Sura ya Fuss’ilat, aya ya 1-7 (Darsa ya 874)
Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur’ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SWT, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.
Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur’ani. Baada ya kukamilisha tarjumi na maelezo kwa ufupi ya sura ya 40 ya Ghaafir au Muumin, kuanzia darsa hii ya 874 tutazungumzia sura ya 41 ya Fuss’ilat. Sura hii imeteremshwa Makka na ina jumla ya aya 54. Kama zilivyo sura nyingine za Makka, muhtawa na yale yaliyomo ndani ya Suratu-Fuss'ilat yamejikita zaidi katika kuzungumzia asili ya ulimwengu na uumbaji, maadi na kufufuliwa viumbe na ishara za qudra na uwezo wa Allah SWT kwa mwanadamu na ulimwengu kwa ujumla. Baada ya utangulizi huo mfupi, tunaianza sasa darsa yetu hii kwa aya ya mwanzo hadi ya nne ya sura hiyo ambazo zinasema:
حم
H'a Mim
تَنزِيلٌ مِّنَ الرَّحْمَٰنِ الرَّحِيمِ
Ni uteremsho kutoka kwa Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu.
كِتَابٌ فُصِّلَتْ آيَاتُهُ قُرْآنًا عَرَبِيًّا لِّقَوْمٍ يَعْلَمُونَ
Ni Kitabu kilicho pambanuliwa Aya zake, cha kusomwa kwa Kiarabu kwa watu wanao jua.
بَشِيرًا وَنَذِيرًا فَأَعْرَضَ أَكْثَرُهُمْ فَهُمْ لَا يَسْمَعُونَ
Kitoacho bishara na chenye kuonya. Lakini wengi katika wao wamepuuza; kwa hivyo hawasikii.
Kama tulivyowahi kueleza hapo kabla kwamba kuna sura 29 za Qur’ani ambazo zimeanza kwa herufi za mkato. Katika sura hizo na baada ya kutajwa herufi hizo, huashiriwa adhama ya kitabu hicho kitukufu cha mbinguni. Suratu-Fuss’ilat, nayo pia iko hivyo na imeanza kwa herufi mbili za haa na miim na kisha kufuatiwa na maelezo kwamba, kuteremshwa kitabu hicho cha mbinguni kunatokana na rehma za Mwenyezi Mungu. Kwa hivyo aya zake ni rehma kwa watu wote. Hata hivyo waumini, wao wananufaika na rehma za Qur’ani, lakini makafiri wanajikosesha wenyewe rehma hizo. Inapasa tuashirie pia hapa kwamba, aya za Qur’ani hazikuteremshwa kwa sura ya maandishi na wala Bwana Mtume SAW pia hakuziandika aya hizo kwa ajili ya kuwafikishia watu; bali alikuwa akiwasomea yale aliyokuwa akiteremshiwa kwenye moyo wake kwa njia ya wahyi. Na kwa sababu hiyo zimeitwa Qur’ani, yaani maneno yasomwayo. Bwana Mtume SAW aliwaamuru masahaba zake wanne, wayaandike yale aliyokuwa akiwasomea watu katika wahyi huo aliokuwa akiteremshiwa na Allah; na kwa sababu hiyo jina jengine la Qur’ani ni kitabu, yaani maneno yaandikwayo. Qur’ani tukufu imeteremshwa kwa lugha ya Kiarabu safi na iliyo fasaha na aya zake ziko wazi na wadhiha kabisa kwa mtu atakaye kuujua ukweli. Tab’an mbali na kuwaelewesha watu na kuwaongezea ujuzi wa mambo, Qur’ani inatoa bishara na maonyo pia, ili kuwashajiisha watu kufanya mambo mema na mazuri na kuwatahadharisha na kufanya mambo mabaya na maovu. Jibu la watu wengi kwa wito wa Mitume na vitabu vya mbinguni walivyowaletea lilikuwa ni kupinga na kukataa, kwa sababu wito huo ulikuja na mafundisho yaliyodhibiti na kuyawekea mpaka matakwa ya ghariza zao na matamanio ya nafsi zao na haukuruhusu waseme lolote watakalo au wafanye lolote lile wapendalo. