May 24, 2023 06:14 UTC
  • Sura ya Ghaafir, aya ya 61-65 (Darsa ya 869)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur’ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SWT, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.

Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur’ani. Hii ni darsa ya 869 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 40 ya Ghaafir. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 61 hadi 63 za sura hiyo ambazo zinasema:

اللَّهُ الَّذِي جَعَلَ لَكُمُ اللَّيْلَ لِتَسْكُنُوا فِيهِ وَالنَّهَارَ مُبْصِرًا ۚ إِنَّ اللَّهَ لَذُو فَضْلٍ عَلَى النَّاسِ وَلَٰكِنَّ أَكْثَرَ النَّاسِ لَا يَشْكُرُونَ

Ni Mwenyezi Mungu aliye kufanyieni usiku ili mpate kutulia humo, na mchana wa kuonea. Hakika Mwenyezi Mungu bila ya shaka ni Mwenye fadhila juu ya watu, lakini watu wengi hawashukuru.

ذَٰلِكُمُ اللَّهُ رَبُّكُمْ خَالِقُ كُلِّ شَيْءٍ لَّا إِلَٰهَ إِلَّا هُوَ ۖ فَأَنَّىٰ تُؤْفَكُونَ

Huyo ndiye Mwenyezi Mungu Mola wenu Mlezi, Muumba wa kila kitu. Hapana mungu ila Yeye; basi mnageuzwa wapi? 

كَذَٰلِكَ يُؤْفَكُ الَّذِينَ كَانُوا بِآيَاتِ اللَّهِ يَجْحَدُونَ

Namna hivi ndivyo walivyo geuzwa walio kuwa wakizikataa Ishara za Mwenyezi Mungu.

Aya hizi zinazungumzia tena maudhui ya tauhidi na upekee wa Muumba wa ulimwengu na kutaja baadhi ya neema zake ambazo hazizingatiwi sana na watu na kueleza kwamba: Hata hili giza la usiku na mwangaza wa mchana ni neema mbili kubwa za Mwenyezi Mungu ambazo zina umuhimu mkubwa kwa maisha ya wanadamu na viumbe hai vingi vingine. Mwangaza wa mchana na joto lake vinachangamsha na kuwapa ukakamavu watu wa kufanya kazi na shughuli zao za kila siku na vile vile kustawisha na kunawirisha mimea na mazao ya aina mbali mbali. Nalo giza la usiku, huupumzisha mwili wa mwanadamu na kuipa utulivu roho na akili yake baada ya kazi ngumu za kutwa nzima. Mfumo huo makini wa mabadiliko ya usiku na mchana na mfuatano wenye nidhamu maalumu wa giza na mwangaza ni miongoni mwa mambo muhimu kwa ajili ya uhai wa watu na viumbe wengine hai katika sayari hii ya dunia. Kama usingekuwapo mlingano huu wa giza na mwangaza si hasha joto kali la mwangaza mtupu lingeviunguza viumbe vyote na asingesalia kiumbe yeyote hai ardhini. Hata hivyo kwa masikitiko, watu wengi wanazipita vivi hivi neema hizi kubwa na wala hawamshukuru kwazo Allah SWT. Kuna watu wengine wengi pia ambao si tu hawamshukuru Allah, lakini wanakanusha pia kwamba yuko, na badala ya Yeye Muumba wa ulimwengu wanawaendea kuwaomba wale ambao hawana nafasi yoyote katika majaaliwa yao. Watu hao huvitegemea vitu visivyo na uhai au wanadamu kama wao, ilhali ghairi ya Allah SWT, hao wanaowaendea hawana uwezo wa kuumba wala wa kuendesha masuala ya ulimwengu. Kisha aya zinaendelea kueleza kwamba: Yule aliyekuneemesheni neema zote hizo, ndiye Mwenyezi Mungu, mmiliki na mlezi wenu. Ni Yeye Mola Muumba wa kila kitu na hakuna Muabudiwa mwingine wa haki ghairi yake Yeye. Ni wazi kwamba, Muumba pekee wa ulimwengu na mwendeshaji wake ndiye anayestahiki kutiiwa na kuabudiwa. Kisha aya zinaongezea kueleza kwamba: Baada ya yote hayo, inakuwaje mnaikengeuka njia ya haki, na badala ya kumuabudu Mungu mmoja pekee mnawaelekea na kuwaomba wengie wasiokuwa Yeye? Hapana shaka watu wanaozikadhibisha aya za Mwenyezi Mungu, mwisho wake huikengeuka njia ya haki na kuishia kwenye dhalala na upotofu. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, katika mfumo wa maumbile, usiku umewekwa kwa ajili ya utulivu na mapumziko, na mchana umetengwa kwa ajili ya shughuli za kazi na pirika za maisha. Kwa hivyo inafaa tuuzingatie msingi huu wa maumbile katika ratiba na mipango yetu ya maisha. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, rehma na fadhila za Mwenyezi Mungu na neema zake hapa duniani, zinawajumuisha watu wote; waumini na makafiri au wema na wabaya. Halikadhalika tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba, Mwenyezi Mungu hangojei shukurani za wanadamu ili awateremshie neema zake. Huwarehemu na kuwaneemesha neema zake mtawalia pamoja na kwamba anajua akthari ya watu si washukurivu. Vilevile aya hizi zinatuelimisha kuwa, anayestahiki kuabudiwa ni yule aliye Muumba wa kila kitu na pia mwendeshaji wa masuala ya ulimwengu; na hakuna mwingine yeyote mwenye sifa hizo isipokuwa Allah SWT.

Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 64 na 65 ambazo zinasema:

اللَّهُ الَّذِي جَعَلَ لَكُمُ الْأَرْضَ قَرَارًا وَالسَّمَاءَ بِنَاءً وَصَوَّرَكُمْ فَأَحْسَنَ صُوَرَكُمْ وَرَزَقَكُم مِّنَ الطَّيِّبَاتِ ۚ ذَٰلِكُمُ اللَّهُ رَبُّكُمْ ۖ فَتَبَارَكَ اللَّهُ رَبُّ الْعَالَمِينَ

Ni Mwenyezi Mungu aliye kufanyieni ardhi kuwa ni pahala pa kukaa, na mbingu kuwa dari. Na akakutieni sura, na akazifanya nzuri sura zenu, na akakuruzukuni vitu vizuri. Huyo ndiye Mwenyezi Mungu Mola wenu Mlezi. Basi ametukuka Mwenyezi Mungu Mola Mlezi wa walimwengu wote. 

هُوَ الْحَيُّ لَا إِلَٰهَ إِلَّا هُوَ فَادْعُوهُ مُخْلِصِينَ لَهُ الدِّينَ ۗ الْحَمْدُ لِلَّهِ رَبِّ الْعَالَمِينَ

Yeye ndiye aliye Hai - hapana mungu isipo kuwa Yeye. Basi muabuduni Yeye mkimsafia Dini Yeye. Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wa walimwengu wote.

