Sura ya Ghaafir, aya ya 69-76 (Darsa ya 871)
Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur’ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SWT, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.
Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur’ani. Hii ni darsa ya 871 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 40 ya Ghaafir. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 69 hadi 72 ambazo zinasema:
أَلَمْ تَرَ إِلَى الَّذِينَ يُجَادِلُونَ فِي آيَاتِ اللَّهِ أَنَّىٰ يُصْرَفُونَ
Je! Huwaoni wale wanao bishana katika Ishara za Mwenyezi Mungu? Wanageuziwa wapi?
الَّذِينَ كَذَّبُوا بِالْكِتَابِ وَبِمَا أَرْسَلْنَا بِهِ رُسُلَنَا ۖ فَسَوْفَ يَعْلَمُونَ
Ambao wamekanusha Kitabu na yale tuliyo watuma Mitume wetu. Basi watakuja jua.
إِذِ الْأَغْلَالُ فِي أَعْنَاقِهِمْ وَالسَّلَاسِلُ يُسْحَبُونَ
Zitakapo kuwa pingu shingoni mwao na minyororo, huku wanabururwa,
فِي الْحَمِيمِ ثُمَّ فِي النَّارِ يُسْجَرُونَ
Katika maji ya moto, kisha wanaunguzwa Motoni,
Aya hizi zinazungumzia watu ambao hawako tayari kuzikubali hoja za Mitume na vitabu vya mbinguni walivyokuja navyo na siku zote huamua kuikaidi na kuipiga vita haki. Ni wazi kwamba kuifanyia inadi na kuipiga vita haki huwa sababu ya mtu kuikengeuka njia iliyonyooka na matokeo yake huwa ni kuishia kwenye dhalala na upotofu. Chanzo hasa cha watu kukaidi na kuipiga vita haki katika zama zote za historia, baadhi ya wakati kilikuwa ni kuwafuata kibubusa wazee na wakubwa wao waliotangulia na kuwa na ukereketwa na taasubi zisizo na msingi kwa imani na itikadi walizorithishwa; na wakati mwingine ilikuwa inadi, ukaidi na ubishani tu walioamua kuwafanyia Mitume na wafuasi wao. Badala ya watu kuitafuta haki na kuyaamini maneno ya haki, walikuwa wakiyakanusha na kuyakadhibisha yale ambayo hayakuwapendeza na hayakuendana na matashi yao. Bila ya shaka kama mtu ana nia ya dhati ya kuitafuta haki lakini hakuweza kuifikia na kuielewa, huyo atasameheka mbele ya Allah. Lakini kama mtu ataifahamu haki na akasimama kuipinga na kuikadhibisha huyo atafikwa na adhabu kali. Kwa sababu kwa kufanya hivyo atakuwa ametoka nje ya mipaka ya utu na kuacha kutumia akili yake ambayo ndiyo inayompambanua mwanadamu na mnyama. Bila ya shaka malipo ya adhabu ya shirki na ukafiri hayalipwi duniani, ili watu wanaoamua kuamini na kufuata haki, wasifanye hivyo kwa kulazimishwa, bali wachague kuifuata njia sahihi kwa irada na hiari yao. Lakini pamoja na hayo, njia yoyote atakayoichagua mtu au amali yoyote ile atakayoamua kufanya, athari na matokeo yake hayatabaki kuwa kwenye mamlaka yake yeye. Kwa sababu hiyo, kutokana na alivyohukumu Allah SWT, kama mtu atakufuru kwa sababu ya inadi, taasubi na ukaidi tu matokeo yake yatakuwa ni kuporomoka na kuishia motoni. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, kutalii na kusoma historia na hatima iliyozipata umma zilizotangulia, ambazo ziliishia kwenye dhalala na upotofu kwa kusimama kuwapinga Mitume wa Mwenyezi Mungu, ni miongoni mwa mambo yanayousiwa na Qur’ani. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, jambo hatari zaidi ni mtu kuipinga na kuipiga vita haki pale inapomfikia na akaifahamu, lakini akaamua tu kuipa mgongo. Aidha hizi zinatutaka tujue kwamba, kutajwa adhabu mbali mbali za motoni ni onyo na indhari ya kumtaka mtu achunge tabia na matendo yake na wala asidhani kama yale ayafanyayo duniani yatapita vivi hivi tu bila ya malipo. Wa aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kuwa, kutakabari na kujikweza kwa makafiri hapa duniani kutawafanya wadhalilike na kufedheheka Siku ya Kiyama.
Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 73 na 74 ambazo zinasema:
ثُمَّ قِيلَ لَهُمْ أَيْنَ مَا كُنتُمْ تُشْرِكُونَ
Tena wataambiwa: Wako wapi mlio kuwa mkiwashirikisha.
مِن دُونِ اللَّهِ ۖ قَالُوا ضَلُّوا عَنَّا بَل لَّمْ نَكُن نَّدْعُو مِن قَبْلُ شَيْئًا ۚ كَذَٰلِكَ يُضِلُّ اللَّهُ الْكَافِرِينَ
Badala ya Mwenyezi Mungu? Watasema: Wametupotea, bali tangu zamani hatukuwa tukiomba kitu! Hivyo ndivyo Mwenyezi Mungu anawaachia makafiri wapotelee mbali.