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, Qur’ani ni maneno ya Allah SWT, si maneno ya Bwana Mtume Muhammad SAW. Muhtawa na yaliyomo ndani yake pia yanatokana na rehma nyingi na zisizo na ukomo za Mola Muumba. Na ndiyo kusema kuwa, maneno ya Qur’ani yenyewe na yaliyomo ndani yake pia yanatoka kwa Mwenyezi Mungu, Mjuzi na Mrehemevu. Kwa hiyo ni wazi kwamba, kufanya mambo kwa kufuata mafundisho yake kutaijenga na kuistawisha jamii ya wanadamu na kuifanya itukuke. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, kila lenye taathira na linalochangia kuwajenga kiroho watu na kuwafikisha kwenye uongofu limezungumziwa kwa ufafanuzi na kwa sura tofauti ndani ya Qur’ani tukufu, ikiwemo kubainishwa yaliyozisibu kaumu zilizopita, visa na matukio yenye ibra na mazingatio, mifano ya vitu mbalimbali, kutajwa neema za Mola, maamrisho na makatazo yake, sababu za kuporomoka kwa staarabu, mustakabali wa wanadamu, matukio ya Kiyama, miongozo ya kiakhlaqi n.k. Vile vile aya hizi zinatuelimisha kwamba, Qur’ani inampa mtu elimu, uelewa na mwangaza. Yeyote anayetaka kujua hakika na utambuzi sahihi wa mambo inapasa airejee Qur’ani tukufu. Halikadhalika aya hizi zinatutaka tujue kuwa, kwa mujibu wa misingi sahihi ya malezi, hofu na matumaini, bishara na maonyo ni mambo yanayolazimu kujumuishwa pamoja. Kulipa umuhimu moja na kulipuuza jengine kuna athari zenye madhara makubwa.
Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya tano ambayo inasema:
وَقَالُوا قُلُوبُنَا فِي أَكِنَّةٍ مِّمَّا تَدْعُونَا إِلَيْهِ وَفِي آذَانِنَا وَقْرٌ وَمِن بَيْنِنَا وَبَيْنِكَ حِجَابٌ فَاعْمَلْ إِنَّنَا عَامِلُونَ
Na wakasema: Nyoyo zetu zimo katika vifuniko kwa hayo unayo tuitia, na masikio yetu yana uziwi, na baina yetu na wewe kuna pazia. Basi wewe tenda, nasi tunatenda.
Aya hii inaashiria jibu la washirikina wa Makka kwa wito wa Bwana Mtume Muhammad SAW na kueleza kwamba: Wakati Mtume alipokuwa akiwasomea Qur’ani, badala ya kuisikiliza na kuizingatia, na ili kutaka kumvunja moyo mtukufu huyo katika ufikishaji wa wito wake walikuwa wakimwambia: Ewe Muhammad! Usijisumbue bure. Masikio yetu ni mazito na wala hatusikii uyasemayo. Na kwa yale yapenyayo masikioni mwetu, hayana athari yoyote ndani ya nyoyo zetu; ni kama kwamba kuna kizuizi baina yetu sisi na wewe kinachotufanya tusiukubali wito wako. Kwa hivyo wewe tuache sisi kama tulivyo tufanye vyovyote vile tutakavyo; na sisi pia tunakuacha wewe kama ulivyo ufanye yoyote yale upendayo. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba, aya za Qur’ani ni mithili ya mvua inayomiminika na kupenya kwenye ardhi yenye rutuba, ikaistawisha. Lakini inaponyesha juu ya jiwe na ardhi yabisi, si tu haipenyi ndani yake bali inaishia kutapanyika na kutawanyika. Hivyo ndivyo zilivyo pia nyoyo za watu wakaidi zinapoteremkiwa na aya za Mwenyezi Mungu. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa, kama mtu hana nia ya kuikubali haki, hata maneno ya Allah anayofikishiwa kupitia kinywa cha Mtume wake pia hayatomwathiri, seuze maneno ya watu wengine. Aidha aya hii inatuelimisha kwamba, taasubi na ufuataji mambo kibubusa, huwa mithili ya utando mweusi unaoziba macho ya moyo na kuufanya ushindwe kuiona na kuikubali haki.
Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya sita na ya saba ambazo zinasema:
قُلْ إِنَّمَا أَنَا بَشَرٌ مِّثْلُكُمْ يُوحَىٰ إِلَيَّ أَنَّمَا إِلَٰهُكُمْ إِلَٰهٌ وَاحِدٌ فَاسْتَقِيمُوا إِلَيْهِ وَاسْتَغْفِرُوهُ ۗ وَوَيْلٌ لِّلْمُشْرِكِينَ
Sema: Hakika mimi ni mtu kama nyinyi; ninapewa wahyi kwamba Mungu wenu ni Mungu Mmoja tu. Basi nyookeni sawa kumwendea Yeye, na mumtake maghufira, na ole wao wanao mshirikisha,
الَّذِينَ لَا يُؤْتُونَ الزَّكَاةَ وَهُم بِالْآخِرَةِ هُمْ كَافِرُونَ
Ambao hawatoi Zaka na wanaikataa Akhera.
Kinyume na wao washirikina waliokuwa wakizungumza kwa taasubi na inadi, Bwana Mtume SAW aliwahutubu wapinzani hao wa haki kwamba: Mimi ni mwanadamu kama nyinyi; sidai uungu wala kujikweza na kujifanya bora kuliko nyinyi. Mimi ninatokana na kabila na kaumu yenu. Tofauti pekee iliyopo baina yangu na nyinyi ni kwamba mimi ninateremshiwa wahyi wa kukutakeni muache shirki na mwache kuabudu masanamu na ninakulinganieni kumwabudu Mola pekee wa haki. Nyinyi mnazungumza hivyo na mimi, lakini jueni kwamba mimi sina nia ya kukulazimisheni muyakubali kwa nguvu maneno yangu. Ninachofanya ni kukuonyesheni njia ya haki na kukutakeni muifuate njia ya Allah na kuacha maovu mliyokuwa mkiyafanya huko nyuma ili Yeye Mola akusameheni. Sehemu ya mwisho ya aya hizi tulizosoma inatoa onyo na indhari kwamba, kubaki katika shirki kuna hatima na mwisho mbaya sana. Kisha katika kuwazungumzia washirikina, aya zinaashiria sifa zao mbili ambazo: Moja, ni kukanusha kwao Kiyama na nyingine ni kutowajali wahitaji na kuacha kuwapa msaada wa namna yoyote ile, ambayo nayo pia ni alama mojawapo ya kukanusha Kiyama. Sababu ni kwamba, mtu asiyemwamini Mwenyezi Mungu hutaka kila jambo kwa ajili ya nafsi yake tu na hawi na kitu cha kumtia msukumo wa kutoa kwa ajili ya watu wengine. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, Mitume walikuwa wakiwalingania watu kumfuata Mwenyezi Mungu, na si kuwafuata wao. Na lengo lao pia lilikuwa ni kuwakomboa wanadamu kwa kuwatoa kwenye makucha ya mataghuti wa nje na hawaa na matamanio ya ndani ya nafsi zao. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, kuamini upekee wa Mungu mmoja tu wa haki inapasa kujiakisi na kuonekane katika hali zote za maisha ya mtu. Tauhidi si imani tupu ya moyoni, bali ni dira na mwongozo wa mwenendo na matendo ya mtu katika maisha. Halikadhalika tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba, mtu muumini huwa na msimamo madhubuti na thabiti katika njia ya tauhidi. Hujitahidi kila mara kurekebisha makosa aliyofanya huko nyuma ili aweze kudumu katika kufuata njia ya Allah na kutokengeuka mkondo wa haki. Wa aidha aya hizi zinatutaka tujue kuwa, imani si kitu cha kudai kwa maneno matupu. Kwa hiyo muumini ambaye hatoi Zaka, ajijue kuwa ana chembechembe za shirki na ukafiri ndani ya nafsi yake. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 874 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atuhughufirie madhambi yetu, azifanye thabiti imani zetu na aufanye mwema mwisho wetu. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/