May 24, 2023 08:05 UTC
  • Sura ya Ghaafir, aya ya 82-85 (Darsa ya 873)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur’ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SWT, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.

Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur’ani. Hii ni darsa ya 873 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 40 ya Ghaafir. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 82 ambayo inasema:

أَفَلَمْ يَسِيرُوا فِي الْأَرْضِ فَيَنظُرُوا كَيْفَ كَانَ عَاقِبَةُ الَّذِينَ مِن قَبْلِهِمْ ۚ كَانُوا أَكْثَرَ مِنْهُمْ وَأَشَدَّ قُوَّةً وَآثَارًا فِي الْأَرْضِ فَمَا أَغْنَىٰ عَنْهُم مَّا كَانُوا يَكْسِبُونَ

Kwani hawatembei katika ardhi wakaona ulikuwaje mwisho wa walio kuwa kabla yao? Walikuwa wengi kuliko wao, na wenye nguvu zaidi na athari katika ardhi, lakini hayakuwafaa hayo waliyo kuwa wakiyachuma.

Historia ya wanadamu inaweza kusomwa katika sura mbili: Sura ya kwanza ni kwa njia ya vitabu vya historia ambavyo vimenakili na kualifu matukio yaliyosimuliwa kupitia kinywa cha mtu mmoja hadi mwingine; na njia ya pili ni kwa kutalii athari zilizoachwa na staarabu zilizopita ambazo zinapatikana na kushuhudiwa katika maeneo tofauti ya dunia. Katika aya hii tuliyosoma Qur’ani tukufu inawahutubu madhalimu kwamba: Kama mnataka kujua nini utakuwa mwisho wenu, inatosha mtembee katika ardhi, mkaone nini ulikuwa mwisho wa waliofanya dhulma katika historia! Nguvu walizokuwa nazo zilivunjwa vunjwa, makasri yao yaliporomoshwa na kusawazishwa na ardhi na majeshi yao makubwa yalisambaratishwa na kupukutika mithili ya majani. Hebu na wajiulize, nguvu na umati mkubwa wa watu aliokuwa nao Firauni wa Misri viliweza kumuokoa yeye na majeshi yake yasigharikishwe katika Mto Nile? Majengo makubwa na imara ya kaumu zilizopita yaliyokuwa yamejengwa kwenye vigingi vya milima na kwenye ngome madhubuti yaliweza kuwalinda walioishi ndani ya majengo hayo na adhabu ya Mwenyezi Mungu? Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba, kutalii historia za waliopita, iwe ni kwa njia ya kusoma maandiko au kutembelea athari zilizoachwa na watu hao, ni jambo linalousiwa na kutiliwa mkazo na Qur’ani. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kwamba, kuwa na ghururi kwa sababu ya nguvu na suhula ili kutaka kukabiliana na irada ya Allah huwafanya madhalimu wawe hatarini muda wote kuweza kufikwa na adhabu ya Mola. Halikadhalika aya hii inatuelimisha kuwa, moja ya sababu za kuporomoka staarabu mbalimbali za wanadamu, ni watu wake kutaka kuyapiga vita mafundisho ya Mitume wa Allah. Wa aidha aya hii inatutaka tufahamu kuwa, nguvu za watu, wingi wao na suhula za kisasa walizonazo haviwezi kuwazuia wasishukiwe na adhabu ya Allah.

Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 83 ambayo inasema:

فَلَمَّا جَاءَتْهُمْ رُسُلُهُم بِالْبَيِّنَاتِ فَرِحُوا بِمَا عِندَهُم مِّنَ الْعِلْمِ وَحَاقَ بِهِم مَّا كَانُوا بِهِ يَسْتَهْزِئُونَ

Basi walipo wajia Mitume wao kwa dalili zilizo wazi walijitapa kwa ilimu waliyo kuwa nayo. Basi yakawazunguka waliyo kuwa wakiyafanyia stihzai.

