May 24, 2023 06:21 UTC
  • Sura ya Ghaafir, aya ya 66-68 (Darsa ya 870)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur’ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SWT, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.

Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur’ani. Hii ni darsa ya 870 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 40 ya Ghaafir. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 66 ambayo inasema:

قُلْ إِنِّي نُهِيتُ أَنْ أَعْبُدَ الَّذِينَ تَدْعُونَ مِن دُونِ اللَّهِ لَمَّا جَاءَنِيَ الْبَيِّنَاتُ مِن رَّبِّي وَأُمِرْتُ أَنْ أُسْلِمَ لِرَبِّ الْعَالَمِينَ

Sema: Mimi nimekatazwa kuwaabudu hao mnao waomba badala ya Mwenyezi Mungu, zilipo nijia hoja zilizo wazi kutokana na Mola wangu Mlezi. Na nimeamrishwa nisilimu kwa Mola wa walimwengu wote.

Katika darsa zilizopita tulisoma aya zilizotaja ishara na neema za Allah SWT ambazo ni uthibitisho wa kuwepo Muumba na Mola mmoja tu na pekee wa ulimwengu. Katika aya hii tuliyosoma, Bwana Mtume Muhammad SAW anawahutubu washirikina kwa kutilia mkazo nukta hii, kwamba mimi nimetumwa na Mungu ambaye, hajaruhusu mtu ayaabudu masanamu; na amenikataza mimi pia kufanya hivyo. Kwa hiyo msinitarajie mimi niyaabudu masanamu; na wala msidhani kama mimi siyaabudu masanamu yenu kwa sababu ya inadi na ukaidi, hata na nyinyi mufanye hivyo pia ili kuikataa dini yangu. Ilivyo ni kwamba, mimi ninamwabudu Mwenyezi Mungu kwa burhani za kiakili na hoja za kimantiki na ninajiepusha na kujiweka mbali na kuyaabudu masanamu. Ninamnyenyekea na kumwabudu Mwenyezi Mungu tu ambaye ni Mola na Muumba wetu sote. Na si kwamba ninamwabudu tu Yeye Mola wa walimwengu, lakini pia nimejisalimisha kwake Yeye na ninatekeleza kikamilifu yale anayoniamuru. Sababu ni kuwa mimi ni mja wake Yeye; na wajibu wa mja ni kumtii mola na bwana wake. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba, maamrisho na makatazo ya Mwenyezi Mungu yanatokana na hoja na mantiki na wala hakuna mgongano au mkinazo wowote kati ya wahyi na akili. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa, kujisalimisha kwake na kumtii kunamstahiki yule ambaye ni Mola na Muumba wa walimwengu; na ukamilifu wa ibada ni mtu kujisalimisha kikamilifu kwa Mwenyezi Mungu SWT.

Tunaihitimisha darsa yetu ya leo kwa aya ya 67 na 68 ambazo zinasema:

هُوَ الَّذِي خَلَقَكُم مِّن تُرَابٍ ثُمَّ مِن نُّطْفَةٍ ثُمَّ مِنْ عَلَقَةٍ ثُمَّ يُخْرِجُكُمْ طِفْلًا ثُمَّ لِتَبْلُغُوا أَشُدَّكُمْ ثُمَّ لِتَكُونُوا شُيُوخًا ۚ وَمِنكُم مَّن يُتَوَفَّىٰ مِن قَبْلُ ۖ وَلِتَبْلُغُوا أَجَلًا مُّسَمًّى وَلَعَلَّكُمْ تَعْقِلُونَ

 Yeye ndiye aliye kuumbeni kwa udongo, kisha kwa tone la manii, kisha kwa pande la damu, kisha akakutoeni katika hali ya mtoto mchanga, kisha mpate kufikilia utu uzima, kisha mpate kuwa wazee. Na kati yenu wapo wanao kufa kabla, na ili mfikie muda ulio kwisha wekwa, na ili mpate kutia akili.

هُوَ الَّذِي يُحْيِي وَيُمِيتُ ۖ فَإِذَا قَضَىٰ أَمْرًا فَإِنَّمَا يَقُولُ لَهُ كُن فَيَكُونُ

Yeye ndiye anaye huisha na anaye fisha. Akihukumu jambo liwe, basi huliambia: Kuwa! Likawa.

