Sura ya Ghaafir, aya ya 77-81 (Darsa ya 872)
Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur’ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SWT, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.
Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur’ani. Hii ni darsa ya 872 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 40 ya Ghaafir. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 77 ambayo inasema:
فَاصْبِرْ إِنَّ وَعْدَ اللَّهِ حَقٌّ ۚ فَإِمَّا نُرِيَنَّكَ بَعْضَ الَّذِي نَعِدُهُمْ أَوْ نَتَوَفَّيَنَّكَ فَإِلَيْنَا يُرْجَعُونَ
Basi subiri, hakika ahadi ya Mwenyezi Mungu ni ya kweli. Na ama tukikuonyesha baadhi ya yale tuliyo waahidi au tukikufisha, lakini wao watarudishwa kwetu tu.
Aya hii inamuusia Bwana Mtume Muhammad SAW na wafuasi wake wawe na subira na uvumilivu kutokana na maudhi na manyanyaso ya wapinzani na kuwaeleza kwamba: Ukanushaji wa wapinzani au uafriti wao wa kukuwekeeni vizuizi, usikudhoofisheni na kukufanyeni walegevu. Bali ni kinyume chake, yaani kadiri upinzani wao wa kauli na vitendo unavyozidi, inabidi istikama na uthabiti wenu katika njia ya haki uongezeke zaidi, mpaka muweze hatimaye kuwashinda. Kulingana na ahadi ya Mwenyezi Mungu, wakanushaji haki wataonja adhabu mbalimbali hata hapa duniani pia, lakini tusitarajie na kutaka ahadi hiyo ya Mola lazima ithibiti wakati wa uhai wetu. Ahadi ya Allah ni ya haki na wala haina shaka. Aliloahidi Mola litathibiti tu, sisi tuwepo au tusiwepo. Na adhabu kamili ya wakanushaji haki iko Siku ya Kiyama, ambako watahudhurishwa watu wote na kushuhudia jaza ya mema na malipo ya maovu waliyotenda. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba, Muislamu anatakiwa awe na subira na istikama katika kuyakabili matatizo mbalimbali yanayomfika kwa sababu ya kushikamana na dini yake. Hili ni moja ya masharti ya kushikamana ipasavyo na dini na wala haipasi mtu kuacha dini na mafundisho yake matukufu kwa kuhofia baadhi ya tabu na misukosuko. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa, haifai kuwa na shaka juu ya kuthibiti ahadi ya Allah kwa sababu ya kucheleweshwa adhabu ya waovu.
Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 78 ambayo inasema:
وَلَقَدْ أَرْسَلْنَا رُسُلًا مِّن قَبْلِكَ مِنْهُم مَّن قَصَصْنَا عَلَيْكَ وَمِنْهُم مَّن لَّمْ نَقْصُصْ عَلَيْكَ ۗ وَمَا كَانَ لِرَسُولٍ أَن يَأْتِيَ بِآيَةٍ إِلَّا بِإِذْنِ اللَّهِ ۚ فَإِذَا جَاءَ أَمْرُ اللَّهِ قُضِيَ بِالْحَقِّ وَخَسِرَ هُنَالِكَ الْمُبْطِلُونَ
Na kwa hakika tuliwatuma Mitume kabla yako. Wengine katika hao tumekusimulia khabari zao, na wengine hatukukusimulia. Na haiwi Mtume alete Ishara yoyote ila kwa idhini ya Mwenyezi Mungu. Basi ikija amri ya Mwenyezi Mungu huhukumiwa kwa Haki, na hapo wapotofu watakhasirika.