Aya hii inaendeleza maudhui iliyozungumziwa katika aya iliyotangulia na kueleza kwamba: Madola ya kidhalimu katika historia, ambayo yalikuwa na ghururi kwa sababu ya nguvu yalizokuwa nazo na wingi wa majeshi yao, mengi yao yalikuwa na staarabu zilizoyafanya yadhani kwamba elimu na ujuzi yaliokuwa nao vitaweza kuyakinga na adhabu ya Mwenyezi Mungu. Kwa hiyo yakawa yanayapinga mafundisho ya Mitume wake na kuyafanyia shere na stihzai maneno yao kuhusu asili ya viumbe na marejeo yao kwa Mola wao. Watu hao walijivunia elimu waliyokuwa nayo na wakazichukulia imani na itikadi za dini kuwa ni khurafa na mambo ya uzushi yasiyo na msingi, ambayo hayawezi kuthibitishwa na elimu ya mwanadamu. Lakini pamoja na hayo, wakati wowote ule Allah alipoamua, hawakuweza kushindana na irada yake; na elimu, utaalamu na suhula zao zote ziliangamizwa kwa adhabu ya Mola. Ndiyo kusema kuwa, kile kitu ambacho wao walikiona hakina athari, na si lolote si chochote kwao wao, ndicho kilichowaangamiza. Kwa mtazamo wa Qur’ani, kiburi na ghururi ndicho chanzo hasa cha upotofu na kuharibikiwa watu. Kiburi hicho kinaweza kikatokana na kuwa na utajiri mkubwa wa mali, wingi wa watu na nguvu kubwa za kijeshi au kwa sababu ya ujuzi mkubwa wa elimu na utaalamu. Katika zama hizi na baada ya kupatikana maendeleo makubwa ya elimu, tunashuhudia mfano huo wa ghururi na kiburi hicho kinachotokana na elimu katika jamii zilizoendelea. Tunaweza kusema kwamba, moja ya sababu za kuikana dini na kukumbatia fikra za kilahidi na ukanushaji Mungu ambao umeshuhudiwa katika karne za karibuni ni hiyo ghururi iliyowaingia baadhi ya wasomi na wanasayansi. Kugundua baadhi ya siri za ulimwengu wa maumbile na kufungukiwa zaidi na mwanga wa elimu, kuliwalewesha na kuwatia ghururi wasomi na wanasayansi hao kiasi cha kufika hadi ya kuikanusha misingi na thamani za dini. Mduara huo wa ghururi na majivuno ya elimu waliyokuwa nayo watu ulipanuka na kufikia hatua ya kuzikadhibisha na kuzifanyia kejeli na stihzai elimu tukufu na mafundisho aali yatokanayo na chemchemi ya wahyi. Watu hao walidai kwamba, kutokana na kufikia zama za kunawiri elimu na sayansi mafunzo ya Mitume hayahitajiki tena; na kwa mawazo yao, dini na mafundisho ya Manabii wa Allah yameshatupwa nje ya ulingo wa maisha ya mwanadamu. Hata hivyo ghururi na kughafilika huko kwa wanadamu hakukudumu kwa kipindi kirefu, kutokana na matukio kadhaa yaliyojiri ambayo yalikuja kubatilisha dhana na imani hiyo potofu. Vita Vikuu vya Kwanza na vya Pili vya Dunia vilikuja kuonyesha kuwa, maendeleo ya kisayansi na kiviwanda aliyopata mwanadamu, si tu hayajampatia furaha ya maisha, bali yamezidi kumsukuma mpaka kwenye ukingo wa lindi la maangamizi. Lakini pia kujitokeza aina kwa aina za uchafu wa kiakhlaqi na ufisadi wa kijamii, mauaji, maradhi ya kinafsi na kuenea vitendo vya ukatili na ubakaji kulimfanya mwanadamu abaini kuwa, mafanikio yake ya kielimu hayawezi peke yake kumwondolea masaibu ya maisha yake katika zama hizi mpya, bali katika baadhi ya hali, matatizo yanayomkabili, yameongezeka pia. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba, maneno ya Mitume yanafuatana na miujiza na hoja za wazi, zinazokubalika kwa mtu yeyote yule mwenye kutaka kuijua haki. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa, kama mwanadamu ataingiwa na ghururi kwa elimu haba tu aliyopewa, ghururi hiyo ya elimu itakuwa kizuizi cha yeye kuikubali haki. Ilhali sayansi na jarabati haviwezi kuchukua nafasi ya mafundisho ya dini na kumfanya mtu asihitajie mafundisho yenye nuru ya wahyi wa mbinguni. Vilevile tunajielimisha kutokana na aya hii kwamba, miongoni mwa athari mbaya za ghururi inayotokana na elimu ni kuyadunisha na kuyafanyia shere mafundisho ya mbinguni. Watu wanaosibiwa na maradhi hayo hudhani kwamba, wanaweza kushindana na elimu mutlaki na isiyo na ukomo ya Allah SWT, ambayo vitabu vya mbinguni vimetokana nayo. Wa aidha aya hii inatutaka tujue kuwa, staarabu na tamaduni zilizojaribu kukabiliana na mafundisho ya mbinguni ziliporomoka na kuangamia.

Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 84 na 85 ambazo zinasema:

فَلَمَّا رَأَوْا بَأْسَنَا قَالُوا آمَنَّا بِاللَّهِ وَحْدَهُ وَكَفَرْنَا بِمَا كُنَّا بِهِ مُشْرِكِينَ

 Walipo iona adhabu yetu walisema: Tumemuamini Mwenyezi Mungu peke Yake, na tunaikataa miungu tuliyo kuwa tukiishirikisha naye.

‏ فَلَمْ يَكُ يَنفَعُهُمْ إِيمَانُهُمْ لَمَّا رَأَوْا بَأْسَنَا ۖ سُنَّتَ اللَّهِ الَّتِي قَدْ خَلَتْ فِي عِبَادِهِ ۖ وَخَسِرَ هُنَالِكَ الْكَافِرُونَ

Lakini imani yao haikuwa yenye kuwafaa kitu walipokwisha iona adhabu yetu. Huu ndio mwendo wa Mwenyezi Mungu ulio kuwa kwa waja wake. Na hapo walio kufuru watapata hasara.

Aya hizi ambazo ndizo aya za mwisho za Suratu Ghaafir zinaelezea hatima ya watu ambao, kutokana na athari ya ghururi na ubinafsi, hawako tayari kuikubali haki na wanaamua kuyapiga vita mafundisho ya Mitume. Kwa mujibu wa aya hizi, wakati watu haohao wenye ghururi na majivuno wanaposhukiwa na viashiria vya adhabu ya Mwenyezi Mungu hapa duniani na kujibaini kuwa wao ni viumbe dhaifu na visivyo na uwezo wowote, hujuta kwa waliyoyatenda na kusalimu amri kwa Allah. Hapo hutangaza kujiweka mbali na shirki na ukafiri na kutamka kwa dhati kwamba 'tunamwamini Mola mmoja pekee wa haki na tunawakufuru waabudiwa wengine wote tuliokuwa tukiwashirikisha naye.' Ni wazi kwamba imani ya aina hiyo inayotokana na hofu na ulazimikaji haina thamani yoyote. Mfano wa hali hiyo ni kama inavyosimuliwa na Qur’ani tukufu katika kisa cha Nabii Musa (as) na Firauni, ambapo wakati Firauni alipokuwa anagharikishwa katika Mto Nile alitoa kauli ya kumwamini Mwenyezi Mungu, lakini kuamini kwake huko hakukubaliwa. Na sababu ni kwamba, aliamini baada ya kuwa ameshakata tamaa ya kuokoka na hakuwa na chaguo jengine lolote lile zaidi ya hilo. Hali ya kuwa imani huwa na thamani, pale inapotokana na irada na hiari ya mtu na akawa na uwezo wa kufanya chaguo jengine ghairi ya hilo. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, watu wenye ghururi, waasi na wakaidi, huwa hawako tayari kuamini haki mpaka waione adhabu ya Mwenyezi Mungu; lakini kuamini kwao katika hali hiyo hakuwafalii chochote. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, imani huwa na thamani inapotokana na hiari ya mtu. Kuamini kunakotokana na woga, kulazimishwa na kutokuwa na budi hakuna thamani yoyote. Kwa maneno mengine ni kwamba, imani ya kulazimishwa haimfalii mtu kitu. Wa aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kuwa hasara hasa katika maisha, ni mtu kufa katika hali ya shirki na ukafiri na katika kufuata njia ya batili. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 873 ya Qur'ani imefikia tamati. Darsa hii ndiyo inayotukamilishia pia tarjumi na maelezo ya sura hii ya 40 ya Ghaafir au Muumin. Inshallah tuwe tumeaidhika na kuelimika na yote tuliyojifunza katika sura hii. Na tunamwomba pia Allah atuonyeshe haki na atupe taufiki ya kuifuata na atuonyeshe batili na atuwezeshe kuiepuka. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/