Aya zilizotangulia ziliashiria adhabu itakayowapata makafiri Siku ya Kiyama. Aya tulizosoma zinaendeleza maudhui hiyo kwa kusema: Wakati washirikina na waovu wengine watakapokuwa wanaadhibika motoni huku wakiwa hawana pa kukimbilia, wataulizwa, viko wapi sasa vile mlivyokuwa mkiviabudu badala ya Mwenyezi Mungu na kuvifanya washirika wake katika uendeshaji mambo?! Kwa nini hawaji kukusaidieni wale mliokuwa mkiwaabudu, ambao mlidhani watakisikia kilio chenu na kukuja kukuokoeni na hilaki ya adhabu ya moto wa Jahanamu?! Watu hao watajibu katika hali ya unyonge na idhilali: Vile tulivyokuwa tukiviabudu, ama vitakuwa vimeshaangamia au vitakuwa vinahiliki kwa adhabu motoni kama sisi. Vyovyote iwavyo hakuna habari zao zozote; ni kama kwamba vimeshapotelea mbali, wakati sisi tulikuwa tukiviabudu kwa kutegemea leo vije kutuombea na kukiitikia kilio chetu. Lakini kwa kuwa hali sasa imekuwa hivi, ni kama kwamba sisi hatukuwa asilani tukiviabudu na wala vyenyewe havikuwa vitu vyenye thamani ya kuabudiwa. Sasa imeshatubainikia kwamba havikuwa vitu vyenye maana yoyote kama tulivyokuwa tukidhani. Pamoja na hayo, ungamo na ukanushaji wa watu hao hautafaa kitu Siku ya Kiyama na wala hautakuwa na faida yoyote kwa waovu, kwa sababu matunda ya shirki na ukafiri ni kupotoka na hatimaye kuishia kwenye moto wa Jahanamu. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, Siku ya Kiyama ni siku ya kufichuka hakika za mambo na kila kitu kitadhihirika siku hiyo. Siku hiyo makafiri na washirikina watabainikiwa na upotofu wao. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa kukiri au kukana dhambi Siku ya Kiyama hakutakuwa na taathira yoyote kwa mtu. Kwa sababu Allah SWT ni mjuzi wa yaliyomo ndani ya nafsi za watu na anatoa hukumu kulingana na batini zao. Halikadhalika tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba, kuongoka au kupotoka ni matokeo ya njia aliyoichagua mtu na matunda ya amali na matendo yake.
Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 75 na 76 ambazo zinasema:
ذَٰلِكُم بِمَا كُنتُمْ تَفْرَحُونَ فِي الْأَرْضِ بِغَيْرِ الْحَقِّ وَبِمَا كُنتُمْ تَمْرَحُونَ
Haya ni kwa sababu mlikuwa mkifurahi katika ardhi pasipo haki, na kwa sababu mlikuwa mkijishaua.
ادْخُلُوا أَبْوَابَ جَهَنَّمَ خَالِدِينَ فِيهَا ۖ فَبِئْسَ مَثْوَى الْمُتَكَبِّرِينَ
Ingieni kwenye milango ya Jahannamu, mdumu humo milele. Basi ni maovu yaliyoje makaazi ya wanao takabari!
Aya hizi zinazungumzia sababu za watu hao kufikwa na mateso na masaibu yote hayo ya adhabu ya moto kwa kueleza kwamba: Walipokuwa duniani, kukanusha kwao kuwepo kwa Mwenyezi Mungu na kufufuliwa kuliwafanya waghiriki kwenye lindi la shahawa na matamanio ya nafsi na starehe chafu; si hayo tu lakini walikuwa wakiona raha kuwakandamiza wanyonge na kufurahia kufanya madhambi na kuhalifu amri na sharia za Allah. Naam! Furaha za aina hiyo zinazoandamana na ghururi, kujisahau na kutekwa na matamanio ya nafsi humfanya mtu awe mbali na Allah na kushindwa kuibaini haki na hakika ya mambo. Lakini watakaposimamishwa siku hiyo katika uwanja wa Kiyama, kwa sababu ya kutakabari kwao mbele ya haki, watakuwa dhalili na wanyonge na adhabu ya moto wa Jahanamu itakuwa ndiyo malipo watayostahiki kwa starehe zao chafu na kufuata kwao hawaa na matamanio ya nafsi zao. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, Uislamu haupingi mtu kujifurahisha na kujiburudisha kwa mambo ya halali; ulichokataza ni burudani na starehe zinazochanganyika na madhambi na vitendo viovu. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, raha na starehe chafu wanazojifurahisha nazo makafiri leo hapa duniani zitakuja kuwatia simanzi, majonzi na majuto Siku ya Kiyama. Aidha aya hizi zinatutaka tuelewe kwamba, furaha na burudani nazo pia hupimwa kwa kutumia kigezo cha haki na batili. Kwa mfano furaha na burudani zinazotokana na mambo ya batili ambayo msingi wake ni mtu kufuata hawaa na matamanio ya nafsi yake, kufanya lolote lile bila kujali, kukiuka haki za watu wengine, kuwadunisha na kuwadhalilisha wanyonge na walio chini yake na kufanya mambo mengine maovu, huko ni kumwasi Allah SWT. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 871 ya Qur'ani imefika tamati. Tunamwomba Allah atupe mema duniani na akatupe mema akhera na atulinde na adhabu ya moto. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.../