Aya hii inaendeleza yaliyozungumziwa katika aya iliyotangulia kuhusu subra na istikama na kumfariji Bwana Mtume SAW kwa kumueleza kwamba: Kabla yako wewe pia walikuja Mitume wengi, ambao nao pia walifikwa na matatizo kama hayo, lakini pamoja na hayo walisimama imara katika njia ya haki.Bila shaka ni matatizo ya baadhi tu ya Mitume hao ambayo tumekusimulia na yako ya baadhi yao ambayo hatujakusimulia. Makabiliano na vita vya batili dhidi ya haki vimekuwepo katika zama zote za historia na wala hazihusiani na zama zako wewe tu. Siku zote huwepo kundi la watu wenye kutakabari na wenye ghururi wanaosimama kukabiliana na maneno ya haki na huwa hawako tayari kuyakubali. Na si ajabu hata wasitosheke na kuikataa tu haki, bali wakaamua hata kuwapiga vita pia wanaoifuata haki, kwa kuwaudhi, kuwabaidisha na hata kuwaua ili kuifuta kabisa haki katika uso wa ardhi. Hao kwa hakika ni watu wakaidi na watafutao visingizio;na kila siku huibua nakuzusha jambo jipya. Ni kama ilivyokuwa katika zama za Mitume waliotangulia pia, ambapo watu kama hao walikuwa wakidai waonyeshwe miujiza mipya na kuwataka Mitume hao wawaletee miujiza waliyoitaka wao. Walidai hayo ilhali suala la muujiza liko kwenye mamlaka ya Allah SWT na si Mitume wake. Mitume hawako kama walivyo wachawi na wafanya mazingaombwe, ambao huweza kufanya uchawi na mazingaombwe kutokana na uzoefu na mazoezi ya muda mrefu. Kinyume na wao, Mitume huweza kuleta na kuonyesha miujiza kwa idhini na qudra ya Mwenyezi Mungu. Kwa maneno mengine ni kwamba, muujiza unaletwa ili kuwaonesha watu uongofu, kuhuisha uwezo wao wa kutafakari na kuthibitisha haki na ukweli wa Mtume; na si kwamba kila siku watu wadai muujiza kwa Mtume, na yeye Mtume alazimike kukidhi dai na takwa lao hilo. Sehemu ya mwisho ya aya hii inasisitiza kuwa, Siku ya Kiyama, watu hao wabishi, wakaidi na wanaoshupalia batiliwatahukumiwa kwa haki katika mahakama ya Allah SWT. Siku hiyo njia za kurejea duniani zitafungwa, na vilio na mayowe ya madhalimu hayatafika popote. Wakati huo, waliofuata batili watakula hasara na itawabainikia kuwa wameharibikiwa na kuhasirika kwa kila hali. Hapo ndipo watapoelewa kwamba wamepoteza rasilimali zao zote zenye thamani na hakuna walichokipata kwa kufanya hivyo. Badala yake watafikwa na ghadhabu na adhabu ya Allah SWT. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba, kutalii historia za kaumu zilizopita na maisha ya Mitume wa kaumu hizo ni katika mambo ambayo Qur’ani tukufu imeyausia kuyafanya ili tuweze kuwa thabiti katika njia ya haki na kutokata tamaa wala kuwa walegevu kwa sababu ya vizuizi na matatizo tunanayokabiliana nayo. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa, miujiza ya Mitume inatokana na irada ya Allah, wala hailetwi kwa kutegemea matashi na matakwa ya watu. Halikadhalika tunajielimisha kutokana na aya hii kwamba, hasara hasa ni ile atakayopata mtu Siku ya Kiyama, si ya hapa duniani. Wanaokumbatia dunia wasidhani kuwa madaraka na mali chungu nzima walizonazo ni ishara ya mafanikio na bahati njema. Sababu ni kwamba, dunia hii inapita na kumalizika kwa kasi, na katika ulimwengu wa milele, waovu na waharibifu watabaki mikono mitupu.
Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 79, 80 na 81 ambazo zinasema:
اللَّهُ الَّذِي جَعَلَ لَكُمُ الْأَنْعَامَ لِتَرْكَبُوا مِنْهَا وَمِنْهَا تَأْكُلُونَ
Ni Mwenyezi Mungu aliye kujaalieni nyama hoa wa mifugo, ili muwapande baadhi yao, na wengine muwale.
وَلَكُمْ فِيهَا مَنَافِعُ وَلِتَبْلُغُوا عَلَيْهَا حَاجَةً فِي صُدُورِكُمْ وَعَلَيْهَا وَعَلَى الْفُلْكِ تُحْمَلُونَ
Na katika hao mnayo manufaa kadhaa wa kadhaa, na mnapata kwao haja zilizomo vifuani mwenu; na mnachukuliwa juu yao, na juu ya marikebu.
وَيُرِيكُمْ آيَاتِهِ فَأَيَّ آيَاتِ اللَّهِ تُنكِرُونَ
Naye anakuonyesheni Ishara zake. Basi Ishara gani za Mwenyezi Mungu mnazo zikataa?