Baadhi ya aya zilizotangulia ziliashiria ishara za Allah SWT mbinguni na ardhini na katika vitu vingine vya maumbile. Aya hii ya 67 ya Suratu Ghaafir inazungumzia kuumbwa kwa mwanadamu kutokana na udongo, awamu ya kiinitete anayopitia, kuzaliwa kwake, kuishi kwake duniani na hatimaye kufa kwake. Awamu ya kwanza ya kuumbwa kwa mwanadamu ni inayotokana na udongo, ambayo inamhusisha mtu wa kwanza kabisa, yaani Nabii Adam AS, aliyeumbwa moja kwa moja kwa udongo na ambao unajumuisha pia wanadamu wengine wote, kwa sababu asili ya vyakula vyote vinavyojenga miili ya wanadamu, viwe ni vya mimea au wanyama, inatokana na udongo pia. Awamu ya pili ya uumbwaji wa mwanadamu ni ya kupitia mbegu ya uzazi inayojumuisha manii ya mwanamme na yai la mwanamke, vinavyounganika pamoja kwenye fuko la uzazi la mwanamke. Mbegu hiyo hukua kwa kasi na kugeuka pande la damu ambalo limetajwa ndani ya Qur'ani kwa jina la a'laqah. Awamu inayofuatia ni ya kubadilika a'laqah kuwa mudhghah, ambayo ni kitu kinachoshabihiana na nyama iliyochakuliwa. Kisha ndipo viungo vya mwili vinapoumbika na kukamilika mwili mzima. Awamu inayofuatia baada ya hapo ni ya kuzaliwa mtoto mchanga. Kisha baada ya kukipita kipindi cha utoto na uchipukizi, mtu huingia kwenye awamu ya rika la ujana. Katika awamu hii, mwanadamu hupevuka kiakili na kufikia kiwango cha juu kabisa cha nguvu za kiwiliwili. Pamoja na hayo, ujana pia haubakii wala haudumu; na mwanadamu hana budi kushuka chini kutoka kwenye kilele cha rika hilo kwa kuianza kidogo kidogo awamu ya kudhoofika na kupoteza nguvu za mwili kwa kuelekea kwenye umri wa makamo na baadaye uzeeni. Hatimaye umri na uhai wa mtu unafikia tamati, kwa kifo kumuelekeza mtu kaburini ambayo ni njia ya kuelekea Kiyama. Tab'an kutokana na kufikwa na ajali za aina tofauti au maradhi, baadhi ya watu hawapitii kwenye awamu na marhala zote hizo za kimaumbile; na kwa hiyo huondoka duniani hata kabla ya kufikia umri wa uzee. Nukta ya kutafakari hapa ni kwamba, Qur'ani tukufu haikutumia neno kufa na kutoweka, lakini imetumia neno linalomaanisha kwamba, wakati wa mauti, malaika huipokea roho ya mtu na kuipeleka kwenye ulimwengu wa baada ya kifo. Kutokana na aya za Qur'ani inadhihirika wazi kwamba, kinyume na wanavyodhani watu wengi, maana ya kifo si kutoweka mwanadamu na kumalizika mambo yake yote, ila huo ni ufunguzi na njia ya kuingilia kwenye ulimwengu wa kudumu na wa milele. Kisha aya zinaashiria kanuni jumla ya uumbaji, ambayo ni kujumuisha uhai na mauti na kueleza kwamba: Jambo hili liko kwenye mamlaka ya Allah SWT peke yake na linathibiti kwa irada na utakaji wake Yeye, pasi na kuchelewa hata kwa sekunde moja. Katika aya hizi mbili tulizosoma, yameashiriwa mambo mawili, yaani kifo na uhai, ambayo tab'an yanavihusu viumbe vyote vyenye uhai, ikiwemo mimea, wanyama na watu. Mawili hayo yanathibiti kulingana na mfumo wa maumbile aliouweka Allah; na mwanadamu hana nafasi yoyote katika hilo. Uhai na kifo ni katika madhihirisho ya qudra na uwezo wa Mwenyezi Mungu SWT na yangali yamebaki kuwa siri na mambo yasiyofahamika hakika yake, licha ya maendeleo makubwa ya elimu na sayansi aliyofikia mwanadamu. Inapasa tukumbushe hapa pia kwamba, uhai ni jambo linaloonekana katika hali na sura mbali mbali. Wanyama wenye maumbo makubwa, ndege wapaao hadi mbali kabisa angani au miti yenye urefu wa mita kadha wa kadha, kila kimoja kina uhai wa aina yake. Hapana shaka, uhai wenye hali na sura tofauti ni miongoni mwa anuai za madhihirisho ya ulimwengu wa maumbile. Kutolewa kwenye ulimwengu wa hali ya kutokuwa na uhai na kupelekwa kwenye dunia ya viumbe hai na kuhamishwa kwenye ulimwengu wa uhai kwa kufikwa na mauti, ni mambo yenye siri na maajabu kadhaa na ni moja ya ishara za uwezo na qudra ya Mola mkamilifu wa hekima. Bila shaka hakuna lolote kati ya mambo ambayo, kwetu sisi wanadamu ni tata na magumu, lenye uzito na ugumu wowote kwa Allah SWT; kwani aliamrishapo tu liwe, basi huwa papo hapo. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, kuumbwa mwanadamu mwenye roho na uhai, fikra na hekima kutokana na udongo usio na roho ni miongoni mwa qudra na uwezo wa Mwenyezi Mungu SWT. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, mfumo wa uumbaji ni mfumo wa ukamilifu; na mauti si kumalizika na kufikia tamati maisha ya mwanadamu, ila ni kutenganika roho na mwili kwa ajili ya kuingia kwenye marhala na hatua ya juu zaidi ya kukifikia Kiyama. Vile vile aya hizi zinatutaka tujue kwamba, Mwenyezi Mungu ametutaka tuzitafakari awamu za uumbwaji wa mtu ili tuweze kuelewa adhama ya kuumbwa kwetu na kwa hiyo kutoidunisha hadhi na thamani yetu. Halikadhalika aya hizi zinatuelimisha kuwa, uhuishaji na ufishaji ni mambo yaliyo kwenye mamlaka ya Allah SWT peke yake. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 870 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah, atuoneshe haki na atupe taufiki ya kuifuata na atuoneshe batili na atuwezeshe kuiepuka. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/