May 24, 2023 05:30 UTC
  • Sura ya Ghaafir, aya ya 48-52 (Darsa ya 866)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur’ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SWT, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.

Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur’ani. Hii ni darsa ya 866 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 40 ya Ghaafir. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 48 hadi 50 za sura hiyo ambazo zinasema:

قَالَ الَّذِينَ اسْتَكْبَرُوا إِنَّا كُلٌّ فِيهَا إِنَّ اللَّهَ قَدْ حَكَمَ بَيْنَ الْعِبَادِ

Watasema walio takabari: Hakika sote sisi tumo humo humo! Hakika Mwenyezi Mungu amesha hukumu baina ya waja! 

وَقَالَ الَّذِينَ فِي النَّارِ لِخَزَنَةِ جَهَنَّمَ ادْعُوا رَبَّكُمْ يُخَفِّفْ عَنَّا يَوْمًا مِّنَ الْعَذَابِ

Na walio Motoni watawaambia walinzi wa Jahannamu: Mwombeni Mola wenu Mlezi atupunguzie walau siku moja ya adhabu.

قَالُوا أَوَلَمْ تَكُ تَأْتِيكُمْ رُسُلُكُم بِالْبَيِّنَاتِ ۖ قَالُوا بَلَىٰ ۚ قَالُوا فَادْعُوا ۗ وَمَا دُعَاءُ الْكَافِرِينَ إِلَّا فِي ضَلَالٍ

Nao watasema: Je! Hawakuwa wakikufikieni Mitume wenu kwa hoja zilizo wazi? Watasema: Kwani? Watasema: Basi ombeni! Na maombi ya makafiri hayawi ila ni kupotea bure.

Katika darsa iliyopita tulisema kuwa, vinara wa ukafiri na shirki pamoja na wafuasi wao, watalumbana na kubishana motoni watakoingizwa. Wafuasi wa vinara wa batili, ambao wataamini kuwa waliowafuata na kuwatii ndio waliowafanya waingie motoni, watawataka viongozi wao hao wawasaidie ili waokoke na moto. Aya tulizosoma zinasema: Vinara na wakubwa wa ukafiri na shirki, ambao hawatakuwa na jibu la kuwapa wafuasi wao, watawaambia: Hatima yetu sote ni moja, nayo ni adhabu ya moto, kwa sababu Mwenyezi Mungu ameshahukumu baina ya waja wake; na kwa hukumu aliyotoa, sisi sote tupo hapa leo. Kama sisi tungeweza kupata njia ya kuokoka, tungefikiria kujiokoa wenyewe kabla ya kukuokoeni nyinyi; jueni sasa kwamba hatuna uwezo wa kufanya chochote. Baada ya wafuasi kupoteza matumaini kwa viongozi wao, watawaendea malaika walinzi wa motoni na kuwaomba wawapunguzie adhabu japo kwa siku moja ili waweze angalau kupumua kidogo. Lakini malaika hao watawauliza: Kwa nini badala ya Mitume mliamua kuwafuata na kuwatii waliotakabari? Hawakukujieni Mitume na hoja za wazi na kutimiza dhima juu yenu? Watu wa motoni wataungama kwa kusema, ni kweli, Mitume walitujia na ujumbe wao tuliusikia, lakini tuliyakadhibisha na kuyakataa maneno yao. Malaika watawaambia: Basi kosa ni lenu wenyewe. Lakini kukiri na kuungama hivi sasa na kujuta kwa mliyoyafanya huko nyuma hakukusaidieni wala hakuna faida yoyote kwenu. Kwa hiyo vyovyote mtakavyomwomba Mwenyezi Mungu hamtakubaliwa na wala hamtapata ahueni yoyote ya adhabu. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, wale wanaojivuna na kutakabari hapa duniani na ambao hawako tayari kuitii haki watadunika na kudhalilika Siku ya Kiyama na wala hawatoweza kuokoka. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, hukumu sahihi na ya uadilifu kwa watu wote itatolewa na Allah SWT; kwa hiyo tusijifanye mahakimu wa kuwahukumu watu. Halikadhalika tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba, adhabu ya moto haipumzishiki wala haipunguziki; kwa hiyo madamu tungaliko duniani, tuitumie fursa ya kutubia ili tukaokoke na adhabu ya akhera. Vile vile tunajielimisha kutokana na aya hizi kuwa, makafiri na waovu watakuwa na hali ngumu motoni, kufika hadi ya kuwakimbilia na kuwaomba msaada malaika walinzi wa moto. Wa aidha aya hizi zinatutaka tujue kwamba, utaratibu alioweka Allah ni kuwa, hamuadhibu mtu yeyote kabla ya kutimiza dhima kwake ya kumfikishia uongofu.

Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 51 na 52 ambazo zinasema:

إِنَّا لَنَنصُرُ رُسُلَنَا وَالَّذِينَ آمَنُوا فِي الْحَيَاةِ الدُّنْيَا وَيَوْمَ يَقُومُ الْأَشْهَادُ

Hakika bila ya shaka Sisi tunawanusuru Mitume wetu na walio amini katika uhai wa duniani na siku watapo simama Mashahidi, 

يَوْمَ لَا يَنفَعُ الظَّالِمِينَ مَعْذِرَتُهُمْ ۖ وَلَهُمُ اللَّعْنَةُ وَلَهُمْ سُوءُ الدَّارِ

Siku ambayo hautawafaa madhaalimu udhuru wao, nao watapata laana, na watapata makaazi mabaya kabisa.

Wafuasi wa batili walikuwa wakidhani kwamba, vinara wao wa ukafiri na wenye nguvu na madaraka wanao uwezo wa kuwasaidia wanapohitaji msaada, lakini Siku ya Kiyama vinara na viongozi hao wa ukafiri na upotofu hawataweza kumsaidia yeyote. Lakini kinyume na watu madhalimu na makafiri, Mitume na waja wema watapata auni na msaada mkubwa wa Allah Siku ya Kiyama. Kama aya tulizosoma zinavyoeleza: Mwenyezi Mungu ndiye Mlezi na Mlinzi wa Mitume na waumini na atawapa auni na msaada wake duniani na akhera. Katika aya hizi, Allah SWT analitaja kama kanuni na msingi mkuu, suala la kuwahami na kuwanusuru bila ajizi Mitume na waumini hapa duniani na huko akhera. Hapa duniani anazitia nguvu nyoyo za waumini kwa msaada wake wa ghaibu na kuzijaza woga na hofu nyoyo za maadui zao. Anazima pia njama za maadui hao na kuwapa ushindi waumini wa kweli dhidi ya wapinzani wao. Lakini Siku ya Kiyama, itakuwa siku ya fedheha na msiba kwa madhalimu waliokhitari kufuata ukafiri. Wakati viumbe wote watakapokusanywa, mashahidi watatoa ushahidi dhidi yao na kuwafanya wafedheheke na kuaibika mbele ya hadhara hiyo kubwa. Siku hiyo mashahidi watatoa ushahidi kwa manufaa ya waumini na kuwainua mbele ya waliotakabari. Udhuru watakaotoa mbele ya mahakama ya Allah madhalimu waliotakabari, hautawafalia kitu wala hawatapata chochote zaidi ya laana na maapizo ya wote waliohudhurishwa kwenye mahakama hiyo. Madhalimu hao watakosa rehma za Mwenyezi Mungu na vilevile wataapizwa na kulaaniwa na wafuasi wao pia. Kwa hakika watakuwa na hali mbaya kabisa motoni, huku wakiadhibika na kuteseka pia roho na viwiliwili vyao. Huu kwa hakika ndio msingi na njia inayotumiwa na Qur'ani ya kusimulia historia ya Mitume waliotangulia na kutaja mifano hai ya namna msaada wa ghaibu wa Allah SWT ulivyofanya kazi katika mapambano baina ya waumini mkabala na madhalimu na waistikbari. Inafanya hivyo ili kuonyesha kuwa, endapo waumini watasimama imara na kukabiliana kwa moyo thabiti na majabari wa zama zao, watapata auni na msaada wa Mola na ushindi dhidi ya maadui zao. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, kuwanusuru Mitume na waumini na kuifanya haki mwishowe ishinde dhidi ya batili, ni miongoni mwa taratibu zisizobadilika alizoweka Allah SWT. Tab'an kwa sharti kwamba, waumini wadumu katika istikama na kuwa na moyo thabiti katika kufuata njia ya dini na kuwatii Mitume. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, athari na faida za imani zinawarejea waumini duniani na akhera, na wala hazihusiani na akhera pekee. Vilevile tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba, ahadi ya Mwenyezi Mungu ya kuwanusuru waumini inatolewa ili kuwafariji na kuwapa moyo, matumaini na nguvu za kuweza kusimama imara kukabiliana na vitisho, mashinikizo na maudhi ya maadui. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 866 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah azijaze subira nyoyo zetu, azifanye thabiti imani zetu na atupe ushindi dhidi ya maadui zetu. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/