Aya za sura hii ya Ghaafir au Muumin huwa mara kwa mara zinatukumbusha neema za Allah kwa mwanadamu, huku zikimtakakiumbe huyo aache ukafiri na shirki na kufuata tauhidi na imani ya Mola pekee wa haki. Aya hizi zinaashiria neema za wanyama na jinsi mwanadamu anavyoneemeka na kufaidika nazo. Zinasema: Mwenyezi Mungu amewaumba baadhi ya wanyama kwa ajili ya matumizi yenu nyinyi wanadamu; na hiyo kwa hakika ni ile ruhusa ambayo Allah ametoa kwa ajili ya kuchinja wanyama kama ng’ombe, kondoo na ngamia ili kuweza kutumia nyama zao; vyenginevyo isingemjuzia mtu kutoa roho za wanyama wasio na hatia.Mbali na chakula kinachotokana na nyama za wanyama hao, baadhi yao kama ngamia wanatumiwa pia kama kipandokwenye majangwa ya ardhi yabisi na yenye kuunguza. Ajabu ni kwamba, leo hii, na licha ya vyombo vyote vya kisasa vya usafiri vilivyopo, kuanzia angani, baharini hadi ardhini, nyamahoa, yaani wanyama wa miguu minne, wangali ndio wenzo bora wa kuvukia baadhi ya maeneo ya majangwani au vivuko vilivyo tabu kupitika vya milimani. Alaa kulli hal, kuwatumia wanyama hao kama kipando au chombo cha kubebea mizigo ambako kunatokana na kuweza kwao kufugika na kuzoeleka, ni ishara nyingine ya rehma na ukarimu wa Allah kwa mwanadamu. Neema hiyo ya kuweza kubeba mizigo katika maeneo kama hayo ya nchi kavu kuna faida na manufaa kwa mwanadamu, kama anavyonufaika kwa ubebaji na usafirishaji mizigo kupitia baharini kwa kutumia meli na majahazi. Wanyama hao wa miguu minne wanazo faida nyingine pia kwa wanadamu kama za kuwapatia maziwa, sufu, ngozi na viungo vyao vingine vinavyoweza kutumiwa na kiumbe huyo. Si hayo tu, lakini faida nyingine za nyamahoa ni kutumiwa na watu kwa mambo ya burudani yakiwemo ya mashindano ya mbio na pia kufanywa kipando cha kutembelea. Wanyama hao wanatumiwa kwa safari za nchi kavu, lakini katika aya hizi hizi tulizosoma kumeashiriwa pia kuabiri merikebuni na majahazini, ikiwa na maana kwamba, Allah SWT amewawekea watu vyombo vya usafiri na uchukuzi wa bidhaa zao jangwani na baharini ili kuweza kusahilisha haja na mahitaji yao. Katika sehemu ya mwisho ya aya hizi imeelezwa kuwa, Mwenyezi Mungu Mtukufu anakuonyesheni aya na ishara zake kila mara; na popote mnapoangalia athari zake zinaonekana dhahiri na kwa uwazi kabisa. Kama ni hivyo, kwamba aya na ishara za Allah ziko wazi kwa watu wote, kwa nini baadhi ya watu wanaamua kuwa wakanushaji? Ukweli ni kwamba, mwanadamu si mwenye kuthamini neema za Allah na kwa hivyo hutumia visingizio mbalimbali kuzikanusha aya za Mola Muumba. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, sayari ya dunia na viumbe vyote vilivyomo ndani yake vimeumbwa kwa ajili ya mwanadamu; na Allah amempa mwanadamu ruhusa ya kutumia kwa njia sahihi na kufaidika navyo viumbe hivyo. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, pamoja na kwamba nyamahoa wana nguvu kubwa zaidi kimwili kuliko mwanadamu, lakini Allah SWT amewatiisha na kuwafanya maridhia kwa mwanadamu na hiyo ni moja ya rehma na ukarimu wa Mola kwa kiumbe huyo. Vilevile aya hizi zinatutaka tuelewe kwamba utovu wa shukurani ndiyo sifa ya watu wengi. Wananufaika na neema za Mwenyezi Mungu, lakini wanamkana mtoaji wa neema hizo na hawako tayari kutii maamrisho yake. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 872 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atujaalie kuwa washukurivu wa neema zake, kubwa na ndogo, tunazozijua na tusizozijua. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/