Aya hizi zinaendeleza yale yaliyozungumziwa katika aya zilizotangulia, -ambazo ziliashiria baadhi ya neema za Mwenyezi Mungu-, kwa kutaja nafasi ya mbingu na ardhi katika maisha ya watu na kueleza kwamba: Ijapokuwa ardhi imo kwenye hali ya kujizunguka yenyewe na pia kulizunguka jua; na kutokana na kulizunguka jua unapatikana usiku na mchana, lakini pamoja na hayo sayari hii ya dunia ni mahali pa utulivu na uhakika. Mwenyezi Mungu Mtukufu ametayarisha mazingira yote yanayohitajika ardhini ili kuifanya sayari hii ya dunia kituo na maskani ya utulivu. Ardhi ni mahali thabiti na pasio na mtingisiko, kiasi cha kuwafanya watu wasiuhisi mwendo, harakati na mitikisiko yake; huku vikiwa vimewekwa ndani yake vyanzo na nyenzo wanazozihitaji viumbe hao. Kwa hiyo wanadamu wanaishi ndani yake kwa uhakika na kujishughulisha na pirika na kazi zao. Kisha aya zinaongezea kwamba: Mbingu zilizoko juu yenu ni mithili ya hema na mwavuli uliowekwa kwa ajili yenu nyinyi wakazi wa ardhini ili ukukingeni na hatari chungu nzima. Anga iliyoko juu yenu, mfano wake ni kama hema lililotanda juu ya pande zote za ardhi na kufunika upeo wake. Mwavuli huo mkubwa, unawalinda wakazi wa ardhini na joto kali la jua pamoja na miali na mionzi hatari ya angani. Kwa upande mwingine, unazuia vimondo visiangukie ardhini na kukifuta juu ya uso wa dunia kizazi cha jamii ya wanadamu. Baada ya kubainisha neema za usiku na mchana pamoja na mbingu na ardhi, Allah SWT anamrejea tena mwanadamu mwenyewe na kumtajia moja ya neema zake kubwa alizomneemesha kwa kumwambia: Hii sura nzuri na ya kupendeza na viungo vilivyokadiriwa vipimo na vyenye mlingano ulivyopewa wewe mwanadamu na hivyo kukupambanua na kukufanya bora kuliko viumbe wengine wote, ni miongoni mwa fadhila za Mwenyezi Mungu kwako. Inafaa pia kuashiria kwamba umbo maalumu alililojaaliwa mwanadamu, humwezesha kufanya anuai za kazi na shughuli za utaalamu na ufundi, ziwe nyepesi zinazohitaji ustadi na umahiri au nzito  na ngumu zinazotegemea nguvu kubwa; na kwa msaada wa viungo tofauti vya mwili wake huweza kutumia na kufaidika na neema mbali mbali alizojaaliwa. Katika aya hizi tulizosoma, zimeashiriwa pia anuai za vilaji na vinywaji safi ambavyo wamewekewa wanadamu na Mola wao; vitu ambavyo vinaendana na hamu na mapenzi yao ya kimaumbele na huwapa raha na kuwaburudisha wanapovila na kuvinywa. Baada ya kubainisha neema hizo, Qur'ani tukufu inasema: Basi huyu ndiye Mwenyezi Mungu Mola wenu, Mungu ambaye amewatunukia watu neema hizi na ndiye Mwendeshaji wa masuala ya ulimwengu; Yeye ni wa milele na mwingi wa baraka. Viumbe vilivyoko ulimwenguni vinakuja na kuondoka. Wa pekee aliye hai na wa milele ni Allah SWT tu, Mola aliyetukuka. Na sababu ni kuwa, uhai wake unatokana na Yeye mwenyewe wala haumtegemei yeyote yule. Kinyume na Yeye Mola, viumbe wengine wote hai, maisha na uhai wao ambao ni wa muda na una kikomo unatokana na Yeye Allah SWT. Ni wazi kwamba, anayestahiki kuabudiwa ni yule tu mwenye uhai mutlaki na wa milele na hakuna muabudiwa mwengine yeyote wa haki ghairi yake Yeye. Ibada hiyo inatakiwa iwe ya ikhlasi na yenye kutakasika na kila aina ya shirki na khurafa; na ni Yeye tu anayepasa kuhimidiwa na kushukuriwa. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, ijapokuwa ardhi ina aina kadhaa za mwendo na harakati, lakini Allah SWT ameifanya tulivu kwa ajili ya makazi ya wanadamu. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, kutulia kwa ardhi, kuinuliwa kwa mbingu, kuumbwa kwa mwanadamu na kuteremshiwa anuai za riziki safi na bora, yote hayo yamefanywa kwa ajili ya kumwepesishia mambo yake ili ajengeke na kutukuka kiutu. Aidha aya hizi zinatutaka tulewe kwamba, kati ya viumbe wote, Allah SWT amempa sura bora zaidi mwanadamu, na hiyo ni moja ya neema kubwa kabisa za Mola. Vilevile aya hizi zinatuelimisha kuwa, rehma na baraka za Mwenyezi Mungu zimeuenea ulimwengu mzima na vilivyomo ndani yake wakiwemo wanadamu. Hakuna muabudiwa wa haki isipokuwa Yeye, basi tumhimidi Yeye tu na kumwabudu kwa ikhlasi. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 869 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atujaaliwe kuwa washukurivu wa neema zake, kubwa na ndogo, tuzijuazo na tusizozijua. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.../