponi kwa watu wema na shimo mojawapo la moto wa jahanamu kwa watu wabaya. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, kama tutatawakali na kumtegemea Allah, atatulinda na shari ya maadui madhalimu. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, tukimtegemea Allah, si tu atatusaidia, lakini atawadhoofisha na kuwaangamiza pia maadui waliokula njama dhidi yetu. Vilevile tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba, malipo ya adhabu kwa madhalimu huanza mara baada ya kufa na kuangamizwa kwao, lakini Siku ya Kiyama ndipo watakapokamilishiwa malipo yao ya adhabu kali kabisa isiyohimilika.

Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 47 ambayo inasema:

وَإِذْ يَتَحَاجُّونَ فِي النَّارِ فَيَقُولُ الضُّعَفَاءُ لِلَّذِينَ اسْتَكْبَرُوا إِنَّا كُنَّا لَكُمْ تَبَعًا فَهَلْ أَنتُم مُّغْنُونَ عَنَّا نَصِيبًا مِّنَ النَّارِ

Na watapo hojiana huko Motoni, wanyonge watawaambia walio jitukuza: Hakika sisi tulikuwa wafuasi wenu, basi je, hamtuondolei sehemu ya huu Moto?

Aya zilizopita zimezungumzia adhabu kali wanayopata kina Firauni katika ulimwengu wa barzakhi na kisha kuingizwa kwao motoni. Aya hii inaashiria sehemu moja ya mazungumzo yatakayojiri ndani ya jahanamu baina ya watu wa motoni na kueleza kwamba: Watu watakaotiwa motoni watagombana na kulumbana, kwa kila mmoja kumbebesha lawama mwenzake na kujaribu kuitoa hatiani nafsi yake, ilhali Allah SWT anawapa watu jaza na malipo ya amali zao kwa uadilifu na katu hamtii motoni mtu bila ya sababu. Ni kawaida kwa wale waliokuwa wafuasi wa fikra na itikadi potofu hapa duniani, ambao waliwafuata na kuwatii kibubusa vinara wa ukafiri, kutaraji kwamba kuna kitu viongozi wao hao wataweza kufanya huko akhera ili wao waokoke au angalau wapate tahafifu ya adhabu. Lakini ukweli ni kwamba, viongozi hao wa dhulma, ufisadi na ukafiri watafikwa na adhabu kali kiasi cha kutoweza kujisaidia hata wao wenyewe, seuze kuwasaidia wafuasi wao. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba, kama urafiki na mafungamano ya duniani ya watu hayatoendana na kufuata njia ya haki, Siku ya Kiyama yatageuka kuwa uadui na uhasama baina ya watu. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, shida na matatizo ya dunia hayamjuzishii mtu kujidhalilisha na kuwaridhia viongozi madhalimu na watawala mataghuti. Aidha tunajielimisha kutokana na aya hii kwamba, kufuata batili kutamtia mtu matatizoni. Inatupasa tujiulize tunawafuata watu gani; na je kuwafuata watu hao kutakuwa sababu ya sisi kuokoka au la Siku ya Kiyama? Na vile vile tunajifunza kutokana na aya hii kuwa, watu wa motoni watajuana, watakumbuka maisha yao ya duniani; na kutokana na kuemewa watakimbilia kuomba hifadhi kwa waovu wenzao. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 865 ya Qur’ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atupe mema duniani na akatupe mema akhera na atulinde na adhabu ya moto. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/